FURAHA YA MUNGU KWA WANAOIFANYA KAZI YAKE


         Hakuna lolote  tunaloweza kulifanya  kwa Mungu na kumfurahisha, kama kuwa watenda kazi wanaofanya Uinjilisti, kwa kuwaleta watu kwa Yesu, na kuwalea katika uchanga wao kiroho, mpaka waukulie wokovu. Kila mtu aliyeokoka, angependa na kufurahi kuwa Mtendakazi, kama angejua ni kwa kiasi gani Mungu katika Utatu (Baba, Mwana na Roho Mtakatifu) anavyomfurahia mtendakazi mmoja anayefanya kazi ya uinjilisti. Ili tufahamu furaha ya Mungu kwa watendakazi ni muhimu tujifunze Mungu ni nani kwetu tuliookoka, na sisi ni akina kwake:-
  1.     Mungu Baba ni Mkulima (YOHANA 15:1)-Mkulima anapopita kwenye shamba liwe la migomba, mikahawa, michungwa, mipapai, minazi n., hufurahia sana kuona tawi linalozaa na kulishughulikia sana. Tawi lisilozaa, huliondoa na kulitupa motoni (YOHANA  15:2). Mkulima akiona tawi la migomba lililozaa mkungu na ndizi nzuri, atalitembelea tawi hilo wakati wote, na kuweka mti ili kulikinga tawi hilo na upepo n.k. Ndivyo alivyo Mungu kwa  mtendakazi wake.
  2.     Mungu ni Bwana wa Majeshi (YAKOBO 5:4)-Amiri Jeshi Mkuu, huwafurahia mno askari wapiganaji hodari ambao wanaufanya ufalme wake kukua na kulindwa. Hawa humpa nguvu na sifa, hivyo huwatunuku medali maalum za kitaifa. Ndivyo alivyo Mungu kwa watendakazi wake.
  3.     Mungu ni mwenye mali -   Mungu anafananishwa na mtu mwenye mali aliyesafiri ambaye amewaachia watumwa wake mali ili waifanyie biashara na kupata faida. Mtu mwenye mali wa namna hii akirudi, atamfurahia sana mtumwa yule aliyepeta faida kuliko yule aliyeificha tu, na hakuzalisha chochote (MATHAYO 25:14-30). Ndivyo alivyo Mungu kwa mtendakazi wake.
  4.    Yesu ni Mfanyabiashara mwenye vyombo vya uvuvi- Mfanyabiashara mwenye vyombo vingi vya uvuvi, huajiri wavuvi na kuwapa vyombo vya uvuvi. Wanaporudi kutoka katika uvuvi, humfurahia sana yule aliyeleta samaki wengi na kumpenda mno. Asiyeleta samaki, ana hatari ya kunyang’anywa chombo na asipewe tena. Ndivyo alivyo Yesu kwa mtendakazi wake  aliye mvuvi wa watu (MATHAYO 4:19).
  5.     Yesu ni Mfugaji mwenye zizi la Kondoo –Baada ya kupotea Kondoo wengi katika zizi lake, anawatuma watu kuwatafuta. Atamfurahia mtendakazi atakayerudi na Kondoo wake wengi waliopotea (LIKA 15:3-7)
  6.      Mungu ni mume wetu (YEREMIA 3;14)- Mume  humfurahia sana mke anayezaa sana na kuwalea vizuri wanae. Asipozaa, upendo kati yao huingia dosari, na ndoa huingia mashakani ikiwa ni mataifa. Ndivyo alivyo Mungu kwa mtendakazi wake.
  7.      Yesu ni Mpanzi wa Mbegu (MARKO 4:3)- Hakuna linalomfurahisha Mpanzi kama mbegu ile iliyotoa mazao mengi. Baada tu ya kupanda, mpanzi huanza kuangalia mbegu itakayoota na kutoa mazao mengi. Hiyo huipenda mno. Ndivyo alivyo Yesu kwa mtendakazi wake.
  8.       Yesu ni Mwalimu (YOHANA 13:13)- Mwalimu humfurahia sana mwanafunzi wake anayefanya kama yeye mwenyewe kutokana na jinsi alivyomfundisha. Ikiwa mwalimu anamfundisha mtu udereva lakini  mtu yule ni mzito wa kufanya kama mwalimu wake, hapendezi kwake. Mtendakazi anayefanya Uinjilisti kama mwalimu wake Yesu, anamfurahisha mno.
  9.      Roho Mtakatifu ni Bwana wa mavuno – Anamfurahia sana mtu yule anayevuna roho za watu na kuzileta ghalani mwake, kuliko yule anayeacha mavuno yaozee shambani (MATHAYO  9:38; MATENDO 13:2; YOHANA 4:35-36).
  10.   Mungu ni Baba kwetu (MATHAYO 6:8-9) –Baba yeyote, hufurahi sana kuona watoto wa mtoto wake. Mungu pia hufurahi kuona watoto wa mtendakazi. Kwa sababu Mungu anamfurahia mtendakazi:-
( a ). Uwezo wa majibu ya maombi yake huongezeka (YOHANA 15:16)
( b ). Atang’aa kama nyota milel (DANIELI 12:3).
( c ). Watoto wa mtendakazi humuongezea Ushindi juu ya Shetani (ZABURI 127:4-5)
( d ). Watoto hao watakuwa ni taji ya kujionea fahari, furaha na utukufu wake wakati wa kuja kwa Yesu (1 WATHESALONIKE 2:19-20). BARIKIWA

Comments