UHUSIANO WA SADAKA YAKO KWA MUNGU



Uko uhusiano mkubwa sana wa mtoaji sadaka na MUNGU wake. Sadaka yako inakujengea wewe mtoaji na MUNGU mpokeaji uhusiano mkubwa sana wa kibaraka, kukubarika na MUNGU ikiwa sadaka yako imegusa moyo wa MUNGU kweli.

Lakini pia uko uhusiano mkubwa sana kwa yule mtoaji wa sadaka kwa miungu au kwa waganga. Sadaka yako au fedha yako au wanyama wako unaoagizwa na huyo mganga kutoa hakika unajenga uhusiano nae.

Sadaka yako inajenga na kuimarisha agano kati yako na MUNGU. Anachokifanya MUNGU kwako ni kikubwa mno hasa ni kuachilia baraka za Ibrahimu zikujie na ulinzi wake. Na ikiwa sadaka zako unapeleka kwa miungu hakika ujue kuwa wewe ni mtumwa wa shetani na baraka uzipatazo ni za kitambo kifupi sana tena zimejaa masharti mengi.

KUMBUKA, mahali fedha yako au sadaka yako ilipo ndipo na moyo wako ulipo, palipo na moyo wako ndipo na imani yako ipo. Mathayo 6:21, Luka 12:34.

Ni kweli fedha yako ilipo hapo na moyo wako upo hapo, kama kwa MUNGU moyo wako uko kwake. Kama umewekeza kwa mganga daima moyo, imani yako ipo huko. Hiyo fedha imekujengea mahusiano na huyo mganga.

KANUNU SABA (7) ZA UHUSIANO WA SADAKA ZAKO KWA MUNGU

1. Kibiblia, sadaka zako unazotoa kwa MUNGU huwa zinakufanyia agano la mahusiano na MUNGU hasa pale unapotia sadaka yenye harufu nzuri ya kumridhisha MUNGU. Mwanzo 8:20-21. MUNGU akasema na kufunga agazo na Nuhu kwamba hatailaani nchi tena. Nuhu alitoa sadaka iliyogusa moyo wa MUNGU. Malaki 2:2-5.

2. Sadaka inakufanyia upatanisho na MUNGU. Sadaka inakufutia dhambi, sadaka inakujengea daraja wewe la kumfikia MUNGU, sadaka inakuhuhisha na MUNGU wako. Warumi 5:9-10, Yeremia 32:36-41.

3. Sadaka inaonyesha upendo wako ulivyo kwa MUNGU wako. Sadaka yako inaonyesha moyo wako ulivyo, uaminifu wako ulivyo kwa MUNGU wako. Hivyo, kwa njia ya sadaka zako unaweza kuona jinsi uhusiano wako ulivyo na MUNGU.

Tukumbuke sana habari ya Kaini na Habili. Mwanzo 4:3-7, Luka 21:1-9. Habili anapata kibali na Kaini anapata laana na alama. Tujiulize, sadaka zetu zinapata kibali au laana na alama? Malaki 2:2-5.

4. Sadaka yako inaonyesha moyo wako wa shukrani kwa MUNGU wako jinsi ulivyo. Kumbuka MUNGU amekutendea mambo mengi katika maisha yako kutoka kuzaliwa, kukua, kazini kwako. Sadaka pekee ndio inakuonyesha moyo wako wa shukrani kwake na ndipo MUNGU anatengeneza uhusiano wake na wewe. Zaburi 116:12, Zaburi 136:1, Mithali 8:18.


5. Sadaka yako unayotoa inakuonyesha wewe jinsi unavyomheshimu MUNGU wako kwa vyote ambavyo MUNGU amekufanyia maishani mwako. Kwa mafanikio yako yote unapaswa kumheshimu MUNGU. Mithali 3:9, 3Yohana 1:2, Zaburi 116:12.

6. Sadaka yako inaonyesha utii wako kwake kwa kile ulichokisikia. Kutoa kwako kunaonyesha utiifu wako kwake, hivyo MUNGU kupitia sadaka yako anaimarisha uhusiano wako naye. Kumb. 28:1, Yohana 17:21-24.

7. Sadaka yako inakutambulisha kuwa vyote ulivyonavyo ni mali ya MUNGU, tumepewa kama mawakili tu. Hivyo kutoa kunaonyesha uaminifu wetu kwa MUNGU. Zaburi 24:1, 1Korintho 4:1-2.

BARIKIWA

Comments