Je, Talaka ni Suluhisho la matatizo ya Ndoa? – Sehemu ya Kwanza



Tanzania huwezi kudai talaka bila sababu za msingi kisheria. Wapo wanandoa ambao kabla ya kudai talaka hujaribu kutafuta njia mbalimbali za kupata suluhu kwa mfano, kutafuta ushauri nasaha (marriage counseling), wengine huamua kujitenga kwa maana ya kuhama nyumbani.
==============================
===========
Utangulizi
Ndoa ni taasisi muhimu sana katika jamii. Sheria, imani za kidini na hata mila na desturi nyingi duniani huthamini sana taasisi hii na kuilinda kwa gharama yoyote. Hata hivyo polepole tunashuhudia taasisi hii kama zilivyo taasisi nyingine, ikikumbwa na misukosuko ya kila aina. Maendeleo na uhuru vinapoongezeka, ndivyo taasisi hii inavyozidi kutishiwa kuendelea kuwepo. Kuna hata watu wanadiriki kusema kwamba itafikia wakati taasisi hi itaonekana haina maana wala nafasi tena ( irrelevant) na kufutiliwa mbali.
Mawazo haya japo yanaogofya, hatuwezi kuyapuuza; yatupasa kujaribu kuyafanyia kazi kadiri tunavyoweza. Jamii zote zinakabiliwa na kuongezeka kwa talaka baina ya wanandoa. Haijalishi kiwango cha maendeleo makubwa waliyofikia au umaskini uliokithiri unaozitafuna.
Mfululizo wa makala zangu kuhusu talaka, utajikita katika zile “ndoa za mwanamke na mwanaume” iwe ndoa ya “mke” mmoja au wengi, na siyo vinginevyo! Hapa ninamaanisha kwamba zile “ndoa za watu wa jinsia moja”, au “ndoa ya mwanamke mmoja na wanaume wengi” hazihusiki katika tafsiri yangu ya ndoa na hivyo haziangukii katika wigo wa makala zangu! Aidha mjadala utajikita zaidi kwenye “talaka zinazotolewa kimahakama” na siyo zile za kupeana kienyeji kwa kufukuzana, au zinazotolewa kwa utaratibu tofauti bila kufuata Sheria ya Ndoa ya 1971 inayotumika Tanzania.
Nimeanza na angalizo hili ili tuwe na uelewa wa pamoja tunaposoma kilichoandikwa hapa. Pia ninafahamu kuna mambo yanayoweza kuzua mjadala au kuingiza mambo mengine yahusuyo “haki za binadamu” na hata “imani za kidini” na hivyo kupoteza mwelekeo wa makala na mtizamo wangu. Ninawaomba wasomaji wangu tuepuke kutoa tafsiri tofauti nje ya kile kilichoandikwa na kukusudiwa hapa.
Kusudio la makala hii ni kuanzisha fikra akilini mwa wasomaji, ili nao waweze kutoa maoni yao kwenye hili suala nyeti.

Talaka katika takwimu
Pamoja na kujua kwamba kadiri miaka inavyoenda, talaka zinaongezeka kwa kasi hapa Tanzania kama ilivyo sehemu nyingi duniani kama nchi za Ulaya na Marekani, ni vigumu kuwa na takwimu sahihi kwa vile watu wanapotalikiana hawaendi kuandikisha talaka kwa wakala wa RITA (Registration, Insolvency and Trusteeship Agency) kama wafanyavyo pale kifo kinapotokea au pale mtoto anapozaliwa. Kutokuandikishwa huku kunatokana na sababu nyingi, moja ikiwa ni pamoja na unyanyapaa kuhusu talaka, na kutokujua kwamba talaka nazo ni lazima ziandikishwe kisheria ili pamoja na mambo mengine kuwezesha kukusanya takwimu zitakazosaidia kupanga mipango ya maendeleo na kutunga sera.
Takwimu zilizopo japo hazionyeshi hali halisi, bado zinaashiria kuongezeka kwa idadi ya talaka. Kati ya 2007 na 2008, kesi za talaka zilizoandikishwa RITA ziliongezeka na kufikia 43 ukilinganisha na hali ilivyokuwa kati ya 2005 na 2006 ambao kesi zilizoandikishwa zilikuwa 37 tu! Kwa kiwango chochote kile, idadi hii ni ndogo ukilinganisha na hali halisi.Yatosha tukisema kwamba talaka bado imebakia kuwa kitu cha binafsi baina ya wanandoa wenyewe, japo watu wanapooana mara nyingi haifanywi siri.
