NGAO YA IMANI

 

16 zaidi ya yote mkiitwaa NGAO YA IMANI, amabayo kwa hiyo Mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu”
(efe. 6:16)
Bwana Yesu asifiwe! Ujumbe huu umekufikia kwa kusudi kabisa na ninaamini Mungu atakusaidia na utatoka hatua moja kwenda nyingine. Hebu chukua nafasi twende tujifunze pamoja na ni maombi yangu kwamba Mungu akufunulie akili zako ili uelewe kile ambacho anakwenda kutufundisha!
Kabla ya yote ni muhimu ufahamu kwanza juu ya imani maana tunachojifunza hapa ni jinsi ya kuitumia imani kama ngao wakati shetani atakapokutupia mishale yake yenye moto.
Biblia inasema,”1 Basi imani ni kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo, Ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (ebr.11:1)
Sikiliza tafsiri nyingine kutoka katika Kiswahili cha kisasa biblia inasema hivi,kuwa na imani ni kuwa na hakika ya mambo tunayoyatumainia Kusadiki kabisa mambo tusiyoyaona”
Kwa hiyo kuwa na IMANI ni kuwa na HAKIKA ya mambo uanayoyatarajia au unayoyatumainia. Kwa maana hiyo imani ni sasa hata kama kitu unachotarajia hakipo imani inabaki kuwa sasa, imani inaleta mambo unayoyatarajia kuwa halisi hata kama hujakiona kile kitu! Kitu kingine unachopaswa kujua ni chanzo cha imani na unisikilize hapa nikwambie kitu, kila imani chanzo chake ni kusikia haijalishi ni imani ya kimungu au la zote chanzo chake ni kusikia! Angalia Biblia yako katika kitabu cha warumi 10:17, 17 Basi imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia Huja kwa neno la Kristo”
Kwa nini nataka uelewe chanzo cha imani? Ni kwa sababu watu wengi sana wamekuwa wakiomba kwa Mungu ili waweze kuwa na imani na wengine wamejaribu hata kufunga wakiomba imani, sikiliza ndugu yangu! Imani chanzo chake ni kusikia na si kusikia tu bali kusikia kunakotokana na neno la Kristo, kwa hiyo kama imani chanzo chake ni kusikia kunakotokana na neno la Kristo basi huwezi kuwa na imani kama huna neno la Kristo! Nimesema hivi huwezi kuwa na imani kama hauna neno la kristo! Ndiyo, ni lazima uwe na neno la Kristo ambalo kwa hilo utaamini kile unachoamini! Imani lazima iwe na kitu cha kushikilia huwezi ukaamini kitu from no where lazima uwe na kitu kinachokufanya ushikilie hicho unachoamini na hicho kitu kinaitwa neno la kristo au neno la Mungu (haleluya!) Ngoja twende kwa mifano utanielewa tu,angalia rumi 4:17-21 inasema hivi,
17 Kama ilivyoandikwa,nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi;mbele zake yeye aliyemwamini, Yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu,ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.
18 Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa,ili apate kuwa baba wa mataifa mengi,kama ilivyonenwa,ndivyo utakavyokuwa uzao wako.19 Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani,alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwishakufa,(akiwa amekwishakupata umri wa miaka mia),na hali ya kufaya tumbo lake sara. 20 Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwaimani,akimtukuza Mungu;21 huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi”.
Nitafafanua vizuri hii habari huko mbele lakini nachotaka uone hapo ni hiki chanzo cha imani ni kusikia neno na kama ni hivyo chanzo cha imani ni neno la Mungu na utaona kwenye habari hiyo hapo juu ibrahimu alikuwa na miaka mia na mpaka anafikisha miaka mia hakuwa na mtoto lakini kama ni msomaji mzuri wa biblia utakumbuka kuna maneno aliyatamka Mungu kwa ibrahimu huko nyuma kuhusu mtoto na biblia inasema Ibrahimu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kuwa ni haki kwake. Ilipita miaka mingi na ibrahimu hakuwa na mtoto kwa hiyo kama mwanadamu alianza kufikiri hali ya mwili wake(uzee alionao maana alishafikisha miaka mia) akafikiria na hali ya kufa kwa tumbo la mkewe sara maana kibinadamu sara hakuwa na uwezo wa kubeba mimba tena, lakini akiiona AHADI ya MUNGU, hakusita kwa kutokuamini bali ALITIWA NGUVU kwa imani……….. sikiliza! hapo anaposema akiiona ahadi ya Mungu umeshawahi kujiuliza ni ahadi gani hiyo? Na anaposema alitiwa nguvu umeshajiuliza alitiwa nguvu na kitu gani? Sikia ahadi aliyokuwa akiiona Ibrahim ilikuwa ni NENO ambalo Mungu alimuahidi huko nyuma na kwa neno hilo imani ya Ibrahim ilijengwa hapo,(kumbuka nataka uelewe chanzo cha imani ili uache kufunga na kuomba imani)! Na kwasababu neno hilo ambalo imani ya Ibrahim ilijengwa hapo ndilo lilikuwa likimpa Ibrahim nguvu ya kuendelea kuamini japokuwa uzee ulikuwa umemlemea na hali ya kufa kwa tumbo la mkewe Sara ilikuwa inamzonga lakini akiiona ahadi ya Mungu (neno) hakusita kwa kutokuamini bali alitiwa nguvu! (haleluya!)
