KUMTAFUTA BWANA MUNGU

Mwl. Sospeter Simon S. Ndabagoye.
New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania.


Lengo Kuu la Somo: Kutambua umuhimu wa neno la Mungu kwetu, umuhimu wa maombi na kujifunza kumtumikia Bwana.
Lengo Mahususi: Kutambua umuhimu wa kumtafuta Mungu, njia ya mwanadamu kumtafuta Mungu yaani Dini na namna Mungu anavyomtafuta Mwanadamu kupitia Wokovu.
Matarajio: Msomaji, kupata uelewa wa kutosha juu ya kumtafuta Mungu na kuwa mwanafunzi Bora wa Yesu Kristo. Namwomba Roho Mtakatifu, asikuache bila kukuhudumia wewe,unayesoma ujumbe huu, Bwana asikupungukie katika shughuli zako,muda huu aulipe kwa wingi wa hekima zake. Usipotee bure Muda huu; kwa jina la Yesu.

Utangulizi.
Neno la Mungun ni Muhimu sana katika maisha yetu, sisi kama viumbe wa Mungu, aliowaumba kwa mpango maalumu wa kiutawala pamoja na yeye. Ifahamike kuwa, “mtu” ni mwili, roho na nafsi. Mtu kama yu hai, maana yake anayo roho, na kama mtu ana roho, ni dhahiri kuwa anamwili, kwa maana, maandiko yanasema wazi kuwa, “Roho, huupa mwili uha”i, na “mwili ndilo hekalu la Roho”.
Kwa kuwa mwili, umejengwa kuwa dhabahu la Roho, kumbe mtu anenapo, basi huyo ni Roho ananeye, awe roho wa Mungu, au wa shetani! Kikubwa hapa, ni kujua kuwa, mwanadamu, huongozwa na uwezo mkubwa wa kiroho, ambao matunda yake, hutuonesha kuwa, roho huyo ni wa MUNGU au la. Ndiyo maana maandiko yanaeleza wazi kuwa, “ulimi hunenana yaujazayo moyo”. Ina maana kuwa, kuongea,huanzia ndani kabla ya kutokeza nje, hushuhudiwa na nafsi.

