SAFARI YA KUZIMU NA KUMBUKA NENO HILI ''MUDA UNAISHA HARAKA SANA''

Ushuhuda wa Victoria Juu ya Kuzimu



Muda Unaisha Haraka!
Huu ni ufupisho wa ushuhuda wa Victoria Nehale
Nilizaliwa na kuishi Namibia maisha yangu yote; na niliyatoa maisha yangu kwa Yesu tarehe 06 Februari 2005. Bwana Yesu Kristo ameshanifunulia mambo mengi katika ulimwengu wa roho ikiwa ni pamoja na safari za kuzimu. Bwana alinipa maelekezo kwamba niwashirikishe watu uzoefu wangu; pia alinionya kuwa nisiongeze wala kupunguza chochote katika vile alivyonionyesha na kuniambia. Wakati nikiandika kitabu hiki, mwishoni mwa 2006, nilishatembelewa mara 33 na Bwana Yesu Kristo. Kila aliponitembelea, Bwana alikuwa akiniambia kabla ya kuondoka: MUDA UNAISHA HARAKA!

Safari ya kwanza kuzimu
Katika wikiendi ya tarehe 23 Julai 2005, nilipanda taksi kwa ajili ya safari ya dakika thelathini kutokea mji wa Ondangwa ambako ndiko ninakofanya kazi na kuishi, hadi kijijini kwetu, kwa lengo la kwenda kuwa na wazazi wangu wakati wa wikiendi ile. Wakati nikielekea nyumbani, nilipata hisia kwamba kuna jambo lisilo la kawaida ambalo lingetokea jioni ile. Nilifika nyumbani kwenye saa 12 jioni; na hapo watu walikuwa wanaandaa chakula cha jioni. Nilikuwa jikoni pamoja na familia yetu, huku nikiwa nimelala kwenye mkeka. Watoto wa hapo nyumbani walikuwa wakiimba nyimbo zao za Shule ya Jumapili. Ghafla nilijisikia upako mzito ukinishukia; mwili wangu ukawa dhaifu sana; na nikawa nimetoka kwenye mwili kutokana na nguvu za Mungu. Nilimwona mwanamume amevaa joho jeupe refu likiwa limefungwa kwa kamba ya rangi ileile; akiwa anatembea kuelekea pale nilikokuwa nimelala. Kulikuwa na nuru imemzunguka kana kwamba ilikuwa ikitokea kwake. Alikuwa amevaa viatu vya wazi vya kahawia. Mwonekano wake ulikuwa kama wa watu wa Mashariki ya Kati, huku akiwa na ngozi nzuri ya hudhurungi. Uso wake ulikuwa mpole sana na umejaa utukufu lakini sikuweza kumtazama machoni. Alipoongea, sauti yake ilikuwa ya upole, na upendo, lakini pia  yenye mamlaka; mawimbi ya upendo yalikuwa yakitoka kwake.
Alinyoosha mkono wake kwangu na kuninyanyua kutokea pale nilipolala. Ghafla nilijiona nikiwa nina mwili mzuri sana. Nilijiona niko kama nilivyokuwa ningali na miaka kumi na nane. Nilikuwa nimevaa joho jeupe na kamba nyeupe. Japokuwa joho langu lilikuwa jeupe, lilitengenezwa kwa matirio tofauti na ya joho la yule mwanamume.  Joho lake lilikuwa la hariri huku liking’aa kiasi kwamba hata nashindwa namna ya kuelezea.
Alisema, kwa sauti ya upendo na upole sana: Victoria, nataka uende nami; nitakuonyesha mambo ya kuogopesha na ninakupekela mahali ambako haujawahi kufika katika maisha yako.” Alinishika mkono wa kulia na tukaondoka. Nilijiona kama vile tunatembea hewani na muda wote tulikuwa tukielekea tu juu. Baada ya muda, nikawa nimechoka sana, na nikamwambia kuwa nisingeweza kuendelea na safari. Hivyo nikamsihi aniruhusu nirudi. Hata hivyo, alinitazama kwa upendo na kusema, “Haujachoka – uko sawa tu. Kama ukichoka, nitakubeba, lakini kwa hivi sasa uko tu sawa. Amani iwe kwako. Tuendelee.”
Tulifika mahali ambako ni pakavu sana; pakavu kuliko jangwa lolote analojua binadamu; hakukuwa na dalili zozote za uhai. Hakukuwa hata na mti mmoja au hata jani au kiumbe chochote hai. Lilikuwa ni eneo linalofadhaisha sana.