Biblia inasema imani huja kwa kusikia wala haijasema imani huja kwa kufunga na kuomba na hata ukiomba upewe imani Mungu atakupeleka kwenye neno lake tu ambalo ndiyo chanzo cha imani. Angalia mfano huu labda tutamalizia hapa kwa habari ya chanzo cha imani, luka 17:5,6 inasema hivi,
5 mitume wakamwambia Bwana, tuongezee imani. 6 Bwana akasema,kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali,mngeuambia mkuyu huu,ng’oka ukapandwe baharini nao ungewatii”.
Unaona kitu ambacho mitume walikuwa wanaomba! Walikuwa wanaomba waongezewe imani lakini kumbe hata hiyo imani yenyewe amabayo wao walitaka waongezewe hawakuwa nayo hata kidogo! Ndo maana unaona Bwana anawaambia kama wangekuwa hata na hiyo imani ya kiasi cha chembe ya haradali wangeuambia mkuyu ng’oka ukapandwe baharini nao ungewatii, mi sijui kama unaelewa alichokuwa anamaanisha Bwana lakini kama unaisoma Biblia kwa kuitafakari mistari yake utagundua alichomaanisha Bwana ni kwamba imani ina chanzo chake ni kama mwanzo wa mti ambapo kwanza huanza mbegu ndogo sana lakini unapoipanda inakua na kuwa mti mkubwa sana. Kitu ni kilekile ukirudi kwenye somo tunalojifunza ni kwamba kama unataka kuwa na imani ni lazima uwe na mbegu ambayo ukiipanda itaota na kukua nakukufaya uwe na imani kubwa sana na hiyo mbegu ni neno la Mungu! Angalia kitabu cha luka 8:11 inasema, 11 Na huo mfano,maana yake ni hii
MBEGU ni NENO la MUNGU”
Hapo Yesu alikuwa akifafanua mfano wa mpanzi ambapo anafananisha moyo wa mtu na shamba (udongo) na mbegu anazifananisha na neno lake, kwa hiyo neno la mungu ni mbegu ambayo kama ukiipanda ndani ya moyo wako itakua na kuzaa matunda sawasawa na ulivyolipanda, ukipanda mahindi utavuna mahindi ukipanda neno la imani utavuna imani sawasawa na ulivyoamini! Ni matumaini yangu wewe uliyekuwa ukifunga na kuomba upewe imani utakuwa umepata kitu cha kukusaidia.
Hebu sasa nikumbushe maneno ya Mungu yanayoongoza somo hili ambayo tunayapata katika efeso 6:16 inasema , “16 Zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani,ambayo kwa hiyo Mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu”.
Hapa mtume Paul alikuwa anazungumzia silaha za Mungu ambazo wsomaji wengi wa biblia tumekuwa tukizisoma na tumekuwa tukifundishwa na watumishi wa Mungu lakini sijui kama umeshawahi kukaa ukatafari hizi silaha mojamoja! Sasa katika silaha alizotaja mtume paul mojawapo ni hii ngao ya imani na kumbuka kila silaha zilizotajwa kila moja ina kazi yake na wakati wake wa kuitumia na ndo maana paul mtume anasema mkiitwaa ngao ya imani ambayo kwa hiyo yaani hiyo ngao ya imani mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu (shetani). Kwa hiyo kama mristo unapaswa kuwa na silaha hii muhimu kabisa ili kujikinga na mishale inayorushwa na adui, hii siyo imani ya kusema namwamini Yesu kristo kama Bwana na mwokozi hii ni imani inayotumika kama silaha. Ok! wengi tunafahamu ngao ni nini? Ngao ni kifaa kinachotengenezwa maalum kwa ajili ya kumkinga mtu anayeitumia dhidi ya silaha zinazotoka kwa adui anaye au anaopigana nao na hii ni silaha ya zamani sana ambayo ilitengenezwa kwa kutumia miti au ngozi ngumu au shaba laikini vilevile hata sasa inatumika na baadhi ya makabila machache pamoja na askari wakati wanapozuia fujo za waandamanaji wanaorusha mawe chupa n.k. mtume paul ametumia mfano huu wa ngao ili kuwaelewesha watu waweze kumuelewa au kelewa kazi ya imani inapotumika kama silaha.
