MAANA HALISI YA NDOA

Mathayo 19:4-6{Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe}

Nikawaida kusikia; heri nisingeolewa au nisingeoa, na wengine hata kama hawasemi kwa maneno lakini mioyoni wanajuta kwanini waliingia kwenye Ndoa, wanatamani kutoka lakini hawawezi. Kitu cha kushangaza ni hiki; wakati wengine wanatamani kutoka katika ndoa, wengi wanatamani kuingia ili na wao wajionee. Na wengine bila aibu wanawaambia vijana "Ndoa ni ngumu mtaiweza?". Kimsingi NDOA sio NGUMU ila wanadamu wanaingia katika NDOA bila kuwa na Elimu ya NDOA.

Leo hebu tuanze kuangalia kuwa, Je! ni mpango wa Mungu Ndoa ziwe na hali ya kukatisha tamaa namna hiyo? kama sivyo, matatizo yanatoka wapi? make utaona vijana wakati wa uchumba walikuwa wanabembelezana zaidi ya Mtoto na Mama, wananyweshana juice huku mmoja amempakata mwenzie, akiwa anamwangalia usoni kwa tabasamu lisilo na mfano, utafikiri wako peponi. Unashangaa baada ya kuoana na kuishi takribani mwaka mmoja, na wengine hata miezi mitatu haipiti, MAMBO YANAANZA KUBADILIKA TARATIBU LAKINI KWA UHAKIKA.

Majibu ya mikato unaanza kuyasikia, makelele na kununiana vinaanza kujitokeza, hata kwenye uwanja wa mpira, mambo yanaanza kuharibika, AMRI kama za jeshi zinaanza kutumika kwenye chumba cha faragha, ni "Mguu pande - Mguu sawa, nyumaaaaaa geuka! mwiliiii legeza !!!!!". Wapendwa! sehemu za kutuliza mawazo zinageuka kuwa KARAHA!. Hali kama hizo zinatoka wapi? na tufanye nini kuepukana na hali hizo? 

Tatizo kubwa ni kukosa elimu juu ya Ndoa na Kutomruhusu Mungu aliyemwanzilishi wa Ndoa kutawala maisha ya wanadoa. Leo naomba uelewe jambo hili: NDOA ni muunganiko wa WATU WAWILI WENYE MAPUNGUFU walioamua kuungana kuwa mwili mmoja. Kwakuwa wengi wanaingia kwenye ndoa bila kujua jambo hili wanapata shida wanapoanza kuona tabia za wapenzi  wao zikibadilika. Mara nyingi TABIA huwa hazibadiliki, ila ni Tabia za ASILI ambazo Zilikuwa sio rahisi kuonekana wakati wa uchumba, ni Mungu peke yake aliyekuwa anajua madhaifu hayo. Zingatia kuwa Hujaoa au hujaolewa na Malaika, kila binadamu aliyezaliwa katika ulimwengu wa Dhambi ana Mapungufu ambayo - Ni Mungu pekee anayeweza kuwafanya wana NDOA kuchukuliana, ndani ya UPENDO wa KWELI unaotokana na Mungu mwenyewe. 

Hesabu ya 1 + 1 = 1, Ni ngumu kuielewa kibinadamu, hesabu hiyo ukifanya kibinadamu lazima utatoa jibu ambalo ni 2, kwa upande wa Mungu jibu hilo ni KOSA. Hiyo ndiyo shida Mambo ya Mungu tunataka kuyatolea Majibu kwa kutia akili zetu, tutakwama tu. Hebu Mungu atusaidie kutupatia uwezo wa kutambua maana ya NDOA, ili ndoa zipone. Kwa leo naishia na utangulizi huu mfupi - Tutaendelea siku zijazo, usije ukakosa mada hizi, kwani MUNGU yupo kwa ajili ya kutusaidia.

Comments