UNAZIFANYIA NINI SIKU ZAKO ZA KUISHI DUNIANI?

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Tuko leo duniani Kwa kusudi maalumu la MUNGU.
Tuko leo duniani Kwa sababu maalumu ya Muumbaji.
Tuko Leo duniani Kwa mpango maalumu Wa MUNGU.
Tuko Leo duniani Kwa kipindi maalumu.
Tuko Leo duniani Kwa muda maalumu.
Muda maalumu ukiisha kila mmoja ataondoka.

Mhubiri 3:1-2 ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; ''

Kila jambo hakika lina wakati wake.

Muda wa kuishi mwanadamu ni mfupi sana ukilinganisha na milele ijayo.
Milele ijayo ina makazi ya aina mbili; 
kuna makazi ya watakatifu yaitwayo uzima wa milele na kuna makazi ya watenda dhambi waliokataa kuokoka wangali wakiishi duniani, makazi yao hao yanaitwa jehanamu ya moto kwenye mateso ya milele.
Wakati huu mwanadamu anaishi duniani ndio wakati wa kuamua ni wapi atakuwa milele ijayo.
Siku za kuishi duniani za mwanadamu ni chache sana na hizo chake mwanadamu anatakiwa azitumie katika kumcha Muumba wake na kuishi maisha ya wokovu ulio pekee katika KRISTO YESU.

Miaka yako michache ya kuishi duniani unaitumiaje?

 Ayubu 14:1-2 ''Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.''

Biblia inathibitisha kwamba miaka ya mwanadamu kuishi duniani ni michache sana ukilinganisha na miaka isiyohesabika ya milele ijayo.
Katika miaka hii michache ya mwanadamu kuishi MUNGU kwa upendo wake mkuu akaamua kuleta Wokovu kwa wanadamu.
Wokovu ni mpango wa MUNGU kumuokoa mwanadamu. Na Mpango huo wa MUNGU kumuokoa mwanadamu uko pekee katika KRISTO YESU, BWANA na Mwokozi wa watu wote watakaomtii.

1 Yohana 4:14-15 ''Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa BABA amemtuma MWANA kuwa MWOKOZI WA ULIMWENGU. Kila akiriye ya kuwa YESU ni Mwana wa MUNGU, MUNGU hukaa ndani yake, naye ndani ya MUNGU.''

Mpango maalumu ni kila mmoja aokoke na aishi maisha matakatifu.
Anayeokoa ni BWANA YESU na yeye siku zote anawangoja wanaompokea na kulitii Neno lake ili awape uzima wa milele.

BWANA YESU analithibitisha hilo kwa kinywa chake akisema; 

''Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.-Yohana 10:28-30''

 Kwa maandiko hayo ukweli ni kwamba hakuna mwanadamu hata mmoja anayedai yeye yuko upande wa MUNGU wakati anakataa kuokolewa na YESU KRISTO.
=Hakuna mwanadamu hata mmoja ambaye atasema yeye ana MUNGU wakati huo huo yeye hataki kuokolewa na YESU KRISTO.
=Ukweli ni kwamba kila mwanadamu anayeutaka uzima wa milele ni lazima awe chini ya YESU KRISTO.
=YESU KRISTO na MUNGU BABA ni umoja tena ni mmoja, mipango yao ni mimoja kama andiko hapo juu linavyosema. 
Na kwa Biblia ya kingeleza andiko hilo la  Yohana 10:30 imeandikwa hivi '' I and my Father are one.'' 
=Hivyo hakuna mwanadamu aliye upande wa YESU KRISTO harafu tena eti huyo mwanadamu asiwe upande wa MUNGU.
=Hakuna mwanadamu aliye upande wa MUNGU kama mwanadamu huyo hayuko upande wa YESU KRISTO.
Mwanadamu asiye upande wa YESU KRISTO huyo mwanadamu anakuwa pia hayuko upande wa MUNGU na kama hayuko upande wa MUNGU moja kwa moja mwanadamu huyo anakuwa hahusiki na uzima wa milele.