Sasa unisikilize! Ninapozungumzia ngao ya imani ninazungumzia NENO LA IMANI. Usichanganyikiwe!!! Ndo maana hapo nyuma nimeanza kukufundisha kwanza imani na chanzo chake ili uweze kuelewa huku tunakokwenda. Sikia! hakuna NENO hakuna IMANI -hakuna MATENDO hakuna MATOKEO. Ili uweze kushindana na mwovu unahitaji kuvaa silaha za Mungu,ili uweze kuizima mishale yenye moto ya yule mwovu unahitaji kuwa na silaha inayoitwa ngao ya imani na labda utajiuliza hii mishale ya mwovu ni ipi au inakujaje na nitatumia vipi ngao ya imani? Swali zuri, sasa fungua biblia yako nikupe mifano ambayo itakutoa hatua moja kwenda hatua nyingine na ninaamini hautakuwa kama ulivyo bali utatoka imani hata imani, amen? Lakini kabla sijakupa mifano sikiliza maneno haya,
12 Piga vita vile vizuri vya imani,shika uzima ule wa Milele ulioitiwa,ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi” (1Timotheo 6:12)
Ili uweze kupigana vita hivi vya kiimani ni lazima uwe na neno au maneno ya imani yatakayokuwa kwako kama ngao wakati adui atakapourushia mishale yake yenye moto! Angalia tena 1timotheo 1:18 inasema,
18 Mwanangu Timotheo nakukabidhi agizo hilo liwe akiba,kwa ajili ya MANENO ya unabii yakiyotangulia juu yako, ili KATIKA HAYO uvipige vile vita vizuri”.
Sikiliza tafsiri nyingine ambayo inatupa ufunuo zaidi, inasema hivi,
18 Mwanangu timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii Yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie MANENO HAYO yawe silaha yako katika
Kupigana vita vizuri”.
Bwana asifiwe! Tafsiri nzuri kabisa na inayoeleweka kwa urahisi kabisa. Hapo juu tumeona jinsi Paul akimwambia Timotheo kwamba avipige vita vizuri vya imani kisha anendelea kumkumbusha kuwa kuna maneno ya unabii alipewa na hayo maneno ayatumie kama silaha ya kupigania vita vya imani. Sijui kama unafahamu kwamba maneno ni silaha na kama ulikuwa hufahamu kwamba maneo ni silaha sasa ufahamu hilo na maneno haya yakiwa upande wa mwovu yanakuwa ni kama silaha ambayo kwako ni mishale yenye moto, lakini kwa kutumia maneno ya Mungu (maneno ya imani) ambayo yana-act kama ngao utaweza kuizima hiyo mishale ya mwovu. Nadahani sasa unaanza kuelewa mahali tunakoelekea! Ngoja niseme hivi labda utanielewa. “ ngao ya imani ni neno au maneno ya imani ambayo yanakusaidia kukukinga wakati adui anapoleta maneno au mawazo ya kukukatisha tama juu ya kitu unachoamini na kukitarajia kutoka kwa Mungu ”.
Sasa angalia marko 5:35,36 inasema,
35 Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi wakisema, binti yako ameshakufa kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? 36 Lakini Yesu aliposikia LILE NENO likinenwa,akamwambia mkuu wa sinagogi,USIOGOPE AMINI TU”.