Hatimaye tulifika kwenye geti moja na yule mwanamume alinigeukia na kusema: “Victoria, tutaingia kupitia geti hili na mambo ambayo utayaona yatakuogopesha na kukufadhaisha – lakini uwe na uhakika kuwa kokote nitakakokupeleka, utakuwa na ulinzi mkamilifu. Wewe fungua tu macho yako na kutazama kila nitakachokuonyesha.” Nilijawa na hofu na kuanza kulia. Nilikuwa nalalamika na kumwomba anirudishe. Nilimwambia kuwa sikutaka kuingia kwenye sehemu ile maana tayari nilikuwa naona kupitia getini kile kilichokuwa kikiendelea ndani. Aliniangalia na kusema,  “Amani iwe nawe; niko pamoja nawe. Ni lazima tuingie ndani, maana muda unakimbia haraka.”
Tuliingia kupitia getini. Siwezi kukusimulia utisho wa mahali pale. Nina uhakika kabisa kuwa hakuna sehemu yoyote ulimwenguni ambayo ni mbaya kama ile! Sehemu ile ilikuwa ni kubwa sana na nilipata hisia kuwa inaendelea kupanuka muda wote. Ilikuwa ni sehemu ya giza totoro na joto lake halipimiki; ilikuwa ni joto kuliko moto ulio mkali kabisa. Sikuona miali yoyote ya moto au chanzo cha joto lile lakini kulikuwa ni JOTO! Kulikuwa na wadudu wa kila ukubwa; wa kijani, weusi, na wa kijivu - ila aina ya wadudu unaoweza kuwafikiria. Zaidi ya hapo, kulikuwapo pia kila mahali funza wafupi, wanene, weusi, ambao wanapanda juu ya kila kitu. Walianza kupanda juu yetu na wadudu nao walikuwa wametuzunguka kila upande. Mahali pale kulikuwa na harufu mbaya mno; hakuna maneno ya kutosha kuelezea harufu ile. Harufu ilikuwa kama nyama iliyooza lakini ilikuwa ni mbaya mara mia zaidi ya nyama iliyooza  niliyowahi kunusa maishani mwangu mwote! Kulikuwa na kelele za vilio na kusaga meno, pamoja na vicheko vibaya vya mapepo.
Kibaya kabisa kwenye sehemu hii ni kuwa pamejaa watu. Walikuwa ni wengi sana kiasi kwamba hawahesabiki. Walikuwa ni mifupa tu. Ninaweza kusema kwa ujasiri na uhakika kabisa kwamba mifupa hii ilikuwa ni wanadamu kwa vile niliweza kuwatambua baadhi ya ndugu zangu wa karibu na watu kutoka kijijini kwangu. Mifupa yao ilikuwa ya kijivu cheusi na mikavu sana. Walikuwa na meno marefu makali kama wanyama wa porini. Midomo yao ilikuwa mikubwa na mipana na ndimi zao zilikuwa ndefu na nyekundu sana. Mikono na miguu yao ilikuwa na vidole vyembamba virefu, na kucha kali, ndefu. Baadhi yao walikuwa na mikia na pembe.
Kulikuwa na mapepo yakichanganyika na watu: mapepo yalionekana kama mamba na yalitembelea miguu minne. Yalionekana yanajisikia vizuri tu kwenye mazingira yale na mara zote yalikuwa yakiwachokoza na kuwatesa wanadamu. Kelele kutoka kwa yale mapepo zilikuwa ni kama vile yako kwenye sherehe; maana yalionekana yana furaha. Yalikuwa pia yakicheza na kurukaruka muda wote. Wanadamu kwa upande wao, walionekana wana mateso na fadhaa; walikuwa katika hali ya kukosa msaada. Kelele za wanadamu zilisababishwa na maumivu. Walikuwa wakilia, wakipaza sauti na kusaga meno yao; na walikuwa katika hali ya mateso makali yasiyo na mfano.
Watu katika sehemu ile, walikuwa ni wengi mno, lakini niliweza kuona kuwa wengi wao walikuwa wanawake. Waligawanyika katika makundi mbalimbali. Japokuwa walikuwa katika makundi, ilikuwa haiwezekani kukadiria idadi yao katika kundi lolote maana makundi yenyewe yalikuwa ni makubwa kupita kiasi!
Mwanamume yule alinipeleka hadi kwenye kundi mojawapo upande wa mashariki wa sehemu ile. Kisha alinitazama na kusema: “Victoria, hili ni kundi la watu ambao walikataa kuwasamehe wengine. Niliwaambia mara nyingi na kwa njia nyingi kuwa wawasamehe wengine lakini walinikataa; Mimi nimewasamehe wao dhambi zao zote lakini wao walikataa kuwasamehe wengine. Muda wao uliisha na wakajikuta wako hapa. Watabakia hapa milele yote; wanakula matunda ya kazi yao milele na milele. Hata hivyo, inaniuma sana kuwaona kwenye sehemu hii mbaya na katika sehemu hii ya milele – maana ninawapenda.”
