JE SHOKA LIJISIFU JUU YAKE ALITUMIAYE?



 
BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Je shoka lijisifu juu yake anayelitumia?

Je Msumeno ujitukuze juu ya anayeutumia?


Isaya 10:15 ‘’ Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. ‘’


-Shoka ni silaha ambayo hutumiwa na wanadamu kukata miti au vitu mbalimbali,  Mwanadamu ndiye mwenye mamlaka yote kuhusu shoka, annaweza kulitumia shoka hilo au anaweza asilitimue.

Biblia inatuita wateule wa MUNGU kwamba sisi ni silaha za vita vya MUNGU.


Yeremia 51:20-23 ‘’ Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake; na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke;  na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng'ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida. ‘’


-MUNGU  aliwatumia waisraeli kama silaha za vita vyake.

-Silaha ni kama shoka ambayo inatumiwa na mtumiaji, shoka haitakiwi kujisifu au kuchukua utukufu wa kutumika kwake bali heshima yote hupata aliyeitumia.

MUNGU aliwatumia Waisraeli  kama silaha  za kuangamiza Yeriko iliyokuwa imejaa waabudu miungu, kazi ya Waisraeli ilikuwa tu kupiga kelele na kupitia kelele hizo MUNGU alitenda makuu na maadui za MUNGU waliangamia.

Hata wewe ndugu unaweza leo kutumika kama silaha ya MUNGU kupitia maombi yako ya kuharibu kila kazi ya wachawi iliyoinuka katika jamii yako. Lakini hautakiwi kujisifu baada ya baada ya ushindi bali mpe MUNGU heshima maana ndiye aliyekushindia.


Isaya 45:9 ‘’Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?’’


Kanisa linapoomba kwa ajili ya amani ya nchi na MUNGU akailinda nchi sio kazi ya kanisa kujisifu bali ni nafasi ya kanisa kumtukuza MUNGU kwa matendo yake makuu kwa kuilinda nchi.

Mfalme Ahabu baada ya kumwasi MUNGU, MUNGU alimtumia Nabii Eliya kama silaha za vita vyake, kazi ya Eliya ilikuwa kutumia Mamlaka ya KRISTO iliyokuwa ndani yake kuamua na kutomba  na hakika BWANA aliwaadhibu Israeli wote hadi mfalme wao Ahabu. Eliya hakujiinua na wala hakujisifu bali alimtukuza MUNGU.

Je shoka lijisifu juu yake alitumiaye?

Kama mtumishi wa MUNGU wewe hakika umekuwa chombo na  silaha za BWANA. BWANA YESU anaweza hata akakupeleka kwa njia ya maono kwenye kikao cha wachawi na ukaisikia mikakati yao yote, ukawaeleza kanisa na kanisa likaomba  hata mipango yote ya wachawi yote ikafa. Ni jukumu lako uliyeona maono kumtukuza BWANA na pia ni jukumu la kanisa kumtukuza MUNGU na sio kutumia nafasi hiyo kujisifu na kujitangaza kama kanisa badala ya kmtangaza KRISTO YESU anayeokoa. Kanisa ni silaha lakini BWANA ndiye anayeitumia silaha hiyo hivyo silaha haiwezi kujisifu wala kujiinua juu yake anayeitumia.

 Je msumeno ujitukuze juu yake anayeutumia?

Leo Watumishi  wengi wamefanyika silaha za BWANA za vita na MUNGU amewashindia, MUNGU amelishindia kanisa,MUNGU amelishindia taifa,, MUNGU amepigana mwenyewe kupitia waombaji. Je waombaji  au watumishi wa MUNGU kwanini kujiinua?


Wakolosai 1:16-17 ‘’ Kwa kuwa katika yeye(KRISTO) vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. ‘’


-Kuna watu zamani walikuwa watumishi wa KRISTO lakini kwa baadae wamegeuka na kujiona na wao ni sawa na KRISTO. KRISTO ni MUNGU na ndiye aliyewaumba watumishi hao lakini ajabu watumishi hao wamejiinua na kumsahau muumba wao. Hawahitaji tena kumtii BWANA wala kumwabudu.


Wakolosai 3:9-11 ‘’ na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika MUNGU aliyeviumba vitu vyote;  ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya MUNGU iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho;  kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika KRISTO YESU BWANA wetu. ‘’


Ndugu zangu, je aliyeumba ajiinue juu yake aliyemuumba?


Warumi 9:20-22 ‘’ La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye MUNGU? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?  Ni nini basi, ikiwa MUNGU kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;  ‘’


Leo makristo  wa uongo wengi wanaanzisha makanisa na dini na kujipa sifa ya KRISTO na kujipa heshima ya KRISTO wakati wao ni wanadamu tu wa kawaida na wote wanahitaji neema ya KRISTO YESU BWANA wetu, hawa wote wako kimyume na BWANA YESU na wanapotosha wengi.

Ndugu zangu, jambo la kukumbuka ni hili, BWANA YESU siku moja atarudi na kuhukumu, BWANA atamlipa kila mwanadamu sawasawa na matendo yake.


Isaya 29:16 ‘’ Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu?   ‘’
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments