JE UMEADHIRIKA NA KUTOKUTII WAZAZI?

Kutoka 20:12{Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.}


Agizo la kuheshimu wazazi ni kati ya Amri kumi za Mungu, tatizo la watoto na vijana kutowatii wazazi linaendela kuwa sugu kila kunapokucha, si ajabu kusikia mtoto anaporomosha matusi ya Nguoni kwa baba au mama yake, mgeni akifika nyumbani utasikia mama anasema “nyie watoto mpishe mgeni akae” au “Amkia mgeni”, hiyo inaashiria nini? kwenye Mabasi utakuta Mama mja mzito amesimama huku watoto wa shule wamekaa, ni mara ngapi tunaona watoto wanafyonya watu wazima?. Wazazi wamepewa wajibu wa kuwa mawakili wa Mungu hapa duniani, hivyo ni lazima watoto watii na kuheshimu ushauri wa wazazi.

Angalia Mifano ifuatayo ya Vijana waliokaidi Ushauri wa wazazi wao na matokeo yake, kumbuka wazazi sio wale tu waliokuzaa ni watu wote wanaokuzidi Umri na wenye mamlaka juu yako.

1.      Kijana mmoja alikodi vijana wa kihuni kuja kumpiga baba yake, kwa sababu anamkataza kwenda Disko, mzee alivamiwa na kupigwa hadi mauti, hadi leo yule kijana ni kichaa, anayekula kwenye majalala ya taka.

2.      Binti mmoja alikuwa akionywa kuwa ni hatari kukaa faragha (kukaa na mwanaume katika chumba mkiwa wawili, au sehemu ya Giza), hata angekuwa mchumba wako, mtazini tuu. Binti alimuona mama yake amepitwa na wakati, akaamua kwenda kwa rafiki yake wa kiume, bila kutarajia alijikuta amezini, na hapohapo goli likafungwa, bahati mbaya alipomuambia kijana juu ya mimba yake, alimruka futi mia, mwisho wa yote yule dada akaamua kujiua kwa Sumu ya panya.

Kijana! kama umeamua kutozini, usijidanganye kuwa utashinda zinaa katika mazingira ya kukaa wawili chumbani. Uliona wapi wembe usinate kwenye Simaku vikiwa karibu? Au Ukalie jiko la Mkaa usiungue? Mapenzi ni moto mara moja, au umeme “transformer”. Kuna sehemu ambayo ukifika akili inapotea, kwa lugha ya kigeni inaitwa (Point of no Return), usijidanganye, wengi wamejikuta wana ukimwi, waja wazito, wameharibiwa usichana wao bila matarajio, kuishi au kuolewa na mtu asiyemtarajia n.k. kwa sababu ya kutozingatia ushauri huu.

3.      Kufungiwa nira na wasioamini, soma, 2Korintho 6:14-15. Hili ni tatizo sugu katika kizazi chetu, wala msije mkaiga jambo hili, Binti mmoja mkristo aliyekuwa amekaidi ushauri na kuamua kuolewa na Kijana wa Imani tofauti, alikutwa amefariki kwa kuwekewa sumu kwenye chakula, na mke mwenza ambaye hakutaka mume wake amuoe, ila kutokana na Imani ya mumewe kuoa wake wengi ilikuwa ruksa, hivyo akaoa na ndipo ugonvi ukaanza. Tunashuhudia matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kuabudu kwenye imani yako, watoto kukosa misingi ya Imani, Ndoa haiwi mwili mmoja tena kwa misingi ya Biblia, kwa sababu ya Imani, mwisho ni kujitenga na Mungu.

Mungu akikataza jambo, anamaanisha hivyo, usifanye, ukikaidi Mungu anasema, hata Maombi au sala yako ni CHUKIZO kwake “Yeye agauzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo” Mithali 28:9. Unaweza kusema mbona naomba na ananiskia? Kumbuka hata mwizi anaomba anapoenda kuiba na anarudi salama, unafikiri nani anayejibu maombi? Na mwisho wake ni upi?

Kuna mashauri mengi kwa vijana ambayo tutaendelea kujifunza siku zijazo, ninachowaasa vijana ni kwamba msimjaribu Mungu kwa kufanya mambo aliyokataza, matokeo yake ni maangamizi ya kutisha yanayoujia Ulimwengu. Wale walio tayari wameathirika na kutosikia ushauri, ni wakati wao kumrudia Mungu, atawasamehe ili mradi waamue kuachana na njia za majuto. Waswahili wanasema "Asiyesikia la Mkuu huvunjika Guu" na "Majuto ni Mjukuu". Hebu Bwana atuangazie nuru yake ili tuwe na Amani sasa na hata milele.

Comments