KUISIKIA, KUITII NA KUITUNZA SAUTI YA MUNGU.

Na Mtumishi Peter Mabula

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tena karibu sana tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.

Kumb 4:35-36 ''Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa BWANA ndiye MUNGU, hapana mwingine ila yeye. Kutoka mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake toka kati ya moto.''

MUNGU alisema na watu wa Israeli kama ambavyo pia anaweza kusema na wewe leo.
Sauti ya MUNGU waliisikia kama ambavyo leo MUNGU anaweza kusema na wewe kwa sauti yake na wewe ukaisikia.

Licha ya MUNGU kusema na watu lakini sio wote huitii sauti ya MUNGU na sio wote huitunza sauti ya MUNGU.
Sauti ya MUNGU huendana na Neno lake MUNGU yaani Biblia. 
Kwa sababu Biblia ni ya MUNGU, MUNGU anaposema na sisi haendi kinyume na Neno lake Biblia.
Siku moja watu waliisikia sauti ya MUNGU ikimthibitisha Mwokozi wa ulimwengu, YESU KRISTO.

Marko 1:11 '' na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.'

Ni kweli MUNGU husema na watu wake lakini Lakini nataka uelewe mambo haya muhimu kwamba.
Kuna tofauti kati ya kuisikia sauti ya MUNGU, Kuitii sauti ya MUNGU pamoja na kuitunza sauti ya MUNGU.
=Kuna watu huwa wanaisikia sauti ya MUNGU ila hawaitii.
=Kuna watu huisikia sauti ya MUNGU na kuitii kwa muda kisha wanasahau.
=Kuna watu huisikia sauti ya MUNGU kisha wanaitii na kisha wanaitunza.
Hao kundi la mwisho hufanya vyema sana


Luka 9:35 ''Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.''

Sauti ya MUNGU ilisikika kwa wanadamu kwamba MUNGU anataka wanadamu wote wamsikie YESU KRISTO, Wamtii na washike kile anachokiagiza.
Sauti ile ya MUNGU hata leo iko wazi sana kwa kila mtu anayesoma Biblia.

Je wewe licha ya kuisikia sauti ya MUNGU.
Je unaitii sauti ya MUNGU?
Je unaitunza sauti ya MUNGU ili hata ushawishi mbaya ukija kwako sauti ya MUNGU uikumbuke na kukataa ubaya huo?

Waebrania 3:12-15 ''Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na MUNGU aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa KRISTO, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho; hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha.''

Ni muhimu sana kuitunza sauti ya MUNGU.
MUNGU husema na wewe kwa njia nyingi sana.
Alivyosema MUNGU jana inaweza kuwa tofauti kabisa na atakavyosema leo.
Kama ulikariri MUNGU aseme na wewe kwa ndoto kama alivyosema na wewe jana, leo MUNGU anaweza kabisa akasema na wewe kwa njia ya Neno lake wala sio ndoto kama ulivyokariri.


Isaya 40:28 ''Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye MUNGU wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.''

Akili za MUNGU hazichunguziki hivyo anaweza kutumia njia nyingi tu ili wewe uisikie sauti yake.
Lengo la MUNGU kusema na wewe ni ili utii kile cha MUNGU na sio kile cha wanadamu.


MUNGU anaposema na wewe jambo fulani na kukuhakikisha kwamba hilo utalipata, haina maana kwamba vikwazo na changamoto havitakuwepo, bali vitakuwepo lakini Kwa sababu MUNGU alisema na wewe, na wewe hujaondoka katika agano hilo la MUNGU basi hakika jambo hilo utalipata.
Changamoto unazokutana nazo ni kuhakikisha tu huitunzi sauti ya MUNGU, Lakini mpendwa nakuomba sana usonge mbele huku ukiitunza sauti ya MUNGU.

MUNGU alisema na Musa juu ya mipango yake MUNGU ya kuwatoa waisraeli Misri.
Musa aliitunza sauti ya MUNGU japokuwa Farao aliita wachawi wote wa Misri wamkwamishe Musa. Lakini Musa aliitunza sauti ya MUNGU na akashinda



Wako watu MUNGU alisema nao.
Kwa miaka kadhaa waliitunza ile sauti ya MUNGU.
Waliitii sauti ya MUNGU na hawakwenda kinyume na Wokovu wa KRISTO.
Baadae waliiacha ile sauti ya MUNGU hata hawakuitunza na mwisho wao ukawa mbaya hata kama mwanzo walisimama katika kweli.




Yakobo 4:7-8 ''Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.''

Ndugu, Ni muhimu sana kuitunza sauti ya MUNGU na kuitii siku zote.


