SIKIE MUNGU, ANENA NAWE.


Sospeter Simon S. Ndabagoye


Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wengine, hasa waliowanyonge....(Warumi 12:16).Msiwe na majivuno wala kiburi! Nyenyekeeni, pendaneni, fanyeni kazi ya Mungu kwa umoja, Mungu anaupenda umoja, hata Yesu na Mungu ni umoja. Kuna siri katika umoja.

Ombeaneni, na saidianeni, kila mtu, amwone mwenzie kuwa bora zaidi, mwenzio akipungukiwa hekima au maarifa, mwombee na umrejeshe kundini kwa upole na upendo, Usikubali hata mmoja apotee machoni pako. Iweni wenye nia ya Kristo ndani yenu.

Jengo la Kanisa lako, au gari la huduma yako, visikutenge na wapendwa wengine, wala, usijivune kwakuwa, umepata elimu kubwa ya Dini au ya dunia, Mwinue Yesu aliyekupandisha, huku ukimwombea mwenzio.

Usikubali kwakuwa umepata kazi nzuri, mke mzuri au mme, ukawaona wengine hawafai, Mshukuru Mungu aliyekufikisha hapo, huku ukimwombea rafiki yako na wote ambao hawajapata.....

Ukiona ndoa yako imetulia, hakuna ugomvi, umekula, umekuywa na kulala vizuri, pengne watoto wanaenda shule bila matatizo, hata kama yapo ni ya kawaida, ombea na mwenzio afike hali hiyo.

Bebeaneni mizigo.Je, haufahamu kuwa sote tu viungo katika mwili wa Kristo, na Yesu ndiye Bwana wetu sote? Je, mguu ukiuma, mkono hauukuni, na pengine njaa ikiuma, mkono hauweki chakula mdomoni ili meno yakisage, hatimaye koo hukipitisha ili kulijaza tumbo hilo liache kuuma? Kama mdomo ungeliche tumbo,ingekuwaje njaa ikiliuma tumbo? Na endapo, miguu ingeacha kukimbia, Simba akikuvamia ingekuwaje, si kichwa na tumbo vingeraruliwa? Tupendaneni jamani, tuifanye kazi ya Mungu kwa umoja. Kila mtu anakitu maalumu Mungu kampa, ambacho mwingine hana, hakuna ambaye Mungu hakumpa kipawa flani.

Ndugu yangu, leo Mungu anasema na wewe juu ya upendo, ushirikiano na umoja. Jitafakari mwenyewe, jipime ulivyokaa na majirani zako, ulivyokaa na mwenza wako wa ndoa, Jipie mwenyewe, kisha "Itii sauti hii", chukua hatua mara moja "tembea na kanisa lako, tembea na mme wako, tembea na mke wako", kila mara omba juu ya rafiki yako, ombea watoto wako, omba juu ya watumishi wengine, sheria za kidunia na mifumo ya kututenganisha wana wa Mungu usivikubali. Tembea na maono ya watu wote kumjua KRISTO, wakiri dhambi, wabatizwe kisha waokoke, wapate kuurithi ufalme wa Mungu aliotuandalia wateule wake. Haleluya!

Kheri asomaye na Kuelewa Ujumbe huu, maana akiutendea kazi, atapata Baraka. BY
Sospeter Simon S. Ndabagoye

Comments