MANENO SABA(7) YA YESU MSALABANI



Katika ujumbe maalumu wa PASAKA na kutakiana heri katika sikukuu hii muhimu naomba tuangalia MANENO 7 YA BWANA YESU pale msalabani kabla ya kufa na kufufuka ili wanadamu wote tupate uzima wa milelel katika yeye kwa kila aaminiye, kwanza namba saba, kama ilivyo namba arobaini katika desturi za Kiyahudi ina maana ya utimilifu au ukamilifu. Namba saba inathibitisha kuwa kitu ni kamili au kinajitosheleza. Tutafakari kwa pamoja maneno saba ya Yesu msalabani:

1.“Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo”

Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema,“Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo”
Wakagawana mavazi yake, wakapiga kura.
Luka 23:33-34
Neno la kwanza la Yesu msalabani lahusu msamaha. Msamaha ni tabia kuu ya Mungu.
2
.“Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mbinguni.”
Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, “Je, wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.” Lakini yule wa pili akamjibu, akamkemea, akisema, “Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa.” Kisha akasema, “EeYesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mbinguni.”
Luka 23:39-43
Neno la pili la Yesu msalabani lathibitisha kuwa msamaha una nguvu kuliko dhambi. Yesu amefundisha juu ya msamaha . Yesu ameonesha kuwa yeye ni Mungu kwa kutumia tabia kuu ya Mungu ya kusamehe. Yule mhalifu ametambua kosa lake na amemtambua Yesu kuwa ni Mungu na akaomba msamaha; Yesu mara moja akamsamehe kwa kumpa nafasi mbinguni.

  3. “Mama tazama mwanao; Tazama mama yako”
Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, “Mama tazama mwanao.” Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, mama yako.” Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.
Yohane 19:25-27
Neno la tatu la Yesu msalabani alimwambia mamaye:Wazazi ndiyo waliomleta mtoto duniani, wanaomlea na kumfundisha katika hatua zake za kwanza za maisha. Mungu mwenyewe ametufundisha kuwa mzazi anachukua nafasi ya pili; nafasi ya kwanza ni Mungu. Katika amri 10 za Mungu; amri 3 za kwanza zahusu uhusiano wetu na Mungu, amri 7 zilizobaki zahusu uhusiano wetu. Katika hizo amri 7 zinazohusu uhusiano uhusiano wetu sisi wanadamu, amri ya kwanza (yaani ya nne) inahusu wazazi wetu: Waheshimu Baba na Mama upate miaka mingi na heri duniani.

4. “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”
Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, “Tazama, anamwita Eliya”.
Marko 15:33-35
Neno la nne la Yesu msalabani lahusu kilio chake kwa Baba yake. Kilio hicho kina ladha ya kukata tamaa. Je, ni kweli kuwa Yesu aliachwa na Baba yake? Je, ni kweli kuwa Yesu alikata tamaa? Kilio cha Yesu msalabani hakikuwa ni kilio cha kuachwa na Baba yake; wala hakikuwa ni kilio cha kukata tamaa.
Yesu pale msalabani alikuwa anasali Zaburi ya 22. Zaburi hii ilitungwa na mfalme Daudi na akaiita ni zaburi ya mateso na matumaini ya mwadilifu. Katika zaburi hii ukisoma utaona kuwa mtu huyo anaanza kumuuliza Mungu kwa nini amemwacha, kisha anaanza kuelezea sifa za Mungu. Halafu ndiyo anaanza kumweleza Mungu wake mateso yake, lakini katika hayo mateso anamwambia Mungu kuwa yeye ni tegemeo na tumaini lake. Na mwisho anamhakikishia Mungu kuwa hata katika mateso yake ataendelea kumsifu na kumtukuza Mungu mbele za watu wote.

