NI VIZURI KUONGOZA WATU KATIKA KUTENDA HAKI PAMOJA NA KATIKA KUMJUA MUNGU.


Neno la Mungu linasema kwamba:
"Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele." - DANIELI 12:3.
Kila Mkristo anapaswa awe miongoni mwa "...hao waongozao wengi kutenda haki..." Ipo thawabu kubwa sana kwa wale WANAOWAONGOZA WATU WENGI katika kutenda HAKI. Kutenda haki ni pamoja na kuwafundisha watu njia ya kweli ya uzima wa milele (wapate kumjua Yesu Kristo kuwa Ndiye njia ya uzima wa milele).
Tusiwe Wakristo wasiozaa matunda mema, bali kila mmoja wetu anapaswa kuihubiri injili kwa kila mtu ili injili iwafikie watu wote duniani. Yawezekana AIBU inakufanya ushindwe kuhubiri injili; lakini fahamu Bwana Yesu anasema kwamba:

"Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, na Mimi nitamkiri mbele za Baba Yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, na Mimi nitamkana mbele za Baba Yangu aliye mbinguni." - MATHAYO 10:32-33.
THAMANI YA MKRISTO NI KUHUBIRI INJILI NA KUWAFANYA WATU WENGI KUWA WANAFUNZI WA YESU.
Waongoze watu wengi katika NJIA YA HAKI pamoja na katika KUIFAHAMU KWELI; na hapo ndipo nawe UTANG'AA KAMA NYOTA MILELE NA MILELE.
Kumbuka kwamba siku ya hukumu hatutatoa hesabu ya utajiri wa mali ambao tumeupata hapa duniani; bali KILA MTU ATATOA HESABU YA MATENDO YAKE SAWA SAWA NA JINSI ALIVYOFANYA KAZI YA MUNGU. Mungu anatupatia utajiri ili tuutumie kwa ajili ya utukufu wa Mungu wala si kwa ajili ya kujionyesha kuwa tunamali nyingi mbele za watu. Kila mtakatifu atalipwa thawabu sawa sawa na jinsi alivyomtumikia Mungu. Wale wenye bidii ndio watapata thawabu kubwa; kwa maana Neno la Mungu linasema: "... hao WAONGOZAO WENGI kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele." - DANIELI 12:3.

Si kila mtu ATANG'AA kama NYOTA, bali Biblia Takatifu inasema "... hao WAONGOZAO WENGI kutenda haki..."
KUHUBIRI INJILI SI KAZI YA MCHUNGAJI PEKEE, BALI NI KAZI YA KILA MKRISTO. Wewe ni mtumishi wa Mungu; TAMBUA NA UYATUMIE MAMLAKA ULIYOPEWA katika jina la Yesu Kristo.
Wafundishe neno la Mungu hao ndugu zako, jamaa, marafiki, maadui, na kila mtu ili nawe upate thawabu kubwa siku ya hukumu. Fanya sasa; badilika sasa; tubu sasa; anza sasa kuhubiri injili; nawe hakika utabarikiwa katika jina la Yesu Kristo.

USIOGOPE kwa sababu Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya kukutia nguvu, kukuongoza, na kukushindia.
Kama wewe umeguswa na neno hili, tambua Mungu amekuteuwa kwa kazi maalumu. Anza na hicho ulicho nacho ndani ya moyo wako. Kila Mkristo anao ujumbe wa neno la Mungu; anza na huo uo ujumbe kisha zidi kusoma Biblia, epuka mizaha na maneno yasiyofaa, jifunze kutoka kwa watumishi wa kweli, pia dumu katika maombi; ndipo utaona unakua kiroho hatua baada ya hatua.
Kumbuka kwamba:

"... hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele." - DANIELI 12:3.
Nawatakia baraka tele katika jina la Yesu Kristo. Amina.
By Mwl  Masanja Sabbi

Comments