Yohana 3:16-18 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU  aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

Ni Muhimu sana kumuamini YESU KRISTO, kumpokea na kuliishi neno lake.
Najua kuna maelfu ya watu wameshampokea BWANA YESU na wanaishi maisha matakatifu, na najua pia kuwa kuna watu bado hawajaokoka lakini kupitia ujumbe huu ambao ROHO wa MUNGU amenipa basi wataokoka, maana miaka inaenda na muda wa kuishi mwanadamu ni mchache sana ukilinganisha na milele ijayo.

Ndugu zangu,Kwa jinsi kila tunavyoiona siku mpya ndivyo pia muda maalumu Wa kukaa duniani unaendelea kuisha.
Kabla muda wa kukaa duniani haujaisha ni muhimu sana kila mwanadamu kuokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Kabla ya muda wa kuishi duniani haujaishi  Ni muhimu sana kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli.
Kanisani Hatuhitaji Uzoefu Bali Utakatifu. 
Uzoefu Wetu Wa Ibada Na Miaka Yetu Mingi Ya Kuwa Washirika Wa Kanisa Havina Maana Hata Moja Kama Hatuishi Maisha Matakatifu.
Ndugu yangu, ishi maisha matakatifu maana hilo ndilo kusudi la MUNGU kwa mtu baada ya mtu huyo kumpokea YESU KRISTO kama BWANA na Mwokozi wake.

Tunayo neema ya MUNGU BABA maana Hatuishi duniani Kwa bahati mbaya Bali tunaishi Kwa sababu ni haki yetu kuishi aliyotupa JEHOVAH MUNGU muumba wetu. 
Katika hiyo haki yetu ya kuwa hai sasa, MUNGU anataka tuitumie hiyo haki yetu katika utakatifu na kumtumikia.

shetani naye kwa sababu anaujua uzuri wa mbinguni kwa sababu aliwahi kuishi huko kabla ya kufukuzwa, basi huyo hujaribu kuwafanya wanadamu wasiende huko uzima wa milele.
shetani amepanda vitu vingi kwa siri ili tu kuwafanya wanadamu wamuasi Muumba wao.
shetani ameleta dini nyingi ili tu kuwavuruga wanadamu ili wasiokoke.
Hata walimu wengi wa uongo shetani amewaleta ili tu kuwafanya wanadamu wasimpokee YESU hata wakaokoka.

Kuna siri zingine shetani hataki watu wengi wajue ndio maana analeta vita kubwa mno ili watu wasifundishwe kweli ya MUNGU. Lakini habari njema ni kwamba jina YESU KRISTO ni ngome imara, tukikimbilia tunakaa salama.

Mithali 18:10 ''Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.''

Katika JEHOVAH linapatikana jina la YESU KRISTO.
Katika jina la YESU KRISTO kunapatikana ushindi na mamlaka kuu ya kuangamiza hila zote za shetani.

Waliompokea YESU KRISTO hao wamefanya agano na MUNGU BABA. 
Agano hilo ni mapatano matakatifu ambayo mwanadamu anatakiwa ayazingatie ili baada ya muda wake wa kuishi duniani kuisha aende uzimani.

 Masharti Mawili Ya Agano Kati Mwanadamu  Na MUNGU Ni 
(1)Kutii Sauti Ya MUNGU
(2)Kushika Agano La MUNGU.

=Kutii sauti ya MUNGU ni kumpokea YESU KRISTOna kuanza kuishi maisha matakatifu.
=Kushika agano la MUNGU ni  kuifuata Biblia kile  inachofundisha na kukiishi, pia kushika agano la MUNGU ni kuyazingatia maungano ya ukiri wako wa kumpokea YESU. Yaani sala ya toba ile uliyoongozwa  ni ungamo ambalo unatakiwa ulishike siku zote.

