YAKO MAMBO TUNAPASWA KUYAOMBEA KATIKA ROHO NA KWELI.



Mwl Vicent Mwengo


Ndugu yangu, mpendwa wa Mungu, mkristo katika roho na kweli nikusalimu katika jina la Yesu wa Nazareth aliye hai.

Ndugu zangu habari hizi si mpya, ni zile zile tu ambazo mmekuwa mkizisika katika maeneo mbalimbali kwa nyakati tofauti. Iko shughuli tunapaswa kuifanya na iko sababu ya kuifanya.

Kwanza kabla ya yote anza kufanya tathmini ya maisha ya jamii zetu na kitaifa kwa ujumla kabla ya kizazi hiki na sasa na je wasaa kidogo hapo mbele itakuwaje. Maisha ya mtu yeyote yanagusa nyanja kadhaa hususan kwa nchi kama hii ya Tanzania; utawala na maamuzi yanayoigusa nchi moja kwa moja, dini na mwenendo wa injili, huduma ndani ya jamii zetu, mahusiano yetundani ya jamii, mitazamo yetu juu ya maisha, uchumi wetu kwa mtu mmoja mmoja na kitaifa, usalama wetu na mstakabali wa amani ndani ya jamii zetu na taifa kwa ujumla. Kwa kuwa maisha ni mjumuisho wa mambo kadhaa zaidi ya hayo niliyoyaainisha si mazuri na sababu kuu ikiwa ni kukiukwa kwa utaratibu sahihi wa mambo hayo kwa kuikwepesha kweli inayostahili.

Jambo lolote ukilifanya nje ya kweli yake matokeo yake mara nyingi huwa ni hasi.
kwa mfano; ninaposemea dini na mwenendo wa injili, dini kama namna ya kumwabudu Mungu na injili kwa maana ya kuzihubiri habari za Mungu vyote kwa pamoja vinamgusa Mungu, lakini ndani ya mambo haya ukiacha habari za kimungu na kuchanganya na mambo mengine ndipo huzua migogoro ndani ya makanisa, mipasuko ndani ya makanisa, kukejeliana ndani ya huduma kati ya mtumishi huyu na yule, kujiona kuwa ni bora kuliko wengine na magonvi baina ya dini zingine. Kwa upande wa injili, injili yoyote yenye majigambo, kejeli juu ya watu wengine, kulazimisha watu wengine waamini kama wewe na hali unapaswa kuwashawishi kwa matendo na si kulazimisha, injili ya kulazimisha miujiza kwa njia isiyo ya kimungu, injili yenye tamaa ya mali nk. Ndizo zinazozua mtafaruku ndani ya uwanda huu wa kiroho. Lakini je ukimuhubiri Mungu katika kweli na roho na yeye akajiachilia kwa matendo yake makuu mitafaruku baina ya madhehebu au watumishi itatoka wapi?

Mfano mwingine ni utawala na maamuzi yanayoigusa jamii kwa ujumla. Ndani ya tasnia hii kwa ujumla ikiitwa siasa ziko taratibu ambazo ziliwekwa na zinaendelea kuwekwa zikiwa na nia njema juu ya taifa zima. Pamoja na nia njema yake lakini kwa sababu ziliingiliwa na watu dhalimu (kutenda mambo kwa ulagai-lagai) basi taratibu hizo inawezekana hazijafuatwa kwa jinsi inavyopaswa na ndio maana jamii imevurugana na sasa haijitambui kuwa ifanye nini. Kama mwakilishi ametumwa kusemea matatizo ya eneno lake lakini akifika kwenye kikao anaanzisha matakwa yake si kukiuka utaratibu? kama serikali ikiingilia muhimiri mwngine si kukiuka utaratibu? vipato vya kidhalimu ndani ya utawala si udhalimu? kuyatumia matatizo ya wananchi kama daraja la mafanikio yako ya kisiasa na ndio maana kwa sasa huyatekelezi ili uje uyatumie tena baadae si udhalimu huu? lakini je, ukizingatia sheria na utaratibu uliowekwa matusi, vurugu, kejeli kwenye vikao vya kiserikali vitatoka wapi.

Kwa kukiukwa utaratibu wa nyanja yoyote ile niloitaja hapo juu naamni unaungana na mimi kuwa mwenendo wa maisha kwa sasa si mzuri,kiwango cha maisha kwenye nyanja yoyote kinaongezeka kwa kupungua kila eneo (inreasing in decreasing)yako mengi ya kutolea mifano lakini msingi wangu si huko bali nilitaka kukuonesha tu kwa ufupi kwa nini tunapaswa kuomba katika kweli na roho.

1.KULIOMBEA KANISA.
kwa sasa kanisa linapita katika kipindi chenye changamoto ya kushuka kwa imani kwa kizazi hiki, ukiwa mtaani utaona vijana wengi lakini makanisani kumebaki viti, hoja yao ni kwamba kanisani hakuna lolote, hawasemi moja kwa moja kwamba hawajisikii kwenda. zaidi wamebaki kujiita kuwa ni wakristo kwa kuongeza vyeti vya madhehebu yao(mbingunui tunakwenda kwa vyeti?); elewa vizuri hapa, simaanishi kuwa vyeti ni ubaya au havifai, mimi ninazungumzia wale wanao jivumnia vyeti na kuisahau kweli ya Kristo. Inasikitisha badala ya watu kufikiria ni nini mtu anapaswa kufanya nakaa kujivunia vyeti; “nilikuwa kiongozi, nilikuwa mwanachama wa jumuiya fulani” itawasaidia kiasi gani. lakini piainawezekana ni kwa sababu wameyaangalia matendo ya baadhi ya watumishi waliowaamini yakienda mrama nk lakini hawajawahi kuchukua hatua ya kumsikiliza Mungu anasemaje juu ya mwenendo wa imani sahihi. Lakini huko ndiko kushuka kwa imani pia. Migogoro na mitafaruku ya kila aina ndani ya ukristo ni kwa sababu ya kukiukwa kwa taratibu za kikiristo. Ukihubiri injili yenye kweli ya maneno yaliyoandikwa kwenye Biblia kwa kuongozwa na roho nakuhakikishia huwa hamna matatizo. Mtume Paulo aliwasihi wakristo wa korintho kwenye wara wake.

1 korintho 1:10 Basi ndugu zangu nawasihi kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Wakati naitafakari mitafaruku ndani ya ukristo na maneno haya ya mtume Paulo ndipo nikafikiria nia na shauri la ukristo ni nini.

2thesalonike 3:1 Hatimaye ndugu tuombeeni neno la bwana liendelee na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu. 2.ukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. 3.lakini bwana ni mwaminifu atakaye wafanya imara na kuwalinda na yule mwovu … … … 5. Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu na saburi ya Kristo..

ili injili izidi kupamba moto inatupasa kuiombea injili ya kweliyenye ufahamu, maarifa, hekima na elimu ya ufunuo wa kimungu. Na hapa ndipo tutakuwa tunakamilisha maana halisi ya kumtukuza Mungu na ufalme wake.

NB: Kwa ajili ya kanisa omba juu ya haya;
•Injili ya kweli ihubiriwe na kufundhishwa kwa ufasaha.
•Mungu ainue watumishi wenye kuihubiri injili katika roho na kweli na si kujali fedha.
•Kuomba nguvu ya kimungu ili matendo yake makuu yadhihirike kwa uweza wa jina lake lililo hai.
•Kukemea roho ya majivuno, kejeli baina ya madhehebu au dini nyingine yanayoleta mafarakano ndani ya kanisa na kuomba Mungu atujalie Roho wa upendo ndani ya kanisa ambao ni msingi mkuu wa imani ya kikristo.
•Mungu awaguse kwa mkono wake ambao bado hawajaijua kweli yake yeye kristo na wamkumbuke Mungu kwa kuuacha uovu.

2.WAOMBEE NDUGU ZAKO WA DAMU NA MARAFIKI ZAKO.
Kwa nyakati tofauti na kwa namna tofauti umejaribu kuwashawishi ndugu zako na rafiki zako kumkumbuka Mungu kwa kuacha yanayokatazwa na Mungu kama ngono, ulevi, uongo, dhulma nk, lakini bado hawakuzingatia. Kila kukicha unazidi kujinyenyekeza kwa Mungu lakini kwa kuwa dhambi ni tamu kwao, hivyo bado imewashika. Hujui na sasa ufanye nini kwa ajili yao, jifunze kitu hapa, acha dhana ya kuwachukia eti kwa kuwa wanatenda dhambi. Unakumbuka hata wewe ulikuwa mtenda dhambi kabla ya kuokoka, je kama Mungu angekuchukia wakati wewe ukiwabado hujaokoka heri yako ingekuwa nini? Tambua watu tunaokoka kwa neema tu na si kwamba eti tunatenda mema ndio tunaokoka! Basi ndugu yangu kama unawapenda kweli ndugu zako na rafiki zako, basi chukua hatua ya kumweleza Mungu ashughulike nao yeye mwenyewe. Mungu wetu ni Mungu wa upendo. Kwa wakati wake atawagusa na watageuka kama wewe ulivyogeuka kwa kuuacha uovu. Jitie nguvu, omba kwa kuwataja majina moyoni mwako mmoja baada ya mwingine, na Mungu atafanya kitu.

