NJIA ZA KUTAMBUA KOSA



         

1:Kutambua kwa jinsi ya rohoni, Na hii huja baada ya tukio.  
Mathayo 27:3.-
''Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, NALIKOSA nilipoisaliti damu isiyo na hatia.'' Yuda alitambua kosa lake baada tu ya kutenda na akataka arudishe pesa kwa wale makuhani ila alikua amechelewa sana na pia jambo hilo lilipelekea kujiua jambo ambalo ni baya zaidi.
 
2:Kugundua wewe mwenyewe. 
Mwanzo 3:9-10.
''BWANA MUNGU akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, NILIOGOPA KWA KUWA MIMI NI UCHI,NIKAJIFICHA. '' Baada ya kutenda dhambi Adamu na mkewe walijiona wako uchi, wakaogopa na wakajificha na hii ni baada ya kutambua kuwa wametenda tofauti na maagizo mema ya MUNGU baada ya kuutendea kazi uongo wa shetani. ni jambo baya walifanya na hata wewe ndugu yangu ukitenda dhambi kwa bahati mbaya hakikisha unatubu na kutokurudia tena uovu huo maana toba ya kweli ni toba ambayo hurudii tena kutenda dhambi.
 
3: Kwa njia ya kuambiwa na wengine. 
2 Samweli 12:9-10 ''''Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. '' Wakati mwingine tunatambua uovu wetu kutokana na kuambiwa na wengine mfano mzuri ni hapa ambapo Daudi baada ya kutenda dhambi ya kuchukua mke wa mtu neno la ufunuo kutoka kwa MUNGU liliingia kwa Nabii Nathani na akaenda na kumwambia Daudi juu ya uovu wake na MUNGU alielezea na adhabu sahihi kwa Mfalme Daudi kupitia kinywa cha yule nabii, hivyo usichukie ndugu unapoelezwa uovu wako na watu wengine, jambo la muhimu ni kuacha dhambi maana hatuwezi kumwona MUNGU pasipo kuwa watakatifu iwe kumwona kwa baraka zake kwetu au kumwona baada ya kuwa tumeshinda ya dunia tukiwa watakatifu tuliookolewa na YESU KRISTO.(Waebrania 12:14)
 
4:Ni kuambiwa na MUNGU au ROHO MTAKATIFU, 
Mwanzo 17:1''Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni MUNGU Mwenyezi, uende mbele yangu, UKAWE MKAMILIFU.''  MUNGU alimchagua Ibrahimu kama ambavyo anaweza kukuchagua wewe au amekwishakuchagua tayari kwa ajili ya kazi yake. lakini MUNGU hapa anamwambia mtumishi wake kwamba UKAWE MKAMILIFU, kwa nini alimwambia hivyo maana yake ni kwamba mwanzo hakuwa mkamilifu hivyo MUNGU alimtaka awe mkamilifu, maana MUNGU ni mtakatifu/mkamilifu na hawezi kukubariki au kukutumia wewe kwa kazi yake kama wewe sio mkamilifu. MUNGU hachangamani na waovu hivyo ndugu ili MUNGU akutumie kwa viwango vya juu katika huduma yako au akubariki katika kazi yako au biashara yako hakikisha uko mkamilifu daima na mwaminifu mbele zake. Hivyo kwa kutusaidia MUNGU hutujulisha kabisa uovu wetu kupitia ROHO MTAKATIFU.
 
5:Ni kusoma BIBLIA .
Mithali 11:1Mizani ya hadaa ni chukizo kwa BWANA; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza. Kipimo sahihi cha kupima kama unampendeza MUNGU au unamchukiza ni kusoma neno la MUNGU maana neno la MUNGU li hai na linayajua makusudi ya moyo pia neno la MUNGU lina pumzi ya MUNGU na hatuwezi kujificha kwenye neno la MUNGU.  Hivyo kwa kusoma BIBLIA utajua kabisa uovu wako mfano utasoma kwamba uasherati, uchawi,ibada ya sanamu na ufisadi ni dhambi(wagalatia 5:19-21) hivyo utatakiwa kuacha uovu huo maana watendao matendo hayo wasipotubu hawataurithi ufalme wa MUNGU. Hivyo kwa kusoma BIBLIA utatambua uovu wako na ukiachana na uovu huo utakua umefanya jambo jema sana.
 
6:Kuangalia yote uliyopitia kuanzia asubuhi hadi jioni kabla hujalala, kuweka kumbukumbu kwa yote unayoyafanya.
 Ufunuo 2:5.''Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.'' Ndugu ni vizuri kuangalia ni wapi ulikoangukia yaani ni kwenye tukio gani na muda gani ulitenda uovu iwe kwa kuwaza au kutenda na unatubu. Hivyo usiku unaweza ukakumbuka kabisa ni wapi ulikosea muda fulani tangu asubuhi, yawezekana ulisema uongo, ulisengenya au ulitenda kosa ambalo wewe unaliona dogo lakini dhambi ni dhambi tu hakuna kubwa wala ndogo, hivyo ukitambua kosa ni muhimu kutubu na pia tambua kuwa kutenda dhambi huku unatambua kabisa kwamba hiyo ni dhambi ni vibaya sana.
 
7: Kuomba MUNGU akujulishe kosa  kama hutaona hauna amani moyoni. Mara nyingi sana nimekosa amani kwa sababu ya kukusudia kutenda jambo fulani ambalo kwangu nimeoa sio dhambi lakini kumbe jambo hilo ROHO MTAKATIFU halitaki na hali hiyo inapelekea kukosa amani hivyo hulazimika kufanya maombi ya kutubu na amani baadae inarejea, Hivyo wakati mwingine wewe uliye na ROHO MTAKATIFU ndani yako 
  ukikosa amani kwa sababu ya kutaka kutenda jambo fulani acha nalo hata kama unaona ni jambo jema maana sana kwako, na kama hujaokoka hakikisha unampokea BWANA YESU ili uzaliwe upya kwa jinsi ya ROHO na ROHO wa MUNGU aje kwako na akusaidie kutenda haki na kuishi katika mapenzi ya MUNGU.
MUNGU wa mbinguni akubariki sana na hakikisha una YESU KRISTO maishani mwako.
Ni mimi ndugu yako Peter Michael.

Comments