HASARA ZA KUFANYA NGONO KABLA YA NDOA.


Mwl. Patrick Samson Sanga
 Andiko la Msingi ni Mithali 5:1-20
"Mungu ndiye aliyewaumba mtu mume na mtu mke, akawaweka bustanini ili wamtumikie. Mungu akamuumba mwanadamu na kumpa viungo mbalimbali katika mwili. Akawapa wanadamu maungo maalumu kwa ajili ya tendo la ndoa na kisha akaliweka tendo la ndoa kuwa takatifu, tena la halali kwa wanandoa tu, tena hasa wale waliounganishwa na yeye."
Sasa katika kizazi cha leo tunaona watu wengi hasa vijana ambao bado hawajaoana (kwa maana ya kuwa wanandoa) vijana hao wanafanya tendo hilo la ndoa (ngono) tena kwa uchafu usio wa kawaida, wanafanya kwa kuzidi mipaka ambayo Mungu amempa mwanadamu, maana yake wanatumia isivyo (mis-use) maumbile/ maungo ambayo Mungu amewapa.
Soma warumi 1:24-27. Sasa wao wanapofanya haya hawajui kwamba kuna hasara kubwa wanayoipata na wao wanafikiri ndio wanakwenda na dunia. Lengo la ujumbe huu ni kukueleza hasara za kufanya tendo la ndoa kabla ya ndoa nazo ni;
(1)Ni dhambi
Kufanya ngono kabla ya ndoa ni dhambi na warumi 6:23a inasema mshahara wa dhambi ni mauti; na pia katika Ezekiel anasema Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa, hivyo kwa sababu hiyo hicho kitendo kitakusababishia kifo cha kimwili na kisha utahukumiwa tu na mwisho kutupwa jehnamu.
(2)Kuwashibisha wengine nguvu zako
Mithali 5:10 Tendo la ndoa ni tendo linalohitaji mtu atumie nguvu, hivyo kadri mtu (hasa mwanume) anapofanya  mara kwa mara anajipotezea nguvu zake anawashibisha wengine nguvu zake na hivyo dhoruba itamkuta katika ndoa yake pindi atakapooa kwa sababu hatakua na nguvu tena kama awali.
(3)Utavunjiwa heshima
Mithali 5:7, Siku zote yule unayefanya naye tendo la ndoa kwanza atakuona wewe ni mpumpavu kwa sababu anajua afanyaye tendo hilo hana akili kabisa (mithali 6:32) kwa hivyo atakudharau, zaidi atakutangaza kwa wengine na wewe mwenyewe pindi utapooa au kuolewa kwa kuwa nguvu zako uliwashibisha wengine basi utavunjiwa heshima na huyo mwenzi wako.
(4)Unafanya jambo litakaloiangamiza nafsi yako
Mithali 6:32. Nafsi kwa kiyunani inaitwa Psuche, ndani yake kuna hisia, akili na maamuzi ya mtu. Hivyo kuiangamiza nafsi yako ni kuangamiza future yako na mipango yako uliyokuwa umejiwekea ya mbele.
(5)Unajitengenezea majeraha na fedheha maishani
 Mithali 6:33. Sikiliza katika ngono unaweza ukapata kilema cha maisha, na magonjwa ya hatari kama vile kaswende, ukimwi n.k. Haya magonjwa yatapelekea nyama na mwili wako kuangamia utashindwa kufikia malengo uliyojipagia, utabakia kujuta tu na watu watakufanyia fedheha na wakati huo upo kitandani hujiwezi.
(6)Kuwapa wengine miaka yako
  Mithali 5:9 , Uchunguzi chunguzi unaonyesha kwa mtu anayependelea kufanya ngono mara kwa mara hasa anapoanza kabla ya ndoa mara nyingi hawezi kuishi kwa muda mrefu si hivyo tu lakini pia tumeona mara nyingi vijana wakijiua/wakiuana /wakifa kwa ajili ya mapenzi, wengine wanaugua hadi wanakufa wadogo na kupatwa na magonjwa mabaya, na hivyo muda waliostahili waishi hapa duniani na hivyo wanakuwa wamewapa wengine miaka yao.
(7)Kuvamiwa na maroho machafu
 Katika kufanya ngono, wengine wanaenda hadi kwa waganga wa kienyeji na wachawi na huko wengine wanapewa madawa ya ajabu ambayo yanapelekea kuwamiwa na mapepo ya ajabu, na wengine kwa kupenda ngono wamefanya ngono na majini bila wao kujua na tayari yamesha wamiliki na hawaji watatokaje kwenye kifungo hicho.
Mimi nimekuonyesha hasara zile za kibiblia tu, sasa zipo za kijamii, kitaifa, kifamilia nk. Naamini baada ya kuwa umesoma ujumbe huu, kama bado unafanya ngono basi utabadili tabia yako na kuacha ngono mpaka wakati utakapo fika na kama haujaokoka nakusihi uokoke ili Yesu akupe nguvu za kushinda hiyo dhambi.
 Bwana Mungu akulinde na kukutunza.
Mwl. Patrick Samson Sanga +255 755 816 800
You might also





Comments