(1) Roho na Mwili, kipi bora zaidi?
Kwa mtazamo huo tulipata kwatika utangulizi, yatupasa kujua kuwa, kama vile mwili unavyohitaji kula vizuri, kuvaa vizuri, kulala na kupumzika, kuburudika kwa nyimbo na hata sherehe mbalimbali; Roho yako,ni zaidi. Ndiyo maana, maandiko yanasema, “Linda moyo wako,kuliko yote uyalindayo “. Hapa tunapata kujua kuwa, “roho ni bora kuliko mwili”. Kwamaana, mwili, hutoa matokeo ya kilichofanywa na roho. Kwa maneno mengine, ukiona mtu anatukana, jua kuwa, yale ndiyo matokeo ya Roho aliye ndani yake. Kadharika, kama mtu ni mgomvi daima, huyo ndiye roho aliye ndani yake! Je, hujawahi kuona hata watumishi wa Mungu wanasemana na kutupiana vijembe? Basi ndizo roho zinenazo ndani yao.
Zingatia: “Ninachotaka ujifunze hapa ni kuwa, yale ufanyayo, ni uthihirisho wa roho aliyeko ndani yako” hivyo, kama watoto wa Mungu, tunapaswa kuuthilishia umma, kuwa, tunaye roho wa Mungu kwa matendo yetu, wala si kwa kusema tu. Kumbuka neno linasema” imani pasipo matendo imekufa” je, yafaa nini tukiwa na imani pasipo matendo? Daima, tunapaswa kuwa na matendo mema,yatakayothirisha uwepo wa roho wa Mungu ndani yetu.
(2) Roho anapaswa kulelewaje?
(a) Kulishwa neno.
Ndugu yangu, roho aliyeko ndani yako, anapaswa kulishwa vyakutosha. Biblia inasema, “Neno la Mungu ni chakula cha roho” tena “neno la Mungu ndiyo uzima” kumbe, ili tupate uzima, ni lazima huyu Roho ashibishwe vya kutosha kupitia maandiko matakatifu ya Mungu yaitwayo Biblia( Rejea, karatasi ya kwanza na ya pili kwenye Biblia yako inaeleza maana ya Biblia).
Kwa kigezo hicho, yafaa sana, mtu apate mafundisho kwa wingi sana ili aupe mwili uhai. “Roho ndiye autiaye mwili uhai” Hii inamaana kuwa, Roho ikifa, na mwili hupoteza uhai wake. Kumbe yatupasa kuijali sana Roho kuliko mwili.
Kwa jinsi ya mwili, mtu hupenda kuulisha mwili zaidi kuliko Roho, na mwili unapotaka kulishwa hudai hata kwa nguvu. Hata kama uko safarini, mwili hupata chai, hupata maji,hupata chakula na wakati mwingine huzidisha unapokuwa nyumbani, mara mishikaki, mara uji, mara juice. n.k. mwili unapopata hitirafu kidogo, hututibiwa haraka haraka, tena wengine hushituka sana, juhudi juu ya kuukokoa mwili huwekwa pamoja, majirani hushiriki, ndugu, marafiki na hata wapiti njia tuu, hushiriki katika kuhakikisha mwili unakuwa salama. Je, roho tunaijali kweli? Ebu fikiria kwa leo tu, umafanya mangapi kwaajili ya mwili? Umepiga mswaki, umeupaka mafuta,umeuvika, umeupa chai na hata milo yote, umeupumzisha; lakini swali ni je, umeridhika, kesho hautadai? Roho je, umeilisha, umesoma neno la Mungu mara ngapi? Ni mara ngapi umesali licha ya kuombea chakula na kujihami kwa kusema “Mungu wangu!” kwa kushituliwa na gari lililotaka kuugonga mwili huo?
Ndugu yangu, neno la “Mungu ni tamu kuliko asali”(Zaburi 19:11,Mithali 24:13), au pengine niseme, ni tamu kuliko kile chakula ukipendachom zaidi. Tamani sana kuwa na neno la Mungu la kutosha moyoni mwako, Yesu alimshinda shetani kwa neno, na lazima ujue kuwa asili / chanzo cha kila kitu ni neno (Yohana 1:1&3) na pasipo huyo neno,hakuna kilichofanyika. Kumbe, afya inatoka kwa neno, mke/mme mzuri anapatikana humo kwenye neno, utajiri unapatikana humo humo, mali na fedha unavyotamani,watoto wazuri vimeumbwa katika neno! Kwa maana hiyo, ni neno tu, linaweza kukupa haja ya moyo wako.
(b) Kulishwa maombi.
(Mithali 8:17&18),”Nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidiiwataniona. Utajiri na heshima ziko kwangu; naam, utajiri udumuo, na haki pia” pia (Luka 18:1-6) utabaini kuwa, tunapaswa kudumu katika maombi, na kupitia maombi ya kila mara,basi utaona Mungu akikujibu kwa kadri unavyoonesha kuomba kwa bidii. (Yakobo 5:16b) “kuomba kwa mwenye haki,kwafaa sana,akiomba kwa bidii”. Hii inamaana kuwa, unapaswa,kuijaza roho maombi kwa wingi mno. Kupitia maombi haya, basi yatamgusa Mungu kama tulivyoona katika (Luka18:6), naye atakujibu kwa kadri ya maombi yako.

