HATARI YA KUSAHAU

Na Mch. Josephat Gwajima | SNP


Mungu katika Neno lake Mara nyingi anawaambia watu wake wakumbuke. Kuna uwezekano wa kusahau mambo ya nyuma na kuna hatari kubwa kusahau mambo fulani. Wana wa Israel walipokuwa wanatoka utumwani wakiwa njiani kuelekea nchi ya ahadi, Mungu alikuwa akiwalisha mana na baadae walipofika kwenye nchi ya Kanani. Mungu aliwambia watunze mana kwa ajili ya ukumbusho jinsi Mungu alivyowalisha jangwani. Kuna nguvu inayotokana na kukumbuka mambo makuu alikuyotendea Mungu.

KUMBUKUMBU LA TORATI 32:7
Kumbuka siku za kale, Tafakari miaka ya vizazi vingi; Mwulize baba yako, naye atakuonyesha; Wazee wako, nao watakuambia.

KUMBUKUMBU LA TORATI 7:18~19
Usiwaogope; kumbuka sana Bwana, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote; uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje Bwana, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya Bwana, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa.

KUMBUKUMBU LA TORATI 15:15
Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa Bwana, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo.
Dhambi nyingi za watu hutokana na kusahau mambo waliyotendewa na Mungu. Na maranyingi Mafanikio katika maisha humfanya mtu asahau alikotoka. "Mafanikio yako ya leo ni adui wa kwanza wa mafanikio yako ya kesho"

KUMBUKUMBU LA TORATI 32:15
Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake. Mafanikio yaweza kukufanya usahau ulipotoka.

LUKA 16:25
Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.

Yesu anataka tukumbuke alivyojitoa na kufa kwa ajili yetu.

1kor 11:23-25

HATARI 15 ZA KUSAHAU

1. Mtu anayesahau ni dhalimu. Mungu si dhalimu maana hasahau kazi yetu.

WAEBRANIA 6:10
Maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia.

Mungu anathibitisha kuwa wanadamu wanaweza kusahau hata mambo yanayoonekana.

JEREMIAH 2:32
Je! Mwanamwali aweza kusahau mapambo yake, au bibi arusi mavazi yake? Lakini watu wangu wamenisahau mimi kwa muda wa siku zisizo na hesabu.

2. Wanaomsahau Mungu mwisho wao ni kunyauka na kuangamia - laana ya kunyauka

AYUBU 8:11~13
Je! Hayo mafunjo yamea pasipo matope Na makangaga kumea pasipo maji? Yakiwa yakali mabichi bado, wala hayakukatwa, Hunyauka mbele ya majani mengine. Ndivyo ulivyo mwisho wa hao wamsahauo Mungu; Na matumaini yake huyo mbaya huangamia;

3. Ukisahau utarudi ulikotoka
Ukishahu kuwa ni dhambi iliyokufanya uishi maisha ya dhiki utatenda dhambi na kurudi ulikotoka.

4. Ukisahau kiburi kinaota - unasahau kuwa huko nyuma ulikuwa dhaifu. Ni muhimu kukumbuka ulikotoka ili umtukuze Bwana. Usahulifu humfanya mtu asikumbuke kuwa ni Mungu ampate nguvu ya kufanikiwa. Kukumbuka huleta unyenyekevu

KUMBUKUMBU LA TORATI 8:12~18
Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.

5. Kusahau humtia Mungu hasira - Kumb 9:7

KUMBUKUMBU LA TORATI 9:7
Kumbuka, usisahau ulivyomtia Bwana, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya Bwana

6. Usahulifu huleta kuangamia - Kumb 8:19

KUMBUKUMBU LA TORATI 8:19
Lakini itakuwa, kama ukimsahau Bwana, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka.

7. Zaburi 88:10-12 - ukisahau unapoteza haki zako. Haki yetu inatokana na ahadi za Mungu maishani mwetu

ZABURI 88:10~12
Wafu je! Utawafanyia miujiza? Au waliofariki watasimama na kukuhimidi?Fadhili zako zitasimuliwa kaburini? Au uaminifu wako katika uharibifu?Miujiza yako itajulikana gizani? Au haki yako katika nchi ya usahaulifu?

8. Kumb 15:12-18 - kukumbuka kunaleta shukrani na kuwatendea wema wale katika hali duni ukiyokuwanayo huko nyuma

KUMBUKUMBU LA TORATI 15:12~18
Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako. Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu; umwangalie kwa wema katika kundi lako, na sakafu yako ya nafaka, na kinu chako cha divai; mpe kama alivyokubarikia Bwana, Mungu wako. Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa Bwana, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo. Hata itakuwa, akikuambia, Siondoki kwako; kwa sababu akupenda wewe na nyumba yako, kwa kuwa yu hali njema kwako; ndipo utwae uma, uupenyeze katika sikio lake uingie katika ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako milele. Na kijakazi chako naye mfanye vivyo. Wala usione ugumu, utakapomwacha huru kuondoka kwako; kwani amekutumikia miaka sita kwa ujira mara mbili wa mwajiriwa; na Bwana, Mungu wako, atakubarikia kwa yote utakayofanya.

9. Kumb 4:9 - anayesahau hana la kuwaambia wanawe.

KUMBUKUMBU LA TORATI 4:9
Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako;

10. Hosea 4:6 - ukimsahau Mungu yeye pia atasahau uzao wako.

HOSEA 4:6
Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.

11. Hosea 8:14 - ukisahau Mungu atatuma moto uteketeze ulichokijenga. Unaweza kumsahau Mungu na kujishughulisha na kujenga vitu vingine lakini Mungu atatuma moto kuviharibu

HOSEA 8:14
Maana Israeli amemsahau Muumba wake, naye amejenga nyumba za enzi; na Yuda ameongeza miji yenye maboma; lakini nitapeleka moto juu ya miji yake, nao utaziteketeza ngome zake.

12. Zaburi 9:17 - Kumsahau Mungu kunaweza kumfanya mtu arejee kuzimu.

ZABURI 9:17
Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.

13. Ukikumbuka ulikotoka unajaa shukrani mbele za Mungu.

14. Kukumbuka ni silaha ya kushinda vita iliyo mbele yako -
Daudi alipokumbuka alivyomshinda dubu na simba alipata nguvu ya kumkabili Goliathi na kushinda vita

15. Kukumbuka ulikotoka ni nafasi ya kuudhihirisha utukufu wa Mungu. Unapoyasema mambo ya udhaifu uliyokuwanayo na jinsi mungu alivyokuvusha utukufu wa Mungu huwa dhahiri na Mungu hutukuzwa.


-Mch. Josephat Gwajima | SNP
Ufufuo na Uzima

Comments