IKIMBIE ZINAA

MWALIMU CHRISTOPHER MWAKASEGE
Je! Unaamini ya kuwa Mungu anaweza kusema na watu kwa njia ya ndoto? Najua ni rahisi kuamini kuwa Mungu alisema na watu zamani kwa njia ya ndoto kama tunavyosoma katika Biblia; lakini je! Unaamini ya kuwa Mungu anasema na watu kwa njia ya ndoto siku hizi? Najua kuna watu wanaoamini na wengine hawaamini. Sijui wewe uko upande gani. Lakini nataka nikueleze hivi; Kufuatana na Biblia kuna ndoto za aina tatu; (a) Kuna ndoto kutoka kwa Mungu. Soma kitabu cha Hesabu 12:6, na Yoeli 2:28. (b) Kuna ndoto zinakuja kwa sababu ya shughuli nyingi. Soma kitabu cha Mhubiri 5:3. (c) Kuna ndoto za uongo zinazotoka kwa shetani aliye baba wa uongo. Soma kitabu cha Yeremia 23:52 na Yohana 8:44. Unaweza kutofautisha kwa namna gani tofauti iliyopo kati ya hizi ndoto? Na utajuaje kuwa ndoto uliyoiota imetoka kwa Mungu? Kila ndoto lazima ipimwe na Neno la Mungu. Ikiwa imetoka kwa Mungu, ni lazima utakuta neno la Mungu ambalo linaeleza maana yake. Mara nyingine ndoto toka kwa Mungu huja kama fumbo; lakini Roho Mtakatifu ajuaye kuyafumbua mafumbo ya Mungu (1 Wakorintho 2:10,11), atalifunua fumbo hilo kwa kukuonyesha neno la Mungu linalofanana na ndoto hiyo. Si busara kuzikubali ndoto zote unazoota bila ya kuzipima katika Neno la Mungu. Na pia si busara kuzikataa ndoto zote bila kuzipima katika Neno la Mungu. Nimeona nianze kwa kukueleza haya kwa kuwa chanzo cha kuandika kitabu hiki, ni ujumbe wa Mungu ulionijia kwa njia ya ndoto. Ndoto yenyewe ilikuwa hivi: Niliona katika ndoto mtu mmoja mkristo, tena aliyeokoka akifanya mambo ya zinaa bila hata kuogopa. Na wakati nilipokuwa nikimtazama na kusikitika, nikasikia sauti toka juu yangu ikisema; “ NITACHUKULIANA MPAKA LINI NA MWANADAMU AFANYAYE MAMBO YA JINSI HIYO?” Baada ya kusikia maneno hayo nikaamka. Wakati huo ulikuwa ni alfajiri, na ndoto hiyo ilinipa maswali na masononeko mengi moyoni mwangu. Na niliamua kumshirikisha mke wangu Diana juu ya ndoto hiyo. Mke wangu akaniuliza; “ Maana yake nini ndoto hiyo?” Nilipotaka kufungua kinywa ili nimjibu uchungu mzito ulijaa moyoni mwangu, nikasikia kuugua rohoni, na mara nikaanza kulia! Unaweza ukaniuliza; “Mwakasege kwa nini ndoto ikulize machozi?” Hili ni swali zuri. Hata mimi nilijiuliza kwa nini nitoe machozi kwa ajili ya ndoto. Lakini baada ya kulifuatilia jambo hili katika maombi na katika neno la Mungu nilielewa sababu yake. Je! Unafahamu matokeo ya Mungu kusema “Nitachukuliana mpaka lini na mwanadamu afanyaye mambo ya jinsi hiyo?” Ukisikia maneno ya jinsi hii ujue Mungu amekasirika na kuna maangamizo mbele. Hebu na tulifuatilie jambo hili katika biblia ili tulione uzito wake. Nuhu na Gharika. Ni vizuri ukumbuke ya kuwa gharika ilitokea wakati wa Nuhu kwa sababu ya zinaa. “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliona hao binti za wanadamu – ni wazuri; WKAJITWALIA WAKE WO WOTE WALIOWACHAGUA. Bwana akasema, ROHO YANGU HAITASHINDANA NA MWANADAMU MILELE, kwa kuwa yeye ni nyama; basi siku zake zitakuwa mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile, tena baada ya hayo, wana wa Mungu WALIPOINGIA kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA AKAONA YA KUWA MAOVU YA MWANADAMU NI MAKUBWA DUNIANI NA KWAMBA KILA KUSUDI ANALOWAZA MOYONI MWAKE NI BAYA TU SIKU ZOTE. BWANA AKAGHAIRI KWA KUWA AMEMFANYA MWANADAMU DUNIANI, AKAHUZUNIKA MOYONI. Bwana akasema, Nitamfutilia usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambulisho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.” (Mwanzo 6:1-8) Ukiendelea kufuatilia habari hii katika Biblia utaona ya kuwa baada ya gharika ya maji walibaki watu nane tu! Wanadamu wengine wote waliangamia kwa sababu ya nini? – Zinaa! Sodoma na Gomora Wasomaji wa Biblia wanafahamu kabisa ya kuwa miji ya Sodoma na Gomora iliteketezwa kwa moto baada ya Mungu kuihukumu kwa sababu ya uasherati uliokuwa ukifanyika ndani yake. Soma Mwanzo 19:4-25. Na pia katika