 MUNGU wakati mwingine hutushirikisha mipango yake.
Mfano anaweza kukuambia kuwa anataka kumuokoa kijana fulani au binti fulani.
Kwa sababu MUNGU amekushirikisha wewe basi unatakiwa wewe ukamhubiri yule kaka au dada uliyemuona ambaye MUNGU anataka kumuokoa. 

Sababu za MUNGU kumuokoa ndugu huyo anazijua MUNGU na sio wewe.

 Mara nyingi sana MUNGU husema na wewe kupitia Neno lake mfano kama unavyojifunza ujumbe huu.
MUNGU anaposema na wewe kwa Neno lake ni muhimu kumtii MUNGU na Neno lake.
Neno la MUNGU ni la MUNGU tu.
Neno la MUNGU linajua Yote.
KRISTO ni Neno juu ya Neno la MUNGU.
MUNGU anatutakasa kwa Neno.

Ukweli Ni Kwamba Kila Agizo Analotoa MUNGU Ni Agizo Halali Siku Zote.
 Jitahidi Sana Kuipenda, Kuishika Na Kuitii Sauti Ya BWANA Na Sio Sauti Za Wanadamu.
Uhakika wetu uko katika Neno la MUNGU hivyo MUNGU anaposema na wewe kwa njia ya Neno haijalishi ni kupitia nani basi tii Neno la MUNGU maana Neno la MUNGU siku zote hutuelekeza kwenye Mema tu aliyotuandalia BWANA YESU.

2 Timotheo 2:15 ''Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.'' 

 Japokuwa wakati mwingine adui huleta sauti zake ili kuwapoteza watu wa MUNGU, Lakini kama ROHO MTAKATIFU yumo ndani ya mteule huyo hakika janja ya shetani itajulikana.
Ni Muhimu kujua kwamba Kuna Sauti Takatifu Na Kuna Sauti Isiyo Takatifu Hata Kama Kibinadamu Hiyo Sauti Isiyo Takatifu Kwa Baadhi Ya Watu Itaonekana Takatifu. shetani hujaribu kuiga utakatifu lakini kwa sababu ROHO MTAKATIFU yuko kwetu hakika lazima tutazijua hila za shetani.

2 Kor 2:11 '' Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.''

 Shetani naye hutuma mawakala wake ili kuwapotosha watu wa MUNGU lakini tunayo mamlaka kuu ya jina la YESU KRISTO na kwa hiyo mamlaka tunashinda hila za shetani.
Kuna Sauti Ya Kumtoa Nyoka Pangoni Na Kuna Sauti Ya Kumuua Nyoka Huko Huko Pangoni. Sauti Ya Kumtoa Nyoka Pangoni Ni Sauti Ya Watambikaji, Wasihiri, Waganga Na Wachawi Ikiambatana Na Udi Na Ubani Lakini Sauti Inayomuua Nyoka Pangoni Ni Sauti Ya Maombi Katika Jina La YESU KRISTO Ikiambatana Na Damu Ya YESU KRISTO. 
Heri Kumuua Nyoka Kuliko Kumtoa Pangoni. 
Nyoka Ni Majini, Vibwengo, Mapepo, Mizimu Na roho Za shetani Zote. 
Haribu Nyoka Na Sio Kumcheka Nyoka, Omba Na Utashinda Kwa Jina La YESU KRISTO.

Warumi 16:20 '' Naye MUNGU wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya BWANA wetu YESU KRISTO na iwe pamoja nanyi. [Amina.]   ''

 Sijui Kama Unaijua Hii, Lakini Kama Uijui Ni Kwamba; Kwa Baadhi Ya Mambo MUNGU Akikuambia Jambo Usilitekeleze Hakuambii Jambo Jipya Mpaka Utakapolifanyia Kazi Lile Alilokuambia Mwanzo.
Binafsi Huwa Najitahidi Sana Kufanyia Kazi Kile Anachoniambia BWANA Ili Nipate Nafasi Ya Kuambiwa Kingine. 
Mfano Ni Huu, Kuna Watu MUNGU Aliwaambia Watubu Wao Wakopotezea, Lakini Kwa Sana Wanahitaji Mke/mume Mwema Na Kila Siku Wanatamani MUNGU Aseme Nao Juu Ya Hilo Lakini Mbingu Ziko Kimya Hadi Watakapofanyia Kazi Lile MUNGU Aliwaambia Mwanzo.
 Sauti ya MUNGU ikiondoka kwa mtu huwa hairudishwi kwa namna yeyote isipokuwa kwa kutubu toba ya kweli.
MUNGU hurudi baada ya toba ya kweli.
Toba ya Kweli pekee ndio ndio inayoweza kuirudisha sauti ya MUNGU katika maisha ya mtu.

Kumb 28:1-7 '' Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, MUNGU wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, MUNGU wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, MUNGU wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.  Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. '

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments