KATAA KUTUMIWA WALA KUTUMIKISHWA NA SHETANI.

Na Mtumishi Peter M Mabula
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la uzima.
Kutoka 23:24 ''Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande.'' 
-Kusujudia sanamu au miungu maana yake unaitumikia na kuiabudu. ni machukizo kwa MUNGU wa mbinguni.
-Ni Jukumu La Kila Mtu Kukataa Kutumiwa Na shetani Na Pia Kukataa Kutumikishwa Na Dunia. 
MUNGU anakutaka kukataa kutumikia shetani na kama unamtumikia shetani geuka leo.
Yoshua 24:15 ''Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.''
-BWANA  huwa halazimishi wanadamu kumwabudu lakini  kumwacha YESU KRISTO na kugeukia injili za namna nyingine ni kujiangamiza.
Warumi 6:23 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA wetu. ''
-MUNGU hakulazimishi umwabudu lakini ni madhara makubwa kumwacha MUNGU aliye hai na kuanza kuabudu sanamu au kuabudu wafu na machukizo yote. 
Dunia Itapita Na shetani Hana Nafasi Kwenye Ufalme Wa MUNGU.
1 Timotheo 4:1-2 ''Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;''
=Wakristo maana yake ni wanafunzi wa KRISTO na wanamtii KRISTO lakini leo hali imebadilika.
-Kuna wakristo lakini kiongozi wao wa kanisa ni wakala wa shetani na ndio maana huwafundisha uongo na kusema kwamba yeye ndiye Kristo wa pili, kiongozi kama huyo ni mkuu wa giza kabisa. Kuna wengine leo hujiita Mungu wa majeshi, hao  ni wakuu wa giza kutoka kuzimu. mkuu wa giza ni zaidi ya jini ni watu wabaya sana.
Kuna watu leo wanajiita Kristo, hao ni wakuu wa giza wa daraja la juu sana kuzimu. lakini kuna watu ambao huwafuata na kupewa viapo na vitisho vya kishetani na kujikuta wamekuwa mateka, wanatumikishwa na shetani na wanatumiwa na shetani kabisa. ni siku za mwisho ndugu zangu. 

 Mithali 16:25 ''Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti.''
nakuomba kama uko katika dhehebu la namna hiyo hama haraka maana ufahamu wako umetekwa hata huoni rohoni. wasio na MUNGU ni jambo rahisi sana kuwajua maana shetani huwapa sheria ngumu sana ambazo watazishika na mwisho ni jehanamu. kuna kanisa waumini wa kanisa hilo hawaruhusiwi kusikiliza mahubiri ya wahubiri wateule wa BWANA YESU. Ni siku za mwisho na maelfu ya watu wanatumikishwa na shetani. ndugu hama huko na usikubali kutumika kwa shetani tena.
 Kuna wakati nilitamani kulia maana kuna ndugu mmoja aliniambia kwamba kanisani kwao mhubiri   jumapili katika ibada alihubiri somo lenye kichwa cha ujumbe usemao ''KUNYWENI POMBE KADRI MWEZAVYO MAANA NI NZURI''
Unaweza ukajiuliza huyu ndugu ni mkuu wa giza wa kuzimu au ni joka kabisa anahubiri maana hakuna mhubiri hata mmoja anayemtii BWANA YESU anayeweza kuhubiri hivyo.
 Mithali 29:23 ''Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa''

 -Ndugu, nakuomba Jitenge Na Vyote Vinavyozuia Juhudi Zako Za Kwenda Uzima Wa Milele.  Ni siku za mwisho na kuna mafundisho ya mashetani mengi sana na wanaofundisha mafundisho hayo ya mashetani wanaweza hata kutumia Biblia lakini kumbe wanahubiri mafundisho ya mashetani. Mtu anaweza akaitumia Biblia na kusema kwamba BWANA YESU hakumaliza kazi ndio maana yeye huyu ndugu ametumwa ili kuimalizia kazi, ndugu ukisikia hivyo tambua kwamba huyo anayedai hivyo ni shetani mwenye mapembe kabisa. BWANA YESU ni MUNGU mkuu na ndiye aliyewaumba wanadamu wot, Hakuna mwenye mamlaka zaidi yake, ukimweka Pembeni BWANA YESU kwenye mahubiri yako basi tambua kwamba wewe unatumikwa kwa shetani hata kama unatumia Biblia.
2 kor 4:3-6 ''  Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU. Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali KRISTO YESU ya kuwa ni BWANA; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya YESU. Kwa kuwa MUNGU, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa MUNGU katika uso wa YESU KRISTO. ''
 -Watu Wengi Wanajua Dini Ila Hawamjui MUNGU, Watu Wengi Wanajua Madhehebu Ila Hawamjui MUNGU. Kuna madhehebu MUNGU wala hajawahi kuwako huko. huwezi kufundisha mafundisho ya mashetani harafu ukasema una MUNGU wa mbinguni. haiwezekani.
Huwezi kujiita Kristo harafu MUNGU wa kweli akawa upande wako. Huwezi kujiita Mungu wa majeshi harafu ukadhani una MUNGU wa kweli. kuna madhehebu MUNGU wa mbinguni wala hayajui kama yapo hata kama yana waumini maelfu ya watu.
Mithali 18:7 ''  Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake. ''

 Tofauti Ya Mipango Anayokupangia BWANA YESU Na Ile Mipango Ya Yule Joka Adui Yetu. 
wakati shetani anapanga kukuangamiza YESU Anakupangia Uzima Sasa Na Kisha Uzima Wa Milele
Yohana 10:7-11 '' Basi YESU aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. ''
- shetani kazi yake ni kuwatendesha dhambi, Lakini BWANA YESU Kazi Yake Ni Kuzivunja Na Kuziharibu Kazi Za shetani
1 Yohana 3:8 '' atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. ''
-Atendaye Dhambi Ni Wa shetani lakini ukimpokea YESU Anakuweka Huru
Yohana 8:36 ''Basi Mwana(YESU) akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.''
-Mkimbilie BWANA YESU ili uwe huru mbali na kutumikishwa na shetani.
Zaburi 1:5-6 '' Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki. Kwa kuwa BWANA anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea. ''
 Kile Utakachochagua Ndicho Kitafanyika.
-Ukichagua Kufa Hakika Utakufa.
 -Ukichagua Kuheshimiwa Hakika Utaheshimiwa.
-Ukichagua Kuonewa Na Wachawi Hakika Watakutesa Miaka Yote.
-Ukichagua Kukiri Udhaifu Hakika Udhaifu Wote Unaoupanga Utakupata. 
-Waza Ushindi Kupitia Jina La YESU KRISTO.
-Kataa kumiwa na shetani, kataa kutumikishwa na shetani. 
BWANA YESU anasema 
'' Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.-Mathayo 10:39''
-Ndugu usikubali kumtumikia shetani kwa starehe ya muda mfupi tu kisha unaenda motoni.
Hata wanandoa msikubali kutumikishwa na shetani na wala msikubali kumtumikia shetani maana kuna jehanamu kwa watenda dhambi.


 -Kama Wewe Mama Una Mme Wako Ni Mwizi Basi Tambua Hata Kukusaliti Anakusaliti Maana Mtenda Dhambi Ni Mtenda Dhambi Tu. Haiwezekani Huyo baba Asiwe Na Hofu Ya Kuiba Tu Harafu Awe Na Hofu Ya Kuwa Na Nyumba Ndogo. Mimi Siamini. 
-Na Wewe Baba Kama Una Mke Muongo Usidhani Kwamba Hawezi Kukusaliti, Maana Mtenda Dhambi Ni Mtenda Dhambi Tu, Haiwezekani Asiwe Na Hofu Ya Uongo Harafu Awe Na Hofu Kukusaliti. Dhambi Ni Mbaya Ndugu Zangu. 
BWANA YESU Alikuja Ili Kuwatoa Watu Dhambini Na Kuwapeleka Kwenye Nuru Yake Ya Ajabu. Mtu Akiwa Hana Hofu Ya MUNGU Nakuhakikishia Ndugu Huyo Anaweza Kufanya Dhambi Yeyote. Ni Saa Ya Kutubu Na Kurejea Kwa BWANA. Ndugu, Kataa Dhambi, Ogopa Dhambi, Ikimbie Dhambi Na Usifanye Dhambi.
Mithali 18:12 ''Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. ''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
mabula1986@gmail.com
+255714252292.
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili

Comments