MAOMBI HUSABABISHA NGUVU ZA MUNGU ZIFANYE KAZI

PASTOR AMOS UKANULA KATIKA MAOMBEZI HUKO KANISA LA PAG  CHUKWANI ZANZIBAR
PASTOR BOMBAY KATIKA MAOMBEZI KWENYE VIWANJA NYA KANISA LA FPCT MWAKAJE ZANZIBAR
PASTOR FROLIAN KATUNZI WA EAGT CITY CENTER KATIKA MAOMBEZI HUKO VIWANJA VYA SABASABA DAR ES SALAAM
Maombi husababisha nguvu za Mungu zifanye kazi.
Mambo makubwa sana yanayofanyika hapa duniani Mungu ameyafanya yategemee maombi ya watoto wake, kama ilivyoandikwa katika 1Wafalme:18:36-39 "Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa  Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe  Mungu katika  Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na yakuwa nimefanya mambo yote kwa neno  lako. Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe  umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe , na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema BWANA ndiye Mungu BWANA ndiye Mungu."

Kama Eliya  asingechukua hatua ya kuomba, Mungu asingetenda jambo lolote lakini tunaona maombi ya Eliya yaliweza kumgusa Mungu hata akaweza kuziachilia nguvu zake, (ndipo moto wa BWANA ukashuka) mambo yaliyotendeka ni makubwa sana  na watu wote wakamtukuza Mungu. Na jambo hili limekuwa ukumbusho mbele za Mungu na katika kizazi hiki pia.
 
Katika 2 Wafalme  6:17-18 imeandikwa hivi: "Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA nakusihi, umfumbue macho yake,  apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote. Na walipotelemka Elisha akamwomba BWANA,  akasema, uwapige nakusihi watu hawa kwa upofu akawapiga upofu sawasawa na neno la Elisha."

Elisha aliomba mbele za Mungu na Mungu akatenda. Kwa sababu hiyo waliweza kuwateka maadui zao na kuwafikisha mbele za mfalme wa Israeli pasipo wao kujua. Bila shaka jambo hili lilikuwa kubwa sana ambalo Mungu alilitenda kupitia maombi ya Elisha.
 
Mara kwa mara tunahimizwa  tuombe kwa ajili  kazi ya Mungu, Mungu abadilishe mioyo ya watu waweze kutubu. Sisi sote tunajua kwamba Mungu ana uwezo mkubwa sana. Ni kwa nini basi tunatakiwa tuombe ili Yeye aitimize kazi yake? Swali hili ni gumu hatuwezi kulijibu kama inavyotakiwa. Lakini kwa kifupi ni kwamba huo ni utaratibu wake ambao ameupanga kwamba inatupasa kuomba ili Mungu aweze kutimiza kazi yake.
 
Mungu ameona ni vyema kabisa sisi tushiriki kufanya kazi pamoja na Yeye na hili jambo ni zuri na linapendeza sana kwamba Mungu ametukubali na kututhamini. Na katika jambo hili ni muhimu sisi tuweze kutambua kwamba wokovu wetu umetoka kwa Mungu, na yakwamba sisi tumeupata kwa njia ya neema tu ya Mungu. Hivyo tukumbuke kwamba wapo watu waliofunga na kuomba  kwa ajili yetu na neema hii ya wokovu  ikatufikia. Hivyo basi ni wajibu wetu sisi pia kuomba kwa ajili ya ndugu zetu marafiki zetu, wafanyakazi wenzetu na hata nchi yetu na watu wote Ulimwenguni ili Mungu aweze kuitimiza kazi yake  ya kuwaokoa.
Tunaweza pia kumwomba Mungu kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya watu wengine; wafunguliwe katika vifungo mbalimbali, wamjue Mungu wa kweli, wasamehewe dhambi na kutakaswa na damu ya Yesu, watoke katika laana za aina mbalimbali, waponywe maradhi mbalimbali n.k. Tunapoomba miujiza mbalimbali hutokea. MUNGU awabariki sana

Comments