Na Mchungaji ADRIANO MAKAZI, UFUFUO NA UZIMA |
Biblia imeongelea kiundani habari ya udhaifu
Mwanzo 41: 19 "Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu.Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono."
Mathayo 4: 23 "Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu."
Injili ya Ufalme aliyokuwa anahubiri Yesu, ilikuwa ni injili ya kuponya Magonjwa na Udhaifu wa kila namna. Bwna Yesu kabla hajaenda msalabani alikuwa akizunguka kwenye kila kijiji akiponya magonjwa na udhaifu wa kila aina kwa watu.
Mathayo 8: 16 :Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.:
Udhaifu wako ukiondolewa neno la Mungu linakuwa limetimia, hata wewe udhaifu wako na hali ya ugonjwa ulionao ukiondoka linakuwa limetimia Neno lake.
"Katika jina la Yesu yeye mwenyewe aliuchukua udhaifu wangu na kuchukua ugonjwa wangu kwa jina la Yesu, naamuru magonjwa na udhaifu ulionipata viondoke kwa jina la Yesu" {unapokuwa unatamka maneno hayo inakuwa vilevile}
Mathayo 9: 35 "Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina."
Mathayo 10: 1 "Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina."
kuna baadhi ya watu wanafikiri Yesu hawezi kuponya magonjwa yote bali anaponya baadhi tu kitu ambacho sio kweli, lakini Biblia inatuonyesha yeye mwenyewe aliwaita wanafunzi wake {marko 16:17}. Wanafunzi wa Yesu ni wale watu walio mwamini na kumpokea ndio wenye uwezo wa kufanya zile kazi alizokuwa amezifanya.
Udhaifu na magonjwa yanayowapata watu ni pepo wabaya ndio wanaowaingia watu na kuwasababishia magonjwa na udhaifu kwenye maisha yao.
Luka 13:10- 10 "Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako."
Hapa tumemwona mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo wa udhaifu aliyempindisha mgongo wake kwa muda wa miaka 18 lakini aliponywa na Bwana Yesu. Maana yake inawezekana kuna mtu alimtuma pepo huyo amwingie na kuupindisha mgongo wake akose uhuru wa kufanya shughuli za kawaida kwenye maisha yake. kuna wengine wanatumiwa pepo wa uvimbe kwenye miili yao na wakienda hospitalini wanapewa sababu ya kula vyakula vya siku hizi, anakuwa anapewa sababu za kutokumvunja moyo ili aone ni tatizo la kawaida tu kumbe kuna pepo wa udhaifu ameingia ndani yake. Lakini udhaifu huo unafunguliwa kwa jina la Yesu.
Inawezekana umetembea makanisa mbalimbali, umetembea sehemu mbalimbali lakini shida yako ipo palepale kumbe kuna mtu yupo sehemu ana madhabahu ambayo huwa anaingia ili kutuma mapepo na majini yaje kukuzidishia udhaifu kwenye ndoa yako au biashara yako au sehemu yoyote katika maisha yako.
Yupo Bwana Yesu ambaye alishatupa ushindi kwa kuchukua udhaifu wetu na magonjwa yetu. unatakiwa usimame ili mahali popote ambapo umeshikiliwa pabomoke kwa damu ya Yesu kristo.
Ukiri:
"Katika jina la Yesu ninabomoa madhabahu ya udhaifu kwenye maisha yangu kwa jina la Yesu"
Inawezekana huna mwelekeo kwenye maisha yako umefika mahali fulani huelewi ufanyeje, Yupo Mungu mwenye nguvu ambaye anakuonyesha njia ya kuiendea na kukutoa kwenye hali uliyo nayo kwa jina la Yesu.
Usifikirie pale ulipofikia ndipo hatima ya maisha yako, Hapana Mungu ameapa anataka akupeleke mahali unapotakiwa kufika, usiridhike na hapo ulipofika bado unayosafari ya kuiendea. Yawezekana kuna nguvu umeikosa ya kutoka na kwenda mahali unapotakiwa kwenda, maandiko yanasema mtapokea nguvu atakapowajia Roho wa Bwana na sasahivi Mungu amekupa nguvu ya kwenda kwenye kusudi lako kama alivyompa Musa nguvu ya kuanza na kumaliza usiogope na hali uliyowekewa sababu hiyo hali uliyo nayo umevishwa.