Nilipelekwa kwenye kundi linalofuata, na mwanamume yule aIiniambia kuwa watu wa kundi lile la pili walikuwa ni wale waliokuwa na madeni: walikuwa na uwezo wa kulipa madeni yao lakini waliendelea kuahirisha. Walikuwa wakisema kuwa tutalipa kesho, wiki ijayo, mwaka ujao, hadi muda ukawaishia. Hapa ndipo watakaa milele; wanakula matunda ya kazi yao.  
Aina ya pili ilikuwa ni ya wale ambao walikuwa na madeni na walikuwa na uwezo wa kuyalipa; na walikuwa tayari kuyalipa, lakini walikuwa wakiogopa matokeo maana, labda, kama wangesema kweli, wangeishia kukataliwa, au wangefungwa, au labda kile ambacho walitenda kingejulikana duniani kote nao wangeaibika. Yule mwanamume akasema:  “Hakuna kati yao ambaye alinijia kuniomba njia ya kufanya. Kama wangeniomba, ningewaonyesha njia rahisi kabisa ya kutoka kwenye hali zilizowakabili. Muda wao uliisha na wakajikuta wako hapa ambako ndiko watakuwako milele. Wanakula matunda ya kazi zao.”
Kisha akasema: “Kundi la tatu walikuwa na madeni ambayo hawakuwa na uwezo wa kuyalipa, lakini pia, nao hakuna hata mmoja ambaye aliniambia kuwa ana deni asiloweza kulipa. Kama wangefanya hivyo, ningewalipia madeni yao. Pia, walijaribu kutumia ufahamu wao na hekima yao, kitu ambacho hakikuwasaidia kwa njia yoyote. Hivi sasa wamejikuta mahali hapa ambako ndiko watakakoku. Wanakula matunda ya kazi yao. Moyo wangu unauma kwa ajili ya watu hawa wote maana ninawapenda sana.”
Katika kundi la kwanza, niliwaona ndugu zangu wawili wa kike wa karibu sana pamoja na mtoto wa miaka kumi na mbili, naye pia akiwa ndugu yangu. Nilijua alikuwa na miaka kumi na mbili maana huo ndio ulikuwa umri wake wakati anakufa. Katika kundi la pili nako pia niliwaona baadhi ya ndugu zangu, pamoja na Mchungaji ambaye nilimfahamu vizuri sana. Rafiki yangu wa kiume, Jakes, ambaye alijiua kwa sababu mimi niliamua kumpa Kristo maisha yangu, naye alikuwa kwenye kundi la pili. Niliwaona baadhi ya majirani zangu kwenye makundi yote pia.
Niliwatambua watu niliowajua kabla ya kufa kwao; nao pia walinitambua. Ndugu zangu walijawa na hasira sana waliponiona na wakaanza kunitukana. Walikuwa wakitumia lugha chafu kabisa wakati wakinitukana. Mmoja wao alisema kuwa sikustahili kumfuata mwanamume yule ambaye nilikuwa naongozana naye; walikuwa wakiongelea mambo ambayo nilikuwa nikiyafanya kabla ya kutoa maisha yangu kwa Kristo. Hawakuwa wakisema uongo. Mambo waliyokuwa wakinituhumu nayo yalikuwa ya kweli. Jakes alikuwa akisema kuwa mimi nilikuwa wa kwake na kwamba nilitakiwa kwenda pale alipokuwa maana nilitenda dhambi zilezile kama alizotenda yeye. Mara ya kwanza, yule mchungaji alionekana amefurahi kuniona na akasema nimefanya vema kuja, lakini alibadilika ghafla pale alipomwona yule niliyekuwa nimeongozana naye; kisha naye akajiunga na wale waliokuwa wakinilaani kwa matusi. Mwanamume yule aliyekuwa nami akaniambia nisiwajali maana hawajui walitendalo.
Nilipigwa na bumbuazi na kujawa na huzuni kubwa sana. Mwili wangu ulikuwa ukitetemeka na sikuweza kusimama. Nilikuwa nikilia bila kuweza kujizuia. Mwanamume yule alinigeukia, akanikumbatia, na kusema: “Amani iwe nawe, Victoria.” Nguvu zangu zilinirejea na nikajisikia salama mikononi mwake. Kisha akaniambia kuwa tulitakiwa kuondoka pale na kurudi. Alinitazama na kusema: “Victoria, nimeshakuonyesha. Sasa inabidi uchague ni kundi lipi unataka kuingia; uchaguzi umo mikononi mwako. Ni lazima uwaeleze watu kila kitu ulichokiona lakini usiongeze au kupunguza chochote.”
