NAMNA PASAKA ILIVYO {2}

 Na Mtumishi Gasper Madumla
SOMO : NAMNA PASAKA ILIVYO * Sehemu ya pili * Haleluya….

Jina la Bwana Yesu lisifiwe…
Karibu katika sehemu ya pili ya somo hili linalokujia kwa wakati na muda sahihi ndani ya kipindi hiki cha sikukuu ya PASAKA.
Lengo langu kwako ni kutaka kukufundisha namna sikukuu hii iweje.Maana Dunia ya leo imejaribu kuipindua maana halisi ya sikukuu hii.
Kwa upande wa Dunia,hiyo ni sehemu ndogo tu,kwani mbaya zaidi ni pale maana potofu ya sikukuu hii ya PASAKA ilivyoingia hata makanisani .
Leo utafaidi mengi wewe mpendwa usomaye ujumbe huu ikiwa kama utafungua moyo wako kupokea mafundisho haya mahali hapa.

PASAKA NI NINI ?

Swali hili nilikuuliza na nikakujibu vizuri sana katika sehemu ya iliyopita. Lakini leo nijibu tena ;

JIBU :* jibu la kwanza *
Pasaka ni sikukuu iliyoamriwa na Mungu kwamba Wayahudi waihadhimishe sikukuu hiyo kila mwaka mara moja katika mwezi wa ABIBU au mwezi wa NISANI.
Mwezi wa ABIBU ulifanyika kuwa ni mwezi wa kwanza kwao Waisraeli ( Kutoka 12 : 1-2)
Hivyo kupitia mwezi huo,Bwana Mungu alifuta miaka yote ya wana wa Israeli waliyokuwa wameishi Misri.
Hivyo sikukuu hii ilikuwa ni ya kukumbuka siku hiyo ambayo Bwana Mungu aliyatoa majeshi ya Israeli nchini Misri.
Tunasoma :
Kutoka 12 :14 ;
“NA SIKU HII ITAKUWA UKUMBUSHO KWENU, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele”
Tazama hapo namna BWANA MUNGU akisisitiza juu ya kukumbukwa kwa sikukuu hiyo kwa amri ya milele.
Tunasoma pia
;Kumbukumbu 16 : 1-2 ;
“Utunze mwezi wa Abibu, ukamfanyie pasaka Bwana, Mungu wako, kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa Abibu alipokutoa Misri usiku Bwana; Mungu wako.
Nawe umchinjie pasaka Bwana, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng'ombe, mahali atakapochagua Bwana apakalishe jina lake. ”

JIBU:* Jibu la pili *

Pasaka ni KUPITA JUU (Passing over…)
Mungu alipowaokoa Waisraeli, alipita juu yao baada ya kuona DAMU katika miimo. Damu ilikuwa ni ishara kwao kwamba Mungu apitapo juu yao asiwaguse.
Tunasoma ;
Kutoka 12 : 13;
“ Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, NITAPITA JUU YENU , lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. ”
Pia tunasoma Kutoka : 12 : 27 ;
“ Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya Bwana, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia. ”
Tazama maandiko hayo vizuri,utagundua kwamba BWANA MUNGU alipopita juu yao (Juu ya Wana wa Israeli) ilikuwa kwamba wasipatwe na madhara pale BWANA alipoachilia mauaji kwa wazaliwa wa kwanza wa Misri.

Ikumbukwe kuwa :
Wazaliwa wa kwanza wana nguvu na hazina za pekee wanazoshikiria katika familia.
Na siri hii Wamisri walikuwa wanaijua,na ndio maana wao walikuwa wanawatoa wazaliwa wao wa kwanza kama malimbuko,au kama sadaka kwa ajili ya kupata mafanikio
( Tazama hata siku hizi,Baadhi ya watu wajinga wanaotaka kufanikiwa maisha katika hali ya kiujanja ujanja,utakuta wanawatoa wazaliwa wao wa kwanza kwa kuwaua au kuwavuluga akili zao )
Katika agano la kale palikuwa na sikukuu za namna nyingi tu,mbali na sikukuu hii ya PASAKA,Mfano ;

• Sikukuu ya Vibanda
• Sikukuu ya Pentekoste.n.k
SASA NI NAMNA GANI PASAKA INAPASWA KUWA.
Sehemu hii ndio kiini cha somo hili.
Tuliona kuwa pasaka ya kale,ilikuwa ikiadhimishwa kila mwaka mara moja. Swali langu kwako,
Je na wewe mpendwa unahadhimisha PASAKA mara moja kwa mwaka ?
Labda nikuambie kuwa PASAKA haisherekewi hivyo,kwamba mara moja kwa mwaka.
Sasa fuatana nami ili unielewe vizuri.
Hapo mwanzo katika agano la kale,walikuwa wakikumbuka kila mwaka mara moja namna Waisraeli walivyotolewa kule Misri.Katika mwezi wa ABIBU,
ilihitajika damu ya mwana-kondoo imwagike,kwamba kwa damu hiyo ilikuwa ni ISHARA kwa Israel.
IKUBUKWE HII ;
Waisrael walihitaji damu kwa ajili ya kuondoa dhambi zao kwamba Mungu asizikumbuke,Lakini ilikuwa baada ya mwaka kupita,MUNGU alizikumbuka tena dhambi zao.
Tunasoma
Waebrania 10 : 3-4;
“ Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka.
Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. ” Baada ya watu kushindwa kulishika agano la kale,maana walilivunja,Ndipo sasa tunaona Mungu akilifanya agano jipya
Yeremia 31:31-32 :
“Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.”
Hivyo ikaitajika YESU awe PASAKA, damu yake iwe ukombozi wetu sisi tuliokuwa dhambini.
Nami ninasema hivi kila siku ;
Kwamba hakuna wokovu nje ya damu ya BWANA YESU KRISTO.Yaani kama isingelikuwapo msalaba ( kwamba haupo,)Basi ukristo wetu ungelikuwa ni bure kabisa,tena tungekuwa tunaendelea kugandamizwa na mapepo na majini mpaka leo,Likini Yesu akafanyika mwanakondoo.
Tunasoma : Yoh.1 :29 :
“Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! ”
Pia Yoh.1 : 36 :
“ Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! ”
Haleluya…
Jina la Bwana libarikiwe…
Hivyo ,BWANA YESU ni mwanakondoo asiyekuwa na ila. Ambaye kwa damu yake sisi tumekombolewa .
1 Petro 1: 18-19 :
“ Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;
bali kwa damu ya thamani, kama ya MWANA-KONDOO ASIYE NA ILA ,ASIYE NA WAA,YAANI,YA KRISTO. ''
Okey;
PASAKA ya agano la kale iliadhimishwa mara moja kila mwaka,Bali PASAKA yetu sisi wapendwa ni ya kila siku,kukumbuka kusamehewa kwa dhambi zetu.Wayahudi walipofanya PASAKA kila mwaka ( Kutoka 12 : 14)
Sisi tunaifanya kila siku ya kwanza ya juma
Mathayo 26 : 26-28:
“ Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu
Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;
kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. ”
Hivyo namna ya PASAKA ilivyo ni ukumbusho wa kusamehewa kwa dhambi zetu ambapo twaweza kukumbuka kila siku ya Bwana tusalipo,au kila siku .
Maana Wayahudi walikuwa wakiadhimisha kwa kukumbuka siku ambayo walikombolewa nchini Misri
Bali sisi twakumbuka ule MSAMAHA tulioupata pale msalabani kwa njia ya PASAKA wetu ambaye ni KRISTO (1 Korintho 7 :7 )

ITAENDELEA…
UBARIKIWE.

Comments