BARAKA NI NGUVU YA MUNGU YA UWEZESHAJI KATIKA MAISHA YA MTU.

BARAKA
Baraka ni nguvu ya Mungu ya uwezeshaji wa Mungu katika maisha ya mtu. Kweli sisi tuliookoka tunaposema habari ya baraka tunakuwa tunasema habari ya Mungu kuachilia nguvu au uwezeshaji ndani ya maisha yetu. Kumbukumbu la Torati 8:18 ”Bali wewe utamkumbuka Bwana Mungu wako maana yeye ndiye akupaye nguvu  ya kupata utajiri.“ Katika eneo hili neno nguvu lina maana ya:
-ufahamu
-maono
-kibali
-uvumilivu
-bidii pamoja na mambo mengine ambayo yatakufanya wewe kupanda juu kwa haraka ambayo Mungu ameikusudia.

Kila mtu aliyeokoka anatakiwa kuwa na nguvu hii kusudi aweze kufanikiwa katika maisha yake. Panapokuwepo hii nguvu, maisha ya mtu aliyeokoka katika hali yeyote lazima yatabadilika na kuwa mazuri zaidi ya yalivyokuwa mwanzo. Hivyo kila mtu aliyeokoka yampasa kuitafuta na kuhakikisha nguvu hii ipo kwake.

MFANO WA NGUVU (BARAKA)
  • Yusufu alikuwa mtoto mdogo miaka 17 tu
  • Alikuwa anafanya kazi ndogondogo za nyumbani,
  • Alipenda kukaa na wazazi wake
  • Yusufu alimcha Bwana naye alichukia dhambi na ndio maana alipendwa na Mungu. (Mwanzo sura 39). Ndugu zake Yusufu walimchukia sana Yusufu, nao wakamuuza, naye akaenda kuwa mtumwa.

YUSUFU  KAMA  MTUMWA
Katika hali ya kawaida Yusufu alikuwa kama watumwa wengine tu, lakini kwa Yusufu ilikuwepo nguvu ya Mungu (uwezeshwaji wa Mungu). Mstari wa 2 ”Bwana akawa pamoja na Yusufu“ Uweza wa Bwana wa kustawisha ulikuwa pamoja na Yusufu.

KAZI YA UWEZA HUU
Nguvu hii huleta ustadi wa kazi
Yusufu alipewa ustadi wa kazi, wakati wowote Yusufu alipopewa kazi aliifanya kama bwana wake (Potifa) alivyotaka, na hivyo kuufurahisha moyo wa bwana wake (Potifa). Mwanzo 39:3”bwana wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye ,na ya kuwa Bwana anafanikisha mambo yote mkononi mwake.“ Nguvu hii ni ya muhimu sana katika maisha yetu. Nguvu hii ni ya muhimu katika biashara zetu na kazi za aina yoyote.Tutakapoweza kufanya kazi au biashara kwa ustadi, na kwa akili ya KIMUNGU, basi jua mafanikio ni makubwa sana.

Nguvu hii huleta kibali.
Mwanzo 39:4. ”Yusufu akaona neema machoni pake akamtumikia“ Kibali ni jambo muhimu sana kwetu sisi ikiwa ni kazini ama kwenye biashara, maana watu wakitupenda ndivyo watakavyokuja kwa wingi kwenye biashara zetu, na mabosi wetu watatuwazia mema wakati wote. Tutakapoingia sehemu yeyote na kusema neno au tendo basi tutaonekana sisi kwanza

Nguvu hii huleta bidii
Tunaona Yusufu alivyofanya na kumaliza kila kazi aliyokuwa amepangiwa na hivyo bosi wake kuona ampe majukumu makubwa zaidi. Kama Yusufu angekuwa stadi na ana kibali lakini kazi zinalala, bwana wake asingempa majukumu makubwa.

Nguvu hii huleta uvumilivu
Wote tunafahamu maisha ya mtumwa, hutumwa hovyo, hupewa kazi nyingi, tena ngumu, lakini Yusufu alivumilia akachapa kazi na watu wale wakashangaa. Pamoja na mengine mengi nguvu ya Bwana ilimfanya Yusufu kuonekana si mtu wa kawaida katika nyumba ya Potifa.

Nguvu hii huatamia yale ambayo tunayafanya,
Mstari wa 5 ”…mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba na katika shamba.“ Kusudi uweze kufanikiwa unatakiwa kuwa na nguvu hii juu yako.Mungu wa Yusufu ndiye Mungu wetu; kama alivyokuwa na Yusufu ndivyo atakavyokuwa na sisi pia. Jambo la kukumbuka: palipo na mbaraka huu haijalishi wewe ni wa namna gani. Katika sehemu zote mbili alizopitia Yusufu, ya utumwa na ufungwa utaona mwisho wa Yusufu ni juu sana.

Hali uliyo nayo isikufanye kukata tamaa bali tafuta mbaraka wa Bwana uwe maishani mwako. Kutokusoma, kutokuwa na mtaji, kutokuwa na refa, sio sababu ya kukufanya wewe kutokufanikiwa maana wewe ni mtu ambaye unawezeshwa na NGUVU maalum ya Mungu katika maisha yako. Nguvu hii tunaiona tena katika maisha ya Yakobo nyumbani kwa Labani, Mwanzo 30:25-43

Yakobo hakuwa na mahari ya kukomboa wake zake na watoto wake kusudi aweze kwenda kuishi mwenyewe, hivyo aliamua kufanya kazi nyumbani kwa mkwe wake Labani. Lakini tunaona wazi tangu mwanzo wakati Yakobo amefika kwa Labani. Labani hakuwa tajiri kama baada ya  kukaa na Yakobo. Utajiri wa Labani ulipatikana baada ya mtu mwenye nguvu ya Baraka ya Mungu  kushika mali zake. Mstari wa 27, ”…maana nimetambua ya kwamba Bwana amenibariki kwa ajili yako“
Mstari wa 30. ”Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja…Bwana akakubariki kila nilikokwenda“

Mtu wa Mungu ambaye nguvu ya Mungu  ya ongezeko imo ndani yake anapofanya jambo lazima hilo jambo lifanikiwe sana. Baada ya Yakobo kuwa na wanyama wake na Labani kuwa na wanyama wake, nguvu ya Baraka  ya  ongezeko ilikuwa juu ya wanyama wa Yakobo, hivyo basi Yakobo aliongezeka sana mpaka ukoo wa Labani ukaanza kumuonea wivu. Mwanzo 30:43, ”Kwahiyo mtu huyo akazidi mno akawa na wanyama wengi na wajakazi na watumwa na ngamia na punda.“ Mungu wa Yakobo ndiye Mungu wetu.

Yesu anapofundisha habari ya nguvu hii anasema. ”…msisumbuke basi mkisema,
(1)Tule nini, (2)Tunywe nini, (3)Tuvae nini?“ (Mathato 6:24-33). Mstari wa 35, Maana watu wasio na Mungu, wasio na nguvu hii ya baraka kutoka kwa Mungu hao ndio wanaosumbuka. Lakini sisi Baba yetu wa mbinguni anajua kuwa tunataka hayo naye ataleta nguvu hiyo ya kutuwezesha ili kutufanya tuwe nayo yote tunayoyahitaji. Mstari wa 33. Hivyo basi utafuteni kwanza ufalme wa Mungu  na hiyo nguvu  na yote yatakuja.

Mwandishi wa Zaburi anasema katika Zaburi 1:1-3:
Heri, amebarikiwa, amepewa nguvu, atafanikiwa mtu yule, aitendaye sheria ya Bwana. Mstari wa 3, kila alitendalo litafanikiwa.

Wapendwa yatupasa kwanza kuitafuta hiyo nguvu ndipo tutakapoona mambo makubwa na ya ajabu yakitendeka maishani mwetu. Wana wa Mungu yatupasa kuelewa kuwa (BARAKA) nguvu hii ya kutuwezesha ni roho kamili toka kwa Mungu kama tunavyoona Mungu mwenyewe anamwambia Musa katika kitabu cha Kutoka 31:3 - 4 Nimejaza Roho ya Mungu ndani yake. Roho hii ya Mungu ambayo Mungu ameweka au anaweka ndani yetu inaleta mambo yafuatayo
-  Hekima
-  Maarifa
-  Ujuzi wa mambo ya kazi za kila aina

Kutoka 35:31–35. Naye amejaza Roho ya Mungu katika
-  Hekima
-   Akili
-  Ujuzi
-  Kazi za ustadi
-  Kuvumbua kazi za werevu
-  Amejazwa akili za moyoni.

Roho hii itakapokuwapo juu yako nataka kukwambia huwezi kuwa masikini lazima neno la Mungu litimie kwako lile linalosema ”Na watu wote watakuita mbarikiwa“ Nguvu hii au Roho hii kamili toka kwa Bwana  haitolewi kwa upendeleo bali ni kwa kila mtu aliyeokoka na kukubali kutembea katika njia za Bwana. Kumbukumbu la Torati 28:1-2 Bwana anaweka msimamo jinsi ya kupokea nguvu hii ya muhimu kwenye maisha yetu; anasema ”Itakuwa utakapoisikia sauti ya Bwna, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kufanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana Mungu wako atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya dunia na Baraka hizi zote zitakujilia na kukupata“
 
Hebu tutazame mambo yafuatayo:
1.     Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana Mungu wako
2.     Kwa bidii
3.     Kutunza kufanya maagizo yake yote
 
Matokeo:
Ndipo baraka (Nguvu) hizi zote zitakujilia na kukupata Isaya 1 :19 ”Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi.“ Warumi 2:10 ”Bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema…“
(Mambo ya Walawi 26:3 – 13, Kumbukumbu la Torati 8:12 – 15). Pamoja na maandiko mengine mengi utaona ya kuwa siri kubwa ya kupata mbaraka au nguvu hii ni kutenda sheria ya Bwana. Hapo juu tumeona  mambo matatu muhimu ambayo Mungu anataka kwetu.
  1. Kusikia sauti ya Bwana, kinyume sana na tulivyozoea watu wengi tunapokuwa na pilika ya kutafuta pesa tuna kosa muda wa kuja kanisani kwenye mafundisho na hata tukirudi nyumbani tumechoka hatuwezi kusoma Neno. Lakini kumbe kama tunataka kuendelea yatupasa kujitahidi sana kusoma Neno na kuhudhuria mafundisho. Ndani ya Neno utaona wazi wazi yale ambayo Mungu anataka tufanye na yale ambayo Mungu hataki tufanye.
  2. Kwa bidii, tunaona tena wazi pale ambapo tunatafuta pesa, watu wengi tunaweka bidii sana kwenye pesa , lakini sharti la Bwana linasema tulitafute Neno kwa bidii sana.
  3. Kutenda sawasawa, tunapaswa kutenda sawaswa na yale ambayo Mungu ametuagiza kutenda

Tutakapokuwa tumefanya mambo hayo tutaona wazi wazi nguvu ya Bwana ya mbaraka ikiwa juu yetu .

Maombi.
Hatuwezi kuwa na kiu  na bidii ya kusoma Neno pamoja na kutenda sawasawa kama tutakuwa sio waombaji. Maombi ndio njia pekee ya kutupatia nguvu za kuweza kuyatenda hayo. Kwa kifupi kabisa niseme hivi nguvu ya Mungu ndani ya maisha yetu italetwa na mambo makuu matatu
-  Kusoma neno kwa bidii
-  Kutenda sawa sawa na neno
-  Kuomba kwa bidii

Baada ya kuona mambo ambayo yatatupata tutakapokuwa chini ya laana ama tutakapokuwa chini ya mbaraka wa Mungu tutazame sasa neno MTAJI.

Comments