kitabu cha Yuda 1:7 tunasoma hivi: - “Kama vile Sodoma na Gomara, na miji iliyokuwa kando kando, waliofuata UASHERATI kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele.” Ikiwa Mungu aliwatenda hivi watu wa Sodoma na Gomora, ni kitu gani kinamfanya mwanadamu wa siku hizi adhani ya kuwa Mungu amebadilika juu ya kuadhibu wale wote wafanyao uasherati? Katika miji hiyo miwili ni watu watatu tu waliobaki – Lutu na watoto wake wawili! Wanadamu wengine waliokuwa katika miji hiyo waliteketezwa kwa sababu ya nini – Zinaa! Kuhani Eli na watoto wake. “Basi Eli alikuwa mzee sana, naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi WALIVYOLALA NA WANAWAKE waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania.” (1Samweli 2:22) Hata baada ya baba yao kuwaonya hawakusikia, na matokeo yake ni:- 1. Watoto hao wawili, Hofni na Finehasi walikufa wote siku moja; 2. Wana wa Israeli walipigwa na adui zao Wafilisti na Sanduku la agano likatekwa; 3. Kuhani Eli alikufa. Yote haya yalitokea katika taifa ambamo watoto wawili wa kiongozi waliuwa wakifanya mambo ya Zinaa bila hata kujali maonyo. Je! Bado unajiuliza kwa nini nilitoa machozi baada ya kusikia sauti ya Mungu katika ndoto ikisema “Nitachukuliana mpaka lini na mwanadamu afanyaye mambo ya jinsi hiyo?” Siku za Mwisho. “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi…….Kwa maana katika hao wamo wale WAJIINGIZAYO KATIKA NYUMBA ZA WATU, NA KUCHUKUA MATEKA WANAWAKE WAJINGA WENYE MIZIGO YA DHAMBI, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi. (2 Timotheo 3:1,26). Je! Siku hizi wanawake hawatekwi mateka na wanaume ili wafanye mambo ya zinaa? Vishawishi vimekuwa vingi, na wanawake wengi wameanguka katika mitego hiyo ya kupenda fedha na anasa, na mwisho wake ni kufanya uzinifu. Kwa nini wanaume wengi wamekosa akili juu ya jambo hili. Ni kitu gani kimewapofusha macho wasione ya kuwa uzinifu ni mbaya? Biblia inasema; “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; afanya jambo litakalomangamiza nafsi yake.” (Mithali 6:32) Ni dhahiri ya kwamba palipo na zinaa pana uharibufu, na wengi wanaangamia. Na nataka nikuambie ya kuwa Roho Mtakatifu akikuwekea mzigo huo ndani yako na kuliona jambo hili jinsi linavyomhunish Mungu, hakika hutatulia; na hapana budi macho yako yatajaa machozi juu ya kizazi hiki kinachojiangamiza chenyewe kwa sababu ya zinaa. Sababu ya mambo haya kuandikwa. Mambo haya hayakuandikwa kwa bahati mbaya, wala si kwa ajili ya kuonyesha historia ya watu Fulani tu. Bali yaliandikwa kwa kusudi maalumu na muhimu. “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili KUTUONYA SISI, tuliofikiriwa na miisho ya zamnai – Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.” (1 Wakorintho 10:11,12) Na mimi nimependa kuyaonyesha wazi ili tujue tunapozungumza juu ya zinaa, Bwana Mungu anakuwa na mawazo gani juu yake. Nafahamu si mara kwa mara hata katika mahubiri na mafundisho, jambo hili huguswa kwa undani. Lakini naona umefika muda wa kulichambua jambo hili kwa undani zaidi. Hali ilivyo sasa. Mtu mmoja aliniuliza “Je, mtu aliyeokoka anaweza kufanya mambo ya uasherati – je, anaweza kuzini?” Nikamwambia, “Mtu aliyeokoka hatakiwi kufanya mambo ya uasherati, kwa kuwa kufanya hivyo ni dhambi, lakini asiposimama katika Kristo sawasawa anaweza kuzini.” Halafu huyo mtu akaendelea kuuliza, “Je, Unamfahamu Fulani? (Akamtaja jina lake). “Ndiyo namfahamu.” Mimi nilimjibu, na nikaendelea kusema; - “ kuwa ni mtumishi wa Mungu, ingawa sijamwona muda mrefu umepita sasa”. Ndipo akasema, “Unafahamu ya kuwa alianguka na akazini na msichana Fulani (akamtaja jina lake) ambaye pia ameokoka, na sasa yule msichana amezaa?” Mimi nilishangaa na kushutushwa na habari hizo. Nikamuuliza “Unasema kweli ndivyo ilivyotokea?” Akasema, “Ndiyo” Ndipo Roho wa Mungu aliponikumbusha ndoto ile aliyonipa. Katika ujumbe ule wa ndoto, Mungu alinionyesha mkristo aliyeokoka akifanya mambo ya uasherati. Kwa