MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU,BALI JAWABU LA ULIMI HUTOKA KWA BWANA. (Mithali 16 :1 ) * Sehemu ya mwisho *



Mtumishi Gasper Madumla akiwa na mwanae Isaac Gasper


Haleluya…
Bwana Yesu asifiwe…

Mpaka mtu aongozwe kwa roho,ipo kazi ya ziada,sio rahisi,wala si mchezo mchezo tu,bali ni kuacha yote kwa ajili ya ufalme wa Mungu.
Mungu anapokuwa namba moja katika maisha yako,unakuwa sio mtu wa kawaida.Roho ili iwe kiongozi katika mwili ni lazima iwe na nguvu,Nguvu hupatikana katika chakula,Chakula cha roho ni NENO LA MUNGU.

Neno la Mungu linapopata nafasi ya kutosha katika roho yako,hapo sasa kinachofanyika ni kupanua misuri ya roho yako na kuanzia hapo sasa unakuwa ni BAUNSA wa kiroho,mtu mwenye kuleta athari/machafuko katika ulimwengu wa roho maana mapepo na washirika wao wote,watakimbia mbele zako,

Tazama ibilisi alivyokimbia mbele ya Bwana Yesu Kristo baada ya Yesu kujaribiwa kule jangwani.Kilichomfanya Bwana Yesu amshinde ibilisi ni UWEPO WA NENO LA MUNGU lililojaa ndani yake.

Mathayo 4 : 10
“ Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. ”

Tunaona kisha shetani akaondoka kwa sababu hana nguvu ya kushindana na nguvu za Mungu,Bwana Yesu alikuwa ni BAUNSA kiroho dhidi ya shetani alikadhalika hata kwako ikiwa utafanya maandalizi mazuri ya moyo wako kwa kuijaza neno la Kristo,nawe utakuwa ni baunsa kiroho,hali katika mwili wako yamkini waonekana ni mdogo,lakini kiroho ni mkubwa.
Hatua hizo zote ni mchakato unaokuja kwanza kabisa kwa Kuuandaa moyo wako.

Labda nikupe mfano kidogo :
Kuna watu waendao kanisani wakiwa ni wanyonge mioyoni mwao,Mioyo yao ikiwa imeinama,hawana chang’amko la rohoni.
Watu wa namna hii husema “Nikifika kanisani leo,nitachanga’mka,nitamsifu Bwana”

Watu hawa husubiri kupata bubujiko la ndani mpaka wafike kanisani,na wakifika kanisani,mara nyingi huwa ni ngumu kupata kile wanachokiitaji,utakuta mchungaji akitumia nguvu nyingi kuwalazimisha wachangamke

Lakini ni tofauti sana na watu wenye Kufanya maandalizi ya mioyo yao.
Kwani hawa kabla ya kufika hata kanisani wanakuwa wameshalipuka mioyoni mwao,mioyo yao inachangamko lisiloelezeka,
yaani wakiwa nyumbani wanajiandaa kutoka basi utawakuta wakiwa na furaha kweli kweli,hata tenzi za rohoni zikitoka mioyoni mwao,na wakifika tu kanisani panakuwa hapatoshi, USTAARABU unakufa,na kinachochukua nafasi ni ROHO na sio USTAARABU.

Oooh Haleluya.

Watu wa namna hii ndio waliofanya MAANDALIZI YA MOYO.
Pindi watakapoomba ,basi jawabu la ulimi wao linatoka kwa Bwana Mungu,kwa maana wao wamefungua mioyo yao.

Kati ya maombi muhimu kwa mkristo ni kuomba moyo mpya,moyo wa Ibada.Tazama hata Daudi aliifahamu siri hii akamwambia Bwana “ Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu ” Zaburi 51 : 10

Sikia :
Ingawa Daudi alikuwa ni mtu aliyekuwa akifanya makosa mara kwa mara,lakini bado Mungu alikuwa akimpenda,kwa sababu alikuwa na moyo wa tofauti sana,moyo wake ulikuwa ni moyo wa toba,moyo uliompendeza Bwana Mungu.

Leo ,Mungu atusaidie sana,ili tuwe na moyo safi,maana mbingu ni ya watu wenye mioyo safi,Tazama
Mathayo 5 :8
“Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. ”
Biblia haikusema heri wenye kuomba sana watamuona Mungu,Wala haikusema heri wenye kwenda kanisani kila siku watamuona Mungu,Bali imesema “ Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. ”

Kwa hiyo fursa ya kumuona Mungu imetolewa kwa wale wenye mioyo safi tu. Na ukimuona mtu anasema amemuona Mungu kwa namna tofauti ,swali la kujiuliza je mtu huyo ana moyo safi ? ikiwa hana moyo safi basi usipoteze muda wako kwa mtu huyo maana ni lazima atakuwa ni muongo tu.

• Kuwa na moyo safi ni maandalizi,na pia mara nyingine ni NEEMA tu.

Mtu anapoandaa moyo wake vizuri,inampelekea kutokufikiri-fikiri wakati anapotoa majibu mbele ya watu wa mataifa /wasioamini neno la Mungu,maana siye yeye ajibuye bali ni Bwana ndiye atoaye majibu hayo yote .

Mfano :
Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa anawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu (Mathayo 10 : 16)Haikuwa ni rahisi kondoo amwendee mbwa-mwitu,kwa sababu kondoo alikuwa ni chakula tu kwa mbwa-mwitu. Lakini sasa tazama wanafunzi ndio wanatumwa kama kondoo kati ya mbwa –mwitu.na anawaambia tena juu ya habari ya kutokufikiri-fikiri watakayojibu.
Tunasoma:
Mathayo 10 : 19
“Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.

Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. ”
Kondoo wa leo ni wewe na mimi,tunatumwa twende kwa watu wa mataifa tukawape habari njema,
Ikiwa kama tutakuwa na maandalizi mazuri ndani ya mioyo yetu kwamba roho wa Bwana akipata nafasi ,
Basi ni dhahili tutaweza kuifanya kazi ya Bwana vizuri tena wala sio sisi tuifanyayo bali ni roho mwenyewe atakayefanya.

Bali ikiwa kama hatuna maandalizi ya mioyo yetu jawabu la ulimi halitatoka kwa Mungu,na kusababisha tutumie akili zetu badala ya akili za Mungu.Hivyo tutashindwa kuifanya kazi ya Bwana.

Wito wangu kwako mpendwa ni kufanya maandalizi ya kutosha katika moyo wako, Maana hata saa wala wakati hatujui ajapo mwana wa Adamu,basi ajapo atukute tuna mioyo safi ili tuweze kumuona Mungu.

MWISHO.
UBARIKIWE.
Mtumishi Gasper Madumla

Comments