Sasa katika roho na kweli
•Omba toba kwa ajili ya ndugu zako, rafiki zako na jamii yako pia omba rehema za Mungu ziwe pamoja nasi kwa ujumla.
•Unatamani waokoke wamjue Mungu katika kweli lakini mioyo yao imefanywa migumu sasa omba mkono wa Mungu uwaguse ndani ya mioyo yao na waitambue thamani ya neema yake Mungu, na kwa utambauzi huo huo wakabadirishe matendo yao.
•Kemea na kusitisha laana, mikosi, na mabalaa mbali mbali yanayoletwa na shetani na mawakala wake kwenye maisha ya ndugu zako wa damu, rafiki zako na jamii yako kwa jina la Yesu Kristo.
•Kwa kujinyenyekeza mbele za Mungu, omba kwa jina la Yesu baraka za kiafya ya kiroho na kimwili, baraka za kiuchumi, kazi ya mikono yako na ndugu zako zikawe na mafanikio nk.
•Waombee hekima/maarifa, ufahamu na elimu ya ufunuo wa kimungu katika maisha yao

3.KUIOMBEA AMANI NDANI YA JAMII ZETU NA NCHI NZIMA.
Katika kitabu cha Nabii Isaya 1:4 Inasema “Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu: wamemwacha BWANA wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israel”.
Hii inaonesha kuwa kuyumba kwa taifa kwa kuzingatia taifa letu ukiyaacha ya nje, kuna uwezekano mkubwa ni kwa sababu tumekiuka utaratibu wa Mungu, maagizo yake kupuuzwa nk.

Kila kunavyokucha serikali na taasisi mbalimbali zinajaribu kuirejeza amani ya Tanzania ile iliyowafurahisha babu zetu na ikawafanya waendelee kwa kiwango chao, lakini kwa kadri inavyoendelea mizozo na migogoro bado inaendela kufukuta. Inawezekana sana tungekuwa tumepiga hatua kubwa ya kimaendeleo lakini kwa sababu ya kukosekana kwa haki, usawa, uwajibikaji, sera nzuri za nchi, mtafaruku wa kimfumo nk. Lakini mambo bado.

ISAYA 59:8-9 "Njia ya amani hawaijui wala hapana hukumu ya haki katika miendo yao, wamejifanyizia njia zilizopotoka kila apitaye katika njia hiyo hajui amani. kwa sababu hiyo hukumu ya haki I-mbali nasi, wala haki haitufikilii; twatazamia nuru na kumbe latokea giza, twatazamia mwanga lakini twaenda katika giza kuu......."

Ijulikane kuwa ndani ya nchi yetu kuna tofauti kadhaa za kila namna, kila mtu akiishi kwa jinsi ya tofauti yake mstakari wake si mwema. Lakini sasa Wakristo tunapaswa kuitafuta njia sahihi kwa kuomba ushirikiano wetu, upendo wetu, miongozo ya maisha na sharia ziwe na hofu ya kimungu na si kuwaogopa wanadamu. ndani ya nchi hii tunapaswa kuihubiri amani, nnachotambua; Amani ni msingi wa shughuli zote za kimaendeleo ndani ya nchi hii.

1timotheo 2:1 basi kabla ya mambo yote, nataka dua na sala na maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote, kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani katika utauwa wote na ustahivu….

NB: Kwa ajili ya nchi.
•Shukuru kwa wema wa Mungu anaotujalia kila siku watanzania,
•Ombea Roho ya upendo baina ya mtu binafsi na mwingine,
•Kemea roho wa mafarakano kwenye kila Nyanja yenye mamlaka ya kiserikali.
•Kemea roho wa ubinafsi, ukatili wa maamzi yanayokandamiza wanyonge, ubadhilifu wa kila aina, nk.
•Ombea viongozi wa taifa hili wawe na maamzi yenye hofu za kimungu na misingi ya haki ikazingatiwe.
•Ombea Amani ya Tanzania kwa ujumla.
•Omba Mungu awainue watu wenye uwezo mzuri wa kuongoza na wakiwa na nia njema watakaobadilisha mtazamo wa taifa la Tanzania.

Yako mambo unaweza ukayaona kuwa ni magumu na hayawezekani lakini maneno matakatifu yanahimiza kuwa tuombe kwa imani na tutapokea kwa imani (yuko Mungu anayejibu). Mungu wetu wa mbinguni hashindwi kwa lolote. Chini ya jua hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Inatupasa kuitambua misingi na kuiombea, (msingi ukiharibika je mwenye haki atafanya nini). Sio lazima kuyaombea yote haya kwa pamoja bali chukua muda kuliombea moja baada ya jingine kwa kadri utakavyopata wasaa wako kumueleza Bwana Mungu wetu naye atajibu kwa wakati wake.

Asanteni sana,
ZAIDI UWEPO WA MUNGU UWE PAMOJA NA NCHI YETU.

Comments