5. “Naona kiu”
Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, “Naona kiu.” Kulikuwa huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.
Yohane 19:28-29
Neno la tano la Yesu msalabani lahusu hitaji la msingi la uhai wa watu; maji. Hapa kiu ya maji inawakilisha njaa. Kati ya majanga makubwa kwa wanadamu ni njaa, kukiwa njaa basi kifo kimeshafika, tena ni kifo cha taratibu kwa mateso makubwa. Yesu ametumia neno kiu na sio njaa kwa kuwa kiu huuma zaidi kuliko njaa. Ni kweli kuwa njaa ya chakula na kiu ya maji huenda pamoja, lakini kiu ya maji inatesa zaidi kuliko njaa ya chakula. Mwanadamu bila chakula na kinywaji hakika hawezi kuishi bali atakufa. Chakula na kinywaji ni hitaji la lazima katika maisha.
Kiu aliyonayo Yesu pale msalabani haikuwa ya kinywaji; ilikuwa ni kiu ya kuona kuwa kazi aliyoianzisha inaendelezwa. Yesu alikuja duniani kutangaza msamaha wa dhambi; hivyo basi ni kiu yake kubwa kuona kwa watu wanamuelewa na wanaomba msamaha wa dhambi zao kwa Mungu. Mafundisho yote ya Yesu na miujiza yake yote inajikita kwenye msamaha wa dhambi. Kanisa lake alilianzisha ili lifanye kazi hiyo ya kusamehe na kuondoa dhambi: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”.

6.“Imekwisha/ Yametimia”
Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, “Imekwisha”. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.
Yohane 19:30
Neno la sita la Yesu msalabani lina uhusiano mkubwa na neno la sita; au ni mwendelezo wake. Ni neno linalohusu kiu. Ajabu ni kwamba Yesu alipopewa ile siki ili ainywe, hakuinywa bali akasema kuwa kiu yake imekwisha. Hapa ndipo twatambua kuwa Yesu hakuwa na kiu ya maji kama kinywaji, bali alikuwa na kiu ya kuona wanafunzi wake au wafuasi wake wanabadilika. Mabadiliko anayoyaleta Yesu ni toba. Toba ni tendo la mtu kutafuta rehema au huruma ya Mungu. Katika Agano la Kale watu walipotaka kumpendeza Mungu walimtolea sadaka. Kumbe katika Agano Jipya Yesu anatuambia kuwa Mungu hataki tena sadaka bali anataka rehema. Rehema ni tendo lenye pande mbili; upande mmoja ni mtu kutambua dhambi zake na kuziungama, upande mwingine ni Mungu kumsamehe mkosefu aliyezitambua na kuzijuta dhambi zake.

7. “Ee Baba mikononi mwako naiweka roho yake”
Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha kusema hayo alikata roho.
Luka 23:44-47
Neno la saba na la mwisho la Yesu msalabani lahusu kifo. Kifo ni tukio la mwisho kwa mtu yeyote na ni tukio lisilokwepeka. Kila mtu ni lazima akutane na kifo; apende asipende, ajue asijue, kifo kipo na kinatungojea. Wakati ule adhabu ya msalaba ilikuwa na lengo la kumuua mtu; ilikuwa ni hukumu ya kifo. Hii ilikuwa ni adhabu ya Warumi. Kumbe kwa Wayahudi kutundikwa msalabani ilikuwa ni jambo paya zaidi ya kifo; ilikuwa ni kifo cha laana: kwani aliyetundikwa juu ya mti amelaaniwa na Mungu.
Kifo cha Yesu pale msalabani kilihesabika kuwa ni laani kadiri ya imani ya Wayahudi. Lakini kumbe Yesu kwa kufa msalabani aliigeuza hiyo imani yao ya kale na kuwaingiza katika imani mpya:
Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa: Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.Wagalatia 3:13-14. MUNGU awabariki sana na pia nawatakia PASAKA njema. BWANA YESU AMEFUFUKA , AMEFUFUKA KWELI KWELI AMEN
.

Comments