1 Petro 3:7“Kadhalika
ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa AKILI; na kumpa mke heshima, kama
chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima,
kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”
Kwa
asilimia kubwa matatizo yanayotokea katika ndoa chanzo chake ni
mwanaume kutojua kuishi kwa akili na Mke wake. Ni kweli kuna wanawake
wajinga ambao biblia inasema wanavunja nyumba zao kwa mikono yao
wenyewe, pamoja na hayo kama mwanaume ataomba Mungu ampatie Hekima au
akili Ndoa inadumu. Kumbuka kila unalotenda kwa mwenzio linazaa tendo la
kutendewa likiwa baya au jema. Tatizo likitokea katika ndoa, kaeni
chini mtafute chanzo cha tatizo, Mume ana sehemu ya kutumia akili
aliyopewa na Mungu kurudisha mahusiano. Hebu tuangalie baadhi tu ya
mambo anayotakiwa mwanaume kumtendea mkewe:
MUME AMHESHIMU MKE WAKE:
Kuna wanaume wanadharau wake zao, utakuta mke anatukanwa, kupigwa,
anakosolewa mbele ya watoto au hata mbele ya watu kama house girl. Mara
ngapi tunasikia wanaume wakigomba “Mama Fulani chakula gani hiki mbona
ugali haujaiva vizuri?”, lawama hizo mbele za watu au mabinti wa kazi –
ni kumuaibisha mkeo, na kwake ni tatizo kubwa. Mke ni tofauti kabisa na
watoto au wasichana wa kazi, anatakiwa kupewa Heshima, huyo ni mwenzi
wako na mshauri wako. Kufanya Mapenzi na wanawake wengine ni
kumdhalilisha mkeo na kwa sababu mapenzi hayagawanyiki lazima matatizo
yataanza.
MUME AMJALI NA KUONYESHA UPENDO KWA MKE:
Mwanamke ana hisia kali za mahusiano, anabadilika kulingana na
anavyotendewa, wakati mwingine wanakuwa kama watoto, unaweza kumdanganya
hata kwa kitu kidogo ili mradi kiashirie kumpenda. Siku moja jaribu
kununua Pipi, halafu mwambie “sweet” au “Darling” nimekuletea zawadi
kubwa, twende nikakupe chumbani, halafu toa pipi huku ukimtazama usoni,
utashangaa yatayotokea. Onyesha kuwa unamjali, unamthamini, unampenda na
unafurahia ukiwa nae. Hata kama ana kazi yake, Mnunulie nguo rasmi kama
zawadi. Neno Pole Mpenzi, Samahani, Umependeza n.k. yana maana sana kwa
Mwanamke. Mume awe na muda wa kuongea na Mke wake, kushinda kwenye
Mabaa hadi usiku, kuwa busy na TV au Kompyuta muda wa usiku ni tatizo
kwa mwanamke. Wanaume wengi wanacheka na kupiga porojo na wanawake
wengine maofisini, lakini akifika nyumbani utafikiri ameambiwa yuko
mahakamani penye amri ya usipige kelele.
MUME NI KICHWA CHA NYUMBA:
Tangia mwamzo Majukumu ya kutunza familia ni ya Baba, mwanamke ni
msaidizi, siku hizi mambo yamegeuka, akina mama ndio wanaachiwa mizigo
ya kulea familia, Mke akiwa na kazi au biashara ndio usiseme, Nguo za
watoto, chakula, ada n.k. yote anaachiwa Mama. Baba hakikisha unaacha
fedha za kutosha nyumbani, wengi wanapenda chakula kizuri huku wanaacha
fedha za fungu moja la mchicha, na wengine wanakula vizuri wakiwa kazini
– Supu, Biliani, Pilau mbuzi, Juice – familia nyumbani ni maharage
wakibadilisha Mchicha.

Comments