Mchungaji Maximillian Machumu |
Na Mchungaji Maximillian Machumu (RP)
Ujumbe huu ni ujumbe ambao waweza kubadilisha maisha yako kama utaamua
kufungua moyo wako, kwasababu mwenendo wa maisha waweza kukufanya uhisi
kuwa hakuna matumaini lakini leo baada ya kusoma somo hili unaenda kuona
mwanga mpya kwenye maisha yako.
Ezekieli 37:11 "kisha akaniambia, mwanadamu mifupa hii ni nyumba yote ya
Israeli tazama wao husema mifupa yetu imekauka matumaini yetu
yametupotea, tumekatiliwa mbali kabisa"
Ukiendelea kufuatilia kwa karibu kwa habari ya Ezekieli utagundua sababu
ya Mungu kumleta katika bonde lile lililojaa mifupa. Kwanza, Imani ya
Ezekieli ilikuwa imani yenye matumaini. Ingawa hali halisi ya mifupa
ilikuwa imekwisha kauka, yeye alibaki na tumaini kuwa mifupa ile yaweza
kuishi.
Hatua kubwa sana ya kudhihirisha kuwa mtu anamjua Mungu, ni ile ambayo
mtu mmoja katikati ya vita, au hali za kukatisha tamaa, au hana
analolitegemea katika maisha yake lakini bado anataja mambo yajayo,
anataja matendo makuu ya Mungu.
Mungu hapendi ukate tamaa, wala umkufuru yeye katikati ya magumu na kwa
taarifa yako tu ni kuwa watu wakubwa katika biblia hata walioitwa na
Mungu, walipitia magumu lakini katikati ya magumu hayo walitamka maneno
ya ushindi. Pia, kutamka maneno ya matumaini katikati ya magumu
kunakufanya utoke mapema kwenye hali mtu aliyoko.
Inawezekana unapitia katika hali ngumu kwa sasa, lakini utakalolinena
ukiwa katika dhiki hiyo itakufanya ama utoke ukiwa shujaa au
aliyeshindwa. Na ndio maana hata Ezekieli alipowekwa mbele ya mifupa
mikavu na kuulizwa 'je mifupa hiyonyaweza kuishi?' Naye alijibu kuwa
'wewe Bwana wajua', akionyesha kuwa hakuna jambo la kumshinda Bwana. Na
ndio maana hata alipopewa nafasi ya kutamka neno alitamka uzima. Ni
muhimu kujua maneno ya kutamka pindi unapopitia katika hali ngumu.
Ni muhimu kujua unachokiongea leo ndicho utakachokiishi kesho; wengine
hujikuta wanaongea maneno mabaya juu yao wenyewe, huku wakisahau kuwa ni
shetani ambaye anawafanya waongee maneno hayo ili apate nafasi ya
kuharibu maisha yao baadaye.
Isaya 57:10 "ulikuwa umechoka kwaajili ya urefu wa njia yako, lakini
hukusema hapana matumaini, ulipata kuuhishwa nguvu zako, kwasababu hiyo
hukuugua" kumbe watu hawa, hali yao halisi iliwafanya wakate tamaa ya
kufika wanapokwenda lakini pamoja na urefu wa njia bado walikiri kuwa
matumaini yapo. Na kwasababu ya ukiri huo walipewa nguvu mpya. Usikiri
udhaifu, Mungu anayetenda miujiza yupo na ukimkimbilia yeye, ataiondoa
aibu yako na kukuvika kicheko.
Ukifuatilia habari ya Yusufu ambaye maisha yake yalianza kwa kuuzwa na
ndugu zake kwa wamisri. Na alipouzwa waliigawa kanzu yake maana yake
aliuzwa bila mavazi, lakini akiwa Misri na matumaini yakaanza kuja
likatokea jambo jingine la kukatisha tamaa. Mke wa potifa akamsingizia
kuwa anataka kumbaka, hivyo akatupwa gerezani maisha katiaka hali hiyo
ni dhahiri kuwa Yusufu alikata tamaa kabisa. Lakini alipotoka gerezani
Yusufu akawa waziri mkuu, jiulize, Mungu aliyemfanya kuwa waziri mkuu
alikuwa wapi kipindi anauzwa? Au jiulize alikuwa wapi kipindi anawekwa
gerezani?
Ni muhimu kujua kuwa sio kuwa kwa unayopitia hali ngumu ukahisi Mungu
amekuacha, si kweli; Mungu bado yupo pamoja na wewe na matumaini bado
yapo. Yesu Kristo ni tumaini la kutosha kwenye maisha yako. Leo sikia
sauti yake hii ikisema BADO YAPO MATUMAINI. Pata muda kuingia kwenye
maombi na Mungu anakupa tumaini jipya leo. Inawezekana unapitia shida za
ndoa, matatizo kazini, vita shuleni, roho ya kukataliwa mpaka umejihisi
hakuna kesho ile uliyoiwaza. Leo tambua kuwa hata Ayubu katikati ya
dhiki kuu hakuwahi kumkufuru Jehova bali aliweka tumaini lake kwake na
kwa saa sahihi matumaini makuu yalionekana.
Hata kama ndoto yako inaonekana inataka kuzimika, inawezekana ulikuwa na
ndoto za kusoma katika maisha yako lakini sasa unaona muda umeenda
nakwambia bado lipo tumaini. Inawezekana madktari walikwambia kuwa
mwisho wa kuzaa ni miaka 45 na wewe sasa unajiona unaelekea huo umri
ukiwa hauna mtoto lakini nakwambia neno ambalo Yesu amenituma kwalo kuwa
USIKATE TAMAA BADO YAPO MATUMAINI!!!!!
Mchungaji Maximillian Machumu (RP) 12/6/2013
Comments