HATUA KUELEKEA WOKOVU

Mwl Sospeter Simon S. Ndabagoye.
New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania

Kuokoka ni mpango wa Mungu,kwa mwanadamu katika kuishinda dhambi. Ifahamike kuwa, wokovu ni mpango wa Mungu kumtafuta mwanadamu, aliyepotea, kupitia dini, Roho mtakatifu na watumishi wake. Mara nyingi, mwanadamu amekuwa akijiuliza, afanye nini ili kuishinda dhambi? Ni dhahiri kuwa, hakuna njia yoyote ya kuishinda dhambi, nje ya kumpokea Yesu Kristo, kupitia wokovu.

Hatua ya Kwanza, ni sharti ujue kuwa Wewe ni mwenye dhambi, na umepotea!Hivyo unahitaji kuifuata njia ya kweli, ambayo ni kupitia Wokovu kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Biblia inasema"Kwasababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na Utukufu wa Mungu"(Warumi 3:23)

Maneno hayo, yanatudhirishia kuwa, kila mtu amepotoka, na anahitaji kumrudia Mungu wake, atoke upotevuni na kuweza kuwa na utukufu tena. Neno hili ni ushahidi tosha kuwa, wote tunapaswa kuutafuta utukufu wa Mungu "Tukisema hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani mwetu" (1Yohana 1:8) tena "Sisi sote kama kondoo, tumepotea;kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe..."(Isaya 53:6)

Maneno hayo, yanatutaka tujitambue na kujitathimini juu ya ukamilifu wetu, lakini zaidi sana, tunahitaji kutambua wapi tumepotoka na kujirudi. Waswahili wanasema"kupotea njia, ndiyo mwanzo wa kuijua njia" lakini pia kujua tatizo ni nusu ya utatuzi wa tatizo". Mpaka hapa, unapaswa kujitathimini na kujua ulipoanguka, ulipopotea,na kuamua kubadili njia zako.
Ndugu yangu, kuiacha Dhambi, ni jambo la kijasiri na ushujaa mkubwa, na ni jambo la aibu na fedheha kuifuga dhambi ukunyanyase chini ya Ibilisi Shetani. Kuionea aibu dhambi, ni kujadharirisha, na kuitubu dhambi ni kuiaibisha na ni tendo la kishujaa.

Hatua ya Pili, Lazima ujue kuwa huwezi kujiokoa mwenyewe, ila inakutaka uchukue Uamuzi mwenyewe " Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako, ya kuwa ni Bwana , na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”(Warumi 10: 9&10).

Pia ni sharti ijulikane kuwa, njia pekee ya wokovu ni Yesu Kristo, na wala hakuna njia nyingine, "....Mimi ndimin njia , na kweli na uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi" (Yohana 14:6),Lakini ni lazima hili liwe kichwani mwako kuwa njia pekee ya kufika mbinguni, nikufanya maamuzi ya dhati ya kumtafuta Mungu, na kujitoa kwa Yesu kikamilifu" Mtu asipozaliwa mara ya pili,hawezi kuuona ufalme wa Mungu" (Yohana 3:3).

Hatua ya Tatu, Ndugu yangu mpendwa, ni sharti ujue kuwa, Unahaki ya kuokoka, na haki hii, umepewa kama neema kutoka kwa Mungu, unachotakiwa kufanya ni kuamini tu,
"Kwa maana mmeokolewa kwa Neema, kwa njia ya Imani....ni kipawa cha Mungu, wala si kwa matendo.....(Waefeso 2:8&9).

Hatua ya Nne, ni sharti ujue kuwa Kuokoka ni Mpango wa Mungu juu yako, ndiyo maana akauvaa uwanadamu na kuja duniani na kutufia msalabani. Kuja kwa Yesu duniani, ulikuwa ni mpango kamili wa Mungu juu ya kuwakomboa wanadamu waliopotea. “ Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kilichopotea” (Luka 19:10). Na tena, alikuja kuwaokoa waliopotea,”Ni neno la kuaminiwa,tena lasitahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu, alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi’ ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Timotheo 1:15). Kwa kauli hii, kukataa kuokoka ni kupinga mpango wa Mungu wa kumwokoa mwanadamu, hivyo ni dhambi. Pia kukataa kuokoka ni kumpinga Kristo, na hili ni upinga Kristo, ambayo ni roho ya Ibilisi, hivyo ni dhambi, ndiyo maana Biblia inasema”Kuokona ni lazima” na kumpinga Yesu, ni Uasi.

Hatua ya Tano, Katika hili, lazima ujue kuwa, wokovu ni zao la upendo wa Mungu kwa wanadamu, “Bali Mungu alionyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwaajili yetu,tulipokuwa tungali wenye dhambi.(Warumi 5:8) hatua ya kuokoka, inakutoa kwenye dhambi, na kukuweka kwenye hali, na kukataa kuokoka, ni ishara ya makusudi ya kwendelea kumpinga Mungu, na kukataa kupendwa na Mungu, aliye muumba wako. Hivyo, ni kumuunga mkono Ibilisi, na kuuangusha utawala wa Mungu kwa kuujenga utawala wa Ibilisi.