Nimekwambia hapo juu kuwa maneno ni silaha sasa hii ni habari inamuhusu mkuu wa sinagogi ambaye alikwenda kwa Bwana Yesu kuomba uponyaji wa binti yake aliyekuwa akiumwa na sote tunafahamu kuwa Yesu alikubali kwenda kwa yule mkuu wa sinagogi lakini wakiwa njiani kuelekea kwa mkuu wa sinagogi wasomaji wa biblia wanakumbuka juu ya yule mama aliyekuwa akitoka damu jinsi alivyomgusa Yesu akapona ugonjwa wake. Wakati alipomgusa Bwana aliuliza nani amenigusa? Ule muda walioutumia katika kuulizana maswali yule mtoto wa mkuu wa sinagogi akafa. Wakatumwa wajumbe wamebeba ujumbe ambao kwa yule baba ulikuwa ni kama mshale wenye moto, “binti yako ameshakufa usimsumbue mwalimu”. Biblia inasema Yesu aliposikia lile neno likinenwa ooh! Akamkinga na ngao ya imani, akamwambia usiogope amini tu! Lile neno lilikuwa ni mshale wenye moto na Yesu kwa kuwa ndiye mwenye silaha hizi za kujikinga ambazo tunajifunza hapa alimkinga yule baba kwa ngao ya imani alimkinga yule baba kwa neno la imani! Haleluyaa!!!
Sikiliza mfano mwingine, wengi tunafahamu juu ya habari ya Daudi na Goliati,wakati Israel ikipigana vita na wafilist alitokea shujaa mapiganaji wa jeshi la wafilist aliyeitwa Goliati na akayatukana majeshi ya Mungu wa Israel kisha akawaambia watoe mtu mmoja apigane naye na kama mtu huyo akimshinda itahesabika kuwa jeshi zima la wafilist limeshindwa lakini pia kama atashindwa muisrael basi itahesabika jeshi zima la Israel limeshindwa. Sasa unisikilize kwa historia ya Goliati hapakutokea mtu yeyote kwa upande wa Israel ambaye alithubutu kujitokeza kupambana naye kwa kuwa kiumbo alikuwa ni mkubwa na kiuzoefu alimkuwa ni mtu wa vita maisha yake yote! Wakati huo akatokea kijana mmoja kutoka familia ya Jese jina lake Daudi, akiwa ametumwa kuwapelekea chakula ndugu zake vitani akasikia jinsi mfilist anavyoyatukana majeshi ya Israel na jinsi alivyokuwa akitamba. Basi Daudi akajitolea kupigana na mfilist yule habari zikamfikia mfalme Saul kwamba kuna kijana kutoka nyumba ya Jese amejitolea kupambana na Goliath, Saul akaamuru aletwe kwake na Daudi alipofika kwa mfalme, mfalme alimtazama kisha akamwambia maneno haya:-
34 …Huwezi wewe kumwendea mfilist huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; Na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake”. (1sam. 17:33)
Nilikwambia hapo nyuma maneno ni silaha na yakiwa upande wa adui ni kama mishale yenye moto ili kukukatisha tamaa usiendelee kuamini kile unachoamini na kukitarajia kutoka kwa Mungu, sasa hapa Daudi anakutana na mishale ya mwovu iliyokuwa ikitaka kumchoma(kumkatisha tamaa) ili asiendelee kuamini kile alichokuwa anaamini ya kwamba kupitia yeye Mungu atakwenda kuleta ushindi juu ya taifa la Israel! Kumbuka maneno mtume Paul alimwambia timotheo akisema:-
18 Mwanangu timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii Yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika Kupigana vita vizuri”.
Katikati ya maneno (mishale) ya kukatisha tamaa Daudi anakumbuka maneno na matendo ambayo Mungu alimfanyia huko nyuma na anaamua kuyatumia kama ngao kwake dhidi ya mishale ya mwovu iliyokuwa inataka kumchoma ili akate tamaa ya kupigana na mfilisti, ooh! Daudi anasimama mbele ya mfalme Sauli na kumwambia,34 ………Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba au dubu akamkamata mwanakondoo wa lile kundi, 35 mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake nikampiga nikamwua……….37 Daudi akasema, BWANA aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu ataniokoa na mkono wa mfilisti huyu…………”. (1sam. 17:34-37)
Kitu ni kilekile hata kwako wewe unayesoma ujumbe huu wakati mwingine unapita kwenye magumu na shetani anatupa mshale wake kwako akikwambia hapa hautavuka au hautafanikiwa na wewe kwa kuwa hauna ngao ya imani (neno la imani) unakata tamaa, lakini leo ujumbe huu umekufikia kukutoa hapo uliponaswa, hebu changamka kumbuka kitu ambacho Mungu aliwahi kukufanyia huko nyuma kumbuka neno ambalo Mungu alikupa huko nyuma na ulitumie katika kupigana vita vizuri vya imani!! Daudi alipokatishwa tamaa(aliporushiwa mshale na adui) alijikinga kwa neno la imani na kupitia neno hilo la imani alishinda vita! Haleluya! Nikupe mfano mwingine, wakati Fulani mtume paul aliingia kwenye mapito Fulani lakini kwa kuwa alikuwa na ngao ya imani (neno la imani) hakutetereka bali alisimama imara na kusema, 12 Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa;katika hali yoyote na katika mambo yoyote,nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. 13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. (filipi 4:12,13)
Sijui kama unaelewa nguvu iliyopo katika haya maneno! Yaani paul alikuwa anamaanisha, kwake kuona njaa au kushiba,kupungukiwa au kuwa na vingi, kudhiliwa au kufanikiwa ni kawaida kwa sababu ameshafundishwa na Mungu. Kwa hiyo haimpi shida kabisa anapokutana na hali yoyote haimsumbui, kwa nini? Kwa sababu anayaweza yote katika yeye amtiaye nguvu. Sasa jiulize wewe mwenyewe kimya kimya unapopita kwenye magumu anayoyaelezea mtume Paul unafanyaje? Una silaha gani ya kukukinga na mishale hiyo? Sema nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu!!!