Biblia inasema usiogope kwa mambo yanayokupata maana shetani atazuiliwa siku kumi, wachawi wanayo njia ya kumwingiza mtu mautini lakini Bwana Yesu anayo njia ya kukutoa toka mautini, pale alipopigwa msalabani aliifungua njia ya kutoka kwenye laana, magonjwa, taabu na dhiki kwenye maisha yetu.
Siku moja Yesu alipokuwa anaingia Yerusalem aliona jinsi watu walivyotiwa upofu wasijue mambo yajayo yatakayowapata, kwenye maisha watu wengi wametiwa upofu wasiyajue mambo yawapasayo, yupo mungu wa dunia hii [ibilisi] ambaye amewapofusha watu wasiamini wafu wanafufuka, wasiamini kwamba watu wanaibiwa kwenye vifo vya utata na baadhi ya watu wawatumia kwenye kujitajirisha kwenye biashara zao kwa kutumia watu wengine.
Mungu ni mwenye haki amempa kila mtu kitu chake lakini shetani ni mwizi hawezi kuumba chake, yeye amejipanga kuiba kile mtu alichopewa au amejipanga kukizuia au kukitumia kwa mapenzi yake mwenyewe, hivyo unatakiwa upigane mpaka ule udhaifu wako uondoke, pigana mpaka upate kila unachotaka kitokee kwenye maisha yako kwa jina la Yesu.
Mtume Paulo alimwona Bwana Yesu kwenye maono na ndiye nabii aliyefanikiwa kuandika vitabu vingi kwenye agano jipya kuliko wale mitume kumi na wawili kwasababu alijua haijalishi kuwa karibu na kuhani mkuu bali alijua ni lazima kupigana ili kufanikiwa kwenye Ufalme wa Mungu. Kama umechoka na mazingira yalyokuzunguka lazima uamue kupigana kwa jina la Yesu, kwa maana hakuna kushinda bila kupigana.
"Kwa jina la Yesu leo natoka kwenye mioyo ya kuzimu iliyonishkilia muda mrefu kwa jina la Yesu"
Mwanzo 12: 7 "Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea."
Mwanzo 8: 20 "Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu."
Mungu alisikia harufu nzuri ya kumridhisha alipojengewa madhabahu na Nuhu na akaahirisha adhabu ya kupiga nchi kwasababu moyoni mwa mwanadamu kuna mawazo mazuri.
Kutoka 17: 15 "Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yehova-nisi; akasema, Bwana ameapa; Bwana atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi."
Wewe ni mdhaifu kwasababu kuna mtu mahali amejenga madhabahu na kuitolea kafara kwaajili ya kukuzidishia udhaifu wako.
Mhubiri 9: 11 "Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote."
Wagalatia 4: 4 "Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria"
kwa mpambanaji yeyote lazima uangalie kwamba si wenye mbio washindao katika michezo wala si walio hodari washindao vitani, Jina la Bwana ndilo linalowaokoa watu kwa jina la Yesu na Saa ikiwadia lazima upate kile unachotakiwa kukipata na udhaifu wako unaondoka wote kwa jina la Yesu.
Kwenye maisha ya kila siku utakuta Baba mzazi kwenye maisha yake ya ndoa kuna mgogoro wa ndoa na ukirudi nyuma kidogo utaona kuna mgogoro huohuo ulimptaka babu yako, maana yake ni kwamba kuna mahali imejengwa madhabahu juu ya ukoo huo ili kizazi baada ya kizazi wawe na tatizo la ndoa linalofanana. leo hii kataa jambo kama hilo kwenye kwenye maisha yako kwa jina la Yesu.
