PILATO ALIMSHINDA SHETANI KWA KUKWEPA KISASI, JIFUNZE KUSAMEHE.



Bwana Yesu asifiwe sana, namshukuru Mungu kwa fursa hii tena ninapokukaribisha katika so o letu linalohusu Msamaha.

Ndugu yangu, Dhana ya Kusamehe inaweza kufasiliwa kama hali ya huachilia, yaani kupuuza, hili ni jambo ambalo kila mmoja wetu analijua na pengine kila mmoja wetu limemgisa, aidha kwa kusamehe au kusamehewa! KWA UFUPI, GHARAMA YA MSAMAHA HUWA NI YA ANAYESAMEHE, JAPO ANAYELIPA NI ALIESAMEHEWA.
Naomba unielewe vizuri, unaposamehe, kwako huna dukuduku, ila aliyesamehewa hubaki na maswali aghalabu kama hakutegemea kusamehewa.Hii inadhihirisha kuwa, mara unaposamehe, anayesamehewa anabaki na maswali kichwani kuwa kweli kasamehewa au la, na hii ndiyo gharama halisi.

Wengine husema, katu siwezi kusamehe, na hata nikisamehe siwezi kukusahau, lakini Biblia inatueleza (Mathayo 6:12)"Msipowasamehe wengine Makosa yao,wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu" Hii ina maana gani? Hapa Mungu anatudhihishia kuwa, Kanuni anayotumia katika kukusamehe, ni ile ile uliyotumia katika kuwasamehe wengine; Yaani kwamba, kama hujawasamehe wengie, hata wewe huwezi kusamehewa

Ni wazi kuwa kumsamehe mtu aliyekuumiza sio jambo la mzaha na wala si suala la dogo lakini hapo hapo ndipo Mungu anapotaka kuona utu wako na uvumilivu wako. Wengine machoni pa watu hudiriki kusema "Yameisha" mara nyingi baada ya USULUHISHO, lakini ndani ya mioyo yao bado hajasamehe.

Rafiki, naomba ujue kuwa, kabla mtu hajakuudhi, kuna nguvu inayokuwa nyuma yake ambayo humwongoza ili akuumize! Usipojua hilo, utaangamizwa na nguvu hiyo, kwasababu nguvu hiyo ni ya roho iliyotumwa kukuangamiza hata kupitia hasira, chuki na kutokusamehe. Angalia mfano huu wa gari linapomgonga mtu serikali haishtaki gari bali anayeshtakiwa ni dereva. Hii ina maana kwamba, anayekukosea huwa ana anayemhimiza kufanya hivyo! Vivyohivyo ukiumizwa unatakiwa uangalie ile nguvu iliyopo nyuma ya aliyekuumiza. Kimsingi kuna nguvu inayotenda kazi nyuma ya aliyekuumiza na usipoijua hiyo nguvu utajikuta unashindwa kusamehe.

Usichoke kusamehe, kwa kuwa neno linasema samehe saba mara sabini tena kwa kwa kutwa, tena linaongeza, usichoke kutenda wema maana Bwana atatulipa tusipozimia mioyo, Naomba unielewe vizuri hapa, Hii inamaana kuwa, kwanza una kheri wewe uliyepewa ufunuo hata ukajua kuwa yule kakutendea uovu, je si kazi yako kumsamehe na ndipo uanze kumuelimisha?
Hili linaenda hata Kwa wazazi, nawaombeni watoto wenu wanapowakosea wakati mwingine mtumie njia mbadala kuwaadhibu na siyo kuwachapa tu, kwani huyu pengine hajui kama ametenda kosa na pengine ni bahati mbaya tu, kwani sisi kama tungekuwa tunaadhibiwa mara tutendapo dhambi hata kwa kiboko kimoja tu, si wengine tungekuwa hatuna ngozi kabisa?

Mpendwa, naomba nikwambie kuwa, kwa kusamehe, unajipatia kibali mbele za Mungu na kukuondolea magonjwa yako yote. Zaburi 103:3 "Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote". Magonjwa haya si lazima uwe hoi kitandani, pengine unaweza hata ukawa na hasira tu, basi wee samehe ili Mungu akuondolee hasira hiyo, Samehe ili Mungu afute kumbukumbu ya ulivyokosewa na wala usije ukakumbuka tena.
Tena ukimsamehe ongea nae vizuri, mtolee ushuhuda mzuri na umwombee sana ili Mungu amrehemu-Haleluya!

Nawasiki,tuepuke misamaha ya kinafiki ya kusema eti sitakusahau, huu si msamaha wa kweli., msamaha huu hautoki kwa Mungu, huu umetoka kwa shetani.Epuka na mizigo hiyo. Kumbuka Isaya 1:18,....dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa nyeupe kama sufu, na kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi. Rafiki yangu, inakuwaje wewe ukisamehe ukumbuke, ebu uache moyo wako mweupe usio na madoamadoa, usio na kinyongo! Kwanini Mungu amesema dhambi zako zitakuwa nyeupe wala si njano, orange au hata kahawia? Yesu anataka aweke utukufu ndani yako kupitia msamaha, achilia moyo wako, ili Bwana aingie akuponye magonjwa yote, aoundoe BP zako zote, aondoe vidonda vya tumbo katika jina la Yesu Kristo. Samehe uwekwe huru.
Waefeso 1:7 Katika yeye huyo (YESU) kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha (yaani mingi na mikubwa) ya dhaambi sawa sawa na wingi wa neema yake. Nakuomba usihesabu makosa bali uhesabu utukufu wa Mungu unaoupata kupitia Masamaha.
WEWE ULIYEGUSWA MAFUNDISHO HAYA RUDIA SALA HII HAPA CHINI.

Baba katika Jina la Yesu Kristo ninaomba nguvu ya msamaha wako; leo nimetambua kuna nguvu inayotenda kazi nyuma ya mtu aliyenikwanza,ninawasamehe wote walionikwaza katika Jina la Yesu. Ninatangaza msamaha, ninavunja madhabahu ya makwazo na kutokusamahe ndani yangu katika jina la Yesu Kristo. Baba ninaomba uniponye na matatizo yaliyoingia ndani yangu kwasababu ya kutokusamehe katika Jina la Yesu.

BASI BAADA YA KUPOKEA NGUVU YA ROHO MTAKATIFU NAOMBA NIKUOMBEE SASA ILI UDUMU KATIKA PENDO LA KRISTO.

Baba katika Jina la Yesu Kristo ninakushukuru kwa neno lako na msamaha wako kwa watoto wako, Ahsante Yesu kwa wote waliokili ujumbe huu!Baba naomba rehema zako ziwe juu yao tangu sasa, katika jina la Yesu Kristo, uwajaze roho ya msamaha na upendo. Ondoa magonjwa yao yote yaliyowatesa siku zote, futa visasi na laana za kutokusamehe katika Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu uliye hai.

Kwa Mawasiliano zaidi.

Mwl. SOSPETER SIMON
SLP 1275
TABORA

sos.sesi@yahoo.com
+255 784/757 464 141
+255 712 909 021.

Mwl. SOSPETER SIMON

Comments