MWANADADA ZUIA MFUMKO WA NGONO.



by Vicent Mwengo


BWANA YESU APEWE SIFA,
Habari yako ndugu popote hapo ulipo, najisikia kukuandikia jambo hili leo hussani wewe mdada/binti, sikufundishi ila ninachukua wasaa huu kukukumbusha tu jambo dogo sana linalohusiana na ngono.

Ngono ni neno moja zito ambalo linamaanisha ufanyaji wa tendo la ndoa katika utaratibu usio sahihi katika jamii. Nianze hivi kwenye jamii yoyote jambo lolote huwa lina utaratibu, kama jamii Fulani imezoelea jambo Fulani na kulikubali basi jambo hilo hufanywa kuwa sehemu ya utamaduni wa jamii hiyo. Kwa mfano; kama jamii Fulani wameukubali utumiaji wa bangi na wote kwa pamoja wameuukubali, basi jamii hiyo itakapoambiwa kutumia bangi ni mnafanya makosa hawawezi kukubali kwani limekubalika kwenye jamii yote na mtazamo wao uko sahihi.

Tendo la ndoa katika jamii yoyote lina utaratibu wake, wazee wetu walienenda katika misingi ya jamii yao ilivyokuwa, wengi mmesimuliwa habari za wazee na wazee wenu hivyo watu mnazijua vilivyo, sitaki kuzizungumzia sana. Unapozungumzia ngono, mimi ninalizungumzia jambo hili kwa mtazamo wa “kibiblia”. Kwa dhana ya utaratibu, hata kwenye Biblia kuna utaratibu wake, lakini utaratibu wa kwenye Biblia hauna tofauti sana na wa jamii za wazee wetu, kwani wazee wetu walifanya japo Biblia kwao ilikuwa bado haijakolea. Lakini pia hata walipoijua walienenda sawasawa kwa kuacha kuwa na wake wengi. Kuyaleta yote haya ni kutaka tu kukuongezea uwanja wa kulitathmini jambo hili.

Kwa mtazamo wa kibiblia ngono iko katika sehemu mbili ambazo ni uasherati (kufanya tendo la kabla ya ndoa) na uzinzi (kufanya tendo la ndoa nje ya ndoa). Naogopa kuzungumzia habari za ndoa kwani uhalisia wangu haufundishi habari za ndoa (sijaoa). Nitajikita kwenye ngono kwa maana ya Uasherati kama nilivyotolea maelezo hapo juu.

NB: Je wewe mwanadada unatambua kwamba unauwezo wa kuzuia mfumuko wa ngono kwenye jamii???

Ni swali moja rahisi lenye majibu yenye utata, lakini lina suluhu ndani ya jamii nzima. Nilipowuliza wanadada mahala Fulani swali hili; mmoja alikuja juu kwelikweli, na kusema “waambie kwanza wanaume waache kutufuata”. Mwingine akasema Mwengo, ninyi wanaume ndio chanzo cha tatizo la ngono kwenye jamii kwa sababu mnapenda kweli! Mwingine kwa sauti ya upole, Vicent siku zote kwenye mapenzi mwanaume ni kama jiko la mchina na sisi ni kama jiko la mkaa hivyo ninyi wanaume ndio chanzo cha tatizo. Wengine walikuwa wasikilizaji tu wa mazungumzo, kwani tulikuwa tumemaliza kazi yetu na tumechoka nikaamua kuzua mjadala wa kutupumzisha. Achana na hayo lakini leo ninakuandikia wewe mdada ili ujue na kama ulijisahau basi uzingatie upya. Ndugu wale waliotoa majibu yao, yamkini hata wewe unapokuwa unalitathmini jambo hili na wewe pia unamajibu kama yao, yanaweza yasiwe kama yao lakini yanafanana na hayo. Lakini sasa hebu pata mtazamo uliosahihi juu ya habari hizo.

