VIZUIZI VYA KUSHINDWA KUFANYA HUDUMA YA MUNGU IPASAVYO.* sehemu ya nne*

Mtumishi Gasper Madumla



Bwana Yesu asifiwe…
Haleluya…

Kumbuka kwamba tunachoangalia katika fundisho hili ni sababu za msingi zinazowafanya watumishi au mkristo yeyote Yule kushindwa kufanya kazi ya Mungu ipasavyo.
Sababu hizo zinazomzuia au kumfanya mtu aliyeyebeba huduma ya Mungu isiweze kuifanya katika viwango vya juu.
Sababu hizi hujulikana kama VIZUIZI au VIKWAZO.

Zipo sababu mbili zilizowafanya wanafunzi wa Yesu kushindwa kufanya huduma ya Mungu ipasavyo, Kupitia andiko letu la msingi la Mathayo 17 :14-21

Nazo ni :
• Upungufu wa imani
• Kushindwa kuishi maisha ya kufunga na kuomba

*(Fuatilia sehemu zilizopita ili uelewe kiundani maana ya “ Upungufu wa imani ” ambayo ni Kizuizi/sababu ya kwanza ya fundisho hili. )
Leo tunaendelea pale tulipokuwa tumeishia,

JE NINI DAWA YA IMANI PUNGUFU ?

01.Kusikia mara kwa mara neno la Kristo.( Warumi 10 :17)

Imani ni mbegu inayostahili kupandwa na kumea ndani ya roho zetu. .Nasema ni mbegu,
Mbegu ndio yaweza kumea na kuwa mti,mti mkubwa mithili ya mti wa mbuyu.Kuna gharama kubwa unazotakiwa kulipa ili imani yako iwe kama mti wa mbuyu,
Gharama ya kwanza kuacha vyote kwa ajili ya Bwana na sio kumuacha Bwana kwa ajili ya vyote.
Nasema ghalama ya kwanza ya kutibu ugonjwa wa UPUNGUFU WA IMANI ni KUACHA VYOTE KWA AJILI YA BWANA.

-Maana ya kuacha vyote ni kukubali kumtegemea yeye kuwa ni Mungu pasipo kumtegemea yoyote Yule,ni kumtanguliza Mungu kwanza katika kila jambo ulifanyalo,Maana yake ni kuwa na Mungu mmoja tu…

02. Kuishi maisha ya utii wa neno la Mungu.
Baada yakusikia neno la Mungu,kisha IMANI ikatengenezeka ndani ya mwamini,Sasa kinachotakiwa ni kutii sauti ya Bwana.

*Hakuna imani pasipo kuishi maisha ya utii wa Neno la BWANA MUNGU.
Kutokutii sauti ya Bwana ni Sababu/Kizuizi cha kushindwa kuitimiza huduma ya Bwana iliyopo ndani yako.
Ikiwa Yeye Bwana Yesu ambaye ni kielelezo chetu,alikuwa ni mtiifu hata kufa. (Wafilipi 2 :8 )

Yatupasa pia,na sisi tutembee katika maisha ya UTII ili tumuone Bwana Mungu kwa namna ya tofauti.
Labda ngoja nikupe mifano miwili ya watu wa Mungu walioshindwa kutii sauti ya Bwana.

Kwanza tumtizame
SAULI.

Pale Sauli aliposhindwa kutii sauti ya Bwana (1 Samweli 15: 1-34 )
Biblia inasema Bwana akamuacha Sauli mara moja,
Kisha ufalme wake Sauli akapewa Daudi aliyeupendeza moyo wa Bwana.Tena roho ya BWANA ilimuacha Sauli ( 1 Samweli 16 :14) baada tu yakushindwa KUTII sauti ya Bwana Mungu.

Tazama pia mfano wa pili ni Musa mtu wa Mungu.
Musa alishindwa kutii sauti ya Bwana,
Basi hapo hapo ikawa ni chukizo kwa Bwana.
MUSA ambaye alifanya vizuri tu,lakini pale aliposhindwa kusikia na kutii sauti ya Bwana,ilikuwa ni kwazo /Kizuizi cha kumfanya ashindwe kuingia katika nchi ya ya ahadi.

Tunasoma Hesabu 20 :7-8,11
“ Bwana akasema na Musa, akinena,
Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao.
11 Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.”

