AGIZO KUU LA BWANA YESU KWA MITUME WAKE. * sehemu ya mwisho. *








Tunasoma Mathayo 28 : 19-20

“ Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. ”

Haleluya…
Bwana Yesu asifiwe sana…

Kwa hiyo sisi ambao ni wanafunzi wa Bwana Yesu,tumepewa majukumu haya yafuatayo kulingana na andiko hilo :
01.Kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wa Bwana Yesu.
02.Kubatiza kwa jina la Baba na la Mwana na Roho mtakatifu.
03.Kuwafundisha kuyashika yote aliyotuamuru Bwana Yesu.

Mambo hayo matatu ni kazi tuliyopewa tuifanye mimi na wewe, Ikiwa wewe ni Mchungaji,au Mwinjilisti,au Mwalimu,au Nabii,au Mtume,au Mfuasi wa Kristo aliyeokoka,
Basi huna ujanja wa kukwepa agizo hilo au kazi hizo na wala sio ngumu kuzifanya maana Yeye azifanyaye ni Bwana mwenyewe kupitia wewe tazama Yesu asemavyo hapo katika andiko hilo hilo anasema;

“, ...mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. ”

Yaani yeye hatatuacha wenyewe bali atakaa pamoja nasi muda wote wa huduma tuzifanyazo na ndio maana anasema kuwa Yeye yupo pamoja nasi hata ukamilifu wa dahari.
Leo hii kuna kundi kubwa la watu wanaohitaji mafundisho ya kweli ili wawe huru,Watu hawa wa mataifa tunaishi nao,wengine ni baba zetu,wengine ni mama zetu,wengine ni ndugu zetu N.K

Jukumu letu kwao,ni kuwafanya wawe wanafunzi wa Bwana Yesu kwa kuwafundisha yale yote aliyotuamuru Bwana Yesu Kristo.

Haleluya…
Kisha sasa wakishaamini mafundisho ya Bwana Yesu,ndio unakuja wakati sasa wabatizwe kwa jina la Baba na la Mwana na Roho mtakatifu.
Naipenda tafsiri ya andiko hilo katika kitabu cha Marko namna inavyoelezea zaidi.
Tunasoma
Marko 16:15-16
“ Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.”

Tazama hapo,tumeambiwa tuende ulimwenguni mwote kwa kazi ya KUHUBIRI INJILI KWA WOTE neno “wote”
likimaanisha kwa wale waliookoka na hata wale wasiookoka,kwamba tunahitajika tukawape habari njema ili watakaposikia tu basi IMANI itaanzia hapo maana imani huja kwa kusikia neno la Kristo ( Warumi 10 :17)

Sikia :

Katika agizo hilo hatukutumwa tukahubiri injili kwa binadamu pekee yao,bali tumetumwa tukahubiri kwa kila kiumbe, "Go into all the world and preach the gospel to every creature.”
Yaani yatupasa tuwahubirie hata wanyama wote,maana wanasikia katika ulimwengu wa roho,
Kumbuka wanyama wote wako chini yetu,hata ardhi tumepewa kuitunza,Hivyo katika suala la KUSIKIA utiisho wa neno la Mungu,navyo vyaweza kusikia na kutiishwa katika ulimwengu wa roho.
Na ndio maana tunaona Eliya aliweza kuhihubiria Mvua na mvua haikunyesha,

Tunasoma Yakobo 5 : 17-18
“ Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.
Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.”

Eliya aliweza kuitamkia mvua kutokunyesha na mvua ikasika,na hakunyesha.Ikiwa kama mvua ilisikia basi hata ardhi yaweza kusikia,tena hata wanyama waweza kusikia,na kila kiumbe chaweza kusikia.Ndio maana neno linasema;

“… mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.”
Hivyo basi kila kiumbe chaweza kutiishwa kwa neno la Mungu maana vyote viliumbwa na yeye,naye ndie Bwana Mungu ni Mungu wa vyote.
Kisha tunasoma;

“Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” ( Marko 16 :16)

Huyu atakaye amini,ni lazima kwanza asikie habari za Bwana Yesu Kristo,ndipo aamini.
Tunasoma
Matendo 8 : 31
“ Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza?
Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. ”

Huyo aliyesema maneno hayo ni towashi,mtu wa kushi aliyekuwa akirejea kutoka kuabudu Jerusalemu,
Wakati akiwa garini mwake akisoma chuo cha Nabii Isaya,
Lakini pasipo kuelewa kile akisomacho.
Ndipo Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia,
Aende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa,huko atamuona towashi,mtu wa kushi,aikiwa garini mwake,ikisoma maandiko.

Na filipo alipofika,akamueleza,kwa kumuhubiria habari za Yesu Kristo wa Nazareti.
Alichokifanya Filipo ni kutimiza AGIZO LA BWANA YESU.
Baada ya Filipo kuhubiri injili,ndipo tunaona Towashi anaanza kuamini na baadae anabatizwa.

Tunasoma
Matendo 8 : 37-38
“ Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]
Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye AKAMBATIZA ."

Huyu towashi alikuwa hajawahi kuokoka hata siku moja,ingawa alikuwa akienda Jerusalemu kuabudu,
Tunafundishwa hapo kwamba Ile namna ya kwenda kanisani kuabudu haimanishi ndio kuokoka.Kuokoka ni mchakato mwingine ambao huja baada ya kusikia neno la Kristo,na ndio maana Towashi aliposikia habari za Yesu,kisha IMANI ikaumbika ndani yake,na hapo sasa akabatizwa na kuokoka.

Haleluya…
Sikia ;
• KUAMINI huja baada ya kusikia neno la Kristo.
• KUOKOKA huja baada ya kuamini neno la Kristo,(kwa kukiri kwa kinywa chako kuwa Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yako )
• KUBATIZWA huja baada ya kuamini neno la Kristo.

MATHEMATICALLY


• Kuamini + Kuokoka =Kubatizwa

Hivyo yeye abatizwae pasipo kuamini habari za Yesu Kristo,ikiwa atamwagiwa maji ya kunyunyiza kama wengine wale wa mapokeo ya wanadamu,au azamishwe majini pasipo lakini pasipo IMANI,basi ubatizo huo ni bure.

Na ndio maana anahitajika mtu mzima anayeweza kuamini kwanza,tazama mfano wa Towashi( Matendo 8 : 27-39)

Wito wangu kwako wewe mpendwa ni kufahamu kwamba ipo kazi kubwa ya kufanya ambayo yenye thamani machoni pa Bwana ya kwenda ulimwenguni mwote kuhubiri injIli pasipo kumuonea haya mtu yeyote Yule.

Lakini kwanza uokoke na kudumu katika fundisho kila siku,kisha tukiwa tayari tuwaendee watu wote kwa kuanzia watu wa karibu wanaotuzunguka mpaka mataifa yote.

UBARIKIWE.

Comments