JINSI NILIVYOSAMEHE JAMBO AMBALO NILIAPA KUTOKUSAMEHE.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU KRISTO atukuwe ndugu.
Kama kijana  nilipanga maisha yangu yatakuwaje baadae.
Nilipanga mipango mingi sana ya maisha na jambo kubwa nilipanga kwamba ni lazima nioe nikiwa na miaka 24, huo ni utaratibu wangu ambao niliupanga tangu zamani sana.
Mwaka 2007 Nilienda kuishi Zanzibar mara tu baada ya kutimiza miaka 21.
Namshukuru MUNGU maana baada tu ya kukaa huko kwa miezi kadhaa BWANA YESU aliniokoa( nitashuhudia jinsi nilivyookoka siku moja maana ilikuwa ni ajabu ya ajabu sana)
.
Baada ya kuishi maisha ya wokovu kwa miaka 2 nilipata mchumba ambaye tulipendana sana. alikuwa ndio amemaliza sekondari na tulikubaliana kwamba tusubiri matokeo yake ya Form 4 ndipo tutajua kwamba tuoane lini. Binti yule alikuwa mtumishi kanisani na hakika alikuwa mcha MUNGU mzuri.
Baada ya matokeo kutoka yalikuwa sio mazuri sana maana hayakumruhusu kuendelea kidato cha 5 japokuwa baadhi ya masomo alikuwa amefaulu sana.
Aliamua kuchagua kwenda Ualimu ili baadae atajiendeleza.
Tulikubaliana kwamba tutaoana baada tu ya yeye kumaliza masomo ya chuo cha ualimu na mimi kwa muda huo nilikuwa najiandaa kwa ajili ya harusi.
Nakumbuka siku tunaagana alilia sana maana hakutaka kuwa mbali na mimi.
Nilimtia moyo na kumwambia kwamba nitakuwa namuombea kila siku na hakika tutafikia tu hatima yetu njema.

Akaanza masomo ya chuo cha ualimu na mimi nilikuwa msaada sana kwa masuala ya kipesa na maombi.
Kwa miaka miwili nilifunga zaidi ya mara 10 na muda mwingi nilimuombea sana.
Miezi ilikatika na hatimaye mwaka ukaisha kila kitu kilikuwa sawa.
Mwaka wa pili ukaanza na ambao ni wa mwisho  na hakika kwangu ilikuwa furaha kubwa na nilitamani amalize ili tufunge ndoa yetu ambayo kila tukipigiana simu tulikuwa tunaizungumzia jinsi itakavyokuwa.

Likizo ya mwisho ya mchumba wangu alikuja Zanzibar lakini niliona utofauti mkubwa.
Hakunichangamkia kama zamani, na alikuwa makini sana na mimi ili nisiguse simu yake.
Siku moja akiwa likizo kuna kitu kilimshinda kuseti ikabidi anipe nimsetie niliichukua simu hiyo na kuiseti lakini muda huo wa kama dakika 3 nilikuwa nimeikagua yote na nikagundua jina langu amelisave vibaya sana pia kulikuwa na meseji mbaya za watu wengine.
Nilimuuliza kwa upole tu akanijibu kwamba yeye ni msichana mzuri na mrembo hivyo kutongozwa kwake ni jambo la kawaida tu ila amenichagua mimi pekee katika maisha yake.
alisema kwamba anamuogopa MUNGU hivyo hawezi kunisaliti.
Kuhusu jina akasema chuoni kwao Wakufunzi ni wakali sana hivyo aliamua kulibadilisha jina ili hata wakikagua wasitambue.
Kwa sababu nilikuwa namuamini sana na tena nampenda sana nilimuona ni mkweli na hata siku moja nilijua hawezi kunisaliti.
Kwa sababu nilikuwa pia sijawahi kusalitiwa maishani mwangu basi nilimwamini zaidi.
Aliporudi chuoni maisha yaliendelea kama kawaida japokuwa akipiga simu muda mwingi alikuwa mkali tu na anayetaka hela.
Kwa sababu ya upendo wangu kwake niliona jambo la kawaida tu na niliongea maneno ya kumfurahisha na tunaishia kucheka na maisha yanasonga.
Miezi 3 kabla hajamaliza chuo kuna ndoto nilianza kuziota lakini nilidharau kwa jinsi nilivyompenda.
Kuna wakati nilimuona kwenye ulimwengu wa roho akitaka kuzini lakini ghafla nilianza kukemea na kudai kwamba hizo ni hila za shetani maana shetani siku zote hatutakii mema. kumbe ilikuwa ni kweli maana hayo yalikuja kuthibitika baadae.
Kila mara nilimuona kwenye ulimwengu wa roho akiwa na mwanaume na wakielekea gest, nilipuuzia maana nilimwamini sana na tena nilijua kwamba yeye ni kiongozi kanisani na ana msimamo mzuri wa imani.