Nakumbuka kuwa tuliondoka pamoja kwenye ile sehemu ya kutisha lakini sikujua nimemwacha wapi maana fahamu zangu za kawaida zilinirudia. Nilifungua macho yangu na kujikuta kwenye mwili wangu wa nyama, huku nikiwa nimelazwa kwenye Hospitali ya Oshakati. Nilikuwa nimetundikiwa dripu kwenye mkono wangu wa kushoto; na nilimwona mama yangu na ndugu zangu wengine wa kijijini kwenye kona moja ya chumba, ambako walikuwa wakiniangalia kwa mshangao. Niliona kwenye uso wa mama yangu kwamba alikuwa analia. Nilimwuliza nesi mmojawapo kama alikuwa anafahamu tatizo langu lilikuwa nini lakini alinifanyia tu mzaha na kusema: “Umerudishwa. Labda ulifanya kosa fulani na unatakiwa kutubu.” Nesi alikuwa anajaribu kuelezea kwa lugha nyepesi namna hali yangu ilivyokuwa, lakini nilibaini kuwa alikuwa anaogopa kunikaribia. Nilimwomba aniitie daktari aliyenihudumia. 
Daktari alipofika, alisema kuwa hakujua kulikuwa na tatizo gani kwangu. Mwanzoni, alidhani kuwa nilikuwa na malaria lakini vipimo vilionyesha kuwa sikuwa nayo. Aliendelea kunieleza kuwa joto langu, mapigo ya moyo, na shinikizo la damu vilikuwa chini sana kwa viwango vya hatari lakini hakuweza kujua sababu yake. Alisema kuwa hakuwa na cha kufanya tena kwa ajili yangu. Hakuweza hata kuniandikia kulazwa maana sikuwa na ugonjwa. Dripu waliyoniwekea ilikuwa haifanyi kazi mwanzoni, lakini nilipofungua tu macho yangu, ikaanza kufanya kazi. Alipendekeza kuwa nesi aniwekee dripu nyingine mara ile ya kwanza itakapoisha ili niweze kupata nguvu za kutosha kwenda nyumbani.  
Niliogepeshwa na kile nilichoona mahali pale na sikuweza kujizuia kulia. Harufu mbaya ya pale iliendelea kuwa halisi kama nilipokuwapo hapo. Taswira za pale ziliendelea kunijia wakati wote. Nilishindwa kulala na mwili wangu wote ulihisi maumivu makubwa. Nilijihisi kana kwamba miguu na mikono yangu ilinyofolewa na kurudishiwa tena. Ah, nilijisikia vibaya sana. Nilikuwa na tumbo la kuendesha na kichwa kiligonga kwa wiki nzima.
Niliamua moyoni mwangu kwamba nisingemweleza mtu yeyote juu ya kile nilichoona maana ni nani kwanza angeniamini? Watu watanielewaje? Niliendelea kujiambia kuwa sitamweleza kamwe mtu yeyote juu ya mambo hayo. Mmoja wa washauri wangu alinipigia simu siku tatu baadaye kuulizia kuhusu hali yangu maana nilikuwa nimemtumia meseji aniombee. Bila kujitambua, nilijikuta nikimsimulia kuhusu yaliyonikuta. Niliposhtuka, tayari nilishamweleza karibu kila kitu. Nilitamani kujipiga mateke. Nilikuwa nalia kwa kuwa niliamini kuwa nimefanya kosa kubwa kabisa maishani mwangu. Sasa hadithi nzima ilikuwa wazi; hakukuwa na uwezekano wa kuificha tena. Sasa najua kuwa kama Mungu akitaka jambo fulani lielezwe, lazima litaelezwa. Maana yeye si ni Mungu?
***********
Agosti 19, niliamka huku nikijisikia hali ya upako kwenye mwili wangu wa nyama. Nilikuwa dhaifu na kutetemeka, huku mawimbi ya umeme yakipita kwenye mwili wangu. Jioni, niliona mwanga mkali ukija chumbani kwangu, na katikati yake, alikuwa yuleyule mwanamume. Safari hii alikaa chini kwenye kiti karibu na kitanda changu. Hata sielewi kiti hiki kilitoka wapi lakini kilikuwa pale mara tu alipokuwa tayari kukaa. Kilikuwa ni kiti kizuri cha dhahabu tupu. Umbo lake lilikuwa la kiti cha kawaida, kikiwa na sehemu ya kuegemeza mgongo. Kwenye kila mguu kulikuwa na nyota ya madini ya fedha iliyopachikwa kwenye dhahabu ile; nyota ileile ilikuwa pia katikati ya sehemu ya nyuma ya kuegemeza mgongo. Kulikuwa na magurudumu kwenye kila mguu.
Baada ya kunisalimia, aliniambia kuwa alijua kuwa nina maswali mengi kuhusu yeye ni nani; hivyo alikuja kujitambulisha kwangu na kufafanua mambo kadhaa ambayo tayari nilikuwa nimeyapitia. Alisema: “Mimi ni Yesu Kristo, Mwokozi wako. Kama una mashaka yoyote, tazama mikono yangu. Mahali pale ambako tulienda, ni Kuzimu.” Nilipoangalia mikono yake, niliona makovu ambamo misumari ilimtoboa.