Katika andiko hilo,tunaona Musa akiambiwa na Bwana Mungu,kwamba ATWAE FIPO YAKE,KISHA AKAUAMBIE MWAMBA UTOE MAJI,Lakini tunaona akashindwa kutii hilo agizo la Bwana Mungu kisha badala ya KUUAMBIA mwamba utoe maji
,Bali yeye akaupiga,ilikuwa ni kinyume na neno la Mungu lisemavyo.
Hivyo ikawa ni machukizo mbele za Bwana.

• Mungu atusaidie sana sisi watumishi wa leo,tuweze kuishi maisha ya kutii neno lake pasipo kulizoelea.

-Maana wengine tayari wamekwishaachwa na Bwana muda mlefu pasipo wao kujijua kuwa wameachwa,maana hata sauli alipokuwa ameachwa na Bwana si kana kwamba alikuwa anajua la hasha!
Alikuwa hajui,lakini akiwa na mshangao mkubwa kwamba mambo yake hayaendi,roho mbaya ikimsumbua.

Sawa sawa na baadhi ya watumishi wa leo wasio ishi maisha ya UTII wa neno la Bwana.Labda nikuulize wewe mpendwa kuwa;

*Je wewe ni mtiifu kwa habari ya neno la Mungu?

Maana kama unashindwa kulipa fungu la kumi tu,basi wewe sio mtiifu!
Kwa sababu hiyo moja kati ya sababu nyingi zilizopo ,yatosha kuzuia huduma ya Bwana usiitimize ipasavyo.Yakupasa kuanza moja na Bwana siku ya leo.

*Wakristo wengi leo wana imani pungufu kwa sababu ya kuwa mbali na maisha ya utii wa neno la Mungu.

Haleluya…
Jina la Bwana liinuliwe…

Sasa tujifunze sababu ya pili ambayo ni kizuizi kwako kinachokufanya kushindwa kuifanya Huduma ya Bwana ipasavyo.

02.KUSHINDWA KUISHI MAISHA YA KUFUNGA NA KUOMBA.

Tunasoma Mathayo 17 :21:
“ 21 [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] ”

Hii ilikuwa ni habari ya wanafunzi wa Bwana Yesu walipokuwa wameshindwa kufanya kazi ya Kristo IPASAVYO ndipo mtu mmoja akamwendea Bwana Yesu akimpelekea mashtaka kwamba wanafunzi wake WAMESHINDWA KUMPONYA MWENYE PEPO.
Ndipo Yesu akawaambia ;
“ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]”


Watu wengi wamepotosha maana halisi ya andiko hili,kwa kutafsiri kwamba tupatapo tatizo ndipo tufunge na kuomba juu ya tatizo hilo.Andiko hilo halina maana hiyo,Bali maana halisi ya andiko hilo ni kuishi maisha ya kufunga na kuomba, pasipo hata tatizo kuonekana.

Wengi leo wanafahamu ndivyo sivyo juu ya andiko hilo,yamkini hata wewe usomaye ulikuwa unajua hivyo.Bwana Yesu anasisitiza kuhusu habari ya maisha ya kufunga na kuomba. Mkazo alioutoa Bwana Yesu ni kwa sababu anajua maisha ya kufunga na kuomba ni silaha tosha dhidi ya mapepo na ufalme wao.

Sikia ;
Wanafunzi wa Bwana Yesu walipokuwa katika hali yao ya maisha ya kawaida,gafla mtu mmoja akamletea kijana wake mwenye pepo wachafu. Wanafunzi hawa walikuwa hawategemei kabisa kuletewa mgonjwa wa namna ile maana kila kitu kwao kilikuwa shwari.
Gafla walipoletewa Yule kijana mwenye pepo,nao wakaanza kuomba,kisha waliposhindwa kumtoa yule pepo ndipo tunaona sasa Bwana Yesu akisema kuwa
“ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] ”



Mtumishi Gasper Madumla
Hii ikimaanisha kuwa ,kama hawa wanafunzi wange’faulu kumtoa Yule pepo basi Bwana Yesu asinge’lisema maneno haya “ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] ”
Bwana Yesu aliwaambia hivyo kwa sababu maisha yao yalikuwa ni kula na kunywa muda wote maana wakitumainia uwepo wa Bwana Yesu aliyekua akitembea nao muda wote,

Hata kujiuliza kwamba, ya nini kufunga na kuomba ikiwa Bwana harusi tuko naye ? ndio maana Yesu anawaambia “ [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] ”
Yaani kwa maneno mengine ni sawa na kusema “ iliwapasa muishi katika kufunga na kuomba siku zote ” Na hiyo ndio maana halisi ya mstari huo (Mathayo 17 :21)…

ITAENDELEA…
UBARIKIWE.

Comments