AGIZO KUU LA BWANA YESU KWA MITUME WAKE. * sehemu ya kwanza *


Mtumishi Gasper Madumla

Tunasoma ;
Mathayo 28 : 19-20
“ Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. ”

Haleluya…
Bwana Yesu asifiwe sana…

Katika andiko hilo, tunaona Bwana Yesu akitoa AGIZO kwa mitume wake,kwamba waende kuwafanya MATAIFA YOTE wawe wanafunzi.
Sasa hapo Bwana Yesu anaongea na watu wake,na wala haongei na watu wa mataifa,hivyo ikiwa wewe sio mtu wa mataifa basi ni ukweli usiopingika kwamba AGIZO hilo,leo unaambiwa wewe na linakuhusu sana.

Sikia ;
Bwana Yesu,anawaambia waende kwa watu wa mataifa yote,wala sio waende kwa baadhi ya mataifa,
Bali wayaendee mataifa yote, “ Go therefore and make disciples of ALL THE NATIONS ” Hivyo basi jukumu la kuinjilisha ni la kila aaminiye katika Kristo Yesu.

Swali la kujiuliza hapo,
Je umeshawahi kumleta mtu yeyote kwa Kristo,ukamfanya awe mwanafunzi,na aokoke?
Ikiwa bado basi anza atua sasa, mara tu usomapo ujumbe huu,maana umekusudiwa kwako.

• Ipo gharama kubwa ya kumfanya mtu awe mwanafunzi,maana mtu huyo humtakaye awe mwanafunzi wa Yesu Kristo,pia kumbuka ana imani yake binafsi.

Sasa ile kumbadilisha mtu kiimani ni jambo gumu kuliko hata kazi ya kubeba matofali,au kufanya kazi nyingine yoyote ile.
Hakika kwa kutumia akili zako binafsi huwezi,na ndio maana ninasema ni ngumu,wala hata mimi mwenyewe siwezi.
Bali twaweza kwa msaada wa roho mtakatifu,kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wa Kristo Yesu.

Oooh! kumbe Roho mtakatifu ndie afanyaye kazi !
Basi,simple tu ikiwa roho mtakatifu mwenyewe atakuwa kazini.

• Ipo NGUVU ya ajabu ndani ya Agizo hilo.

Na ndio maana tunaona Bwana Yesu akiwaambia kwanza “ Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” Mathayo 28 : 18.
Akimaanisha kuwa,kazi hiyo ya kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi ipo chini ya mamlaka yake mwenyewe,kwa kuwa Yeye Bwana Yesu ndio mwenye Mamlaka mbinguni na duniani tena Yeye ndio kichwa cha enzi yote na mamlaka ( Wakolosai 2 : 10 ).

Nasema katika kulitekeleza AGIZO KUU hili,ipo nguvu ndani yake,isiyoweza kuelezeka kwa sababu sio wewe ufanyaye bali ni Kristo mwenyewe akiwa kazini,Sasa ikiwa ni kazi ya Bwana Yesu,Je ni nani awezaye kuipima?
Kwamba Nguvu yake ikoje?
Ukweli ni kwamba nguvu ya Mungu haipimiki hata utumie kifaa gani.

Sikia :
Hata nguvu ya Mabomu yote yaliyopo hapa ulimwenguni yanawezekana kupimika,tena na kujulikana asili za kila bomu,lakini sio nguvu ya Mungu,hakuna wa kuipima.

Haleluya…

Na ndio maana Mungu,akikuambia nenda kawafanye mataifa kuwa wanafunzi wake Bwana Yesu,Basi usisite-site wala kuogopa maana si wewe uwafanyaye mataifa kuwa wanafunzi bali ni Yeye Kristo ambaye yu ndani yako,
Tena si wewe uwachaguaye mataifa kuwa wanafunzi Bali ni Yeye Kristo ndiye awachaguaye maana imeandikwa :

“ Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. ” Yoh.15 :16

Ukiamua kulitekeleza agizo hilo,Basi ujue Yeye Bwana Yesu,atakuongoza tu namna ya kuanza na kumaliza ( Mathayo 10 :19)
Labda tumtizame Yeremia pale alipokuwa akitumwa na Bwana Mungu kuifanya kazi yake.Naye akasema hawezi kusema maana yeye ni mtoto.

Lakini Bwana akamwambia,
“ Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.
Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.” Yeremia 1 : 7-8

Wakristo wa siku hizi nao wamegeuka na kuwa kama Yeremia pale alipojibu kwamba hawezi kuifanya kazi ya Bwana.
Nami leo ninakuambia kupitia fundisho hili,roho ya Bwana itakuimarisha na kukutia nguvu kwa upya kabisa ili uweze kutambua jukumu lako wewe mkristo,maana ipo sababu hata fundisho hili likujie wewe kwa wakati na muda kama huu.

ITAENDELEA…
UBARIKIWE.

Comments