KUMTAZAMA NYOKA WA SHABA

Kutodharau maagizo ya Mungu BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa (Hesabu 21:6). Kudharau maagizo yaliyotolewa na Mungu, ni jambo lingine linaloonekana kuchangia kuwaangamiza wana wa Israeli wakati wa pigo la nyoka. Katika hili, ni vema utambue kuwa kuna tofauti kati ya kuangamia kutokana na kujishughulisha na masumbufu yanayosababishwa na matatizo, na kuangamia kutokana na kudharau maagizo yanayotolewa na Mungu. Pasipo shaka yoyote, katika kipindi ambacho wana wa Israeli waliishi nchini Misri, walijifunza kuhusu tiba ya mtu aliyeumwa na nyoka. Kupitia ujuzi huu, walikuwa wanaelewa dawa inayoweza kumwokoa mtu aliyegongwa na nyoka mwenye sumu kali. Kinachowashangaza katika pigo hili ni kuwa, badala ya kupatiwa dawa wanayoijua, Musa aliwaagiza kumwangalia nyoka wa shaba juu ya mti! Yawezekana hali ya kutoona uhusiano uliopo kati ya sumu ya nyoka na kutazama nyoka wa shaba, iliwafanya wengi kudharau agizo hilo. Jambo kama hili, lilitokea pale mfalme wa Israeli alipoenda kuomba msaada wa kivita kwa Elisha. Kwa kuongozwa na Roho wa Mungu, Elisha alimwagiza apige mshale sakafuni. Ingawa mfalme wa Israeli alifanya kama alivyoagizwa, alifanya hivyo mara tatu tu. Hapo Elisha akakasirika na kumwambia, “Ulitakiwa kupiga zaidi ya hapo, ndipo ungeliweza kuwashinda Washami katika kipindi chote cha utawala wako, ila kwa kuwa umepiga mara tatu, utawashinda mara tatu peke yake!” Ni wazi mfalme wa Israeli alitambua kuwa kazi ya mshale ni kurushwa kwa adui, sasa kitendo cha kuupiga sakafuni kina uhusiano gani na kuwapiga Washami? Waamini wengi wako kama mfalme wa Israeli, wakati wanapokutana na matatizo. Ingawa Mungu ameweka neno lake katikati yao, wengi hudharau kuyatendea kazi kutokana na kutoona uhusiano uliopo kati ya ukweli wa neno la Mungu, na matatizo wanayowakabili. Wakati umefika kwa waamini kutambua kuwa, kuna ushindi pale Mungu anapowaagiza kufanya jambo lolote lile hata kama akili zao zinakataa. Kama unatizamana na jeshi lenye mishale na mikuki, akikuambia upeleke kwaya badala ya jeshi fanya hivyo. Hivi ndivyo ilivyofanyika kwa mfalme Yehoshafati. Alipeleka waimbaji katikati ya jeshi lenye mikuki, panga na ngao, na akashinda. Kutii neno la Mungu ni moja ya mambo yanayoleta ushindi, wakati wa kukabiliana na nyoka wenye sumu. Kupambana na roho ya kusahau BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa (Hesabu 21:6). Usahaulifu unaovuviwa na makali ya tatizo, ni jambo lingine linalochangia kushindwa kwa watoto wa Mungu katika vita ya kiroho. Mara nyingi usahaulifu huu unasababishwa na wingi wa sauti zinazodai kuwa na uwezo wa kuhamisha mlima unaotakiwa kuhamishwa. Mwamini asipokuwa makini, sauti hizi zinaweza kumwondolea kumbukumbu ya maagizo ya Mungu dhidi ya matatizo yanayomkabili. Ingawa huko nyuma tatizo hili lilikuwa sio kubwa ndani ya kanisa, miaka ya hivi karibuni ukubwa wa tatizo hili umeongezeka ndani ya kanisa. Kushika kasi kwa tatizo hili ndani ya kanisa, kwa kiwango kikubwa kutokana na wingi wa matangazo katika vyombo vya habari yanayoelezea jinsi ya kutatua matatizo mbalimbali nje ya Mungu. Kwa mfano, kutokana na matangazo yaliyosheheni kila mahali kuhusu tiba za kiganga, waamini