Rafiki, napenda nikueleze kuwa kuzimu si sehemu ya kufikirika tu mawazoni; lakini ni mahali halisi na si kuzuri hata kidogo. Ni mahali ambako hakukutengenezwa kwa ajili ya wanadamu bali kwa ajili ya shetani na mapepo yake. Sehemu inayotustahili ni Mbinguni pamoja na Yesu lakini inatubidi tumchague Yesu kabla hatujachelewa. Leo, unapoisikia sauti yake, usifanye moyo wako kuwa mgumu; mkubali Yesu awe Mwokozi wako binafsi kisha uishi kwa ajili yake. Kuzimu ni kubaya mno: ni sehemu ya hofu na huzuni; ni sehemu ya mateso na vilio vya milele na kusaga meno. Shetani anataka awachukue watu wengi kadiri iwezekanavyo ili aende kule pamoja nao. Usishirikiane naye; shirikiana na Yesu nawe, badala ya kufa, utaishi.
Sikuelewa kwa nini Bwana aliniambia nichague kati ya makundi mawili aliyonionyesha kule kuzimu ilhali mimi tayari nilikuwa Mkristo niliyeokoka. Nimeshamkubali maishani mwangu lakini bado alikuwa akiniambia nichague kama nataka kwenda kuzimu au la! Sikuweza kuelewa. Nilianza kuomba na kumwuliza Mungu anipatie ufunuo juu ya kile alichomaanisha na ni nini anataka nifanye. Bwana alinifunulia kuwa nilikuwa nimeficha roho ya kutosamehe na chuki moyoni mwangu kwa sababu ya dada yangu mmoja, pamoja na binamu yangu mmoja. Nilimwomba Bwana anisamehe kutokana na kutosamehe kwangu. Pia nilimwomba dada yangu anisamehe kwa kuweka hasira na uchungu moyoni mwangu kwa ajili yake. Bwana alinielekeza niende pia nikamwombe msamaha binamu yangu.
Bwana pia alinikumbusha kuwa kulikuwa na wakati ambapo nilipata kazi ya ualimu kwa kutumia cheti cha diploma cha uongo na alihesabu hilo kuwa ni deni na wizi. Nilikusudia kutenda kilicho sahihi na nilimwomba anisaidie kutoka kwenye tatizo hili na anionyeshe njia rahisi ya kutoka humo maana hili lilikuwa ni kosa kubwa na lingeweza kunifannya nifungwe. Alinielekeza niende kwenye Idara ya Elimu nikakiri kosa nililofanya. Nilikuwa tayari kwenda jela kama ingebidi. Nilipata upendeleo wa Bwana kwa kiasi kikubwa sana. Nilipofika kule, mhusika kwenye Idara ya Elimu aliniambia niamue kile ninachotaka kufanya: ama kulipa mshahara ambao nilipokea kutoka serikalini au la. Waliahidi kuwa hawatanishtaki maana walishangazwa na kitendo changu cha kwenda kukiri kosa lile. Mungu wetu ni Mungu mwaminifu ambaye analiheshimu Neno lake.
Kama uko kwenye hali inayofanana na niliyokuwa nayo, napenda nikutie moyo kuwa utende kile kilicho sahihi, bila kujali matokeo. Unaweza kufungwa kwenye jela ya kidunia lakini hiyo ni ya muda tu. Hakuna maumivu au aibu inaweza kulinganishwa na kutengwa na Mungu milele. Kuzimu si mahali pazuri: ni bora kumruhusu Mungu akuhukumu sasa kabla hujachelewa. Hatutakiwi kuogopa hukumu ya Mungu tungali bado kwenye kipindi cha Neema; ni lazima tumruhusu afunue chochote kisicho sawa kwenye maisha yetu tungali bado na muda wa kuweka mambo sawa naye, maana hakuna msamaha upande wa pili wa kaburi.
Safari ya pili kuzimu
Oktoba 18, 2005, niliamka saa 11:30 asubuhi lakini sikuweza kwenda kazini. Nilijisikia hali ya udhaifu sana na  kulewa; sikuweza kusogea au kugeuka kitandani kwangu; na uwepo wa Bwana ulikuwa mzito sana chumbani. Nilikuwa natetemeka na nikahisi kama umeme ukipita mwilini mwangu. Bwana alinijia kabla tu ya saa 2:00 maana kwa mara ya mwisho nilipotazama saa ilikuwa ni saa 1:48; na Yeye alifika muda mfupi tu baada ya hapo. Alinisalimia na kusema kuwa tunatakiwa kwenda tena maana muda unaisha haraka sana. Nilisimama na tulianza kutembea. Utembeaji wa safari hii ulikuwa tofauti kabisa na safari zingine zote. Japokuwa miguu yetu ilikuwa inafanya kitendo cha kutembea, tulikuwa kama vile tunaelea zaidi kuliko kutembea. Wakati tukiwa njiani, Yesu aliniambia kuwa dhambi zote ni mbaya na hakuna kitu kama dhambi ndogo au dhambi kubwa. Dhambi zote mwisho wake ni mauti - ziwe kubwa au ndogo. Bwana aliniambia kwamba tunaenda kutembelea kuzimu tena na akaniuliza iwapo nilikuwa nina hofu. Nilimjibu kuwa nilikuwa nayo.