Kwenye fikra yoyote ile huwa kuna vitu viwili, pata hiyo; “fikra inaweza ikawa sahihi lakini ikawa na mtazamo usio sahihi vivyo hivyo inaweza ikawepo fikra sahihi na mtazamo wake ukawa sahihi vilevile”. Lakini nilichogundua majibu mengi walionayo wanadada ni sahihi lakini mtazamo wake sio sahihi. Kwa kukufikirisha habari za mtazamo naomba uniambie;
kitendo cha mwaume kukufuata na kukutongoza ndio sababu ya wewe kufanya ngono?

Shaka yangu (suspicious reasons); moja kati ya majibu haya ni sababu ya wewe mdada kujihusisha na ngono, ukiachia mbali na kubakwa kwa nguvu.

1.Kutaka, kupenda au kukubaliana wewe mwenyewe
2.Kushawishika kwa sababu wenzio wanafanya
3.Kushawishika na mahitaji (fedha nk.)
4.Tama; ila hii ni sawa na ya kwanza.

Hizo ni sababu shaka zangu, zinaweza zikawepo na zingine ukitaka utatuandikia. Katika sababu nilizozitaja, nyingi zinahusisha ushawishi, kama kweli unampenda Mungu kwa kuyafuata maagizo yake yaliyoandikwa kwenye Biblia, hebu niambie kwa dhati yako; Je kwa sababu ya kushawishiwa basi ndio sababu ya wewe kufanya ngono ???

NB: Mmhh! ni hatari sana usipokuwa na mtazamo sahihi juu ya mahusiano yako ya kimapenzi mdada.

KWANINI WADADA NDIO MZUIE NGONO KWENYE JAMII.

Ninawazungumzia wadada kwa lugha ya kistaarabu sana nikiwaita mabinti, kwani ndio chumvi ya mapenzi. Unajua kabisa kuwa Mungu alimleta mwanamke ili kukamilisha ubinadamu wa mwanaume, lakini wote ni kitu kimoja. Bila mwanamke mwanaume hajakamilika. Nikufikirishe maswali haya tena;

Kwa mabinti, Je ulishawahi kufuatwa na mwanaume ukakataa, alifanya ngono na wewe?
Kwa wanaume wanaosoma ujumbe huu; ulipomfuata mwanamke akakukatalia, je ulifanya nae ngono?

Swali langu la pili linafanana na la kwanza lakini yote kwa pamoja jibu lake ni haikufanyika ngono. Lakini kwa binti mpumbavu jibu lake ni hili, kumkatalia huyu na kumkubalia mwingine na kwenda kufanya nae ngono. Mwanaume alipokataliwa aliondoka zake na kwenda kujaribu kwa wengine, waliokuwa wapumbavu walimkubalia na kuungana nae kuifanya ngono. Mwanaume anafanya ngono kwa sababu anapata ridhaa yako. Kuwa makini na elewa sawasawa hakuna sababu kwa Mungu, eti mimi nilifanya ngono kwa sababu nilishawishiwa. uliona wapi kwenye Biblia ikasema usifanye ngono! ila tu ukishawishiwa! (kukaa karibu na mahakama sio sababu ya kujua sheria) kwa mwanaume yeyote hisia kali zipo kwa mwanaume aliye kamilika. Lakini je si ingekuwa heri kama angekosa binti wa kufanya nae ngono, Mabinti nao wakataka mahusiano kwa hekima za kimungu? Sasa mabinti wote ninaamini mmenielewa ninaposema mna uwezo wa kuzuia mfumko wa ngono kwenye jamii! Pia ninapozungumzia habari hizi moyo wako unaweza kujibizana na maandishi haya kwamba sasa mbona mimi ninaye mmoja tu nab ado hatujafanya tendo la ndoa, la-hasha! mimi sizungumzii idadi ya wapenzi; uwe naye, uwe nao au usiwe naye mimi sijali. Habari hizi mimi nazungumzia kuhusu ngono tu.

NB: Wako wapumbavu wengine wanaowaza mioyoni mwao, hakuna wewe… mbona ninafanya na maisha yanaendelea!!!
Ninapotumia neno upumbavu simtukani mtu, kasome kwenye Biblia limetumika kwa maana ileile ninayoimaanisha mimi.

Hapa naomba nianze kwa kukupa mfano wa kimanunuzi tu usihofu utaelewa tu; Huwa ikiitishwa tenda yoyote mwisho wa siku huchaguliwa mshindi. Hukabidhiwa tenda na kazi kuanza (hii ni kwa ufupi). Fikiria kama wewe ndio mtoa tenda (serikali), inafika wakati wa kukabidhi tenda unakuta kazi imefanyika kwa kutokukamilika, ukiuliza kwa nini unaambiwa fedha imekwisha! na wewe ulitoa fedha kamili. Au wewe unatoa fedha kamili kumpatia mwanao atumie kwa muda Fulani, bila kuwepo kwa mabadiliko ya bei lakini kabla ya muda huo kufika anakwambia imeisha kwa sababu zisizo na msingi. Je itakuwaje? Namaanisha nini kuuleta mfano huu; Mungu alikupatia mwili na moyo wenye hisia za kimapenzi, Mungu kama mtoaji, wewe kama mpokeaji, je unauendeshaje mwili wako. Inaposemwa usifanye uasherati alimaanisha ukifanya utapata dhambi! na sio utapata magonjwa (maana wengine wanadanganyana kutumia kondom nk.). Ingekuwa heri kama kila binti angeijua kweli ya mapenzi. Lakini angalia sasa mapenzi, yamefanywa fani yaani ndio ujanja na ukisasa leo. Angalia sasa watoto wadogo walivyoichosha miili yao kwa ngono, inasikitisha sana. Unapojisemea moyoni mwako mbona maisha yanaendelea...unajua dhana hiyo imesababisha mtafaruku kwenye jamii kiasi gani.

1.Nusu ndoa; mwanaume akishakuzalisha ukifika wasaa wa kuoa anagundua mwili wako umechoka anaahirisha na kukuacha.(inawaumiza sana kisaikolojia)
2.Kutokuolewa, hii ni kwa baadhi kutokuolewa kabisa kwa sababu ya miili yao kuchoka sana na ngono.
3.Kukosa watoto (ugumba); hii ni kwa sababu ya kutoa mimba nyingi ili uonekane hujazaa.
4.Mfumuko wa watoto wa mitaani; hii ni kwa sababu ya kukosa malezi ya baba na mama, mtoto anahitaji malezi ya baba na mama!

Niliyoyasema yanatosha kukukumbusha habari za ngono, nimalizie kwa kusema hivi, kama hujaanza ngono na umeyasoma maandishi haya basi ongeza ujasiri wako kuikataa kabisa ngono, kama umejihusisha nayo na umeyasoma maandishi haya sasa nakushauri kwa moyo wa huruma kwamba acha kabisa, mgeukie Mungu akupatie hekima ya kuyakabili mapenzi kwa jinsi ya maagizo yake. Umefanya ngono ndio! Hilo sio kosa kosa ni kukaidi kuacha. lakini pia tambua kosa lako linasameheka hivyo mtafute mchungaji wako mweleze habari zako ili akusaidie kwa kuomba sara ya toba.
Utukufu wa maandishi haya apewe aliyeniwezesha. Haleluya!!! kwa kadri roho alivyoniongoza kuyaandika maandishi haya juu ya wadada kuzuia mfumko wa ngono kwenye jamii, ninaamini umejifunza kitu, Mungu akusaidie kukifanyia kazi na mwenendo wa mahusiano yako yampendeze Mungu na si kuwapendeza marafiki au ndugu zako. Lakini mwenye nafasi kubwa ya kuacha ni wewe mwenyewe ndio maana Biblia inasema “acha” haisemi Mungu akuachishe, hii ni kwamba jukumu la kuacha umepewa wewe na mimi. Basi na mioyo yenu iimbe; “Ni Yesu huyo ni Yesu huyo!!” maana ndiye anayeniwezesha. Sifa na utukufu apewe yeye.

ASANTENI WOTE;
NDUGU YAKO KATIKA KRISTO;
MWENGO V.

Comments