TOFAUTI YA NEEMA NA NEEMA

Na Frank Philip


“Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu” (Matendo 17:30,31).

“Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao. Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu. Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema? Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake. Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai” (Waebrania 10:26-31).

Nimesikia habari ya Neema, naam, Neema ni kitu chema na kizuri, lakini je! Unajua kwamba Neema ni MWALIMU? Kwa maana imeandikwa “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa” (Tito 2:11,12); Kama Neema inaokoa, basi jua imetupasa kusikiliza inachotufundisha; kukataa ubaya na tamaa za kidunia, nk. Hii ndio Neema!

Mara nyingi nimesikia watu wakifanikiwa kupata MALI, FEDHA, na MAMBO mazuri ya MWILINI, wanasema “ni kwa NEEMA TU”! Sawa, ni kwa Neema tunaingia na kutoka, tunaishi na kufanikiwa, je! Neema haifundishi kuishi maisha MATAKATIFU pia? Mbona Neema haikuanza kwa kusema habari za MALI na FEDHA, ila imeanza kufundisha kuishi maisha matakatifu, na ya kumpendeza Mungu? Je! Tukiisha kuwa na mali nyingi, tutahesabiwa haki yoyote mbele za Mungu zaidi ya KUJIVUNA kwa ubatili na kujilisha upepo, tena mbele ya wanadamu tu?

Ngoja tuangalie Neema iokoayo. Mara nyingi watu wameangalia Neema kama kitu cha mchezo, cha kuingia na kutoka kama soko lisilo na lango. Paulo akasema “je! Tutende dhambi ili Neema izidi?” (Warumi 6:1,2) Kweli watu wanajua Mungu ana rehema, je! Kama Mungu ana rehema ndio “tutende dhambi kwa KUSUDI tu?” (Waebrania 10:26). Kuna tofauti ya mtu atendaye dhambi kwa sababu ya UJINGA (hajui Kweli ya Mungu au hamjui Mungu) na mtu atendaye dhambi kwa MAKUSUDI huku anamjua Mungu. Angalia tena hapa, Je! “Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?” Hapa kuna makundi mawili, watu wenye UJUZI wa Kweli na wasio na ujuzi wa Kweli; wajuao Kweli na “kufamnyia jeuri Roho wa Neema” imewapasa adhabu kubwa zaidi kuliko wale wasiojua. Tena kwa wale wasiomjua Mungu, ambao hapa wanaitwa wajinga, kwao “Mungu anajifanya kama hazioni dhambi zao”. Angalia tena, sio kwamba “hazioni” ila “anajifanya hazioni”, kwa lugha nyingine, Neema imewafunika ili wafikilie TOBA ya kweli na ujuzi wa ile Kweli.

Kila nikitafakari habari za Musa mtumwa wa Mungu, huwa naogopa. Baada ya kufanya kazi nzito ya huduma kwa miaka zaidi ya 40, akiwa mwaminifu na mwadilifu sana, ghafla! Musa anafanya “kosa” ambalo lilimgharimu kutokuingia nchi ya ahadi! Japo Musa aliomba sana, Mungu hakukubali, na alimkataza asiombe tena hilo jambo kwa maana “hatapewa”! Ukiangalia sana utaona hili kosa lilivyo dogo “kibinadamu” ila ni “kubwa kwa Mungu”, tukizingatia KIWANGO cha Musa cha kumjua Mungu. Angalia hapa, “BWANA akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa” (Hesabu 20:12) “hamkuniamini ili kunistahi mbele ya macho ya watu” Umeona hili jambo? Sio habari ya kuvunja amri kumi, ila kwa kiwango cha kumjua Mungu cha Musa, alipaswa kuenenda TOFAUTI na “watu wengine”, ndio maana kosa hilo hilo alilofanya Musa, yamkini walifanya wengine BILA KUJUA, na Mungu “akajifanya haoni” kwa sababu ya ile Neema, ILA kwa MUSA na HARUNI, Mungu aliona na akahukumu pale pale. Angalia MAMBO uyafanyao machoni pa watu, huku wakijua wewe ni “mtu wa Mungu”, ipo adhabu ya kumdhalilisha YESU mbele za watu, kama ilivyo kumwonea AIBU yeye na Neno lake mbele za watu.

Tukijua jambo hili, basi tuwe na hekima, kwa sababu HUKUMU huja kwa sababu ile KWELI tuijuayo na kuipuuza. Ndio maana “Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa” (Yohana 9:41). Angalia tena, sisi tulio nuruni, tunajua kwa sehemu na viwango tofauti Kweli ya Mungu, tujue hatutakaa fungu moja katika KUHESABIWA “haki” japo neema ni ile ile. Kila mmoja atende kwa bidii katika ngazi yake, tukijua ipo siku ya kutoa hesabu ya kila kazi na kila neno lililotoka vinywani mwetu.

Aliyepewa vingi, kwake huyo vitadaiwa vingi, na aliyepewa vichache kwake huyu vitatakiwa vichache. Angalia tena jambo hili ambalo BWANA anatufundisha, “Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi” (Luka 12:48). Hakuna atakayepona kipigo kwa kufanya kosa; ajuaye na asiyejua, tofauti ni VIWANGO vya mapigo tu.

Ukiona mtu anacheza na neema ya Mungu baada ya kuijua Kweli, huyo hajui kitu afanyacho. Hiyo kitu Paulo anaita “kumkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo” (Waebrania 10:26-31).

Mungu atupe kuona hili jambo kwa jinsi ya rohoni na kufanya yatupasayo, ili tuweze kueneda katika Neema hii na kuwa na hofu ya Mungu saa zote.

Frank Philip.

Comments