Alisema, Roho ya woga haitoki kwa Baba yangu au kwangu; inatoka kwa Ibilisi. Woga utakusababisha utende mambo ambayo yatakupeleka kuzimu.” 
Bila imani haiwezekani kumpendeza Mungu na hofu ni kinyume kabisa cha imani. Ni wazi kuwa hofu haimpendezi Mungu kwa kuwa inaharibu imani yetu. Muda wote tulipokuwa njiani, tulikuwa tunatembea kila mmoja peke yake. Lakini mara tu tulipofika kwenye lango la kuzimu, alinishika mkono wangu kwa mkono wake wa kulia kwa muda wote tuliokuwa kuzimu. Nilifurahi sana kwa Bwana kunishika mkono maana kwa namna alivyokuwa amenishikilia kwa nguvu, hofu yote ilitoweka. Sehemu ile ilikuwa bado iko vilevile: hakukuwa na tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Kulikuwa na wadudu, funza, joto kali sana, harufu, mifupa, kelele: kila kitu kilikuwa kama mwanzo nilipoenda pale. Tulipita tena kwenye geti lilelile baya na Bwana akanipeleka kwenye kundi moja la watu. Kulikuwa na watu wengi niliowafahamu wakati wangali duniani. Maskini, walikuwa kwenye hali mbaya sana. Walionekana ni wenye taabu na maumivu makubwa; lakini baya zaidi ilikuwa ni nyuso zao zisizo na matumaini kabisa.   
Bwana alimwonyesha mwanamke mmoja wa makamo ambaye nilimfahamu kabla hajafa. Alikufa kwa ajali ya gari mwanzoni mwa mwaka 2005. Nilipigwa na butwaa kumwona pale maana sote tulimjua kuwa ni mtu aliyekuwa na hofu ya Mungu na aliyempenda Mungu. Bwana aliniambia kuwa mwanamke yule alimpenda na Yeye Bwana naye alimpenda; alimwokoa angali akiwa duniani; aliwashuhudia wengi ambao walimwijia Bwana na alifahamu Neno vizuri sana. Alikuwa mkarimmu kwa maskini na wahitaji; aliwapatia walichohitaji, na kuwasaidia kwa njia nyingi. Alikuwa ni mtumishi mzuri wa Bwana kwa namna nyingi.
Maneno hayo ya Bwana yalinishitua hata zaidi; nami nikamwuliza kwa nini amwache mtu kama huyo aliyemtumikia kwa kiasi kikubwa hivyo aingie kuzimu? Bwana alinitazama na kusema kuwa mwanamke yule aliamini uongo wa Ibilisi. Japokuwa aliyajua Maandiko vizuri, aliamini uongo wa ibilisi kwamba kuna dhambi ndogo na kubwa. Alidhani kuwa dhambi ‘ndogo’ zisingempeleka kuzimu, maana alikuwa Mkristo hata hivyo.
Bwana aliendelea kusema, “Nilimwendea mara nyingi na kumwambia aache kile alichokuwa anakifanya lakini mara nyingi alijenga hoja akilini mwake kuwa kile alichokuwa anakifanya kilikuwa ni kidogo sana na alichukulia kuwa yale maonyo yangu yalikuwa ni hisia zake tu za hatia. Kulikuwa na muda ambapo aliacha kwa muda lakini baadaye alijishawishi tena kuwa maonyo yale hayakuwa yanatoka kwangu, bali ni sauti yake tu kwa kuwa aliona kuwa dhambi ile ilikuwa ni ndogo sana kuweza kumhuzunisha Roho Mtakatifu.”