Niliyoyaona yote kwenye ulimwengu wa roho niliyadharau kwa sababu ya kumpenda kumbe niliyoyaona hadi muda niliouona vyote vilikuwa sahihi na nilikua kuthibitisha baadae kwa kauli yake mwenyewe.
Alivyorudi tu kutoka chuoni baada ya kumaliza masomo ndicho kipindi mimi namaha Zanzibar na kuja Hapa Dar es salaam,
Wiki ile ile baada ya mimi kuhama kule alinipigia simu nimtumie nauli maana anaenda Arusha kumsalimia rafiki yake, kumbe ukweli ni kwamba alikuwa anakwenda kwa kijana ambaye walianza uhusiano wa kimapenzi miezi michache kabla ya kumaliza chuo.
Nililiona tukio hilo kwenye ndoto hivyo nikamshauri asiende kwa huyo aliyedai ni rafiki yake.
Kumwambia hivyo tu ndipo aliponiambia kwamba hanipendi na wala hajawahi kunipenda na tena aliniambia kwamba nichukulie jambo hilo kana kwamba hatukuwahi kuonana, tena nichukulie hiyo kuwa ni ajali tu imetokeo hivyo niendelee mbele na maisha yangu.
Sikuamini kauli hiyo nikampigia tena akaanza kunitukana  kisha akasafiri baada ya kutumiwa pesa na yule mtu wake mpya.
Nilimpigia simu mama yake maana uchumba wetu ulikuwa umepitia taratibu zote za kikanisa na za kifamilia.
Mama yake alimuuliza na kweli na yeye akajibiwa hivyo hivyo nilivyojibiwa mimi.
Mama yule kwa hasira akakagua mabegi ya binti yake na kukuta picha za yule kijana na vitu vingi tu vinavyoonyesha ni wapenzi wazoefu.
Mama yule alimfungia nje yule binti hadi atakapobadili uamuzi wake.
Yule binti alilala nje kwa siku kadhaa.
Yule mama aliitisha kikao cha ndugu ili wamshauri binti lakini ilishindikana.
Binafsi nilikuwa na kibali cha ajabu kwa ndugu zake na kanisani pia hivyo kila mtu alikuja kinyume chake wakati huu.
Mimi nilijaribu kumpigia simu na kumkumbusha tulikotoka na jinsi miaka 2 kabla tulivyosaini mbele za viongozi wa kanisa kwamba kila mmoja atakuwa mwaminifu kwa mwenzake, binti ndio kwanza alizidi kunitukana  na mbaya zaidi alimpa yule kijana ili anishauri maana alisema kwamba muda huo yupo kifuani pake.
Niliumia sana na hakika siku hiyo ilikuwa ni jumapili sikula chakula kwa siku 5 huku nimejifungia katika chumba peke yangu. Kulia nimeshindwa na kuomba nimeshindwa pia.
 kwa siku hizo tano maombi yangu yalikuwa ni maneno haya tu ''MUNGU wangu nisamehe, MUNGU wangu nisaidie''
Maneno hayo niliyatamka kwa siku hizo zote.
Wakati imefika siku ya 3 ya mimi kutokula bila kufunga, nilianza kuona roho ya mauti ikinifuatilia, sikuwa na jambo la kufanya ila kuendelea kusema MUNGU wangu nisamehe MUNGU wangu nisaidie.
Baadae roho ya mauti ilikuwa wazi kabisa huku nimeng'ang'ania tu.
Kumbe wakati huo mimi niko katika wakati huo mgumu kuna watumishi  ambao hata hawakujua niko katika mazingira gani ila MUNGU alisema nao kwa sauti kwamba waniombee maana naweza kufa. Watumishi hao walikuwa zanzibar na wengine hapa Dar japokuwa walikuwa hata hawanijui kwa undani maana nilikuwa mgeni kanisani.
Binti mmoja wa kanisani ambaye ni mmoja wa wale watumishi alidharau baada ya kuambiwa aniombee lakini baadae siku hiyo hiyo akitoka kumsindikiza mchungaji aligandishwa akiwa njiani na mbele yake kukawa kama Tv kubwa iliyonionyesha mimi nikiwa nakufa. Yule binti alilia na kuanza kuomba kwa kufunga siku 7 huku hata namba yangu ya simu hana.
aliitafuta na alipoipata alinipigia simu huku haamini kama mimi ni mzima.
Sikumwambia kile kilichokuwa kinaendelea japokuwa alilazimisha sana nimwambie.
BWANA YESU alimtokea na kumweleza kuhusu utumishi ambao ameuweka ndani yangu hivyo akaendelea na maombi.