(3) Je, dini inaweza kumfurahisha roho?
Ndugu yangu, napenda kukujuza siri hii, itakusaidia, “Dini” kamwe haitampeleka mtu mbinguni, wala hakuna mbingu ya Dini. Kwa kuwa, mtu wa Dini ni mtu wa sheria tu, je sheria zitatupatia mbingu? Ikumbukwe kuwa, Dini ni mpango wa mwanadamu kumtafuta Mungu. Katika kumtafuta huko, mwanadamu hujiwekea utaratibu anaouona utamsaidia kuyaendea makusudi yake ya kumtafuta Mungu wake. Hata hivyo, huweka kitu anachokijengea imani kuwa ndicho sahihi, na kukifuata,na kwa hali hii, hupinga uongozi wa roho na kufuata maongozi ya mwili. Je, mwili unaweza kukufikisha mbinguni, je mwili huu utaiona mbingu, au tutavikwa miili mipya? Je si maandiko yamesema juu ya kuilinda roho kuliko yote tuyalindayo, kwa kuwa hapo ndipo urithio wetu ulipo?
(4) Wokovu ni nini kwani?
Hata hivyo, inakupasa kujua kuwa, Wokovu ni mpango wa Mungu katika kumtafuta mwanadamu. mpango huu ulianzia kwenye kuzaliwa kwa Yesu na kuutimiza katika kifo chake msalabani. Na hapo ndipo, tunapopata uzima wa milele ambao ni uzima wa roho, yaani uzima ulio nje ya mwili. Uzima usiochujuka, uzima udumuo,uzima imara, uzima unaodumu milele yote.
(5) Yatupasa kufanya nini?
(a) Mungu anakutaka umrudie.
Ndugu yangu, uzima huu, unapatikana, kikubwa, ni kukubali kuwa chini ya uongozi wa Roho mtakatifu, ukubali ukombolewe,utoke chini ya sheria kwa kuwa sheria haitakufikisha popote, sheria ni ya mwili tu, sheria inaisha mwili uishapo,lakini neema inadumu milele na milele. Mtafute leo Mungu kwa bidii, nawe utampata,atakuwa Bwana na mwongozi wako (Mithali 1:4&5). Ukisoma (Isaya 55:6-8), “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana. Mwiteni, maadamu yu karibu. Mtu mbaya na aiache njia yake mbaya, na asiye haki,aache mawazo yake. Na amrudie Bwana naye atamrehemu; na arejee kwa Mungu wetu. Maana mawazo tangu si mawazo yenu, na wala njia zenu si njia zangu, asema Bwana”. Maneno hayo, yanatudhihirishia kuwa, kwa njia zetu kama wanadamu, kwa taratibu zetu na miongozo yetu,hatuwezi kumpata Mungu, bali tuziache njia zetu, tumtafute yeye, naye ataturehemu na kutuokoa.
(b) Mungu hupatikana katika roho.
Tunaweza kumpata Mungu katika maombi tu. (Yeremia 29:12-14) nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona mtakapo nitafuta kwa moyo wenu wote; nami nitaonekana kwenu, asema Bwana. Mungu hawezi kuonekana kwa njia za kibinadamu, kwa sheria za mwili, bali kwa kudumu katika maombi na kuutafuta uso wake, kupitia uongozi wa Roho.
(c ) Kubabudu katika roho ni ishara ya kuwa na Mungu.
(Yohana 4:23&24) Lakini saa inakuja, nayo saa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni roho, nao wamwabuduo, inawapasa kumwabudu katika roho na kweli.

(c) Ukimwacha Mungu, naye anakuacha.
Nawe Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, umkaribie, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa Bwana hutafuta-tafuta mioyo yote , na kuyatambua mawazo yote ya fikira, ukimtafuita, ataonekana nawe; ukimwacha atakutupa milele. (1Nyakati 28:9). Pia ukisoma (2Nyakati 20:1-21) utaona Yehoshafati alivyomtafuta Bwana, alipokabiliwa na vita dhidi ya mahasimu wake, lakini alipoamua kumtafuta (mstari wa 3) alimwona na alimtetea.

Ndugu yangu, nakusihi umpende Mungu, na uwe tayari kumrudia naye atakuwa tayari kukupokea, ataibadirisha historia ya Maisha yako, tunavyoongea, atayabadiri na kuwa mapya. Haijalishi umetumia akili yako kiasi gani,katika kuhakikisha ndoa yako inasitawi, haijalishi umehangaika kiasi gani ili kuhakikisha, unafanikiwa kimaisha na hata katika masomo yako! Pengine, biashara yako, imekuhangaisha sana, ebu leo sema yatosha, sasa Mungu nakutaka wewe uwe kiongozi wangu.

Mwl. Sospeter Simon S. Ndabagoye.
New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania.
Box 1275,
Tabora.
E-mail: sos.sesi@ yahoo.com

Comments