VIZUIZI VYA KUSHINDWA KUFANYA HUDUMA YA MUNGU IPASAVYO.* sehemu ya sita*

Mtumishi Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…
Haleluya…

(Ili kupata mtililiko mzuri wa fundisho hili,tafadhali pitia sehemu zilizopita.
Na sehemu hizo zinapatikana hapa hapa haina haja ya kuangaika kutafuta fundisho hili sehemu nyingine. )

…Wanafunzi wa Yesu walishindwa kufanya huduma ipasavyo.Lakini kulikuwepo na sababu za msingi ambazo ziliwapelekea kushindwa kufanya huduma vizuri,
Bwana Yesu leo anabainisha wazi wazi juu ya sababu hizo.

Tunasoma
Mathayo 17 : 20,21:
“20 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya UPUNGUFU WA IMANI yenu.
Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu,
Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.
21 [Lakini namna hii haitoki ila KWA KUSALI NA KUFUNGA .]”

Hivyo basi sababu hizi mbili ziliwapelekea kutotimiza huduma ya Bwana kwa kushindwa kumtoa pepo Yule kijana aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, sababu hizo zilikuwa ni KIZUIZI/KIKWAZO kwao nazo ni :
• Upungufu wa Imani
• Kushindwa kuishi maisha ya kufunga na kuomba.

(Pitia sehemu zilizopita za fundisho hili,Ili ujifunze kiundani juu ya sababu hizo mbili )
Sasa tuendelee tulipokuwa tumeishia katika sehemu ya tano.

02.Kufunga na kuomba.
…Yeye aishie katika maisha ya kufunga na kuomba hafilisiki kiimani. Naye muda wote anakuwa ni mshindi zaidi ya mshindi.
• Yeye afungaye pasipo kuomba,funga yake ni bure.
• Yeye aombaye pasipo kuwa na utaratibu wa maisha ya kufunga na kuomba,MAOMBI yake ni bure.

• Bali Yeye aombaye na kufunga ikiwa ni system/mfumo wa maisha yake,Mtu wa namna hii ni mtu wa kuotea mbali,maana suala la UPAKO kwake sio kitu cha kuuliza.

Mfungo wenye maana ni ule mfungo wenye ;
(i)Kufunga bila shuruti
(ii)Kushukuru
(iii)Dhumuni maalum
(iv)Neno la Mungu
(v)Maombi katika roho

(I) KUFUNGA BILA SHURUTI
-Maana yake ni,kuamua mwenyewe pasipo kushurutishwa na mtu yeyote yule,au bila kushurutishwa na mapokeo ya Dini au Dhehebu,N.K

-Leo hii,wapo Wakristo wafungao kwa kushurutishwa na DINI zao,kwamba ni lazima wafunge katika mwezi Fulani uliochaguliwa na kanisa lao kutokana na mapokeo. Hii ni makosa sana,
Biblia inatuonya kutofanywa mateka wa mapokeo ya Dini yoyote ile wala mtu awaye yote Yule,
Tunasoma Wakolosai 2 : 8
“ Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”

Yeye anayefunga pasipo shuruti hapaswi kusimamiwa na mapokeo ya dini Fulani wala watu Fulani,Bali yampasa ASIMAMIWE NA Kristo pekee,na FUNGA yake itoke katika kilindi cha roho yake akiwa ameji-conect /amejiunganisha na Bwana Yesu.

Kufunga pasipo shuruti ni kule kufunga kwa kujitambua wewe mwenyewe kuwa unautesa mwili wako,kwa ajili ya Kristo.
Kujitambua huku ni ile hali ya kukuenenda kama Kristo atakavyo na sio kuenenda kama DINI zitakavyo.
Maana Kristo Yesu ndiye kielelezo chetu sisi Wakristo.Kushindwa kujitambua ni ile hali ambayo mtu anayefunga akiisha kumaliza mfungo wake na anajikuta akianza kutukana kusengenya,au kusema uongo,au kuwaka tamaa za ngono.

Mtu anayeshurutishwa anajikuta akijijima chakula kwa muda akiamini kuwa amefunga kumbe amekaa na njaa tu, sababu mtu wa namna hii hujizuia kufanya mambo ya kijinga kwa muda tu na akimaliza mfungo wake utamkuta anasengenya,anawaka tama za ngono,anatukana kama kawaida yake. N.K


(II) KUSHUKURU :
Mfungo wenye maana ni ule ambapo mtu aliyezingatia moyoni mwake kuutesa mwili wake kwa ajili ya Kristo kwa KUSHUKURU.
1 Wathesalonike 5 : 18
“ shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.”

Hivyo tuwe watu wa shukrani kila wakati,hata vile uamkavyo salama tu,yakupasa kushukuru sana,maana sio haki yako ya kuamka salama,wala haustahili kuamka salama,U nani wewe hata uamke salama?
Kama si mapenzi yake Bwana?

(III) DHUMUNI MAALUMU:
Yeye afungaye ni lazima awe na kusudi au dhumuni linalompelekea kufunga. Yaani yampasa ajiulize -kuwa ni kwa nini afunge ?

(IV) NENO LA MUNGU.
Mfungaji mzuri lazima asome na kutafakari neno la Bwana juu ya mfungo wake. Maana kinachofanyika ni kuwa :
Mtu anayefunga hujizuia kula chochote kile kwa muda Fulani aliojipangia.
Hivyo anautesa mwili kwa kutoupa mastarehe yake ya chakula,vinywaji.n.k
Wakati huo mwili hudhoofika bali roho yake ukomaa.
Ili roho ya mtu huyo isidhoofike kama mwili wake uliodhoofika Basi inampasa kuilisha chakula roho yake.

Chakula cha roho ni Neno la Mungu.Neno la Kristo ni chakula cha rohoni chenye virutubisho vyote.Hivyo unapofunga na Kula neno la Mungu,utajikuta hata njaa hautaisikia kabisa maana roho i hai kwa namna ya ajabu ya kushangaza kwa sababu roho ndio itiayo uzima,mwili haufai kitu (Yoh. 6 :63)

(V) MAOMBI :
Mfungaji yampasa kuomba katika roho. Kuomba katika roho kunahusisha na kunena kwa lugha kama ishara ya mawasiliano ya roho yako wewe unayefunga na Mungu wako.
Na hapo sasa ndipo ni mahali pekee pa kuvikwa silaha za Mungu (Waefeso 6 :18) Maombi ni bonge la silaha ya vita vya kiroho.Silaha hii imekabidhiwa kwa watoto wa Mungu “2 Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;” Wakolosai 4 :2

ITAENDELEA…
UBARIKIWE.

Comments