Kwa upande wangu wakati nakaribia kumaliza siku 5 bila kula MUNGU alikuwa akisema na mimi mengi sana na ndio muda huo huo nilianza kuuona utumishi uliowekwa ndani yangu.
Wakati huo ndipo nilipoambiwa nitengeneze Blog ya Maisha ya ushindi na mengine.
Baada ya hapo nilirudi kwenye hali ya kawaida lakini niliaapa kulipiza kisasi kibaya tena niliaapa kutokusamehe.
Lakini Roho ndani yangu alikuwa ananionya na kunikataza kila nikiwaza kulipiza kisasi.
Siku chache baade kulikuwa na Semina ya Mwl Mwakasege Jangwani, nilienda huku moyo wangu kwa ndani kama umetoboka toboka kwa sababu ya maumivu niliyotendwa.
Yule mtumishi alinitaja japokuwa hakusema jina langu ila alizungumzia tukio langu la kutendwa na maumivu niliyoyapata na akasema kwamba '' Neno la BWANA kwako ni kwamba Samehe na usahau, maana vitu vingi kwako vimezuiliwa kwa sababu hujasamehe''
Nilisikia kitu kinagonga  huku kinatengeneza roho yangu.
Nilijua nimepona lakini kila nikikumbuka nilivyotendwa hasira kali ilikuja ndani yangu na ninasema ''hapana lazima nilipize tu''
baadae kesho yake nilipokua nafumba macho ili kuomba nilikuwa namuona nyoka kwenye ulimwengu wa roho anatembea na moyoni mwangu nasikia sauti ikiniambia shetani anataka kuleta uongo ili nibaki bila kusamehe.
Muda mwili nilikuwa naomba na baada ya miezi kadhaa nikajua kabisa nimeshasamehe maana hiyo tu ndio dhambi niliyojua inanitesa.
Siku moja nilisikia sauti ikisema ''KUSAMEHE NA KUSAHAU MAANA YAKE UNAKUWA HUUMIZWI TENA NA JAMBO ULILOTENDEWA''
Baada ya sauti hiyo hakika nilijua bado sijasamehe kabisa.
Nilianza  kuomba maombi ya kutaka nisamehewe kwa kutokusamehe kwangu.
Hapo nilianza kuona sasa nakuwa huru na kipimo cha kwamba nimesamehe ikawa pale ambapo nilipoanza kutoumia tena kama nikikumbuka nilivyotendwa.
baada ya muda hakika nilikuwa nimeshasamehe na kusahau.
ilinisumbua sana na ndio maana miezi michache baadae niliandaa somo lililoitwa KUSAMEHE NA KUSAHAU.
baada ya hapo nilipona hakika na namshukuru sana BWANA YESU kwa neema yake kwangu.
Namshukuru sana ROHO MTAKATIFU maana bila yeye ningedhani nimeshasamehe kumbe dhambi yangu bado inakaa maana nilikuwa sijasamehe.
Wakati wa hasira yangu hiyo kuna maandiko nilikuwa nayaogopa hata kuyasoma maana yalinihukumu.
Mfano ni hili andiko la Mathayo 6:14-15 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''
Niliogopa sana nilipokuwa nasoma andiko hilo na pia siku moja nilisoma ushuhuda mmoja ambao kuna mama mmoja alipelekwa kuzimu na kuona maelfu ya watu wanateseka na  alipouliza kwamba wale watu dhambi yao ni nini hata wakawa motoni japokuwa wengine walikuwa watu wa kanisa, alijibiwa kwamba hao hawakusamehe.
Niliogopa sana na kugundua kuwa kutokusamehe ni jambo baya sana.
Ndugu, nimekushuhudia ushuhuda huu sio ufurahi tu bali ujue pia kwamba kusamehe ni muhimu sana.
Kutokusamehe unaweza hata kuzuia baraka zako.
Baada ya mimi kusamehe  nilianza hata kuona matukio kuhusu yule binti kwa miaka ya baadae.
na baada ya miaka 2 haijaisha aliniambia kwamba mimi nilitakiwa kumuombea tu maana nguvu za giza ndizo zilikuwa zinamtumikisha maana alikuwa ameacha wokovu hata kama alikuwa anahudhuria kanisani.
Nilianza kuona wajibu wangu na kazi yangu duniani.
Nilianza kuona hadi mbinguni na kupata neema kubwa kutoka kwa BWANA YESU.
Asiye samehe na yeye hatasamehewa na MUNGU.
Kumbe ni heri kusamehe na kuwaombea maadui zako
Warumi 12:18-21 '' Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA.Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.''
Kusamehe ni jambo la lazima kama unauhitaji uzima wa milele.
ili usamehewa basi samehe na wewe wanaokukosea.
Mathayo 5:44 '' lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,''
Mimi nilisamehe na siku zikaenda nikaona ajali ikitaka kumwangamiza yule dada, nikaomba nikiikataa na pia nikatafuta namba yake na kumwambia asisafiri siku aliyotaka kusafiri.
Akakataa lakini baade akanipigia simu na kusema basi lao limepata ajali mbaya sana na wengi wameumia lakini yeye hata alijishangaa tu yuko nje na alikwaruzika tu kidole.
Mimi nilimshukuru tu MUNGU kwa kumponya na nikamtakia maisha mema.
Kwa sasa yeye ana maisha yake na mimi nina maisha yangu na nimeshaoa tayari na maisha ni mazuri sana ya ndoa.
Sina kinyongo nae chochote maana nimejifunza kusamehe na kusahau.
MUNGU wa mbinguni akubariki na maombi yangu ujumbe huu ukusaidie wewe kusamehe na kusahau.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Maisha ya ushindi blog
mabula 1986@gmail.com
0714252292.
Amen kwa YESU KRISTO.

Comments