TUJIFUNZE KUHUSU MTAJI


Wana wa Mungu tunapoongelea mtaji, watu wengi wanafikiri tunataka kuzungumzia pesa na wanakuwa wapo sawa kabisa. Lakini leo nataka kukupa jambo la msingi kwetu sisi watu wa Mungu.
 
Kwetu sisi watu wa Mungu mtaji wetu wa kwanza ni kuhakikisha nguvu ya Mungu ya mbaraka (baraka) ipo kwetu.
 
Nguvu hii inapokuwepo kwetu swala la pesa sio tatizo.
Tunajifunza neno hili kwa Yakobo katika kitabu cha Mwanzo 29 na 30. tunaona wazi wakati Yakobo anakwenda kuoa hakuwa na pesa ya kulipa mahari hivyo alilazimika kulipa mahari ya nguvu zake na hivyo alitumika miaka kumi na nne ili kupata wake wote wawili.

Katika miaka yote kumi na nne Yakobo aligundua kuwa nguvu ya Bwana ya mbaraka ilikuwa juu yake na ndio maana Labani alipomwambia kwamba sasa nitakulipa mshahara aligoma. Alijua kwamba mshahara ungezuia nguvu ya Bwana ya kumuongeza na kumkuza. Mwanzo 30:30 ”Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja, nayo imezidi kuwa nyingi. Bwana akakubariki kila nilikokweda…“ Kwa maana nyingine Yakobo anamwambia Labani ”Nguvu ya Bwana iliyo juu yangu ndio imekuongeza kiasi hiki ulichonacho, sasa wewe utanilipa nini cha kutosha?“

Mstari wa 31, ”Akamwuliza, Nikulipe nini? Yakobo akasema USINIPE KITU“.
Yakobo akijua kuwa nguvu ya mbaraka ya Bwana ipo juu yake alitaka mali kidogo toka kwa Labani na Labani bila kufahamu hilo alikubali kwa urahisi kabisa. Soma mstari wa 32-33 .

Katika mstari wa 43, Biblia inasema, ”Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama wengi…“ Utajiri tayari.

Wapendwa, nguvu ya Mungu ya mbaraka inapokuwapo upande wetu chochote kile kinachotuzunguka ni mtaji tosha.

Katika hali hii tuliyonayo yatupasa kutafuta nguvu ya Mungu ya mbaraka kwanza kabla ya mtaji wa pesa. ”Tafuteni  ufalme wa Mungu kwanza na haki yake yote mengine yote mtazidishiwa“ Yesu  anaendelea kusema ”Msisumbuke kama mataifa.“ Kwa maneno haya sisemi tusitafute pesa, pesa tutafute lakini yatupasa kujua kuwa pesa sio msingi wa maendeleo kwetu sisi tuliookoka. Kwetu sisi kitu cha kwanza  ni kibali cha Mungu katika maisha yetu. Ni nguvu ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Neno la Mungu linasema katika Kumbukumbu la Torati kwamba Mungu ndiye atupaye nguvu za kupata utajiri. ”Bali utamkumbuka Bwana Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri…“(Kumb 8:18).

Hatua ya pili ni pesa
Baada ya nguvu ya Mungu kuwepo kwetu nasi tukaanza na chochote kidogo kilichopo, hata kama ni kibaya, au cha fedheha, tutaona Bwana anatufanikisha, na yale  mapato yanayoingia ndio unakuwa mtaji wetu mzuri wa kuanzia.
Fedha yoyote tunayopata yatupasa kuitenga au kuiweka katika makundi matano muhimu. Yaani fedha kwa ajili ya:
  • Zaka (Fungu la kumi)
  • Sadaka (Dhabihu)
  • Mtaji
  • Akiba
  • Chakula.

Mtaji lazima uongezeke kila wakati tunapohesabu faida. Kwa maana hiyo basi tunapokuwa tayari tumepata faida yatupasa kutenga kiasi cha fedha yetu na kuiweka kwenye mtaji. Kwa mfano: Nilianza biashara bila kitu pale Kamanga Feri; nilianza nikiwa mpiga debe tu. Samaki zinapoletwa, mimi nachukua toroli na kuanza kuuza huku mwenye samaki hizo amekaa tu. Chochote nachopata kwa siku au kwa wiki lazima nitenge sehemu kidogo ya mtaji. Ikiwa makubaliano yetu ni kuwa kila samaki nitakaye muuza yeye atanipa shilingi 100 basi nikiuza samaki 50 ninapata shilingi 5,000 kwa siku. Kwa wiki shilingi 5,000 x 6 = 30,000.. Kwa mwezi 30,000.00 x 4 = shilingi 120,000.
Kwahiyo hizo shilingi 120,000 zinapaswa kugawanywa katika yale mambo matano muhimu (zaka, sadaka, mtaji, akiba na chakula).

Nguvu ya Mungu inapokuwepo, kiasi kidogo tu cha pesa chatosha kuwa mtaji wa kutuletea mambo makubwa. Mtaji mkubwa wa pesa ni kitu cha muhimu sana lakini kisiwe kizuizi kwetu sisi kuanza kufanya yale ambayo tunakusudia kufanya katika maisha yetu.

Yakobo akijua kuwa anayo nguvu ya Mungu ya mbaraka maishani mwake anamwambia Labani, sitaki unilipe pesa ”nipe lile kundi dogo la wanyama wenye marakaraka hao ndio utakuwa mshahara wangu.“ Labani bila kujua hilo anamkubalia Yakobo. Na Yakobo mwenye nguvu ya Mungu anaanza na yale machache na mwisho wake tunaona Yakobo anakuwa tajiri.

Hivyo nakushauri wewe uliyekata tamaa na maisha, hapo ulipo na kipato ulichonacho chatosha kukufanya wewe kuwa tajiri sana sana.

Tunapokuwa tumeanza kupata pesa yatupasa kujua kuwa kilichotuwezesha ni nguvu ya mbaraka maishani mwetu na sio ujanja wetu,  hivyo ni lazima tuhakikishe kuwa tunaitunza hiyo nguvu ya Mungu ya mbaraka maishani mwetu. MUNGU awabariki

Comments