mtu asiyeokoka siwezi kushangaa akifanya uzinzi, kwa kuwa bado yuko gizani, na yuko chini ya mkuu wa giza, ibilisi – kwa hiyo anaweza kufanya lo lote lile. Ndiyo maana mtu anaweza kusema yeye ni mkristo, na huku anazini mara kwa mara. Mkristo wa kweli aliyeokoka hatakiwi kuzini, wala kushindwa na dhambi. Kwa nini? Kwa kuwa ndani yake ametengwa mbali na dhambi, na amepewa ushindi juu ya dhambi. Ushindi dhidi ya dhambi Uhusiano wako na dhambi unakuwaje baada ya kuokoka, na kufanyika kiumbe kipya ndani ya Kristo? Watu wengi wakiisha-okoka, huwa bado wanasumbuliwa na kuanguka katika dhambi mara kwa mara, na hasa katika zinaa. Na hii inatokea kwa kuwa hawapati mafundisho ya kutosha ya neno la Mungu juu ya jinsi wanavyotakiwa kuenenda katika maisha mapya waliyopita. Kaini aliambiwaje na Mungu? Bwana alimwambia hivi; “ kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa UISHINDE” (Mwanzo 4:7) Na ndivyo ilivyo hata sasa. Bado tumo ulimwenguni humu, ingawa aliyezaliwa mara ya pili yeye si wa ulimwengu huu (Yohana 17:16). Lakini kwa kuwa bado tumo katika ulimwengu uliojaa dhambi inayotutamani kila siku, na tusije tukajisahau. Inatupasa tuishinde. Yanenaje maandiko? Imeandikwa katika kitabu cha (Warumi 6:12-14) “Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki. Kwa maana DHAMBI HAITA WATAWALA NINYI, kwa sababu hamuwi chini ya sheria, bali chini ya neema”. Ikiwa tunaambiwa ya kuwa “Dhambi haitawala ninyi …….” inakuwaje basi wengine wanatawaliwa nayo? Inakuwaje mtu wa Mungu, aliyepakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu aanguke katika zinaa? Kitu gani kinampofusha macho ya rohoni? Je! Ni halali kwa mtu anayekaa ndani ya Kristo kutenda dhambi? Yanenaje maandiko? “Kila akaaye ndani yake (Yesu Kristo) HATENDI DHAMBI; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtamua….atendaye dhambi ni wa ibilisi; kwa kuwa ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” (1 Yohana 3:6,8) Je! Unaona maneno haya yalivyoandikwa kwa ajili yetu? Sidhani kama unapenda tena kuwa Ibilisi kwa kuwa “Apendaye dhambi ni wa Ibilisi” Kwa hiyo ni muhimu ujilinde usitende dhambi. Tena imeandikwa: “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu UZAO WAKE WAKAA NDANI YAKE; WALA HAWEZI KUTENDA DHAMBI KWA SABABU AMEZALIWA KUTOKANA NA MUNGU.” (1 Yohana 3:9) Ikiwa umezaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu, ujue hakika UZAO WA MUNGU unakaa ndani yako. Na uzao huu wa uungu ni Mtakatifu, na unakaa ndani yake bila kutangatanga unakuwezesha kuishi bila kutenda dhambi. Je! Si jambo la kumshukuru Mungu hilo. Si kwamba anatuambia tusitende dhambi bila kutupa njia ya kutusaidia. Anajua sisi wenyewe hatuwezi kuishinda dhambi, BALI YEYE AKIKAA NDANI YETU NA SISI NDANI YAKE TUNAWEZA KUISHI KATIKA USHINDI DHIDI YA DHAMBI NA MITEGO YAKE YOTE. Tena imeandikwa; “Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu HATENDI DHAMBI; bali yeye aliyezaliwa na Mungu HUJILINDA, wala yule mwovu HAMGUSI.” (1 Yohana 5:18) Ee, mtu wa Mungu, jilinde basi kwa kuwa umezaliwa na Mungu, kwa nini tamaa ya uasherati ikusonge? Je?! umesahau ni uzao wa namna gani ulio ndani yako? Ni kweli kwamba mtu akitenda dhambi na akatubu, Bwana atamsamehe, (1 Yohana 1:9). Lakini hatutakiwi kutenda dhambi. Ndiyo maana imeandika; “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba MSITENDE DHAMBI”…. (1 Yohana 2:1) Sasa naona unaweza kuelewa kwa nini inashtusha na kusikitisha unaposikia mtu wa Mungu ameanguka katika dhambi ya zinaa. Ikiwa maisha ya wokovu yatakuwa ni ya kuanguka na kusimama, halafu tena kuanguka na kusimama mara kwa mara; basi ina maana ya kuwa ushindi wa kutosha haukupatikana pale msalabani. Lakini nataka nikuambie hivi, ushindi kamili ulipatikana pale msalabani bila kubakiza kitu! Ndiyo sababu Yesu Kristo alikuwa na ujasiri wa kusema ‘IMEKWISHA’ pale msalabani.
MAMA DIANA MWAKASEGE AKIONGOZA MAOMBI KWENYE KONGAMANO LA MAOMBI DODOMA

Comments