KUMWIMBIA MUNGU KUNAHITAJI "AKILI"

Katika Zaburi 47:7 imeandikwa "Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, Imbeni kwa akili."
Nimekuwa nikipata shida sana hasa ninaposikiliza nyimbo za baadhi ya wanaojiita waimbaji wa nyimbo za injili au nyimbo za kumsifu Mungu. Kinachonisumbua ni kiwango cha kutojua Neno la Mungu na Kumjua Mungu wanayemwimbia kinachooneshwa na baadhi ya waimbaji hao ambacho hakitoi picha ya kweli ya Mungu wanayemwimbia. Baadhi ya nyimbo ni za upotoshaji kwa kuwa hazitoi taswira halisi ya Mungu ambaye baadhi ya waimbaji wamekuwa wakidhani wanamwimbia.
Maneno ya Mungu katika Zaburi ya 47:7 yanaweka wazi kabisa kwamba Tumwimbie Mungu "Kwa akili" tukijua kwamba Yeye ni Mfalme wa dunia yote. Nia yangu leo ni kueleza nini maana ya kumwimbia Mungu kwa akili.
Unapousoma mstari Huu katika Amplified Bible Umeandikwa "For God is the King of all the earth; sing praises in a skillful psalm and with understanding." Ninapenda kuweka msisitizo hapa katika maneno "Skill" na "Understanding" kwa nia ya kuonesha kwamba, matumizi ya "Skill" au kwa kiswahili kile kinachoitwa "Ujuzi" Pasipo "Understanding" au kile kinachofahamika kama "Uelewa" katika suala zima la Kumwimbia Mungu ni sawa na kelele.

Ujuzi pamoja na kipaji ulichonacho (Skill and Talent) vinapata maana hasa katika kumwimbia Mungu pale kinapochanganywa na Uelewa (Understanding) kwamba Unamwimbia Mungu ambaye ni Mfalme wa Dunia Yote.

Biblia katika injili ya Mathayo 7: 24 Inaweka wazi kwamba "Asikiaye Maneno ya Mungu na Kuyafanya" atafananishwa na "Mtu mwenye Akili." Kumbe akili kwa Mujibu wa Maandiko matakatifu ni Uwezo wa kusikia neno la Mungu, Kulielewa, Kupata ufahamu na Kulitendea kazi. Kipaji na Ujuzi vinakuwa na maana kama vitatumika kuweka uelewa wa neno la Mungu katika matendo. Biblia pia inaweka wazi katika Mithali 9 : 10 - "Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu" Hekima ni uwezo wa mtu kutumia maarifa (Knowledge) ili kupata matokeo bora ya kuboresha maisha yake, Tafsiri rahisi ya Ufahamu ni uwezo wa mtu kuelewa mambo. Hivyo ukitaka kujijengea uwezo wa kuelewa Mambo, au kuwa na uelewa mkubwa, Tafuta kumjua Mungu, Ufahamu wako utaongezeka sambamba na uwezo wako wa kuelewa Mambo, ambao Hukusaidia kujua jinsi ya kuyaweka kwenye matendo yale unayojifunza kwa kutumia ujuzi na kipaji ulichopewa na Mungu.

Ukitaka kumwimbia Mungu, Ongeza Uelewa wako kwanza juu ya Mungu unayemwimbia, Usiimbe kwa kufuatisha tu kile alichosema mchungaji wako. Tafuta kujenga msingi wa ufunuo binafsi wa Mungu ni nani kwenye maisha yako ndipo utaweza kumwimbia na kumpa sifa anazostahili. Matumizi ya Ujuzi/Skill pasipo uelewa/Understanding wa Mungu ni Nani kwenye maisha yako binafsi ni kelele mbele za Mungu kwa kuwa hiyo ni ibada isiyotoka ndani ya Roho ambayo haimpendezi Mungu.

Ni ibada/sifa ya mwilini inayofurahisha watu na si Mungu na wala haiwezi kubadili maisha ya watu kwa kuwa ndani yake ina mbegu ya uharibifu kwa kuwa maneno ya Mungu yanaweka wazi kwamba "Nia ya mwili ni mauti, bali nia ya Roho ni uzima" (Warumi 8:5). Na huu ndio udanganyifu wa kiwango cha juu kabisa ambao shetani ameweza kuufanya. Kuwafanya watu waamini wanamwimbia Mungu kwa nyimbo zisizotoa taswira ya kweli ya Mungu, zenye asili ya mwilini na si Rohoni, zisizojengwa katika msingi wa ufunuo binafsi wa Mungu ni nani katika maisha ya Mwimbaji.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya kuimba zaburi 23 ( "Bwana ni Mchungaji wangu,") na "Kumwimbia Mchungaji wako"
Kumjua Mungu ni suala la Rohoni kwa kuwa imeandikwa mambo ya Mungu yanatambulikana kwa jinsi ya Rohoni (1 Wakorintho 2 : 14), na ibada ya kweli huanzia rohoni kwa kuwa Mungu ni Roho na hao wamwabuduo imewapasa kumwabudu katika Roho na kweli.
Ashukuriwe Mungu atupaye kuweza kutofautisha waimbaji wa kweli na wale wanaotafuta pesa kupitia nyimbo za injili isiyo na uhusiano na Mungu wa kweli.

Ni maombi yangu kwamba Mungu akupe wewe uliyesoma fundisho hili kutambua nyimbo zinazokusaidia kukua kiroho na kuzitofautisha na nyimbo za kelele. Mungu akubariki utokapo na uingiapo, katika Jina la Yesu Kristo

Amen
IMETOKA  Light of the World  Ministry

Comments