Hatua ya Sita, ni lazima ukubali kutubu. Dhana ya kutubu, inafasiliwa kuwa ni kugeuka, yaani kuziacha njia mbaya, kwa kuzifuata njia njema. Kugeuke kutoka kumwelekea shetani, na kumwelekea Mungu. Hili huambatana na kuziacha dhambi kwa moyo wote, na kuzijutia dhambi, na kuomba toba kwa Mungu, na kujifunza kuzifuata njia zake.
Biblia inasema ;-
“Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana “(Matendo ya Mitume 3 :19)
“Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki, aache mawazo yake ; amrudie Bwana, naye atamrehemu ; na arejee kwa Mungu wetu, naye atamsamehe kabisa” (Isaya 55 :7).
Hili ni ushindi kwake ajitambuwae na kuamua kuchukua hatua ya kumrudia Mungu. Hatua hii, humpendeza Mungu, na humfanya Mungu amheshimu mtu huyu.

Hatua ya Saba, Lazima ukiri dhambi zako kwa Bwana Yesu Kristo, na unyenyekee ili akusamehe. Ni Yesu pekee mwenye uwezo wa kuokoa, kusamehe dhambi na kukufanya kiumbe kipya. “ ...hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwamaana hapana jina jingine chini ya mbingu waliopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Matendo ya Mitume 4:12). Ni lazima, uwe na ujasili katika kumpokea Yesu Kristo, ili upate utu upya, na kuwa mtoto wa Mungu.

Hatua ya Nane, uwe mkweli na muwazi kwa Yesu Kristo, ili uwe huru kwa Yesu. Usiwe na mnafiki wala usifiche dhambi hata hata moja, kuwa wazi mbele za Mungu. Biblia ianaeleza “ Afichaye dhambi zake, hatafanikiwa,bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema” (Mithali 28:13)

Hatua ya tisa, Ujue dhahiri kuwa, Mungu yuko tayari kukupokea na kukurudisha kundini. Kuwa tayari kufanya maombi, na kusoma neno la Mungu. Kuwa na hamu ya kuzungumz na Mungu kila mara. Fanya bidii katika kuomba.(Isaya 55:6) “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, mwiteni , maadamu yu karibu” pia “Ndipo mtaita, na Bwana ataitika, utailia, naye atasema, mimi hapa...”(Isaya 58:9). Ukweli ni kwamba, ukimwita Mungu kwa dhati, hakika, hatanyamaza kamwe “Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa”(Matendo ya Mitume 2:21). Muda wote, Mungu huwatafuta wale wamtafutao kwa moyo wote, na kwa dhati, ili awaokoe.

Hatua ya Kumi; Lazima, ukubali kuwa mwana wa Mungu. Hili haliwezekani, mpaka kwanza umpokee Yesu moyoni mwako, awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako.
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” (Yohana 1:12)
...ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya Kuwa Mungu alimfufua katika wafu,utaokoka” (Warumi 10:9)

Hatua ya kumi na moja, Uamini kuwa Mungu yupo, na Yesu ni mwana wa Mungu, ndiye anayeokoa, na ndiye njia pekee ya kukufikisha mbinguni. Uwe na imani ya dhati moyoni, na umtafute Mungu rohoni, kwa nia ya dhati yote. Umpende Mungu, na muda wote uwe na imani kuwa hayuko mbali.” Lakini hizi zimeandikwa, ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake” (Yohana 20:31). Na wala Mungu hata mwacha amtafutaye kwa moyo wote kila kukicha “ Kwa maana, mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao” (Waebrania 11:6).

Maombi Maalum.

Mungu ana haja nawe uliyesoma ujumbe huu, Mungu yuko tayari kukupokea na kukurudusha kundini.......Kwa imani kabisa, fuatana nami katika sala hii:-
Bwana Mungu, nakushukuru kwa kuniona na kunifunulia dhambi zangu mbele ya macho yangu, nakili kuwa mimi ni mwenye dhambi na nahitaji neema yako uniokowe kwa maana siwezi kujiokoa mwenyewe. Naomba, rehema zako Bwana, kupitia jina la Yesu, Uniokowe na kuzifuta dhambi zangu zote na kunifanya kiumbe kipya. Naomba unihurumie, unisamehe na kunisafisha kwa Roho wako mtakatifu. Uniondolee hamu ya kutenda dhambi, na kunipa roho ya kukupenda, kukutumikia, na kukutafuta uso wako kila siku.

Ninaamini, umenisikia, umeiona dhamira yangu kwako, na utazidi kunipa ushindi dhidi ya hila za shetani, utazidi kunipa nguvu, uwezo na mamlaka ya kumshinda shetani na mawakala wak; Kwa Jina la Yesu naomba huku nikiamini. Amen
“ Kwala hiyo, Mungu amekusamehe dhambi zako zote, na wala huna deni tena mbele yake, dumu katika kutenda mema na kuomba. Tenga muda wa kusoma Biblia, hudhuria Ibada zinazoendeshwa katika Kanisa la Kiroho lililo karibu nawe, kadri Roho wa Mungu atakavyokuongoza, kuwa karibu na watumishi wa Mungu, ili wakusaidie kukupa huduma nyingine za Muhimu ikiwa ni pamoja na mafundisho ya neno la Mungu zaidi.”
Makala hii imeandaliwa na:
Mwl Sospeter Simon S. Ndabagoye.
New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania

Comments