ILI MUNGU AKUKUMBUKE,SHARTI UJISAHAU KWANZA WEWE MWENYEWE, HUKU UKIMWEKA MBELE YEYE.



Mwl Sospeter Simon S. Ndabagoye
New Elshaddai Ministries NEM-Tanazania


Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwakuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii; Wale waufuatao mwili, hawawezi kumpendeza Mungu........je hujaona hili (1Wakorintho 15:50) "ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu, haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala uharibifu kurithi kusiko kuharibika"
Tena Paulo akasema akiliambia kanisa la Galatia kwenye waraka wake
"Enendeni kwa roho, wala hamtazitimiza tamaa za mwili.Kwasababu mwili hutamani ukishindana na roho na foho hushindana na mwili; kwamaana hizi zimepingana,hata hamwezi kufanya mnayotaka" (Wagalatia 5:16-17)
Ndugu zangu, kumbukeni hata Yesu alisema,"kesheni mwombe,msije mkaingia majaribuni; roho i radhi,lakini mwili ni dhaifu.(Mathayo 26:41). Yeye kama Mungu kamili, alijua kuwa, mwili ni chanzo cha matatizo siku zote, ndiyo maana akaonya juu ya kuusikiliza udhaifu wa mwili na kuufuata!Hapa ana maana kuwa, kuufuata mwili ni kunyume na mapenzi ya Mungu, kwakuwa mwili daima huidanganya roho ili kuiangamiza. Ni katika kuusikiliza mwili, mwanadamu ataweza kuingia majaribuni, hii inamaana kwamba, endapo utausikiliza mwili na kuutii, hutaitii sauti ya Mungu wala sheria yake.
Mungu anataka sote,tumsikilize yeye na kuyafuata maelekezo yake.Anataka, tuiweke sheria yake mioyoni mwetu na kuifanya kuwa ndiyo kiongozi wetu. Ndiyo maana Daudi anasema:-Moyoni mwangu, nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi (Zaburi 119:11). Mungu anawataka watu kama hawa hivi leo, ambao wanatamani sheria yake iwaongoze, watu watakao jisahau wenyewe na mambo yao na kuyaweka mbele mambo ya Mungu kwanza. Rafiki yangu, naomba uelewe kuwa, Mungu hatakusau endapo utakuwa mwanifu kwake, Mungu anawaheshimu sana watu wanaoishika sheria yake. Ndiyo maana, akadiriki kuwaita mboni ya jicho lake. Mungu anataka watu wanaompenda kwa Moyo wote, nguvu zote na akili zote......yaani watu waliojitoa wenyewe, na ujuzi wao wote, mali zao zote na nguvu zote walizonazo. Mungu anakutaka, utumie kila ulichonacho kumtukuza yeye na kwaajili ya kazi yake, ili baada ya hapo ujifunze kumcha ili kwamba aweze kukubariki. Ndiyo maana neno linasema, "Utafuteni kwanza, ufalme wa Mungu, na hayo yote, mtazidishiwa"
Ndugu zangu, neno la Mungu linatuonya mahali pengi juu ya kumpenda Mungu ikiwezekana hata zaidi ya vile tunavyojipenda ili yeye ashughulike na masiha yetu yeye mwenyewe.Paulo anatuonya juu ya kunyenyekea, kuitii na kuifuata sheria ya Mungu, ili aingilie kati maisha yetu, aondoe taabu zetu, aondoe magonjwa yetu, ili aondoe kila laana na mikosi. (1Petro 5:6-7) Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari ili awakweze kwa wakati wake, huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote kwamaana yeye, hujishughulisha sana na mambo yenu. Ndugu yangu mpendwa, neno la Mungu ni hakika, ni pumzi ya Mungu iliyo hai,tena neno hili limehakikishwa kuwa ni kweli iliyotimia! Naomba nikwambie kuwa, Mungu anatamani, aone umejisahau, akuone uko busy na mambo yake, akuone kuwa mawazo yako yote umemwelekezea yeye tu, ili sasa, aingilie kila linalokuhusu!Neno la Mungu halisemi uongo wala halitasema uongo na wala Mungu si mwanadamu hata awe kugeugeu, mwamini leo Mungu, ujitoe wewe kwa nguvu zako zote, kwa akili yako yote na kwa moyo wako wote ili aingilie maisha yako.
Siyo umpende Mungu nusu nusu,hapana! Mpende kikweli kweli, uwe tayari kujitoa mzima mzima. Mkumbuke Ibrahimu alivyomtoa Isaka awe sadaka ya kuteketezwa kwa Mungu (Mwanzo 22:1-14) Ni baada ya Ibrahimu kumtoa Isaka, ndipo Mungu alipomtuma Maraika wake na kumlekeza alipo kondoo wa kuchinjwa kwaajili ya Sadaka, lakini hapa neno liko wazi kuwa,Mungu alitenda yale kwa kuwa Ibrahimu, alijisahau kwanza, akamuweka Mungu mbele, ndipo Mungu akambariki sana. Hata leo,tunapaswa kuitii sauti na Sheria ya Mungu, kama ni kumtuikia Mungu tutumie kila nguvu/akili na uwezo wote, kuhakikisha tunauinua ufalme wa Mungu, tujenge nyumba za ibada, tuweke mapambo, tutowe sadaka, tutii sauti ya Mungu, tunyenyekee kwa Mungu. Tutoe Muda mwingi kumwabudu Mungu, ili aweze kutukumbuka. Kama uko ofisini, umweke mbele yeye, wakati uko dukani,umweke mbele yeye, kama unasoma, umtangulize yeye!kwa lolote unalofanya, ujisahu kwanza, uone unafanya kwaajili yake kwanza, na hapo ndipo Mungu ataonekana katika maisha yako. Usikubali taabu yako ikutenge na sauti ya Mungu, usikubali umasikini wala njaa vikutenge mbali na Mungu, simama imara, naye atakutetea.

MUNGU AWABARIKI NDUGU ZANGU WAPENDWA, MUNGU AZIDI KUWAINUA, NA KUWAFUNULIA MAMBO MAKUBWA YA SIRINI ZAIDI, MDUMU KATIKA KUMPENDA YEYE, NA KUISHIKA SHERIA YAKE DAIMA.

Mwl Sospeter Simon S. Ndabagoye
New Elshaddai Ministries NEM-Tanazania.

Comments