POKEA HABARI NJEMA KULIKO ZOTE.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Yawezekana kabisa siku ya jana ulipokea habari njema za kufaulu usaili,  kuna mwingine yawezekana alipokea habari njema za kulipwa pesa yake, au yawezekana kabisa kuna ndugu alipokea habari njema za kuonana na ndugu zake ambao kwa miaka zaidi ya kumi hakuwaona. Wapo waliopokea habari njema za kushinda kesi na kuna ambaye amesikia wachawi wamehama katika kijiji chao. Hizo ni habari njema lakini hii ninayokuletea leo ndio habari njema kuliko zote.
Habari njema hii njema inaanza kwa BWANA YESU kuwaagiza mitume waipeleke habari hii njema na katika kuipeleka kwao wengi waliipokea na kuipokea huko kulipelekea hadi na wewe leo unaipokea habari hiyo njema.

 Marko 16:15-16 ''   Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. ''

Hii ndio habari njema tena ina uzima ndani yake, ndugu ipokee habari hii njema maana hakuna habari njema zaidi ya hii.

-Yawezekana neno la kwanza kuambiwa siku ya leo lilikuwa baraka kwako , yawezekana umeamka tu na kukutana na meseji kwamba  unahitajika kazini kesho. 
-yawezekana kabisa umeamka tu na kupokea habari njema kwamba mama au baba yako aliyekuwa amelazwa amepona na kuruhusiwa kutoka hospitalini. 
hizo ni habari njema lakini sio njema kuliko hii ninayokuletea leo.
Habari njema kuliko zote ni injili ya BWANA YESU.
Neno ''INJILI'' maana yake ni habari njema za ufalme wa MUNGU.
Hakuna habari njema kama habari za kutoka kwa MUNGU aliyekuumba.
Habari njema za ufalme wa MUNGU ndizo habari njema kwako kuliko kitu chochote kile.
Kupitia habari njema hii, BWANA YESU anakutaka kwanza uipokee hii habari njema kisha utubu na kuanza kuiishi hii habari njema 
Marko 1:14-15 ''....  YESU akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya MUNGU, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa MUNGU umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.'' 

Wengi wanaipokea hii habari njema maana habari hii njema ni Neno la MUNGU, Na ukiliweka hili neno la MUNGU ndani yako litakusaidia usitende dhambi na kukosa mbingu. Mfano wa aliyeliweka neno la MUNGU ndani yake ni huyu ambaye anasema hapa kwamba 
'' Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.-Zaburi 119:11''
-Huyu ameipokea habari njema ili asitende dhambi, na hata wewe ukiiweka moyoni mwako au ukiliweka neno la MUNGU katika matendo hakika hutatenda dhambi.
Ni heri kuishi ukipokea habari hii njema kuliko zote.

Injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU ambao umeletwa kwa wanadamu na BWANA YESU KRISTO .
-Injili ni mpango wa MUNGU wa kuwaokoa wanadamu kutoka mikononi mwa shetani.
Injili ni habari za uzima wa milele ambao unapatikana katika YESU KRISTO pekee.

Yohana 14:6 -7 '' YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na BABA; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. ''

MUNGU Hana Kamati Ya Ushauri, Kwa MUNGU Ni Amri Sahihi. Ndio Ni Ndio Na Sio Ni Sio. 
Hivyo hakuna njia nyingine ya kwenda uzima wa milele ila ni kupitia YESU KRISTO tu, Ukimkataa YESU unaukataa uzima wa milele. MUNGU nimesema hana kamati ya ushauri hata aseme kwamba naomba tumjadili fulani japokuwa yuko jehanamu ili atoke, hakuna kitu kama hicho. 
MUNGU anakutaka leo uamue juu ya kesho yako. kama unataka kesho yako iwe jehanamu basi mkatae YESU na kama unataka kesho yako iwe uzima wa milele hakika mpokee YESU leo.
 Matendo 4:12 ''  Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. ''

 Kama Kuna Habari Njema Rafiki Yako Kukushirikisha Basi Ni Kukuambia YESU Anakupenda Na Hataki Uende Jehanamu.
Ukiipokea habari hiyo njema  basi hakikisha unampokea BWANA YESU na jina lako litaandikwa kwenye uzima wa milele.
Warumi 10:9-10-11,13 ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.
  kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka.   ''


Husika na habari njema hii kwa kumpokea BWANA YESU kama BWANA na Mwokozi wako kisha sema 
 ''BWANA YESU Niongoze Ili Nimalize Mwendo Salama.''
Baada ya kumpokea BWANA YESU hakikisha unajazwa na ROHO MTAKATIFU maana ROHO ni ahadi kwa waaminio wote.
Yohana 14:26 ''Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''

 Tunaitwa Wateule Wa KRISTO Kwa Sababu Tuna ROHO MTAKATIFU Lakini ROHO MTAKATIFU Akikuacha Hautakuwa Na Tofauti Na Wachawi Na Makahaba. Ni Hatari Sana Kuachwa Na ROHO MTAKATIFU. Yeye Ni Mtakatifu Na Atakuacha Tu Kama Utajirudisha Kwa Shetani Katika Matendo Yako.
Ndugu yangu, hakikisha unaenenda kwa ROHO na kuongozwa na ROHO MTAKATIFU maana ROHO MTAKATIFU ndiye ROHO wa KRISTO na mtu asipokuwa na huyo ROHO wa KRISTO basi huyo sio wake KRISTO.
 Warumi 8:9 '' Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake. ''
 Je usipokuwa wake KRISTO unaenda wapi? 
ni hatari sana, kumbe tunatakiwa tumhitaji ROHO MTAKATIFU kwa juhudi kubwa sana

Ndugu, pigania kubaki kwenye habari njema za ufalme wa MUNGU.
 pigania jina lako liandikwe kwenye KITABU CHA UZIMA na sio kwenye chupa za soda.

 Kama uliyeipokea habari njema kuliko zote basi hakikisha unatenda mema sawasawa na habari njema inavyokutaka.
Ni Dhambi Kwa Kila Ajuaye Kutenda Mema Na Hayatendi
Yakobo 4:17 '' Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi. '' 
-Ndugu, hakikisha unabaki kwenye habari njema za ufalme wa MUNGU siku zote.
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments