NDUGU MTEULE VUMILIA DHIHAKA NA MAUDHI YOTE .



BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU.
Kuokoka tu ni kwa neema ya MUNGU wala sio kwa sababu ya ujanja wetu wala chochote chetu, ndiposa  Biblia inasema

''Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.  Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika KRISTO, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo.-Waefeso 2:8-10.''

-Kuokoka mtu huokoka kwa neema ndio maana unatakiwa kuulinda sana wokovu wako ulioupewa bure na MUNGU.
-Tunapookoka tunakuwa vyombo viteule vya MUNGU vilivyoumbwa katika KRISTO YESU.
-Kuna matendo mema ambayo MUNGU aliyaumba ili kila anayempokea YESU KRISTO aanze kuishi katika hayo matendo mema. matendo mema hayo ambayo unapookoka unaanza kuyaishi ndio chanzo cha watu kukushangaa maana ingawa unaishi nao lakini katika matendo yao mabaya uko mbali kama Tanzania na China. Matendo yako mema na ya kitakatifu yanaweza kuwafanya hata ndugu wakafanya kikao ambacho tangu uzaliwe hujawahi kukiona kikifanyika na lengo kuu la kikao hivyo ni kukujadili wewe, sio kwamba umefanya kosa lolote ila ni kwa sababu umeokoka. mwingine akibebeshwa mimba  kabla ya kuolewa katika ukoo wenu wala hutaona kikao, kijana akiiba na kukamata au kufungwa wala hutaona kikao katika ukoo wenu ila wewe kuokoka kikao utakiona, utanyooshewa vidole na kila mtu maana umefanya jambo baya kwao japokuwa katika uhalisia wewe umefanya jambo bora kuliko yote ambayo mtu yeyote katika ukoo amewahi kufanya. Kuokoka ni kutangaza vita na shetani.
Kila aliye upande wa shetani lazima tu akuchukie maana umeokoka.

Ndugu yangu, kumbuka hii kwamba wewe sio wa kwanza kupata misukosuko kama hiyo baada ya kuamua kuchagua njia ya uzima wa milele hata kama siku zilizopita ulikuwa katika barabara pana ya kwenda jehanamu. Ulipookoka maana yake uliachana na barabara pana ya jehanamu na kuamua kuingia katika barabara nyembamba ya uzima wa milele. barabara ya uzima wa milele inaitwa nyembamba kwa sababu tu wanaoiona ni wachache sana ukilinganisha na wale walio katika njia pana ya jehanamu.

Ndugu yangu ulifanya jambo jema sana kuokoka na leo nakutia moyo nikikuomba kusonga mbele hata kama utakutana na ugumu kiasi gani. waza uzima wa milele ndipo utakuwa na nguvu za kusonga mbele. dhihaka na uonevu wakati mwingine upo lakini songa mbele maana BWANA YESU yu karibu na siku hiyo thamani yako ndipo itakapoonekana zaidi.
Biblia inasema kuhusu uvumilivu wako kwamba

''Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi;-2 Wakorintho 4:8-9''

-Ndugu yangu, vumilia dhihaka zote za ambao hawataki wokovu wako ulio wa thamani sana.
-Ndugu, Vumilia maudhi yote ya wanadamu ambao hawataki wewe ubaki katika wokovu.
-Vumilia kwa kila neno baya maana kuna thawabu kuu kutoka kwa MUNGU siku ile ikifika.
-Kwa wateule wa KRISTO kama ulivyo wewe tambua kwamba

''MUNGU kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.-Zaburi 46:1-3''

-Ndugu, vumilia dhiki zote na endelea na maombi maana kesho yako haitakuwa kama ilivyo leo yako. BWANA ana ushindi wako tena ana uzima wako wa milele. MUNGU ndio ngome yako na baki siku zote katika ngome hii ya uzima wako.

''Maana(MUNGU) umekuwa ngome ya maskini, Ngome ya mhitaji katika dhiki yake, Mahali pa kukimbilia wakati wa tufani, Kivuli wakati wa hari; Wakati uvumapo upepo wa watu watishao, Kama dhoruba ipigayo ukuta.-Isaya 25:4''

-Maombi ni maisha ndugu na nakusihi sana kuendelea na maombi pamoja na kumtii ROHO MTAKATIFU maana yeye ndiye msimamizi wa Wokovu wako.
Kwa maombi yako MUNGU atakulinda na kukuponya na kila uovu.
Kwa maombi yako BWANA atakubariki kiroho na kimwili.
Kwa maombi yako MUNGU atakubariki kwa baraka zote unazozihitaji.
Endelea na maombi ndugu.

 ''BWANA ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao.-Nahumu 1:7''

Licha ya kupata misukosuko katika baadhi ya maeneo yako bado wewe mteule una mamlaka kuu kutoka kwa MUNGU, MUNGU kwa upendo wa ajabu sana ameweka mamlaka ndani ya wateule wake.
Yawezekana wewe ni mnyonge kimwili na kwa muonekano lakini wachawi wanaweza wakakuogopa wewe kuliko yule mtenda dhambi tajiri mwenye walinzi 7. kwanini wakuogope wewe?
Ni kwa sababu ndani yako kuna mamlaka ya MUNGU.
Ndani yako kuna jina la YESU ambalo ukilitamka adui anakimbia na mahali pake hapataonekana tena.
Omba ndugu ukiitumia mamlaka ya KRISTO iliyo ndani yako.
BWANA YESU mwenyewe anasema neno hilo kwako mteule wake.

''Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.-Luka 10:19''

Ndugu mtumainie BWANA na songa mbele katika yeye kwa utakatifu na maombi.

''BWANA atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida. Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, BWANA hukuwaacha wakutafutao.-Zaburi 9:9-10''

BWANA YESU ana uzima wa milele na kwa wewe kumpata YESU na kumtii hakika umepata uzima wa milele.

''BWANA anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba.-Zaburi 37:18-19B''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments