WATU WENGI WANATEMBEA CHINI YA LAANA

Mara nyingi wapendwa tunaposoma habari ya laana tunaichukulia kama jambo jepesi na kuona kuwa laana hizi ni kama hazipo ama hazitupati na ndio maana watu tunaendelea kucheza na mambo ya Mungu. Lakini leo nataka kukuonyesha kuwa laana hizi zipo na zinaonekana wazi wazi  katika maisha yetu. Mambo mengine yanaonekana kama ya kawaida katika maisha yetu lakini kimsingi mambo hayo  hayatakiwi kuwapata watu wa Mungu. Hebu sasa tuangalie baadhi ya laana ambazo Mungu amesema. Nabii Hagai anaanza kwa kusema, ”Basi sasa Bwana wa majeshi asema hivi, zitafakarini njia zenu“ (Hagai 1:5) Maana mambo haya yanatokea kwenu; soma mstari wa 6.

Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa lakini hamjazwi na vinywaji. Hii ni hali ya kutotosheka na chakula maana unakuta mtu anakunywa na kula lakini baada ya masaa kadhaa anakula na kunywa tena.

Jambo hili linaharibu bajeti yake kwa kujikuta ametumia hela nyingi kwenye chakula bila sababu ya maana. Bwana anao uweza wa kuondoa hiyo nguvu ya tamaa ya kula na kunywakunywa ovyo na kukufanya utosheke na chakula kidogo na cha kawaida.
 
Mnajivika lakini hampati joto. Hii ni tamaa ya mavazi. Mtu anajikuta hataki nguo au mtindo wa mavazi umpite japo hata kama uwezo wa kufanya hivyo hana. Sisemi kwamba kuvaa ni vibaya lakini lazima tuwe na kiasi na hasa wakati ambapo kipato chetu hakijafikia hatua ya kwenda na fashion.Watu wengi bajeti zetu zimeathiriwa na tamaa ya mavazi.

Yeye apataye mshahara anaweka katika mifuko iliyotoboka toboka. Hii ndio mbaya kuliko zote maana kuna wakati mtu unafanya kazi na kupata mapato yako lakini baada ya siku mbili tatu pesa yote imekwisha na wala ulichofanya cha maana hakionekani na wakati mwingine ni rahisi kuona kuwa labda mtu amekuibia.

Mlitazamia vingi vikatoka vichache, tena mlipovileta nyumbani vikapeperushwa. Kuna wakati mwingi tunafanya kazi na pengine ngumu sana tukitazamia kupata kipato kikubwa lakini matokeo yake yanakuwa madogo. Pengine tunafanya biashara lakini faida inatoka kidogo sana. Pengine tunafanya kazi kwa bidii lakini mabosi wetu ndio kwanza wanatudharau.

Mbingu zimezuiliwa zisitoe umande na nchi isitoe matunda. Hii inatokea pale ambapo nguvu ya Bwana ya mbaraka inapokuwa haipo juu yako. Hivyo hata kama utafanya biashara yaani utapanda mbegu (Mtaji) hutafanikiwa.

Kumbukumbu la Torati 28:15 – 68
  • Mstari wa 21 – 22: Bwana atakuambatanisha na tauni
  • Mstari wa 23: Mbingu zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma
  • Mstari wa 24: Bwana atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na mchanga
  • Mstari wa 28: Bwana atakupiga kwa:
  1. Wazimu
  2. Upofu
  3. Bumbuwazi la moyo
  4. Utakwenda kwa kupapasa papasa
  5. Hutafanikiwa katika njia zako
  6. Utaonewa na kutekwa nyara
     
  • Mstari wa 32: Wanao na binti zako watapewa taifa jingine
  • Na macho yako yataangalia na kuzimia kwa kutamani mchana kutwa
  • Hapatakuwa na kitu katika uwezo wako
  • Mstari wa 33 Matunda ya nchi yako na taabu yako yote vitaliwa na taifa usilolijua
  • Mstari wa 37 – 40 Wewe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau kati ya mataifa, mbegu nyingi utapanda shambani lakini utavuna haba kwa kuwa nzige watazila.
     
  • Mstari wa 43 Mgeni aliye katika nchi yako atazidi kupaa na wewe kushuka
  • Mstari wa 44 Yeye atakuwa kichwa na wewe mkia
  • Mstari wa 48
  • Mstari wa 49 - 51 Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai, taifa usilolifahamu ulimi wake, taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana. Naye atakula uzao wa ngombe zako uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa, wala hatakuachia nafaka ,wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ngombe wako, wala mwana kondoo wako mpaka utakapokwisha kuangamizwa
Yeremia 5:1– 9
Hebu sasa tuangalie maisha ya wapendwa wengi makanisani mwetu. Watu wengi ndani ya makanisa ya watu tuliookoka tumetembea chini ya laana hizi kwani ni kweli kwamba wapendwa wengi maisha yetu kwa ujumla wetu ni duni sana. Laana ambayo imesemwa katika Kumbukumbu la Torati 28:28 ndio hasa imetawala ndani ya watu wa Mungu. Wengi tumepigwa na upofu hatuoni chochote cha kutuendeleza katika maisha yetu. Wakati watu wa mataifa wanaona mambo makubwa, wanavumbua miradi mikubwa, watu waliookoka kwa sababu ya kutokwenda sawasawa tumejikuta kuwa hatuoni chochote kile. Kwa ujumla, wapendwa, laana hizi zipo na zinatembea ndani ya watu wa Mungu. Yatupasa kuamua kama alivyosema Joshua: Hakuna jinsi ya kupona, njia pekee ni kujisalimisha kwa Bwana Mungu wetu.

Comments