TUKIO LA KUSISIMUA NA LA AJABU SANA

Ni siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma
sana. Ilikuwa vigumu sana kulisahau na lilinifanya nijiulize,
inakuwaje Mungu anakuwa mkatili kiasi kile. Lakini bila shaka ilikuwa
ni wakati ule wa ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi na hasa
baada ya kujifunza maarifa haya ya utambuzi.

Ilikuwa ni mwaka 1979 nikiwa nasafiri kutokea Dar es salaam kwenda
Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa
12.30 jioni. Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, sio
kama siku hizi.

Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira, nikiwa
ndio kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja
serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo
sikuridhishwa na kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye
kampuni moja kule Arusha na niliitwa kwa usaili.

Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa ndio mji
maarufu kwa hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na
Arusha. Tulipofika Korogwe basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria
kupata chakula. Niliingia kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo
kwamba ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka
kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi la TTBS ambalo
ndilo nililosafiri nalo.

Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono
mifukoni na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye
hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni
bwana, anakula na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara
tu" Mwenye hoteli alisema kwa kudhamiria hasa.

Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema ni lazima anipeleke
polisi. Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo cha
polisi ili nishughulikiwe……

Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja aliyekuwa amekaa pembeni na
mkewe na watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile alimtuma mhudumu
mmoja aniite. Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kuja
kwa yule bwana.

Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi.
Nilimsalimia na aliitikia, nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana
aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia. Aliniuliza sasa huko
Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili wakati nimeibiwa fedha zote na
ningerudi vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa napanga namna ya kurudi Dar,
kama huko polisi ningeaminika.

Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa angenipa fedha za kutumia
huko Arusha na nikirudi Dar nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa
shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee fedha zake
ofisini kwake. Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkuruma na
kuniambia kuwa ameamua kunisaidia kwa sababu kila binadamu anahitaji
msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko. Nilimshukuru na
kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu.
Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka
Korogwe, lakini haikuchukua muda basi letu lilipata tatizo la pancha
ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili litengenezwe.
Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu.

Karibu na mji wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama
ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya
kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na
wengine huko chini walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake.
Niliposhuka niliona gari ndogo nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo
kando kulikuwa na maiti wawili.

Nilijua ni maiti kwa sababu walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu
kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa kamefungwa kanga
kichwani. Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia, ingawa
sio sana. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama
mitatu. alikuwa ameumia kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila
shaka wale walikuwa ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi
yalinitoka.

Baada ya kupata msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti
wale tulipanda basini kuendelea na safari yetu. Kale katoto
kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Land Rover ya serikali
kukimbizwa hospitalini. Ndani ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu
ajali ile tu, hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha
kwani tulifika kwenye saa tano asubuhi, badala ya saa mbili .

Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni hiyo
kesho, baada ya usaili niliponunua gazeti ambapo nilipata mshtuko
mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya
Same walikuwa ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto
wao ndiye aliyeokoka. Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na
jina la kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi Dar,
pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana, kama mtoto.

Nillishindwa kujua ni kwa nini afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea
mtoto yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo na majibu na pengine maswali ya
kijinga pia.
Nilijua kwamba nilikuwa na deni, deni la shilingi tisini. Kwa wakati
ule shilingi tisini zilikuwa ni sawa na shilingi laki moja za sasa.
Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu yule
aliniamini nakuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu.

Nilikata kipande kile cha gazeti la kingereza kilichokuwa na habari
ile. Nilichukuwa kipande hicho na kukiweka kwenye Diary yangu. Deni,
Ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta nikipiga magoti na kuomba
mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema kwa njia
yoyote. 'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa
sura na namna ujuavyo wewe. Nataka kulilipa deni hili ili nami niwe
nimemfanyia jambo marehemu,' niliomba. Nilirejea Dar siku hiyo
hiyo.Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya matokeo ya usaili ule
kuwa mbaya kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi na kusahau haraka
sana kuhusu mtu yule aliyenisaidia mbaye ni marehemu. Nilifanikiwa
hata hivyo kupata nafasi ya kusoma Chuo cha Saruji na baadae chuo cha
ufundi na hatimaye nilibahatika kwenda nchini Uingereza. Mwaka 1991
nilianza shughuli zangu.

Ilikuwa ni mwaka 1995 nikiwa ofisini kwangu pale lilipokuwa jengo
Nasaco ambalo liliungua mwaka 1996, ambapo lilijengwa upya na
kubadilishwa jina na kuitwa Water Front. Nikiwa nafanya kazi zangu
niliambiwa na sekratari wangu kwamba kulikuwa na kijana aliyekuwa
anataka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema hamjui.
Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa ni
kijana mdogo wa umri miaka kama 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo.
Alikuwa amevaa bora liende , yaani hovyohovyo huku afya yake ikiwa
hairidhishi sana.

Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani niliona atanipotezea bure muda
wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba sikuwa mtu mwenye huruma sana na
nilikuwa naamini sana katika watu wenye pesa au majina. Nilimuuliza,
“nikusaidie nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina
kikao baada ya muda mfupi”. Nilisema na sikuwa na kikao chochote ,
lakini nilitaka tu aondoke haraka.

“Samahani mzee, nilikuwa na shida…..nimefukuzwa shule na sina tena mtu
wakunisaidia kwa sababu …..nime….niko ….kidato cha pili na hivyo tu
natafuta tu kama atatokea mtu……..
Nilimkatisha. “Sikiliza kijana. Kama huna jambo lingine la kusema, ni
bora ukaniacha nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua kumsaidia
kila mtu aliyefukuzwa shule si nitarudi kwetu kwa miguu! Nenda Wizara
ya Elimu waambie……Kwanza wazazi wako wanafanya kitu gani, kwa nini
washindwe …..Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana uwezo,
wanataka sifa?”

“Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa
mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma shule ya Kwiro,
Morogoro. Shangazi ndiye anayenisomesha, naye ana kansa na hivi sasa
hata kazi hafanyi….,” Alianza kulia. Huruma fulani ilinijia na
nilijiambia, kama ni nauli tu na matumizi, kwa nini nisiwe mwema,
angalau kwa mara moja tu. “Baba na mama walifariki lini?” Niliuliza
nikijua kwamba, watakuwa wamekufa kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo
fasheni ya ukimwi ilipoanza, ambapo kila anayekufa huhesabiwa kwamba
kafa kwa ukimwi.

“Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu.
Ndio shangazi yangu akanichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa
kansa.” Yule kijana alilia zaidi. Naomba nikwambie wewe msomaji
unayesoma hapa kwamba, kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba ziko
nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua.

Kitu fulani kilinipiga akilini paaa! Nilijikuta namuuliza yuel kijana.
“Kwa nini umeamua kuja kwangu, ni nani alikuelekeza hapa na wazazi
wako walikufa mwaka gani na wapi?”
Yule kijana alisema, “Nimeona nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye
anaweza kunisaidia, na ndio nimejikuta nikiingia hapa,
sijui……..sikutumwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko Same
na mimi wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka. Niliumia tu hapa.”
Alishika kwenye kovu juu ya paji lake la uso.

Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja kifuani halafi niliona
kama vile nimebanwa na kushindwa kupumua. “Baba yako alikuwa anaitwa
nani?” “Alikuwa anaitwa Siame….Cosmas Siame….” Niliinuka ghafla hadi
yule kijana alishtuka . Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na
kuchakura kwenye droo moja na kutoka na diary. Mikono ikinitetemeka,
nilitoa kipande cha gazeti ndani ya diary hiyo, nilichokuwa
nimekihifadhi.

“Ndio alikuwa anaitwa Cosmas Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto
aliyenusurika.” Nilinong’ona. Nilijikuta nikipiga magoti na kusali.
“Mungu, wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda. Nimeamini baba kwamba
kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia
hapa duniani.” Halafu nillinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha
na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa binadamu kwa kila analofanya.

Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa. Nilihisi kuwa mtu mwingine
kabisa. Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku nikiwa bado
ninalia. “Mimi ni baba yako mdogo, ndiye nitakyekulea sasa. Ni zamu
yangu sasa kukulea hadi mwisho” Naye alilia bila kujua sababu na
alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Nilirudi kwenye kiti na kumsimulia
kilichotokea miaka 17 iliyopita.

Tuliondoka hapo na kwenda kumwona shangazi yake Ubungo, eneo la maziwa
ambako alikuwa amepanga chumba. Kutokana na hali yake nilimhamishia
kwangu, baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyo dada yake Cosmas
alifurahi sana hadi akashindwa kuzungumza kwa saa nzima. Alifariki
hata hivyo mwaka mmoja baadae, lakini akiwa ameridhika sana.

Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na hivi sasa yuko nchini
Australia anakofanya kazi. Ukweli ni kwamba ni mwanangu kabisa sasa.
Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake wanafurahia kile
walichokipanda miaka mingi sana nyuma. Lakini nami najiuliza bado.
Ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu najiuliza ni kitu gani
kilimvuta mwanae Siame hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine
zote? Nataka nikuambie, usiwe mbishi sana bila sababu, kuna nguvu za
ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu…………NGUVU HIZO NI UPENDO WA
MUNGU BABA.

Comments