Naitwa Mzee Simon Lukumay nina miaka 62 na kwa hapa dar es salaam nakaa Sinza Palestina, ni fundi ujenzi na nipo hapa tangu 2006. Mwaka 2001 nikiwa ngalenaro nyumbani Arusha niliamua kutembea kwa miguu kwenda maeneo ya karibu na mjini, na ilikuwa saa 2 usiku na kilichokuwa kinanipeleka huko ni kwenda kuonana na bosi mmoja ili siku inayofuata nianze kujenga nyumba yake iliyokuwa imetengenezwa tayari ila ilibaki kumaliziwa tu. Nikiwa njiani kwenye barabara ya lami, maana niliamua kunyoosha barabara nikidhani ni eneo salama, nikiwa naendelea na safari huku napiga mluzi huku sina wasiwasi wowote nilishangaa kuona watu vijana kama 20 wakiwa wamevaa makoti makubwa na hata sikujua walikuwa wamebeba nini wakanizunguka harakaharaka na kunisimamisha, baada ya kusimama waliparaza silaha ya vyuma ambazo baadae nilikuja kugundua zilikuwa ni mapanga na , mundu na sululu na katika kuparaza huko kwenye lami moto mkubwa ulitoka kila sehemu maana walikua wamenizingira na hali hiyo ilinitisha sana maana nilikuwa sijui kama panga ukiiparaza kwenye barabara ya lami zinaweza kutokea cheche za moto na moto kiasi hicho, hali hiyo ilinitisha sana na hofu nyingi sana ilinijia na hakika nilijua sitapona maana maeneo hayo pia kwa ujambazi yanafahamika kwa miaka hiyo ya nyuma, na kwa tukio la watu 20 kuparaza kwa pamoja vyuma vyao kwenye lami ulitoka moto mwingi sana. Baada ya kuparaza waliniuliza mimi ni nani na mimi bila kujua wala kudhamiria nilijikuta nasema kuwa mimi ni mwanausalama, nadhani woga na hofu ulisababisha nilopoke kuwa mimi ni mwanausalama ili waniache, na baada ya hapo waliniuliza kuwa mimi ni mwanausalama gani? Mwanajeshi, polisi au askari magereza?, sikuwa na jibu na wakasema lazima waniue kwa sababu mimi ni mwanausalama na wakiniacha wamekwisha wao na pia kuna wenzao wawili wamefungwa baada ya kukamatwa na polisi. Niliganda tu huku natetemeka maana nimejiita askari na kuongeza tatizo badala ya kupunguza, mmoja kati yao alinisogelea huku wengine wamenizingira na kusema afande umekwisha na kuniambia niangalie juu nisali sala yangu ya mwisho, nilipoangalia tu juu alinichapa kwa nguvu na ngozi ya kifari maana fimbo zao zilikuwa ni mikia ya wanyama na ngozi za wanyama waliozikata na kuwa kama fimbo inayojikunja mfano wa zile fimbo za wanaolimisha kwa jembe la ng’ombe au pilau, aliponichapa tu mara moja ile fimbo ya ngozi ya faru ilichana koti langu la suti nililokuwa nimevaa na kutoboa hadi shati la ndani hadi fimbo ikachubua mwili wangu na baada tu ya kiboko hicho akiwa anajiandaa kunichapa cha pili nilijikuta naruka na kuwapitia 4 katika wale majambazi na wakadondoka chini na nikaanza kukimbia huku wakinikimbiza kwa nyuma tena kwa spidi kubwa sasa kama sio MUNGU nini nini ? maana kuwaacha vijana 20 kwa mbio na mimi ni mzee isingewezekana na hata sasa huwa nasema ni MUNGU alinisaidia maana walinifukuza umbali mrefu kama km 5 au 6 na nakuhakikishia kama ingekuwa mbio za marathoni basi siku hiyo ningeshinda maana hata sijui nguvu za kukimbia kiasi kile zilitoka wapi?, waliacha kunikimbiza baada ya kukaribia mjini Arusha maana nilikuwa nakimbilia mjini na nakuambia kuwa kama isingekuwa neema ya MUNGU kwangu nisingepona ila namshukuru sana MUNGU kwa kuniepusha na kifo kile na hadi sasa naendelea na maisha kama kawaida. MUNGU akubariki na tuendelee kuombeana

Comments