Ndugu yangu naomba pia ujue kwamba  Kusudi La MUNGU Huonekana Mwishoni Na Sio Mwanzoni.
Asichokizungumza MUNGU Huwa Hakitendi.
Na Alichokizungumza MUNGU kwamba atakitenda hakika hutenda.
 Tunamwita MUNGU Ni Mwaminifu Kwa Sababu Alilosema Hulitimiza.
MUNGU alisema watakaompokea YESU KRISTO na kuishi maisha matakatifu  wataurithi uzima wa milele. Hicho MUNGU alikisema na atakitimiza.

 Ukiokoka ni muhimu pia kumtimikia MUNGU.
Mtumikie MUNGU kwa kila kitu chako iwe ni sauti yako au mali yako.
 MUNGU Anafanya Kazi Na Wanaompenda, Sio Waliookoka Bali Waliookoka Na Wanampenda.
Waliookoka na kumpenda MUNGU hao MUNGU hufanya kazi nao, huwatumia katika matendo makuu na baraka kuu.

Warumi 8:28 '' Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote MUNGU hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. ''


Ndugu Mpendwa, jambo jingine muhimu kujua ni kwamba Kuna Vitu Hutakiwi Kufanya Haraka Kama Tu Vitu Hivyo Una-share Na MUNGU. 
Maana MUNGU Ana taratibu Zake Za Kukufanikisha Wewe Katika Baraka Hizo Njema. 
Mfano;
 Kama Umeomba MUNGU Akufanikishe Kupata Mchumba Sahihi Kwanini Uwe Na Haraka Kana Kwamba Jambo Hilo Unaliamua Wewe Peke Yako? 
Ndugu, Kama Umemshirikisha MUNGU Basi Husika Na MUNGU Zaidi Kabla Ya Mengine.
Husika Na MUNGU Kwa Maombi.
BWANA YESU anasema;
''  Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya MWANA. -Yohana 14:13''

 Jambo jingine nataka ufahamu ni kwamba Kuna Neno la MUNGU na kuna neno la shetani.
Neno la MUNGU ni Uzima tena ni uhai lakini wanadamu wengi hupenda zaidi neno la shetani kuliko Neno la MUNGU.
ni wakati wa kujitafakari sana kila Mtu.


je unalitendea kazi Neno la nani?

Neno la MUNGU ni Biblia na hilo Neno la MUNGU ndilo unalotakiwa kulitendea kazi.
Neno la shetani ni kila kitu kinachopingana na Biblia kiwe ni kitabu au ni maneno ya watu wanayoyatamka kwako.

2 Yohana 1:9-11 ''Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana BABA na MWANA pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu. Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu. '' 

 Jambo la jingine nataka ufahamu ni kwamba Kuna KRISTO na kuna mpingakristo.
KRISTO kazi yake ni kupeleka wanadamu Uzima wa milele.
mpingakristo kazi yake ni kupeleka wanadamu jehanamu.


 2 Yohana 1:7-8 '' Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa YESU KRISTO yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu.''

Naamini kabisa kuna kitu umejifunza, lakini lengo la kwanza la MUNGU ni wewe uokoke. Kama unaishi maisha ya dhambi ndugu nakuomba tubu na okoka.
Kama hujampokea YESU nakuomba umpokee leo na uanze kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya wokovu.
Kama wewe ni mtu wa kanisani lakini maisha yako yamejaa dhambi nakuomba okoka upya na amua kumpendeza MUNGU kuanzia leo.
Kama wewe umegeuza kanisa kama kichaka chako cha kuficha uovu wako , nakusihi sana umche MUNGU maana kuna ziwa la moto kwa waovu, lakini pia kuna uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.
MUNGU wangu akubariki sana na akupe
ufahamu wa kumjua yeye na Neno lake, akupe
ufahamu wa kuliishi kusudi lake jema kwako.
ubarikiwe sana pia kwa kujifunza masomo
yangu.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

 

Comments