MCHUNGAJI JOSEPHAT GWAJIMA |
Na Mchungaji Josephat Gwajima
Utangulizi:
Biblia imeeleza kuhusu nyota ya
Yesu ilivyoonekana kutoka mashariki,(Mathayo2:1); Hii inadhihirisha wazi
kuwa kila mtu ana nyota yake. Hivyo katika mfulilizo wa somo hili tutaona maana
ya nyota, kazi ya nyota, nyota yaweza kufunikwa kichawi, madhara ya kuishi bila
nyota, dalili za kuchukuliwa nyota, nyota yaweza kurudishwa na namna ya
kutambua nyota yako. Hapa hatuzungumzii kuhusu kusoma nyota au utabiri wa nyota
bali tunaangalia nyota kama ilivyo katika Biblia.
MAANA YA NYOTA:
Nyota katika Biblia inawakilisha
kipawa, hatma ya mtu, lengo lililomfanya Mungu akulete hapa duniani na kusudi lako la maisha. Hivyo
tunaposema nyota yako ipo au imechukuliwa maana yake hayo mambo yamechukuliwa
au yapo. Kimsingi hakuna mtu asiye na maana tangu kuzaliwa kwake, kwasababu
kila mtu aliye duniani amekuja kwa kusudi lake.
Kuna tofauti kati ya elimu na
nyota; elimu sio nyota lakini elimu yaweza kunoa nyota. Na si kwamba kujifunza
kunaleta nyota bali nyota ipo kwa wote lakini elimu inainoa nyota; na ndio maana
ni rahisi kumwona mtu hana elimu lakini anamafanikio mahali fulani. Ukisoma Mhubiri 9:11 Biblia inasema wakati na
bahati huwapata wote na sio swala la elimu au ujuzi tu.
KAZI YA NYOTA:
- Nyota humfanya mtu kuwa mahiri katika utendaji kazi wake. (Effectiveness)
- Nyota huleta ubunifu katika maisha ya kila siku (Creativity)
- Nyota inamfanya mtu anatenda kwa ufanisi (Efficiency)
- Nyota huleta mvuto kwa watu kutoka mbali ili kuleta vitu kwa ajili yako. (Attraction)
- Nyota humfanya mtu awe na maisha yenye mwelekeo na kibali mbele za watu. (Acceptance and Favor)
- Nyota humfanya mtu kusikilizwa katika jamii.
Kuna vitu ambavyo mtu anaweza
kuvipata kwasababu nyota yake imeonekana. Nyota yaweza kuvuta zawadi yaani vile
vitu ambavyo hujavitaabikia, na ndio maana Yesu alipokuwa mdogo aliletewa
zawadi na mamajusi wa mashariki. (Mathayo
2:11) kwahiyo nyota ikichukuliwa maana sahihi ni kwamba hayo mambo hapo juu
yote hayapo.
Mathayo 2:1-2; Wakati Yesu anazaliwa kulikuwa na watu wanaitwa
mamajusi, ambao walikuwa na uwezo wa kusoma nyota. Hivyo katika ulimwengu wa roho
waweza kuona watawala wajao, maisha yajayo au yale yatarajiwayo. Na ndio maana Mamajusi wa mashariki ya mbali
waliweza kuifuata nyota ya Yesu.
Nyota inapoonekana inaweza
kufuatwa, yaani watu waona zile kazi zake na kumfuata mtu. Kimsingi tunaposema
mtu hana nyota maana yake umahiri, ufanisi na kibali vimechukuliwa. Lakini
nyota ikionekana maana yake haya mambo
yote yamerudishwa na hapo utamwona mtu anafanikiwa hata kama elimu yake sio
kubwa.
NYOTA ILIYOCHUKULIWA/ ILIYOFUNIKWA KICHAWI:
Nyota ikifunikwa au kuchukuliwa
kichawi maana yake mvuto, umahiri, ufanisi na uwezo unakuwa umechukuliwa au
umefunikwa. Na ndio maana kuna watu wanahangaika kuanzisha kampuni, kujenga
nyumba, kulima, au kufanya biashara kama nyota imefunikwa au kuchukuliwa
kichawi huwezi kupokea mafanikio ya sahihi kwenye maisha. Watu wengi
wanahangaika kuonekana au kukubalika lakini kumbe tatizo lipo kwenye nyota
yaani imefunikwa au imechukuliwa kichawi.
Wachawi wanaweza kuona nyota ya
mtu na kuifunika ili isionekane; na kwa namna hii watu wengi wanaonekana hawana
mafanikio katika maisha kumbe nyota zao zimefunikwa. Hivyo ni muhimu kupambana
Kwa Jina la Yesu ili nyota yako ionekane.
MADHARA YA KUISHI BILA NYOTA YAKO:
- Kwa kuwa nyota ndiyo inamwezesha mtu kuwa na kila kitu, ndio kusudi la mtu, upendeleo wa mtu; hivyo madhara ya kutokuwa na nyota ni kutokuwa navyo vyote vile.
- Siku zote unakuwa unatenda chini ya kiwango (Under performance). Na kwa namna hiyo hakuna mtu anakubali kile unachotenda; yaani elimu na maarifa yote yakuwa chini ya kiwango.
- Utapata na kuibiwa; unapata kazi baadaye unaibiwa au unapata mchumba baadaye anaibiwa. Kimsingi huwezi kudumu na haya mambo.
- Unapata lakini anatumia mtu mwingine.
DALILI ZA NYOTA ILIYOFUNIKWA:.
- Maisha kukosa mwelekeo; mtu akikosa nyota hata kama akiwa na elimu kama nyota haipo lazima mtu huyo atakosa mwelekeo.
- Kukwama kibiashara na kuishi maisha kwenye madeni.
- Unafanya kazi lakini hupati maendeleo. Yaani mtu anapata mshahara mzuri lakini anakosa mafanikio halisi kwasababu ya nyota iliyofunikwa au kuibiwa.
- Wewe ni kiongozi lakini jamii haikutambui.
- Ukichangia hoja za mijadala mbalimbali hakuna anayekusikiliza.
- Umesoma lakini hupati kazi, na ukipata kazi haiendani na elimu yako
- Maisha ya upweke na hakuna anayekujali katika familia.
- Unatenda kazi kwa bidii lakini hupandi cheo.
- Kama ni binti sifa zote lakini hakuna anayekuchumbia maana huonekani.
- Kuandamwa na mabalaa na mikosi.
- Kupotelewa na watu wa muhimu
NYOTA YAWEZA KURUDISHWA:
Hatua ya kwanza kama hujaokoka unatakiwa kuokoka; kuokoka ni
kumpokea Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako ili upate uwezo wa kushindana,
hivyo ukigundua nyota imechukiliwa unatakiwa umpokee Yesu ndani ya moyo wako.
Ni kitu cha kushangaza kuhitaji msaada wa Yesu halafu yeye humtaki kimsingi
kuokoka ni hatua ya kwanza ya kurudisha nyota.
Hatua ya pili ni kushindana kwa maombi; kama mtu anayetaka kurudisha
nyota yake ni lazima achukue hatua ya
kushindana katika maombi. Hivyo baada ya kuokoka hatua inayofuata ni kushindana
ili nyota irudi. Nyota yaweza kurudishwa kwa kuomba katika Jina la Yesu Kristo.
UTAJUAJE NYOTA YAKO NI IPI:
Usithubutu kwenda kwa mganga wa
kienyeji au kusoma kwenye magazeti ili kujua nyota yako. Ni muhimu kujua kilichoibiwa ni kipi katika
maisha yako. Isaya 47:13 “Umechoka kwa wingi wa mashauri
yako; basi, na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila
mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo yatakayokupata.” FALAKI ni elimu juu ya mambo ya nyota;
biblia inataja kuwa kuna watu wanaojishughulisha na usomaji wa nyota. Lakini kuna
mambo kadhaa yanayoweza kukuonyesha nyota yako ni ipi:-
Moyo wako, akili zako na mawazo yako
yanakuwa katika hilo jambo AMBALO NI NYOTA YAKO. Mfano kama nyota yako ni
biashara basi utakuta moyo wako upo kwenye biashara, basi lazima nyota yako ni
k biashara. Kama nyota ni kuimba au siasa lazima moyo utakupeleka kwenye kuimba
na siasa. Hivyo tambua kuwa kwenye nyota yako ndipo kuna Baraka zako.
Jambo ambalo ni nyota yako utalitenda bila
kupambana; Yaani hutatumia nguvu kwenye kulitekeleza jambo hilo.
Kurudisha nyota Iliyoibiwa:
Baba katika Jina la Yesu,
nimetambua kuwa nyota yangu yaweza kufunikwa na kuibiwa; na leo ninaamua
kuirudisha kwa Jina la Yesu kila nyota yangu iliyoibiwa, nyota ya kukubaliwa, ufanisi,
umahiri, biashara, kazi au nyota ya hatma njema naamuru irudi kwa Jina la Yesu
Kristo. Ninaamuru nyota yangu ikombolewe kwa damu ya Yesu, ninaamuru iachiliwe
katika Jina la Yesu.
Kufunua nyota iliyofunikwa:
Katika Jina kuu la Yesu
ninasafisha nyota yangu iliyofunikwa; nyota ya mafanikio ninaisafisha kwa Jina
la Yesu. Katika torati kila kitu husafishwa kwa Damu nami natumia Damu ya Yesu
kusafisha nyota yangu katika Jina la Yesu. Ninatakasa nyota yangu iliyochafuliwa
katika Jina la Yesu. Ninang’arisha nyota
yangu katika Jina la Yesu.
Kuangamiza wasimamizi wa nyota:
Ninasimama kinyume na kila
mashetani, wachawi na waganga wa kienyeji wanaoshikilia nyota yangu katika Jina
la Yesu. Waliofunika nyota ninawaangamiza katika ulimwengu wa roho,
ninateketeza wote walioiba nyota yangu kwa Jina la Yesu. Katika Jina la Yesu
niharibu kazi na utawala wa mashetani wanaoiba nyota yangu katika Jina La Yesu.
Kukiri ushindi:
Ninatangaza kurudishwa kwa nyota
yangu katika Jina la Yesu; ninatangaza maisha yangu kung’arishwa katika Jina la
Yesu. Mafanikio yangu yamerudi katika Jina la Yesu. Nimeshinda kwa damu ya Yesu.
UFUFUO NA UZIMA (THE GLORY OF CHRIST (T) CHURCH)
Comments