Mwelekeo na mtizamo kuhusu Talaka
Suala la talaka haliwezi kuongelewa bila kuangalia mila na desturi na hata imani za kidini. Tafiti zilizokwisha fanyika kuhusu mwelekeo wa kupeana talaka (divorce trends) miongoni mwa jamii za Kitanzania, zinaonyesha kwamba “jamii zinazoishi mijini na kufuata utamaduni wa Kiswahili” (Swahili culture) ziko na mwelekeo zaidi wa kupeana talaka kuliko “jamii za bara zenye mila na desturi au hata mwelekeo wa kiimani hasa ya kikristo” unaopinga talaka. Mara nyingi kuna dhana potofu kwamba wanaume tu ndio huweza kutoa talaka na wanawake wao ni wapokeaji wa talaka ilhali siyo hivyo.
Mtizamo huu unatokana na mila na desturi ambapo mwanamke aliyeolewa kwa kulipiwa mahari, hakuwa tofauti na bidhaa au mali ya muoaji! Hata hivyo, kisheria mwanaume au mwanamke anaweza kuomba mahakama itoe talaka na kusitisha mahusiano yale ya kindoa.Mtizamo wa kudhani kuwa mwanaume tu ndio ana haki au “uwezo wa kumkataa mwanamke” ndio hupelekea watu kuwanyanyapaa wanawake “walioachika” kwamba hawafai, na kuwaogopesha wanawake walioolewa kusita kwenda kuomba talaka mahakamani, hata pale ndoa inapogeuka kuwa kihatarishi cha maisha.
Unyanyapaa kwa wanaume huchukua sura tofauti na mara nyingi huhusishwa na uwezo wa kuongoza. Mwanaume aliyeshindwa “kutawala au kuongoza kaserikali kadogo ka nyumbani” atawezaje kutawala serikali au taasisi kubwa? Hapa tunapata dhana nyingine tofauti kwa nini baadhi ya wanaume nao husita kuachana na wake zao hata pale wanapotamani kusitisha mahusiano ya ndoa.
Tukirudi tena upande wa mila na desturi, katika “utamaduni wa Kiswahili”, mara nyingi ndoa na talaka zilishikamana na imani ya dini na kwa wale wenye kuishika dini ya Kiislam, talaka ni kitu kinachoruhusiwa. Wanawake wengi walisubiri kupewa talaka na kuendelea na maisha yao ambapo kuolewa tena ilikuwa ni uwezekano. Kwa watu wa bara na hasa wenye kufuata imani ya kikristo ile inayosema ndoa ni pingu za maisha, basi ilikuwa vigumu sana kutaka ama kupewa talaka. Pia mwanamke aliyeachika huweza kujikuta haolewi tena kwa vile kikanisa ndoa ya mwanzo bado inatambuliwa na inamzuia kutokufingishwa ndoa nyingine. Tafiti zimefanyika kuonyesha kwamba, wakati wanawake wa kiislam hawakuogopa talaka, wanawake wa kikristo walionyesha kuogopa kupewa talaka kwa sababu imani ya dini inakataza.
Pamoja na unyanyapaa na woga, tunaweza kusema kwa uhakika kwamba mambo yamebadilika sana siku hizi ambapo kutokana na kuongezeka kwa uelewa wa jamii na hasa wanawake wenyewe katika kuzijua haki za kisheria, na hususan Sheria ya Ndoa ya 1971, wanawake wanaoishi maisha wasiyoyafurahia, yenye manyanyaso, hutafuta suluhu kwa kuomba talaka mahakamani lakini kwa gharama na kwa kupitia mchakato wenye changamoto.
Talaka kama mchakato wenye changamoto lukuki
Mchakato wowote ule una gharama zake. Talaka siyo tukio la mara moja bali ni hitimisho la mchakato na kwa kiasi kikubwa humgharibu mtu kwa namna moja ama nyingine kwa maana ya muda, fedha, ustaarabu, heshima, staha nakadhalika. Gharama hizi kwa kiasi fulani huweza kumfanya mtu afikirie mara mbili kabla hajaanzisha huu mchakato wa kufungua minyororo ya pingu za maisha. Mchakato huu unaweza kumfanya mtu aumbuke na kujikuta siri zake nyeti zikianikwa waziwazi bila staha wala heshima mahakamani, kwenye magazeti na hata kwenye machapisho mengine ya kudumu kama taarifa za kisheria ( Law Reports) na kadhalika.
Kabla uamuzi wa talaka haujachukuliwa, aghalabu mambo mengi yanaweza kuwa yametokea baina ya wenza wa ndoa yenye kuleta machungu.Katika jamii nyingine hasa Ulaya na Marekani, ikitokea wanandoa hawaifurahii tena ndoa kwa maana ya kupungua mapenzi baina yao, si ajabu hili pekee likamsukumu mmoja wapo au wote kuona hakuna jinsi isipokuwa kudai talaka na siyo ajabu ukasikia mtu anasema mahakamani “anadai talaka bila sababu”.
Tanzania huwezi kudai talaka bila sababu za msingi kisheria. Wapo wanandoa ambao kabla ya kudai talaka hujaribu kutafuta njia mbalimbali za kupata suluhu kwa mfano, kutafuta ushauri nasaha (marriage counseling), wengine huamua kujitenga kwa maana ya kuhama nyumbani. Mara nyingi Ulaya au Marekani mwanaume huwa ndio mwenye kuhama! Uzoefu unatuonyesha kwamba jamii za kiafrika hususan Tanzania mwanamke “huhamishwa” kwa kufukuzwa au kufanyiwa visa na vitimbi. Wako wanandoa ambao badala ya kuhama, wao hutafuta mtu mwingine kwa siri wa kufarijiana naye na kusogeza siku huku wakitafuta kufikia malengo yao ya maisha kama kulea na kusomesha watoto na mengine. Vyovyote iwavyo, njia hizi siyo suluhisho la kudumu kwa maana ndoa bado ipo na inazidi kujenga ufa zaidi badala ya kujenga ukuta ulioanza kubomoka!
Tukiangalia Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine za kiafrika zilizo maskini, tunaweza kusema kwamba hakuna nyenzo au “miundombinu” ya kuwafanya wanandoa waliochoka ndoa kupata msaada wa kurekebisha ndoa zisivunjike. Ndoa zinapoanza kupitia magumu, msaada wa kwanza huwa ni familia au marafiki wa karibu na siyo taasisi za ushauri nasaha kwa maswala ya ndoa kwa vile taasisi hizi ni ngeni katika tamaduni zetu. Msaada mwingine ni taasisi za kidini na kwa baadhi, huweza kuwa hazina “uzoefu” kwa maana baadhi ya hao viongozi wa kidini wanaofuata kutoa ushauri, hawajawahi kuishi maisha ya ndoa na kujua kinachoweza kutokea humo kwa vitendo. Nadharia ya kusoma kwenye vitabu au kusikia simulizi wakati mwingine inaweza kuwa tofauti na uzoefu wa vitendo. Kutokana na maendeleo na utandawazi, polepole tunaanza kujua umuhimu wa kutumia taasisi zaidi ya familia na zile za dini ili kupata tiba au suluhu kwa matatizo ya ndoa.
Talaka, japo yaweza kuwa suluhu ya matatizo ya ndoa, suluhu hii inaweza kuzaa matatizo makubwa zaidi tena kwa watu wasio na hatia yeyote mathalani watoto wadogo wasioweza kujitegemea bado, wazazi wazee, ndugu wenye kuhitaji msaada na kadhalika. Inawezekana kuzuia talaka kama tutajaribu kuzuia visababishi vinavyomsukumu mwanandoa kutaka talaka.
Kufuatana na Sheria ya Ndoa ya 1971 mahakama haiwezi kutoa talaka kwa vile wanandoa wamekubaliana kuachana (divorce by consent) au kusema kwamba wanadai talaka kwa vile wanatofauti zisizoweza kusuluhishika (irreconcilable differences). Hizi ni dhana ngeni kwetu watanzania. Sheria yetu bado ni ile ya mwaka 1971, kabla ya utandawazi, kipindi ambacho hata hao wanaotumia sababu hizi walikuwa bado hawajapiga hatua na kuwa wabunifu kiasi cha kuwa na jeuri ya kusema wamechokana na wamekubaliana kuachana pasina sababu za msingi.
