KWANINI UNAJIBIZANA NA ADUI?

Na Frank P. Seth
"Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika yake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu. Jihadharini, asije Hezekia akawadanganya, akisema, BWANA atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake na mkono wa mfalme wa Ashuru? Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! Wameiokoa Samaria na mkono wangu? Katika miungu yote ya nchi hizi ni nani waliookoa nchi yao na mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu na mkono wangu? Lakini watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana ilikuwa amri ya mfalme, kwamba, Msimjibu neno." (Isaya 36: 16-21)
Haya ni maneno wa jemedari wa vikosi vya jeshi la Senakeribu, mfalme wa Ashuru akiwatishia watumishi wa mfalme Hezekia. Natazama, jeshi kubwa la Ashuru, kwa umaarufu wake na ushindi wa vita nyingi dhidi ya falme zingine, sasa wanakuja kwa "jitu" la Mungu, mfalme Hezekia, na kusema maneno yale yale aliyowatishia wafalme (watu) wengine, ili aone kwamba na Hezekia ATARUDI NYUMA na kutimiza matakwa ya ADUI kwa sababu ya AHADI za adui au VITISHO vya kuangamia.
Ndipo Hezekia akatoa amri mapema, na kusema, "Msimjibu neno"! Kumbuka, Shida ya Hawa pale Eden ilianza alipoanza KUJIBIZANA NA ADUI. Kwa taarifa tu, ADUI yetu (Ibilisi) anaitwa MWEREVU, wala si MJINGA na hata siku moja hutamshiunda kwa UJANJA/AKILI au NGUVU zako mwenyewe. Kaa KIMYA mbele za ADUI ila usikae kimya mbele za Mungu.
Angalia hapa, Hezekia aliposikia maneno haya, kwanza hakuona AMEDHARAULIWA yeye, ila Mungu wake ndiye aliyedharauliwa na kutukanwa, kwa hiyo hakupigana kwa maana kesi ni ya Mungu na sio yake! (Isaya 37:1-6). Akatuma ujumbe kwa nabii Isaya (watumishi wa Mungu) ili waombe pia (kutafuta msaada wa kiroho).
"Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA" (Isaya 37:14).
Kwa muda huu wote, ADUI hakujau kwamba UKIMYA wa Hezekia, na watumishai wake kugoma kujibu neno, sio ishara ya KUOGOPA au KUSHINDWA, ila IMANI kwa Mungu wao awezaye kuwatetea kwa upesi.
Tazama tena jambo hili, mfalme wa Ashuru alijua kwamba Hezekia akishuka Misri kutafuta msaada kwa Farao, bado hatashinda vita, na siri hii anaitaja masikioni pa watumishi wa Hezekia (Isaya 36:6). Kumbe, Hezekia alijua siri hii mapema na wala hakutelemkia Misri kupata msaada, ila aligeuza uso wake kwa Bwana. Mara nyingi tunashindwa kwa sababu tumemweka Mungu nafasi ya pili, yaani tukishindwa njia ZINGINE ndio tunamwita Bwana!
Kwa sababu Hezekia HAKUJIBIZANA na adui, na alimwita Mungu wake na kumtegemea, safari hii BWANA hakuagiza majeshi yabebayo upanga (majeshi ya wanadamu), ila alienda kupigana kwa namna ambayo adui atajua kwamba ni Bwana amefanya.
"Basi malaika wa BWANA alitoka, akaua watu mia na themanini na tano elfu katika kituo cha Waashuri, na watu walipoamka asubuhi na mapema, kumbe, hao walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu, mfalme wa Ashuru akaenda zake, akarudi Ninawi, akakaa huko. Ikawa alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza, wanawe, wakampiga kwa upanga; wakakimbilia nchi ya Ararati; naye Esar-hadoni, mwanawe, akamiliki badala yake" (Isaya 35:36-38).
Angalia tabia hii ya Mungu, yeye ni SHAHIDI MWEPESI. "Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema BWANA wa majeshi. Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo" (Malaki 3:5-6).
Frank P. Seth

Comments