Wakati mwingine unapita hali ya ugonjwa na hapo adui anakutupia mshale akikwambia utakufa na kwa sababu huna ngao ya imani unainama unasubiri kufa. Sikiliza! Mwambie “sitakufa bali nitaishi nami nitayasimulia matendo ya BWANA”. (zaburi 118:18) wakati neno hili la imani limekukinga imani yako inafanya kazi ndani yako na nguvu za uponyaji lazima zidhihirike! Ninakwambia utapona tu, hakikisha shetani akitupa mishale yake inatua kwenye ngao hii ya imani!! Kadiri unavyoendelea kuyasema maneno ya imani yanafanyika ngome (ngao) ndani yako na unajua kitakachotokea? Shetani atakimbia! Yakobo 4:8b inasema, “mpingeni shetani naye atawakimbia”. Na 1Petro 5:9 inasema,
9 Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika IMANI……..”.
Tulisoma habari za Ibrahim hapo nyuma utakumbuka kuwa wakati Ibrahim ameahidiwa mtoto na Mungu kipindi cha kusubiri adui alimrushia mshale wenye moto kumkatisha tamaa lakini Bilia inasema akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini! Maana yake akiliona neno la Mungu ambalo kwake lilikuwa kama ngao iliyomkinga na mishale yenye moto ya yule mwovu hakusita kwa kutokuamini bali alitiwa nguvu na akapokea ahadi aliyoahidiwa na Mungu!(unaweza kusema amen!)
Unapita kwenye nini? Adui amekurushia mshale gani ambao umekupata na kukujeruhi? Mkumbuke Daudi katika zaburi 23:4 anasema “4 Naam nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,SITAOGOPA Mabaya; kwa maana wewe upo pamoja nami……..”.
Bwana akubariki iko mifano mingi sana katika biblia lakini hebu hii ikupe hamu ya wewe kuingia zaidi ili uweze kupata zaidi. Kumbuka kitu hiki ili uweze kuwa na imani kwa kiwango cha juu unahitajika kulijua neno la Mungu kwa kiwango cha juu pia! Nilikwambia huko nyuma kwamba neno la Mungu ni MBEGU sasa rejea mfano wa mpanzi pale kwenye mbegu zilizodondoka kwenye udongo mzuri kuna nyingine zilizaa moja thelathini nyingine sitini na nyingine mia. Nachotaka kusema hapa ni hiki kiwango cha uelewa wako juu ya neno la Mungu ndicho kitakachowezesha imani yako kuwa nyingi au kidogo ndicho kitakachowezesha imani yako kuwa kidogo au nyingi. Biblia inasema kinywa cha mtu hunena yaujazayo moyo wake, kama umaejaza maneno ya imani moyoni mwako kinywa chako kitatoa maneno ya imani lakini kama umejaza maneno ya kuakatisha tamaaa moyoni mwako kinywa chako kitatoa maneno ya kukatisha tamaaa. Ulichojaza moyoni ndicho utakachokitoa kinywani mwako!!!
BARIKIWA NA BWANA unapozidi kutafari ujumbe huu BWANA akupe na mengine mengi yaliyofichika katika ujumbe huu!!!
50 Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni,kwamba mtu akile asife (Yohana 6:50)
Mwl. Alfred T. Katuma.

Comments