Nilimwuliza tena Bwana ili aniambie ni dhambi gani basi mwanamke yule alitenda. Alinijibu kwamba, “Mwanamke huyu alikuwa na rafiki ambaye alikuwa nesi kwenye Hospitali ya Oshakati. Kila mwanamke huyu alipoumwa, hakwenda hospitali na kulipa kwa ajili kadi yake kama inavyotakiwa kwenye taratibu za kawaida; badala yake yeyé alipiga tu simu na kumwambia rafiki yake amfanyie mipango ya dawa kutoka kwenye  Zahanati ya Hospitali. Na mara zote rafiki yake yule alikubali na kumwambia kuwa apite pale muda fulani kuchukua dawa. Kwanza, aliamua kukubali uongo wa ibilisi juu ya kuwapo kwa dhambi kubwa na ndogo na kuikataa kweli yangu; alimsababisha mtu mwingine atende dhambi na kuiba kwa niaba yake, lakini kibaya zaidi, ALIMHUZUNISHA ROHO MTAKATIFU. Hicho ndicho kilichomfanya afike kuzimu. Haijalishi kwamba utaleta mamilioni ya roho kwa Bwana; bado upo uwezekano wa kuingia kuzimu kutokana na kumhuzumisha Roho Mtakatifu. Si tu kwamba ni lazima ujali wokovu wa wengine lakini pia ni lazima uwe mwangalifu usije ukasahau roho yako. Kuwa makini na Roho Mtakatifu wakati wote.” Baada ya maneno hayo, Bwana alisema ni wakati wa kurudi.
************
Wakristo wengi waliosikia hadithi yangu hii huiona kama ina matatizo. Mara nyingi huwa wanniuliza, “Vipi kuhusu kuhesabiwa haki, rehema, na neema?” na pia “Inawezekana kweli kupoteza Wokovu wako baada ya kuwa umeupokea?”  
“Huko si kuvuka kiwango?”
“Mungu anaweza kuwa mkatili kiasi hicho?”
Kama nilivyosema kwingineko kwenye kitabu hiki, mimi siongei theolojia yangu hapa. Ninasema tu kile ambacho Bwana alinionyesha na kunifundisha – na kile alichoniruhusu kukishuhudia. Tafadhali someni Biblia zenu ili kupata majibu. Tazama aya zifuatazo, kisha uhukumu mwenyewe.
“…bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” (1Wakorintho 9:27)
Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?
Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? (Warumi 6:1-2)
Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake.” (Warumi 6:12)
Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao. (Waebrania 10:26 –27)
Unasema, “Je, naweza kwenda kuzimu baada ya kuwa nimemtumikia Bwana na kuwaleta wengi kwa Kristo?” Hukumu mwenyewe!
Kutokutii
Jumatatu ya tarehe 6 Machi 2006, niliamshwa na saa ya kengele saa 11:30. Nilianza kuomba na nikatambua kulikuwa na upako mzito juu yangu. Mwili wangu ulikuwa dhaifu na nilikuwa nikitetemeka; mawimbi ya umeme yalikuwa yanapita kwenye mwili wangu.
Wakati wa mchana, nikiwa nimelala kitandani, niliona nuru nyeupe ikijaza chumba changu. Niliona shanga ndogondogo, nyeupe, za duara, zenye ukubwa wa kichwa cha pini. Shanga hizi zilikuwa zikianguka kama mvua inavyonyesha na zilipogusa ngozi yangu, zilizama ndani. Zaidi ya hapo, niliona kama wingu linalofanana na ukungu mweupe likija kutokea juu. Nalo pia lilikijaza chumba na likawa likizama kwenye ngozi yangu kila liliponigusa. Baada ya hapo, nilimwona Yesu akitembea katikati ya lile wingu la ukungu kuelekea pale nilipokuwa. Alikaa kwenye kiti chake pembeni mwa kitanda changu. Hata sielewi kiti hiki kinatokea wapi; huwa kinatokea tu mara anapokuwa tayari kukaa.  Ni kiti kizuri kilichotengenezwa kwa dhahabu. Umbo lake ni kama la viti vingi tunavyovifahamu lakini kina sehemu ya kuegemeza mgongo. Kwenye kila mguu kuna nyota ya fedha; na nyota nyingine ya aina ileile, japo ni kubwa zaidi, iko kwenye sehemu ya kuegemea. Kuna magurudumu kwenye kila mguu.
Yesu alinisalimia na akaninyooshea mkono wake na kuniambia niamke maana muda unakimbia haraka sana. Alinivuta mkono wangu nami nikainuka na kukaa kitandani kwangu.
Kisha akaniambia, Victoria, tuombe.” Aliomba kwa lugha ambayo siielewi; nilielewa neno moja tu ‘Amen’. Kisha aliendelea kwa kuniuliza nilikuwa naona nini nami nilimwambia kuwa nilikuwa naona kundi la watu wakienda kazini kwao na wengine wakirudi kutoka kazini kwao. Nilikuwa pia naona vile vishanga vyeupe vikiwaangukia wale waliofika mwanzo kazini kwao. Baada ya kundi la kwanza, kundi jingine nalo lilifika baadaye.  Wakati huo, ile mvua ya vile vishanga iliacha kunyesha.
Niliona pia makundi mbalimbali ya watu, wakiwasili kwenye makanisa mbalimbali Jumapili asubuhi. Mvua ile ingeanza kunyesha mara tu watu wa mwanzo wanapoingia kwenye uwanja wa kanisa. Iliendelea kunyesha kwa muda kisha ikasimama. Wale wanaochelewa hawakuti chochote.  