Zipo madhabahu za aina nyingi zinazo simamiwa na watu ili kurutubisha uovu na lipo tumaini la Mungu ambalo kwa hilo tumeshinda na zaidi ya kushinda na Bwana ameapa kwamba atakuwa na vita na amaleki kizazi baada ya kizazi.
Tumeona Musa amejenga madhabahu na akaiita Jehova - nisi, maana yake kila madhabahu ina jina ambalo linabeba kazi inayofanyika kwenye madhabahu hiyo. Zipo madhabahu duniani zimejengwa ambazo zinafuatilia mtu na mtu, kizazi na kizazi, ukoo kwa ukoo ili kuweka udhaifu na magonjwa vifuatane nao lakini Mungu ameamua kutuonyesha uwezo tulio nao wa kuzivunja madhabahu hizo kwa damu ya Yesu.
Kutoka34: 13 "Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao. Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu. Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake."
Mungu anawaambia wana wa Israeli washughulike na madhabahu na ukimwona mtu hazai inamaana kuna mahali kuna madhabahu iliyojengwa ili mtu huyo asizae na ili mtu huyo aweze kuzaa inabidi ashughulike na madhabahu iliyomsababisha asizae.
Mungu alipotaka amtoe Gideoni kwenye utumwa, alimtaka aitoe madhabahu iliyomshkilia mpaka asiende, na madhabahu hiyo ilikuwa iko kwenye familia yake na ilimbidi aibomoe kwanza ndipo aweze kutoka. Gideoni alikuwa anamwomba Bwana lakini alikuwa anatukanwa, anabezwa, anadhihaakiwa, anadharauliwa na alikuwa anaonekana si kitu kwasababu ya Madhabahu iliyomshikilia.
Inawezekana umeshindwa kusoma kwasababu umekosa ada ya kukusomesha lakini hiyo sio sababu, kuna madhabahu iliyokushikilia ili usimalize elimu uliyo nayo, unaweza ukawa hupendi kusoma kwasababu si wewe unayekataa bali kuna madhabahu iliyojengwa ili usifike pale unapotakiwa kufika, lazima uibomoe madhabahu hiyo ili uende mbele kwa jina la Yesu.
Madhabahu inakuwa imejengwa na kuweka kikomo kwenye maisha ya mtu iwe ni kwenye elimu asimalize kidato cha nne, iwe kwenye biashara asipate zaidi ya sh elfu hamsini, iwe kwenye ndoa aoe/kuolewa na kuachika, iwe ni kwenye kazi afukuzwe kazi au asipate kazi. Kuna madhabahu zipo zimewashikilia watu wasifanikiwe kwenye maisha yao na wapo watu wanaozitolea kafara madhabahu hizo il zitavunjika kwa jina la Yesu.
Kila mtu amepewa eneo lake la utawala na Mungu, shetani na wakala wake wanapoona hivyo wanaingilia na kutengeneza madhabahu za kichawi ili kuwazuilia watu wasitawale kwenye maeneo yao. Wachawi hutumia madhabahu ili kuwazuia wasifanikiwe. kuna watu wengine wametumiwa mashetani ili wagombane na watu wao wa muhimu mfano watumishi wa Mungu bila kufahamu. Mashetani hayo yanatu,wa kuwaingia watu na kuwagombanisha na watu wao wa muhimu ili wakose mambo yake wanayotakiwa wapate.
Zipo kafara za damu ambazo hutolewa ili zirutubishe udhaifu ulionao lakini Bwana Yesu ametupa ushindi na mamlaka ya kuzibomoa madhabahu hizo. Damu hizo huongea na leo zitanyamazishwa kwa damu ya Yesu kristo.
Waebrania12: 24 "na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili."
Damu ya Yesu ndio damu pekee inayonena mema na inayoweza kunyamazisha damu zote zilizomwagwa juu ya madhabahu za udhaifu. Na leo tumia damu ya Yesu kuzinyamazisha damu zote za kafara zilazokuletea udhaifu ili uwe huru kutoka katika jina la Yesu kristo Amen.
Comments