wengi wameanza kusahau ahadi za Mungu kuhusu uponyaji wa kimiujiza. Leo hii, maneno yaliyo karibu pale mwamini anapokutana na mgonjwa, ni yale yanayohusu uzuri wa hospitali au kituo fulani cha tiba mbadala! Kauli ya “Njoo Nikuombee”, imekuwa adimu kwa watu wa Mungu katika kipindi hiki cha siku za mwisho. Yawezekana wana wa Israeli walioangamia katika pigo la nyoka, waliangamia kutokana na kusahau agizo lililotolewa, la kumtazama nyoka wa shaba. Kutokana na ukweli huu, waamini wanatakiwa kupambana na roho yoyote ile, inayolenga kuwasahaulisha njia za kibiblia za kutatua matatizo yanayowakabili. Jambo hili linaweza kufanyika kwa kutokuwa na haraka pale unapofikwa na tatizo linalohitaji hekima maalum katika kulitatua. Ni katika kutulia ndipo mwamini anapoweza kuchukua mwelekeo ulio sahihi, kuhusiana na tatizo linalomkabili. Kama tatizo ni ugonjwa, atakimbilia neno la Mungu, kabla ya kufikiria ufumbuzi mwingine wa kibinadamu. Kukimbilia ufumbuzi wa kibinadamu wakati wa kujaribiwa, ni dalili ya kutenganishwa na neno la Mungu. Kuamini neno la Mungu Mungu anaposema neno, ni lazima wanaolisikia waliamini. Katikati ya makali ya pigo la nyoka wenye sumu, Mungu ndiye aliyewaagiza kumtazama nyoka wa shaba juu ya mti. La kushangaza ni kuwa, bado wako watu walioendelea kufa, kutokana na sumu ya nyoka. Swali tunalokutana nalo hapa ni kuwa, ni kwa nini watu wafe na wakati njia ya ukombozi ikiwa imewekwa bayana mbele zao? Kutokana na hali halisi ya kile kinachotokea wakati wa vita ya kiroho, inawezekana watu walikufa kwa kutoamini maagizo yaliyotolewa na Musa. Hiki ndicho kinachotokea ndani na nje ya kanisa. Kwa mfano, ingawa Mungu amewapa wanadamu neno la wokovu, bado asilimia kubwa ya wanadamu wanaendelea kuishi dhambini. Sehemu nyingine, waamini wanaendelea kuishi kwenye hofu, licha ya Biblia kuwa na zaidi ya maneno 365 yanayosema, “usiogope.” Ili kuishi maisha ya ushindi, watu wa Mungu wanatakiwa kuamini maagizo yote wanayoyapokea kutoka kwa Mungu. Imani juu ya neno la Mungu ni nini? Ni kuamini kuwa katikati ya mazingira magumu, itakuwa kama vile neno la Mungu linavyosema. Kumtegemea Mungu Ingawa Mungu amewapatia wanadamu akili ili ziwasaidie kufanikisha maisha yao, kwa kuwa njia za Mungu ni kamilifu kuliko zile za kibinadamu, hataki kuona njia za kibinadamu zikitangulia njia zake. Katika mazingira yoyote yale, njia za Mungu ni lazima zitangulie zile za kibinadamu. Kwa mfano, wakati wana wa Israeli walipovamiwa na nyoka wenye sumu, kulikuwa na njia za kibinadamu za kushughulikia watu walioathiriwa na sumu ya nyoka. Katikati ya njia hizi, Mungu naye alisimamisha njia yake. Hiki ndicho kinachotokea kila wakati kwa waamini, pale wanapokutana na vita katika maisha yao, kunakuwa na njia za utatuzi za kibinadamu na zile za kimungu. Kutokana na ukweli huu, hekima ya Mungu inapokosekana, Shetani anaweza kuzitumia njia hizi, kurarua imani ya watu wa Mungu. Kuraruliwa huku kunapotokea, kwa asilimia fulani watamtegemea Mungu na asilimia nyingine, watategemea njia za kibinadamu. Katika hili, watu wengine wamefikia hatua ya kutengeneza usemi wa uongo usemao, “jisaidie naye Mungu atakusaidia!” hii haipo popote ila Mungu ndio msaada pekee bila visaidizi

Comments