USHINDI KATIKA UJANA






Kijana ni nani?
Kijana ni mtu wa kike au wa kiume mwenye umri kati ya miaka 15 na 45.

Biblia inasema nini juu ya kijana?
Biblia imenena mambo mengi juu ya kijana, na baadhi ya hayo ni kuwa fahari ya kijana ipo katika nguvu zake (Mithali 20:29). Kijana ana nguvu nyingi, neno la Mungu linakaa ndani yake na kisha amemshinda shetani(1Yohana 2:14b).
 
Yohana  anawaandikia vijana akisema wana nguvu nyingi, pili neno la Mungu linakaa ndani yao na kisha wamemshinda shetani. Nguvu yaweza kuwa ya kiroho au ya kimwili, maana zote ni za muhimu na mara nyingine hutegemeana katika utendaji.
Nguvu moja ikikosekana hujitokeza upungufu unaoweza kupelekea uharibifu kama vile mtu kurudi nyuma kwa sababu ya majaribu. Nguvu ya kimwili ya mtu wa Mungu ikitumika kwa mujibu wa uongozi wa Roho Mtakatifu, yaweza kupelekea mtu kuwa na nguvu ya kiroho iletayo ushindi juu ya hila na mitego ya yule mwovu.Hapa ina maana kuwa, kwa mtu wa Mungu ukiwa na nguvu ya kimwili na unaongozwa na Roho wa Mungu utamtumikia Mungu pasipo ulegevu, tofauti na mzee ambaye anaweza kuhitaji kufanya jambo lakini nguvu ya kwenda kufanya hana, hilo nalo Mhubiri aliliona na kumhamasisha kijana kutumika akiwa bado anazo nguvu. Mhubiri12:1 ”Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako kabla hazijaja siku zilizo mbaya…“ Yohana anawaandikia vijana akionyesha sifa za  aina ya vijana aliokuwa akiwalenga. Anatazamia kwamba kijana akiitumia nguvu hiyo kama ilivyokusudiwa na Mungu, na kulisoma neno, kuomba kwa bidii zake zote, matokeo yake atakuwa na hazina tele ya neno ndani mwake, na kisha atamshinda shetani, maana anazo  nguvu za kiroho na za kimwili. Kijana wa aina hii hana hofu maana hata shetani akija kwa sura gani au akitumia mazingira gani, haogopi maana silaha alizo nazo (Neno) ni tishio kwa adui. Mungu anawatafuta vijana kama hao wabebao silaha hiyo ya Bwana , nyakati zote, kila mahali na kwa bidii.  ”..Nimewaandikia ninyi vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu  linakaa ndani  yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu“(I Yohana 2:14b).

Biblia inasema kijana akilitii Neno la Mungu na kulifuata litasafisha njia yake. Litamkamilisha kwa kiwango anachotaka Mungu, kwa makusudi ya Mungu na kwa utukufu wa Mungu. Kwahiyo ili  kijana aweze kuishi maisha matakatifu, yenye ushindi tele na yanayomtukuza Mungu yampasa kuisafisha njia yake kwa kutii, akilifuata neno la Mungu. Zab.119.9 ”Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.“

Kijana, kufanikiwa kuisafisha njia yako kutategemeana na wewe mwenyewe utakavyotumia nguvu zako. Yakupasa kuelekeza nguvu zako katika maombi, kujisomea Neno la Mungu, hii ni pamoja na kulitafakari na kulitendea kazi. Kwa kufanya hivyo utapata nafasi nzuri ya kumsikiliza Mungu na kujua ni nini mpango na makusudi yake kwako. Kijana hupaswi kulala usingizi tangu jioni hadi asubuhi na tangu January hadi Desemba, huo ni msiba wa kutosha kwa kijana maana Biblia inasema mtu wa aina hiyo atapata umaskini wa kumtosha. Si vema kijana kuzagaa, ukikutwa na adui ukiwa umezagaa atakutumikisha katika matakwa yake. Ni muhimu sana kijana kuwa na mikakati na kuiombea ili kupata uongozi wa Roho Mtakatifu. Mungu anajali sana kijana kuwa na mkakati. Mfano mzuri ni namna alivyomwandaa Yoshua kushika nafasi ya Musa. Awali ya yote alimhakikishia uwepo wake pamoja na kijana huyo,  na akamwahidi kutomwacha wala kumpungukia kabisa: ”Hapatakuwa mtu yeyote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote  za maisha yako…sitakupungukia wala sitakuacha.“ (Yoshua 1. 5).

Hapa Mungu anamhakikishia Yoshua kuwa, hata kutokee tatizo kubwa kiasi gani, hata vitisho viwe vikubwa namna gani, hata ainuke nani, asingeweza kuzuia wala kukwamisha kusudi la Mungu katika huduma aliyokuwa anakabidhiwa na Mungu, ya kuwafikisha Waisraeli nchi ya Kanaani. Hali kadhalika wewe kijana, yumkini bado unawategemea wazazi au ndugu, lakini kwakuwa umeokoka labda wamekutenga, hawataki kukupa huduma, hata masomoni unatishiwa kufukuzwa kwasababu huna karo; yumkini umeoa au umeolewa na huyo mume au mkeo anakutesa kwa ajili ya wokovu; kazini unanyanyaswa  na mkubwa wako wa kazi au wafanyakazi wenzio, halikadhalika kwenye biashara zako wanakutesa kwa njia mbalimbali. Katika hali yoyote ile, jambo la muhimu uwe na uhakika kwamba Mungu yupo pamoja na wewe na kwamba hatakuacha wala hatakupungukia. Hivyo usikate tamaa, azimia kutomwacha Mungu kabisa, simama katika haki na ahadi za Mungu, utaona ushindi mkubwa.

Baada ya Mungu kutoa uhakika juu ya uwepo wake kwa kijana huyo Yoshua, alimpa mikakati ya namna atakavyoweza kufikia lengo ambalo lilikuwa kuwafikisha Waisraeli katika nchi ya ahadi, Kanaani. Mikakati hiyo ni kama ifuatavyo:

1. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi….
Mungu hapendezwi na uvivu, alitaka Yoshua awe hodari tu na ushujaa mwingi na siyo mtu wa kujihurumia hurumia bali awe mwepesi wa kwenda anakotakiwa, kutekeleza majukumu ambayo Mungu angempa inavyotakiwa, kwa wakati unaotakiwa, na pasipo hofu. Huo ndiyo ushujaa.
 
2. ...uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa  kuume au wa kushoto.(Yosh. 1.7). 

Mungu anamwambia Yoshua, aangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuwa ameamriwa na Musa mtumishi wake Mungu. Swala kuu hapa ni utii wa neno la Mungu. Kwamba kijana hatarajiwi kuwa msikilizaji tu wa Neno la Mungu na kuendelea na maisha ya kidunia. Kijana anahitajika kuwa msikiaji na mtendaji/mtekelezaji wa maagizo ya Mungu ndani ya Neno.

Mungu anasisitiza katika mstari wa nane kuhusu kutafakari Neno. Mungu alimtaka Yoshua, kuhakikisha siku zote za maisha yake anafanya Neno la Mungu kuwa sehemu ya maisha yake. Alimtaka akiwaza awaze (atafakari) Neno mchana na usiku, maongezi yake yawe na msingi katika Neno. Kuhusu kutendea kazi Neno, Mungu alimwambia Yoshua aangalie kutenda sawasawa na maneno yote  yaliyoandikwa humo (ndani ya torati/Neno.

”Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo…."(Yoshua 1:8).

Kwa maana hiyo, iwe usiku iwe mchana kijana saa zote unatakiwa kutafakari neno la Mungu siyo kuwaza shida, taabu na masumbufu ya dunia hii. Kulitafakari Neno huja baada ya kulisoma, Daudi alisema: ”Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,  nisije nikakutenda dhambi“ (Zab. 119.11).

Alilisoma na kisha akalihifadhi moyoni. Neno hilo katika hazina ya moyoni, likawa mshauri, mwongozo na faraja  wakati wa majaribu, mapito au mateso. Na kwa kulitamka likafanyika fimbo ya kumwangamiza adui, na kufungua milango ya baraka iliyofungwa na adui na pia likatumika hata kubadilisha mazingira kama Ezekia alivyotamka uhai kwa mifupa, ikainuka ikiwa hai na kuwa kikundi kikubwa cha watu.

Ili uwe na maisha yenye mwelekeo wa ki-Mungu na ya mfano, epuka kabisa kuwaza mambo mapotofu, epuka mazungumzo mafu yasiyo na uhai wa ki-Mungu maana yatakuharibu wewe pamoja na wakusikilizao, pia matendo yoyote yaliyo kinyume na Neno la Mungu epukana nayo. Mungu alijua kuwa kijana huyu Yoshua asiposisitiziwa na Mungu mwenyewe, asipoishi kwa Neno ambalo ndiyo lishe bora ya roho yake, angeharibikiwa, na hapo kusudi la Mungu la ukombozi wa wana wa Israel lingeyumba. Hali kadhalika wewe usipoishi kwa kulitii Neno na kufanya kama linavyokuagiza, adui atayumbisha mpango wa Mungu katika maisha yako, matokeo yake ni kuchanganyikiwa, kukata tamaa na hata kufa kabisa kiroho. Lakini ukisimama pasipo kujali mazingira yanayokuzunguuka, Mungu anao mpango mzuri sana na maisha yako na ndiyo maana amekuokoa (amekuita). Yumkini wewe ndiye wa kwanza kumpa Yesu maisha yako katika familia au ukoo wako. Mungu anategemea kukutumia wewe kulifikisha kundi hilo nchi ya ahadi kama alivyomtumia Yoshua. Zoezi hilo litafanikiwa iwapo utakuwa hodari tu na mwenye ushujaa mwingi, na kutenda sawasawa na Neno kama linavyoletwa kwako na Roho Mtakatifu mwenyewe kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujumbe huu unaousoma sasa.MUNGU akubariki sana

Comments