Yesu aliniuliza iwapo nilikuwa naelewa maana ya maono yale, nami nilimwambia kuwa sikuelewa. Ndipo alinifafanulia kwa kusema kwamba: “Maono haya yanamaanisha kuwa kila mahali ambako unatakiwa kuwako kwa muda fulani na wewe unajua ni wakati gani unatakiwa kuwa pale, mara zote huwa kuna malaika wanagawa baraka kwa ajili ya muda huo. Kama ukifika mapema, utapokea baraka zako, lakini ukichelewa, unakosa baraka zako kwa siku ile maana malaika hugawa baraka kwa muda ule tu. Victoria, nataka kukuonya kwa sababu huwa unaenda kazini kwa kuchelewa, na hasa huwa unaenda kanisani kwa kuchelewa. Ni lazima ujue kuwa kwa nyakati zile huwa unachelewa bila kuwa na sababu za msingi; umekuwa ukikosa baraka zako kwa siku zile; hazitakurudia tena.  Victoria, ni lazima uache jambo hili na usilitende tena, isipokuwa pale unapokuwa na sababu ya msingi ya kuchelewa.”  
Bwana alipomaliza kusema maneno yale, kwa kweli nilitamani kutoweka au angalau nimpatie sababu inayokubalika kutokana na kukosa kwangu nidhamu. Nilimwambia kuwa wakati mwingine napitiliza kulala lakini alinitazama moja kwa moja machoni na kusema kuwa nilikuwa nasema uongo na kwamba nilikuwa nina tabia mbaya ya kurudi kitandani baada ya kuwa nimeamka, ili kutimiza ile shauku ya kusema ‘ngoja nilale kidogo tu.’
Baada ya Yesu kuwa amenionya. alisema, “Simama. Tuondoke sasa. Muda unakimbia haraka sana. Kuna mambo ambayo ni lazima tuyafanye.”
Safari hii Bwana alinipeleka mahali ambako sikuwahi kufika kabla. Ilikuwa pia ni mara ya kwanza kufuata barabara tuliyotembea siku ile. Tulifika kwenye bustani iliyojaa maua mazuri na miti mizuri ya kijani. Hakuna kitu duniani kinachoweza kulingana na mahali pale. Maua yalikuwa ya kila aina ya rangi za kung’aa.  Tulikaa kwenye benchi zuri la bustanini, ambalo lilitengenezwa kwa dhahabu safi huku likiwa na nyota ndogo za madini ya fedha ya kung’aa.
Tulipokaa, alionyesha kidole mbele na kusema, “Victoria, tazama, unaweza kuona mji ule? Nilipotazama, niliona jiji kubwa sana. Lilikuwa zuri kuliko maelezo. Jiji lile lilikuwa na geti la dhahabu inayong’aa, na kwenye geti lile kulikuwa na mwanamume amekaa, mwenye umri mkubwa. Alikuwa na ndevu ndefu nyeupe na nywele nyeupe. Nilishamwona mwanamume huyo kabla; na nilipomwuliza Yesu kuwa mwanamume yule ni nani, aliniambia kuwa alikuwa ni Ibrahimu, baba wa imani.
Niliona barabara nyingi kwenye mji ule, ambazo nazo ni za dhahabu. Kuna majengo marefu, ambayo nayo yalikuwa ya dhahabu inayong’aa. Mng’ao wa mji ule hata hauelezeki!
Yesu alinigeukia na kuniuliza, Unawaza nini juu ya jiji lile?”
Nilimjibu kuwa lilikuwa ni zuri sana na nilikuwa natamani kwenda pale. Yesu alisema: “Nitakupeleka pale kama ukiendelea kuwa mtii maana hapo pia ndiko nyumba yako itakakokuwako. Uendelee tu kuwa mtii – maana ukikosa utii, Victoria, kunguru wataruka kwenye nyumba yako. Nyumba yako itakuwa makao ya bundi na viwanja vya kuchezea vya mizimu. Hata hivyo, usiogope, maana mimi niko pamoja nawe. Wewe uwe mtii tu. Kwa kila mmoja ambaye si mtii, nyumba yake itakuwa na kunguru wakiruka pale; itakuwa ni makao ya bundi na mahali pa mizimu pa kuchezea.”
Yesu ni halisi na anatupenda kwa pendo lisiloweza kuelezeka. Shauku yake kubwa ni sisi tuchague uzima na kuishi milele naye. Moyo wake unauma kwa ajili ya wale watu ambao wanakufa na kuenda kuzimu kwa vile tu wanachagua kukataa Wokovu aliowapa na badala yake wanachagua mauti.
Uwe ni Mkristo uliyeokoka au la, tafadhali siku zote kumbuka jambo hili: Muda unakimbia haraka!

Comments