BAHATI BUKUKU |
MWAKA 1988, RUNGWE, MBEYA
“Lusako amka...Lusako amka, niliisikia sauti ya baba yangu, mzee John Bukuku akiniamsha asubuhi sana tofauti na siku nyingine.
“Lusako ni jina langu lingine ambalo kwetu lina maana ya ‘ngekewa’ au ‘bahati’.
“Siku ile baba alinitaka niamke kwa ajili ya kujiandaa na kwenda kuanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi iitwayo Muungano iliyopo Ilolo, Mbeya.
“Nilikurupuka kutoka kitandani, nilikuwa mdogo mno, miaka saba tu. Baada ya kuisikia sauti ya baba yangu, nikaamka na kutoka nje.
“Naikumbuka siku hii vilivyo kwa sababu ndiyo ilikuwa siku niliyokuwa nikiisubiria kwa hamu kubwa.
“Kila siku nilikuwa nikiwaona watoto wenzangu wakienda shule, walivalia sare zao za shule huku wakiwa na madaftari. Nilitamani sana kuwa kama wao. Nilitamani nami siku moja nibebe madaftari yangu, nivae sare za shule na kuelekea shuleni kusoma.
“Ukiachana na watoto hao waliokuwa wakipita nyumbani kuelekea kwetu shuleni, dada yangu aliyeitwa Selina alikuwa akiniambia mambo mengi kuhusu shule, hasa kunywa uji mwingi wenye sukari, nami nikajikuta nikianza kutamani kusoma.
“Kila nilipokuwa nikikaa, nilitamani siku ifike na mimi nivae sare za shule na kuelekea shuleni. Siku niliziona haziendi, kiu kubwa ya kutamani kusoma ilinishika.
“Kila nilipokuwa nikimsikilizia baba kuona kama alikuwa akitaka kunipeleka shule, hakuwa akifanya hivyo. Niliumia sana moyoni.
“Siku hiyo ambayo baba alikuwa ameniamsha. Nilijiandaa tayari kwa kwenda shule kwani niliamini kwamba siku hiyo ndiyo ingekuwa siku ya kwanza kwangu kuanza masomo shuleni.
“Nikajiandaa huku mama akinivaliasha nguo safi, baba akanishika mkono na kuanza kwenda shule.
“Njia nzima, nilijisikia furaha isiyo kifani, kitendo cha kupelekwa shule siku hiyo kilinifanya kujisikia mtu wa tofauti sana, furaha ilinizidi hadi nikaona tulikuwa tukichelewa kufika shule. Nilitaka na mimi nikae darasani na kuanza kusoma.
“Kwa sababu shule haikuwa mbali sana, tulichukua dakika chache tukafika. Sikuwa peke yangu, bali kulikuwa na watoto wengi ambao waliletwa shuleni hapo na wazazi wao kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo ya Muungano iliyokuwa mita mia moja na ishirini kutoka nyumbani kwetu.
“Kila mtoto aliyeletwa shuleni hapo alionekana kuwa na furaha, kitendo cha kuitwa kwa ajili ya kuanza masomo kilimfurahisha kila mmoja na kuamini kwamba ilikuwa ni lazima tuanze masomo ili na sisi tuanze kuvaa sare na hata kunywa uji kila tufikapo shuleni hapo.
“Staili ya zamani ya kuchagua wanafunzi wa kujiunga na
darasa la kwanza ilikuwa tofauti. Watoto wote walioletwa shuleni hapo,
walitakiwa kusimama na kuupitisha mkono wao kichwani ili kushika sikio la
upande wa pili.
“Endapo mtoto angeweza kushika sikio, basi alikuwa amefaulu
kuanza darasa la kwanza lakini kama alifeli, basi hakutakiwa kuanza shule.
“Baada ya kuona baadhi ya watoto wenzangu wameshindwa
kulishika sikio, nikahofia kwa kuona kwamba hata mimi pia ningeshindwa, hivyo
nikaanza kujipa mazoezi, kila nilipopitisha mkono, nilishindwa kulishika sikio
langu.
“Hapo, tayari nikaona kwamba ningeshindwa kuanza masomo
yangu, nilichokifanya ni kung’ang’ania kutaka kulishika sikio lile ili
ikiwezekana, nilishike tu kisha nimfuate mwalimu huku mkono wangu ukiwa
sikioni.
“Bahati mbaya nilishindwa kufanya hivyo.
“Zamu yangu ilipofika, nikaambiwa niupitishe mkono wangu kichwani na kulishika sikio la upande wa pili, nikashindwa na hivyo mwalimu kusema kwamba sikutakiwa kuanza darasa la kwanza.Nilitakiwa nirudi nyumbani hadi mwaka unaofuata.
“Zamu yangu ilipofika, nikaambiwa niupitishe mkono wangu kichwani na kulishika sikio la upande wa pili, nikashindwa na hivyo mwalimu kusema kwamba sikutakiwa kuanza darasa la kwanza.Nilitakiwa nirudi nyumbani hadi mwaka unaofuata.
Chanzo-globalpublishers
Comments