

Tungeweza kusema kwamba Baraba, mtu mhalifu, aliwekwa huru au aliokolewa katika adhabu ya kifo kwa neema tu! Hakustahili! Kutokana na Yesu kuchukua adhabu hiyo, Baraba akawa huru. Vivyo hivyo, kutokana na Yesu kumpendeza Mungu sikuzote, sisi nasi tunahesabiwa haki ya kuingia mbinguni alikokwenda, kwa imani tu katika Yeye! Kazi njema aliyoifanya Yesu, imetupa kuirithi mbingu aliyokwenda bila sisi kuifanya. Ni kama jinsi ambavyo katika mambo ya dunia, bondia anavyopigana ulingoni kwa shida kubwa, na kisha akishinda na kupewa mamilioni ya fedha; mke wake aliyebaki nyumbani bila kupigana, naye anakuwa milionea! Hii ndiyo Neema! Yesu Kristo, ndiye aliyepigana na Shetani na kumshinda pale alipomjaribu kufanya dhambi, na sisi tunahesabiwa kushinda katika Yeye Yesu, kwa imani tu! Ndiyo maana Biblia inasema katika WAEFESO 2:8-9, “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu (Zawadi ya Mungu), wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”.
Kwa hiyo tunachotakiwa kukifanya, ili tuokolewe, ni rahisi sana. Tunatakiwa kutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha, na kwa imani tu, katika Yesu Kristo, tunahesabiwa mara moja haki ya kuingia mbinguni. Hiyo ndiyo neema ya Kwanza. Aina ya pili ya Neema, ni msaada utokao mbinguni, wa kutuwezesha kufanya mapenzi ya Mungu. Kama tulivyoona, hatuokolewi kutokana na kujitahidi kufanya hili au lile, bali ni kutokana na kazi aliyoifanya Yesu, siyo sisi. Vivyo hivyo, kutokana na upendo wa Mungu, Mungu anajua pia kwamba hatuwezi kufanya mapenzi yake mpaka atupe msaada wa kutuwezesha kufanya hivyo. Biblia inasema katika TITO 2:11-12, “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi na haki, na utauwa (utakatifu), katika ulimwengu huu wa sasa”


Comments