Sheria yetu hii kongwe (iliyopitwa na mambo mengi katika ulimwengu wa utandawazi) ya 1971 imeweka bayana sababu kuu inayoweza kuruhusu mahakama itoe talaka kuwa ni “uthibitisho kwamba ndoa imeshavunjika pasina shaka yoyote”.Kwamba liwake jua, inyeshe mvua wanandoa hao hawawezi kuishi tena pamoja kama mke na mume na endapo watalazimishwa kuishi pamoja inaweza kusababisha madhara makubwa zaidi. Hii ina maana kwamba lazima uthibitisho utolewe kulionyesha kuthibitisha jambo. Kuna matendo ambayo kisheria yanaweza kuvunja ndoa kwa mfano ukatili (Cruelty), Uzinzi (adultery), kutelekezwa (dissertation/abandonment) na hata kubadili dini. Matendo yote haya huweza kuingiliana kwa namna moja au nyingine na ndio maana mahakama inataka uthibitisho wa zaidi ya kosa moja kati ya hayo.
Kwa Tanzania, kisababishi kikubwa zaidi kufuatana na uzoefu wa kusikiliza kesi za ndoa ni ukatili kwa mapana yake yote. Ukatili ni mwendelezo wa vitendo vinavyovuka mpaka wa udhalilishaji na kusababisha madhara ya kimwili na kihisia. Kutokana na habari zinazotolewa katika vyombo vya habari, mara nyingi taswira inayotolewa ni kama vile ukatili na unyanyasaji katika ndoa hufanywa zaidi na wanaume. Vipigo, kunyimwa mahitaji ikiwemo unyumba, na mateso mengine huonekana kufanywa na wanaume zaidi, japo ni jambo lisilofichika tena kuwa hata wanawake nao hufanya vitendo hivyo.
Kutelekezwa (abandonment/desertion) nako huweza kuhesabika kama ni ukatili kwa maana ya kwamba mwanandoa hukoseshwa ile haki ya kuwa na mwenziwe. Wanandoa wanapoasiana na kuishi mbalimbali kuna hali fulani ya mateso hujitokeza hasa kisaikolojia kwa sababu Yule aliyetelekezwa huwekwa kifungoni. Hawezi kuchukua uamuzi wa kuishi maisha yake apendavyo nje ya wigo wa ndoa.
Ndoa nyingi zimeendelea kukosa upendo na kumfanya mwanandoa kutafuta upendo sehemu nyingine kupitia namna mbalimbali. Wengine hujikuta wakiwa walevi wa vileo aina mbalimbali, wengine hujikita kwenye kusali zaidi na hata kutokutimiza wajibu muhimu katika ndoa.Wakati haya yote yanatendeka, wanaoumia zaidi ni wale wanaowategemea wanandoa hususan watoto.
Tukija kwenye uzinzi tunapata kwamba kosa moja la uzinzi kimahakama linaweza lisitoshe kuivunja ndoa. Pia nitahadharishe kwamba mwanamke hawezi kudai talaka mahakamani kwa vile kamfuma mumewe ana mwanamke mwingine siku moja tu! Hata hivyo, wakati mwingine uzinzi huambatana na matendo mengine kama ukatili wa kisaikolojia na pia kuondoa upendo pale mhusika anapozama kwenye mahusiano ya nje na kusahau kuwa kuna mwenza anayehitaji upendo. Kwa miaka ya sasa kuna tishio la UKIMWI pale mwanandoa anapoanza mahusiano nje ya ndoa nah ii inaweza kabisa kuhesabika kama ukatili kwa maana mtendwa hupata mateso kisaikolojia.
Katika suala la kutelekeza, kuna mengi yanaweza kutokea na kusababisha wanandoa wawe mbalimbali na huenda ikawa vigumu kuthibitisha kwamba mtu katelekezwa. Kwa mfano mke au mume anapofungwa kwa muda mrefu, je hii itahesabiwa kuwa ni kumwacha mwenziwe?Katika nchi nyingine huwa tunasoma mara nyingi kwamba mke/mume anaomba talaka kwa vile mwenza wake kafungwa.Je kwetu hili linachukuliwa vipi? Nadhani huu ni mjadala mpana ndugu msomaji na pengine tunahitaji kulijadili hili kwa mapana yake bila kuangalia zaidi mambo ya mila na desturi. Hebu tujiulize, ikiwa mke kafungwa miaka 5 jela, je mume atakaa muda wote huo akimsubiri? Je ni sawa kwa mke kuomba talaka kwa sababu mume kafungwa miaka 10? Ikiwa siyo sawa, je mwanandoa anaweza kukaa miaka yote hiyo akiwa mpweke bila kuwa na haja ya kuliwazwa?
Nini maoni yako?
-Mwl Sospeter Simon S. Ndabagoye
New Elshaddai Ministries NEM-Tanzania

Comments